KITISHO

KITISHO !

Richard MWAMBE

 

 

SURA YA 1

Mbowe Club Saa 1:23 usiku

RADI kali ilipasua anga na kufanya mchoro wa kutisha, mwanga wake ulilipoteza giza kwa sekunde kadhaa, kila kilichojificha kilionekana wazi.

Hakuna mtu hata mmoja aliyekuwa nje muda huo. Ni mvua kubwa na ngurumo za kutisha zilitawala kila kona, ilikuwa ni hali ya kuogofya sana. Mifereji na mito ya dhalura ilianzishwa na maji ya mvua hiyo.

Kama ilivyo ada katika jiji la Dar es salaam, barabara zote zilikuwa zimejaa maji, kama ukiwa dereva mgeni basi hutoweza kujua ni wapi barabara ilipo. Sehemu kubwa ya mji hasa katikati ya jiji gari nyingi ziliegeshwa kando ya barabara kusubiri mvua iishe lakini haikuwa hivyo kwani mvua ilikazana zaidi ya saa nne.

Wakati hayo yote yakiendelea, ndani ya ukumbi mkubwa wa starehe unaojulikana kama ‘Mbowe Club’ watu hawakuwa wakijua kama nje kuna mvua, disco liliendelea kwa nguvu zote, watu walicheza, wakanywa na kuburudika. Katika kaunta kubwa ya ukumbi huo kulikuwapo walevi kadhaa ambao tayari walikwishabadilisha lugha ya mawasiliano kutoka Kiswahili na kuwa Kiingereza.

Gina binti Komba Zingazinga alikuwa ni miongozi mwa watu wachache waliokuiwa wamesaliwa na akili zao na utashi pia, alikuwa akinywa kinywaji chake taratibu huku jamaa mmoja akijitahidi kumzengea zengea lakini asifanikiwe. Kila wakati alionekana kuitazama saa yake aliyoivaa mkononi na aliposhusha mkono aliinua ule uliokamata ile bilauri yenye kiuno iliyojaa mvinyo kutoka Dodoma. Baada ya kupiga funda moja kasha la pili aliiteremsha taratibu na kuiweka juu ya mbao mwororo iliyoifunika na kuipendezesha kaunta ya ukumbi huo. Macho yake yalikuwa yakizunguka huku na kule yakitazama au kutafuta kitu ambacho hata yenyewe hayakukijua.

Upande wa pili wa ukumbi huo, kwenye sakafu iliyojengwa juu kidogo na ili uifikie itakulazimu kuzikwea ngazi kadhaa, kulikuwako watu watatu, wawili wanaume na mmoja mwanamke. Mwanaume mmoja alikuwa na tambo kubwa lililojaa kimazoezi, enzi za utoto wetu tungeweza kumwita Pawa, lakini enzi hizi wanamwita Baunsa, yote hayo ni mabadiliko ya nyakati. Watu wale watatu walikuwa wakiongea jambo Fulani na meza yao ilikuwa imechakazwa kwa pombe kalikali na sahani za nyama zilizokuwa zikipishana, vyote hivyo vilimiminwa katika matumbo hayo matatu. Ilikuwa ni vigumu kusikia nini wanachokiongea kutokana na muziki mkubwa uliokuwa ukipigwa ndani humo. Kati ya kaunta alipokuwapo Gina na ule upande kulitenganishwa na kundi la vijana waliokuwa wacheza muziki huo kwa mitindo mbalimbali. Gina alihakikisha hapotezi macho yake upande ule kwani mwili wake ulikuwa ukisisimka mara kwa mara na hiyo kwake ilikuwa ni ishara ya hatari.

Dakika chache baadae alimuona Yule mwanamke akiinuka na kutoka katika vile viti, akitembea kwa mwendo wa ki-levi levi. Akamtazama na kujua mara moja kuwa alikuwa anaelekea chooni, Gina akajikuta akishuka kutoka kwenye kiti kirefu alichokuwa amekalia, akaigugumia pombe yake yote kinywani mwake, kasha akavuta hatua fupifupi akikumbana na walevi na wacheza muziki akaelekea kule alikokwenda Yule mwanamke.

Halafu nitamwuliza nini? Akajiuliza pa si na kupata jibu. Lakini aliendelea kuvuta hatua kuelekea kule chooni, akapinda kona ya kwanza na kuingia kwenye milango Fulani iliyokuwa ikielekea huko atakako, mbele kidogo alimuona Yule mwanamke akiingia katika moja milango ya vyoo vile. Gina; mkono wa kulia ukiwa nyuma ya suruali yake ndani kidogo ya jaketi lake, sikwambii alishika kitu gani, aliuendea ule mlango, mara ghafla akaanza kuhisi kitu kikimfinya mkononi mwake, ilikuwa ni saa kubwa ya mkononi, saa yenye uwezo wa kupokea nukushi, kupiga picha za mjongeo na mnato, yenye uwezo wa kurekodi sauti na pia unaweza kuitumia kama simu. Akainua mkono na kubofya kitufe Fulani kasha akasubiri kidogo. Wakati akisubiri kijimkanda hicho chembamba kikitoka kwenye saa yake, Yule mwanamake bado alikuwa chooni.

Mama yuko mahututi Shamba, Tena Saan Aisee! Uikuwa ni ujumbe uliosomeaka hivyo katika kile kijimkanda. Akakikata na kukitia mfukoni mwake kisha akaanza safari ya kutoka ndani ya Klabu ile, akili yake ilikwisha sahau juu ya Yule mwanamke, akapita mlangoni na kukumbana kikumbo na Yule mwanaume mwenye tambo kubwa, akielekea kule choo cha wanawake, Gina akasukumwa pembeni; na Yule bwana akapita.

Nje ya Klabu hiyo ndipo alipokutana na mvua ya kutisha, akapachua kikofia katika ukosi wa jaketi lake na kukivaa kisha akaliendea gari lake, mita kadhaa kabla hajalifikia akapiga breki na kuacha kinywa wazi, hakuamini anachokiona. Vioo vyote vya gari yake vilikuwa vimevunjwa, tairi hazina upepo na ndani kulijaa maji ya mvua. Wameiba? Akajiuliza, kisha kwa mwendo wa tahadhari akasogea kwenye lile gari, juu ya kiti cha dereva kulikuwa na bahasha ngumu ya khaki, akatazama huku na kule, alipojihakikishia usalama akaingiza mkono kwa minajiri ya kuichukua ile bahasha ijapokuwa ilionekana kulowana.

 

Daraja la sarenda saa 1:55 usiku.

BMW nyeusi iliyokuwa iking’azwa kwa mwanga wa radi, ilshuka katika barabar hiyo ya Kenyata kwa kasi sana ikitokea maeneo ya Masaki. Ilipofika katika makutano ya barabar hiyo na ile ya Ally Hassan Mwinyi mkabala na Ubalozi wa Ufaransa iliingia barabara kubwa bila kungalia usalama huku ikirusha maji juu kutokana na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha usiku huo.

Madam S alikuwa katulia kwenye usukani akiiongoza gari hiyo ya Mwingereza kwa umahiri mkubwa. Akakunja ushoto na kukanyaga mafuta kueleka mjini. Ilikuwa ni tabu kuona mbele kutokana na wingi wa mvua, barabara imejaa maji, umeme umekatika, ilikuwa ni shida juu ya shida. Madam S hakujali alilikanyaga daraja la Salenda na kuendelea mbele, lakini kabla hajalimaliza, hamad, kulikuwa a mwili wa mwanadamu uliolala barabarani huku mikono yake ikiwa imefungwa nyuma. Akaiyumbisha gari kuukwepa mwili huo, gari ikasota na kukosa muelekeo, akarudisha usukani kulia kuukwepa mwamba wa daraja, akaknyaga krachi na kuachia mafuta kasha akatoa gia ya tano na kushusha ya nne, kutahamaki gari yake ilikuwa ikihamia barabara ya pili, akakanyaga breki lakini ikashindwa kusimama, akaknyaga tena breki bado gari ilikuwa ikiendelea, ikapanda tuta lakutenga barabara, ikajipigia na kutua barabara ya pili, akili ikamrudia, akavuta breki ya mkono na ile BMW ikaserereka na kujizungusha.

Kishindo kikubwa kikasikika, BMW iligongana na Land Rover Defender, ikaangushwa pembeni. Madam S akajikuta kwenye pori la mikoko chini ya daraja la Salenda, akafyatua mkanda, akapiga kioo cha mbele kwa kukikanyaga kwa mguu, akatoka, akajipapasa na kukuta bastola zake zipo salama.

Damu zilizikuwa zikitiririka semu ya paji la uso juu kidogo ya jicho la kulia, wakati akijitahidi kusimama, radi kali ilipiga na kufanya mwanga mkubwa uliong’aza vichaka vyote, Madam S akaona mbele yake kama kivuli cha mtu aliyesimama nyuma yake. Akajua ni mawenge ya ajali tu, akageuka nyuma na mara ghafla akakutana na pigo la kitu kizito kilichotua katikati ya paji la uso, akayumba vibaya lakini mikono yake tayari ilikuwa imekwishachomoa bastola zake, kabla hajafyatua akafunikwa na gza nene lililomfanya ashindwe kuona chchote, akaanguka kama mzigo na bastola zikimtoka mikononi mwake.

 

Ofisi ya Usalama wa Taifa saa 2:00 usiku.

MAAFISA wa Idara ya Usalama wa Taifa walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida usiku huo. Katika moja ya ofisi za jengo hilo, vijana wawili na msichana mmoja walikuwa bize kutazama luninga nyingi zilizowazunguka zinazoonesha maeneo mbalimbali muhimu ya Jiji la Dar es salaam. Kupitia luninga hizo waliweza kuona moja kwa moja kile kinachotokea kwenye maeneo hayo kama Uwanja wa ndege, Bandarini, Stesheni ya Treni, Uwanja wa Sabasaba, Makao makuu ya Rais na maeneo mengine mengi ambayo yamepewa umuhimu wa pekee kwa sababu hii au ile.

Avant, msichana mbichi wa miaka takribani thelathini hivi alikuwa katingwa kuangalia tukio la ajali iliyotokea daraja la Salenda, bado alikuwa anapata shida kujua hasa nini kinaendelea kutokana na ile picha kufichwa na mvua ilikua ikinyesha eneo hilo lakini kila ilipokuwa radi ikipiga ndipo alipoweza kuona kitu, baada ya dakika kadhaa alipuuza na kuendelea kutazama maeneo mengine.

Mubah akajikohoza kidogo na kumgutusha Avanti kutoka pale alipokuwa akitazama.

“Si ukapime, au Mama yako anajua?” Avanti akamtania Mubah.

“Unanianza we mrembo, mi nasubiri time hapa niingie viwanja!” Mubah akajibu, huku akitoka kwenye kiti chake na kukiendea kile alichoketi Avant, akasimama nyuma yake, machoye akiwa kayakaza kwenye ile luninga.

“Shiit! Avant, nini hicho?” akauliza huku akisogea jirani zaidi.

“Ajali, imetokea kama dakika kumi hivi,” Avant akajibu.

“Kwa nini usipige simu polisi wawahi kama kuna chochote cha kuokoa?” Mubah akahoji.

“Sasa Mubah, Salenda pale kituo kipo jirani wataenda tu,” akaeleza huku akimtazama Mubah usoni.

“Yaani wewe! Kitendo cha kuitega kamera pale hatukufanya kwa makosa, lile ni eneo nyeti sana, kama ni ajali lazima polisi wafike mapema ili kuondoa kilichopo, pale vipngozi asilimia 99 wanapita, ikiwa hujuma utalaumiwa wewe kwani ndio eneo lako la kutazama leo!” Mubah akalalamika huku akiliendea kabati dogo lililo hapo jirani.

Avant akainua simu na kubofya tarakimu Fulani Fulani kasha akatoa taarifa hiyo kituo cha polisi cha Salenda. Haikupita dakika tano tayari kupitia luninga yake aliweza kuona gari na nyendo za polisi eneo hilo bila kujali mvua iliyopo. Avant aliendelea kutazama huku akigonga gonga karamu yake.

§§§§§

Gina alivuta hatua na kuingia katika lango kuu la Ofisi Nyeti, Shamba, akabofya namba zake za siri, kasha akaweka kiganja chake juu ya kioo Fulani kilichopo mlangoni na baada ya hapo akafanya kama anachungulia, kijimwanga chekunfu kikapita kati ya macho yake na kitasa cha ule mlango kikafyatuka, akaufungua na kuingia ndani. Moja kwa moja akaingia chumba Fulani na kuvua jaketi alilovaa, akabadilisha nguo na kurudi katika hali ya ukavu, akatoka na kutembea mwendo mfupi kabla hajagonga mlango Fulani kwa mtindo wa pekee na mlango ule ukafunguliwa.

“Karibu Gina!” Dkt Jasmine akamkaribisha na nukta chache baadaeakampatia kikombe cha kahawa.

“Hawajafika?” Gina akauliza.

“Hapana, we ndiye wa kwanza, leo sijui kuna nini, labda kwa sababu ya mvua,” Dkt. Jasmin akaeleza.

Gina akashusha pumzi ndefu, mazungumzo mengine yakaendelea huku wakiwasubiri wengine, kila mara walikuwa wakitazama saa zao, hakuna simu wa taarifa yoyote iliyokuwa ikifika katika nyumba hiyo, Gina na Jasmine wakaanza kupata wasiwasi. Jasmine akainua uso na kuitazama saa kubwa ya ukutani, ikamwonesha kuwa ni saa 3:15 usiku.

“Hapana Gina, hii sio kawaida, tuanze kuwatafuta mmoja baada ya mwingine,” Dkt. Jasmin akamweleza Gina, kasha wote wawili wakaenda kwenye chumba maalumu cha mawasiliano, ndani ya chumba hicho ambamo ndiyo ofisi ya kudumu ya Chiba wa Chiba kulijawa na makompyuta na luninga nyingi huku na kule, simu za upepo, za kawaida na zile za satellite zilikuwepo. Kila kitu kilikuwa kinafanya kazi kwani haikuruhusiwa kuzima chochote labda tu kama kuna matengenezo, kila mmoja akaketi katika kiti chake na kuanza kucheza na simu zao za siri zilizounganishwa moja kwa moja.

Hakuna simu ya mkononi iliyokuwa ikipatikana si ya Madam S wala ya nani, walipigwa na butwaa na kubwa simu za nyumbani zote zilikuwa zikiita bila kukoma hazikupokelewa. Gina akamgeukia Dkt. Jasmine.

“Oya Shost, hapa ni mguu kwa mguu nyumba moja baada ya nyingine tukapate kujua kilichojiri,” Gina akamwambia Jasmine kasha wote wakaingia vyumbani na walipotoka walikuwa katika mavazi ya kazi, kila moja alibeba silaha anazoamini zingemfaa usiku huo kwani hawakujua hatari itakayowakabili. Wakiwa katika harakati hizo ndipo Gina alipokumbuka ile bahasha.

“Nisubiri Jasmine!” akarudi kwenye kile chumba akaichukua ile bahasha, bado ilikuwa imelowa akaichana taratibu na kuitoa karatasi ya ndani kwa uangalifu.

“Nini Gina?” Jasmine akauliza.

“Hii bahasha niliiokota kwenye ari yangu lakini sikuwahi kuifungua ndani,” akamjibu.

Gina alibaki kakodoa macho baada ya kukutana na kichwa cha habari kikubwa kilichosomeka ‘KITISHO!’ kisha chini yake kuliandikwa sentensi moja tu

Mwisho wa zama zenu umefika!

Maneno hayo yalizigonga kwa nguvu nyoyo za wadada hawa, wakabaki wakitazamana, wkageuza macho yao wakaitazama tena ile karatasi.

“Gina!” Jasmine akaita.

“Jasmine!” naye akaitikia na wote wakatoka na kuingia kwenye gari ya Jasmine na kuondoka eneo hilo.

§§§§§§

 

Kerege – bagamoyo saa 4:07 usiku

TOYOTA Hilux Double Cabins, iliingia taratibu getini na kuegeshwa karibu na bustani ya maua iliyotengenezwa ndani ya ngome kubwa iliyobeba jengo la kifahari kuliko fahari yenyewe. Walinzi kadhaa walionekana kwenye kona zake, hawakushughulika kabisa na gari hiyo bali kila mmoja alishika lindo lake.

Dereva akashuka na watu wengine kama watatu hivi wakashuka, wakazunguka nyuma na kufungua funiko kubwa la alluminium lililotengenezwa ili kufunika mzigo uliopo ndani yake.

“Washushe hao, kisha wapeleke Kuzimu,” mmoja wa wale vijana aliyekuwa ameketi mbele akawaagiza wenzake kasha yeye akazikwea ngazi kulielekea jengo hilo lililoendezeshwa kwa taa zenye marembo mbalimbali.

Sauti za viatu vyenye kisigino kigumu zilisikika zikitembea lakini aliyevaa hakuonekana, Bwana Mpaya alibaki kusimama na kutazama kule sauti ile ilikokuwa ikitokea na asione mtu zaidi ya giza lililomlaki isipokuwa aliposimama yeye mwanga ulikuwapo na kufaya nuru ya kupendeza. Kasha ukimya ukatawala na sauti nzito ikalipenya lile giza.

“Ndio Bwana Mpaya, karibu sana, natumaini umekamilisha nililokutuma, sivyo?” alikuwa ni Pancho Panchilio aliyeyafikia masikio ya Mpaya aliyekuwa amesimama katikati ya sebule pana lakini asimwone anayeongea naye, isipokuwa sauti tu.

“Ndiyo Boss, tumewaleta lakini hali zao ni mbaya sana,” akaeleza.

“Vizuri sana, nani na nani mmempata?” akauliza tena.

“Tumempata Boss wao na Mtaalamu wao wa kompyuta,” akajibu.

“Ha! ha! ha! ha! ha!” akacheka cheko la pesa.

“Ok, wape vijana posho yao kama nilivyokwambia kisha unitafutie kichwa cha Kamanda Amata, huyu hasa ndiye mwiba kwangu, nataka apotee kwenye uso wa nchi ili binadamu tule vizuri, kuna pesa ndefu sana nimeiandaa mkilikamilisha hili,” Pancho akiwa mafichoni mwake akakohoa kidogo wakati Mpaya alikuwa akitoka, “Sikia Mpaya, hakikisha ukimuua Kamanda Amata, mkate kichwa, kisha kiwiliwili mkichome moto na kichwa mniletee, mbwa wangu hawajala nyama siku nyingi sana, maana Yule ni shetani anaweza kujiunganisha tena halafu akaangusha balaa, kwa heri!”

Alipomaliza kusema hayo na taa ndani ya jengo lile zikazimika.

 

 

SURA YA 2

KAMANDA Amata akaitazama gari yake aia ya Subaru Forester jinsi ilivyochakazwa kwa risasi, akashusha pumzi ndefu.

Wadude hawa wangeniua! Akajisemea moyoni huku akijaribu kuiwasha nayo ikawaka, akairudisha barabarani na kushika njia ya kwenda mjini, alijipapasa mifukoni hakuiona simu yake, wala saa yake mkononi haikuwepo. Any way! Akajipa moyo. Huku akiendelea kuutafuta mji wa Dar es salaam, saa ya ndani katika gari yake ilimwonesha kuwa ni saa tano za usiku.

Gina sijui kama atanielewa, maana tulikubaliana saa moja na robo, labda nitamkuta! Akaendelea kuongea na nafsi yake,  huku akiiacha Gongo la Mboto na kuitafuta Uwanja wa Ndege. Katikati ya safari yake akafungua redio ndani ya gari na kusikiliza kinachoendelea. Ilikuwa ni kituo kimoja cha redio binafsi kikirusha habari hiyo ya dharula iliyoyanasa masikio ya Amata usiku huo.

…Mwili wa Mheshimiwa huyo umekutwa sakafuni bila uhai na kitu kama matundu ya risasi yakionekana kifuani mwake. Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wake ili kuwakama waliohusika na mauaji hayo…

Amata akakanyaga breki kali na kuitoa gari barabarani kwani taarifa hiyo haikujitosheleza kwake, akaegesha gari pembeni na kutazama huku na kule hakuona mtu kupita eneo hilo, pembeni yake kulikuwa na bar iliyokuwa ikiendelea kuburudisha watu kwa vinywaji na vilaji, akashuka na kuiendea, alipofika tu akakutana na mwanadada mrembo aliyevalia nguo nyeupe juu na sketi nyeusi chini.

“Karibu kaka, karibu kiti,” Yule dada akamkaribisha Amata huku akifuta meza iliyokuwa hapo. Ijapokua haikuwa nia ya Kamanda kuketi, akajikuta amefanya hivyo, “Pole!” neon hilo likaupasua moyo wa Amata akamtazama Yule dada Mhudumu wa bar.

“Pole ya nini?” akauliza

“Una damu kichwani,” akamwambia.

“Shiit!” akang’aka na kujigusa, kweli akahisi maumivu na kitu kama jeraha.

“Asante sana!” akamjibu, “Unaweza kunisaidia simu yako?” akamwuliza.

“Haina salio lakini, halafu ni kisimu cha tochi,” akajibu kwa aibu.

“Naomba hivyo hivyo.”

Yule mwanadada akachomoa simu yake akampatia Amata. Ilikuwa ni simu iliyochakaa, iliyoonekana kupita katika mikono mingi ya watu mpaka kuifikia mikono hii ya huyu Mhudumu wa baa. Ilifungwa kwa mipira ya manati, betri lake lilishikiliwa na kipande cha mpira wa manati. Hakujali, aliitazama vyema kasha akaanza kubofya hapa na pale.

“Haina vocha hiyo!” Yule Mhudumu akaeleza tena.

“Usijali, kaniletee Bia baridi sana bila glass tafadhali,” Kamanda akamwagiza Yule dada lakini alilotaka yeye haikuwa bia ila zile dakika mbili za kubaki peke yake. Vidole vyake vikaanza kutomasa tarakimu Fulani Fulani na alipomaliza, akapumzika, wakati huo bia yake ilikuwa imefika, akaigusa, akamwonesha Yule Mhudumu alama ya dole gumba, kisha akabaki na hamsini zake.

Meseji iliyofuata katika simu hiyo ilikuwa ni kutoka katika kampuni moja ya simu nchini, Kamanda Amata alikuwa amechukua muda wa hewani kwa namna yao ya siri na sasa simu ile Kimeo ilipata uhai.

Akaanza kupiga namba za maswahiba wake wa kazi, Chiba; simu haikuita kabisa, Madam S vivyo hivyo, akaduwaa wa sekunde kadhaa, haikuwa kawaida kwa watu hao kuwakosa kwenye simu, akili ya Kamanda ikiruka chogo chemba. Mbele yake kulikuwa na luninga kubwa iliyokuwa ikionesha matukio mbalimbali ya Kitaifa na lile lililomvutia ni ajali ya Salenda, alisahau kupiga simu na kutazama tukio lile. Kamanda Amata alikaza jicho kutazama picha hizo lakini hakuzitilia maanani kwani wakati wa mvua ajali kama hizo ni za kawaida sana.

“Kaka hadi bia imepoa!” Yule Mhudumu alipita tena kwenye ile mea aliyokaa Amata.

“Oh, sorry,” akamjibu kasha akainua chupa na kujijiminia mafunda kadhaa, alipoishusha ilikuwa nusu tu.

Akaitazama tena ile simu akabofya tarakimu nyingine, akaweka sikioni, simu ikaita na kuita haikupokelewa kama ilivyokuwa kwa simu za nyumbani za Chiba na Madam S, akashusha pumzi. Nini kinaendelea? Akajiuliza. Akarudia kuipiga namba ya mwisho, akaweka simu sikioni, baada ya dakika moja ile simu ikakwapuliwa na sauti nyororo ya kike ikasikika tofauti na alivyotegemea.

“…Polisi Kituo cha Kati, nikusaidie nini?” ile sauti ikauliza.

“Mwenye Ofisi, Inspekta Simbeye yupo?” Kamanda akauliza.

“…Inspekta leo alitoka kama mida ya saa tisa alasiri, hajarudi bado…” Yule mwanadada akajibu.

“Alisema kuwa atarudi au aliacha maagizo yoyote?” Kamanda akauliza.

“…alisema tu kuwa angerudi kabla ya saa kumi na ni kawaida yake kutoka saa tisa na kurudi saa kumi kila siku, lakini leo mpaka sasa hajarudi…” sauti ile iliendelea kueleza.

“We umeingia kazini saa ngapi?” akamwuliza.

“…nimeingia saa nane nitatoka saa nne usiku… samahani lakini naogea na nani?” Yule mwanadada alipouliza hivyo simu ikakatika.

Ndipo Kamanda alipojikuta hayuko peke yake mezani, mbele yake kulikuwa na mwanamke mmoja aliyevaa vazi refu jeusi, hijab na kujificha uso wote isipokuwa macho. Kamanda Amata akamtazama mtu huyo kwa tuo, akainua chupa yake na kupiga funda la mwisho, alipoishusha ilikuwa haina kitu ndani.

“Kwa nini unapenda kudhalilisha dini ya watu? Unaingia baa na vazi kama hilo?” Kamanda akaanza uchokozi, lakini Yule mtu hakujibu kitu, alikuwa akimwangalia tu. Jinni au! Akajiwazia, kabaridi ka haja kakapita kutoka utosini mpaka unyayoni.

§§§§§§

GINA aliegesha gari mita mia mbili hivi kutoka katika lango la kuingilia nyumba ya Madam S kule Masaki, akateremka na Jasmine akafanya vivyo hivyo, kisha wote wawili wakarudi taratibu wakiachina nafasi ya mita kadhaa katikati.

Lango la mbele lilikuwa limefungwa, Gina alitazama huku na huko hakuona hata dalili ya binadamu kupita myaa ule, isipokuwa manyunyu tu ya mvua yalikuwa yakimnyurunyuta mwilini mwake. Akajipapasa katika kiuno cha suruali yake na kufatua kijipini chenye ncha mbili zilizojikunja kwa mtindo wa pekee, kishapo akachukua kipini kingne kutoka kwenye kibanio cha nywele zake, akatanguliza kile chenye ncha mbili katika tundu la funguo ya lango hilo, akachukua kile cha tatu na kukitumbukiza kati, akafanya manuva kidogo tu, kitasa kutoka Uingereza kikafyatuka na kuuruhusu lango lile kuwa wazi.

Skunde mbili zikapita, ya tatu na ya nne bila Gina kuingia ndani ya wigo ule mkubwa, akatazama tena usalama, bado barabara ilikuwa tupu, hakumuona Jasmine, moja kwa moja akajua kuwa kwa vyovyote keshajiweka katika kona maalum ya kumlinda swahiba wake. Akaingia ndani ya wigo huku bastola yake aina ya Winchester ikiwa mkononi. Akatembea kwa hadhari kubwa huku na huko akitazama hakuona mtu. Hatua tatu kuelekea mlango wa nyumba hiyo, ndipo alipoona kitu kilichomshtua sana, akasimama mapigo ya moyo yakimwendea kasi kifuai mwake.

Mbele yake kulikuwa na mwili wa Binadamu uliolala chali ukiitupa mikono yake huku na huko, hakuwa na uhai. Gina akajiweka tayari kwani aliona huo unaweza kuwa mtego kwake, akatazama jumba la Madam S, taa za ndani zilikuwa zikiwaka kwa mwanga wa kupendeza, ina akajikuta anaishiwa nguvu, akainua mkono wake na kuizungusha saa yake kwa namna ya pekee kasha akaisogeza karibu na kinywa chake.

“…Jasmine …” akaita, hakupata jibu, akazidi kuingiwa na wasiwasi. Dina akatulia pembeni ya ule mwili, akahisi kama kuna mtu anayekuja nyuma yake, akakamata bastola yake barabara, liwalo na liwe, akageuka ghafla tayari kwa shambulizi, hakuna mtu.

Shiit! Akajisemea. Akauruka ule mwili na kuufikia mlango wa nyumba ile kubwa, akatoa gloves mfukoni na kuivaa, kisha akashika kitasa kwa mkono wa kushoto uliokuwa na gloves akaingia ndani ya sebule pana, iliyomlaki bila hiana. Kila kitu kilikuwa katika utulivu wa hali ya juu sana, hakukuonekana kama kulikuwa na purukushani yoyote ndani ya nyumba hiyo, akajivuta kuelekea chumba cha Madam S, akaufikia mlango na kuujaribu, ulikuwa umefungwa. Akatumia hila ileile na kuufungua. Hata chumbani kulikuwa tulivu kabisa, hakukuwa na ishara yoyote iliyoonesha kama kulikuwa na pambano la kufa na kupona.

Akaenda pembeni mwa kitanda upande wa kichwani, akachuchumaa na kubonya vijinamba Fulani vya kificho ambavyo kwa mtu wa kawaida huwezi kuvigungua mpaka mmiliki akuoneshe. Droo moja ikafunguka na ndani yake ikajifunua kompyuta kubwa ika simama mbele yake, Gina akatikisa kichwa juu chini, kwani alijua kama hiyo kompyuta haipo mahala pake basi hali ya Taifa iko hatarini. Alikumbuka maneno ya Madam S siku alipomkaribisha nyumbani kwake kwa mara ya kwanza.

….heri mimi nife lakini hii kompyuta ibaki. Nikifa au nikipotea kabla hamjatangaza kifo change hakikisheni mnang’oa kompyuta hii na kuikimbiza Shamba kisha mtangaze matanga. Siri yote ya Taifa hili ipo hapa, mipango yote mibaya na mizuri ipo humu, watu wote wabaya na wazuri wapo humu…

Gina alijikuta analia machozi peke yake, nifanyeje, niondoke nayo?  Akajiuliza, nitaifikisha Shamba salama? Akajiuliza bila majibu. Gina alijikuta kachanganyikiwa, hajui la kufanya, aichukue au aiache, kichwani mwake alielewa kuichukua kompyuta hiyo ina maana kuwa Madam S kafa au katoweka, na je kama kuna wanaotaka na wameshindwa kuipata hatoweza kuwa kawarahisishia kazi?

Ulikuwa ni mgongano mkubwa wa mawazo kati ya roho, moyo na ubongo wake, akaamua kuiacha. Akabofya tena zile tarakimu na ile kompyuta ikajirudisha ndani taratibu na kujigia mahala pake. Gina akashusha pumzi ndefu, akaitazama bastola yake na kunyayuka taratibu, akaufuata mlango na kutoka akiufunga nyuma yake.

 

KAWE – saa 4:02 usiku

LAND CRUISER ya polisi ilikuwa nje ya lango kubwa la nyumba ya Mheshimiwa Mbunge wa jimbo la Miroroso, wananchi wasio na dogo nao walijumuika nje ya nyumba hiyo wakikodoa kodoa macho kushangaa tukio hilo lisilo la kawaida. Hakuna aliyejali mvua ya rasharasha iliyokuwa ikiendelea kunyesha, watu walijikusanya kwa kujikunyata kutazama.

Ndani ya jumba hilo kulikuwa na Polisi waliovaa kiraia wenye bunduki kubwa kubwa wakiwa wanatembea hapa na pale, mwili wa marehemu Mbunge ulikuwa ndani ya chumba chake cha kulala. Polisi waliokuwa huko chumbani wakifanya taratibu zao za uchunguzi walikuwa wamekamilisha kazi yao, walitoka sebuleni na kuwapisha vijana wachache kutoka idara ya dharula ya kampuni binafsi ambayo husambaza gari za wagonjwa mitaani kwa minajiri ya kusaidia hali za dharula kama hizo.

Waliufunga sawia mwili wa Mheshimiwa katika mfuko maalumu na kuupakia kwenye machela yenye magurudumu, kasha wakaisukuma kuelekea kwenye gari yao iliyokuwa imeegeshwa pembeni tu mwa jumba hilo. Vilio vilisikika, wananchi wakalia na kuomboleza, walimpenda Mheshimiwa, ijapokuwa alipojenga jumba lake haikuwa jimboni mwake lakini bado alitoa misaada ya hali na mali kwa waliomzunguka.

“Alikuwa shujaa, kwa vyovyote wametumwa kumuua,” mwombolezaji mmoja alisikika akisema huku akifuta machozi yake.

Baada ya zoezi hilo ndipo Wananchi waliruhusiwa kuingia ndani na kuanza msiba huo. Hakuna aliyeamini kabisa juu ya lililotokea.

Lakini ilibaki hivyo kuwa Mbunge wa jimbo la Miroroso aliuawa na watu wasiojulikana.

§§§§§§

Kamanda Amata aliwekwa kati ya watu wawili huku mmoja na huku mwingine, mbele yake kulikuwa na mwingine tena ukiacha dereva aliyekuwa akiongoza gari hiyo. Wote walivaa maguo yaliyowaficha miili na sura zao. Hakuna aliyeongea; ile gari ilipita daraja la Salenda na kufuata uelekeo wa kwenda Mwenge, baada tu ya kupita daraja hilo, ikakunja kulia na kufuata ile Kenyata Drive, ilipomaliza maofisi ya Mabalozi iliiacha ile ya kwenda Coco Beach na kukunja kushoto, nyumba ya nne mbele ikasimama.

“Usilete makeke yako ya kipumbavu, tunataka kompyuta anayotumia boss wako basi,” akaambiwa na kuteremshwa chini, wakauendea mlango mkubwa na kuufungua, Kamanda Amata akatangulia mbele na wale jamaa wakamfuata nyuma, wote watatu walkuwa na Shot Gun mikononi mwao.

Wakatembea taratibu na kuipita ile maiti pale nje, moja kwa moja wakaingia ndani ya sebule, mmoja wao akasimama nje ya mlango wa sebule kuweka usalama, mwingine akabaki sebuleni na wa mwisho akaenda na Amata mpaka chumba cha Madam S.

“Usilete ujanja wako, tunajua kuwa ni wewe tu unayeweza kuitoa hiyo kompyuta hapo, haya fanya hivyo,” akamwambia huku akiwa kasimama umbali wa mita kama mbili hivi. Kamanda Amata akaiendea ile droo na kuingza mkono wake mahala Fulani, akapapasa anavyojua yeye, mara ile droo ikajivuta mbele na kufunguka, hakuna kompyuta! Yule mjinga akabaki katoa macho, akashangaa mahala pale hakuna kompyuta waliyokuwa wanaitaka ilhali wao walikuwa na uhakika kuwa ipo hapo baada ya kufanya uchunguzi wa kina.

“Haipo?” akauliza.

“Si unaona mwenyewe haipo!” Kamanda akajibu.

“Imeenda wapi?” akarusha swali la kijinga.

“Mimi na wewe tumeingia pamoja sasa nitajuaje ilipokwenda?” Kamanda akajibu kwa swali. Kama kuna kosa alilolifanya Yule mtekaji na atalijutia kuzimu ni ktendo cha kwenda kuhakikisha kwa macho kuwa Kompyuta ile haipo pale. Kamanda Amata kama umeme, kutoka pale alipokuwa amechuchumaa kuitoa ile Kompyuta, alijikunjua na kutawanya miguu yake sentimeta mbili kutoka usawa wa sakafu, Yule mjinga alipigwa ngwala kutoka upande wa nyuma na kujibwaga akitanguliza kisogo, yowe na kishindo vilimshtua Yule wa sebuleni akaja kwa kasi. Kamanda Amata alijirusha upande wa pili wa chumba na risasi zilizotoka katika bunduki ya Yule mtu wa pili zikachimba sakafu.

Kabla Yule bwana hajajiweka sawa, mwendo wa sekunde moja tu aliyoitumia kufanya shabaha ya pili dhidi ya Kamanda Amata, alijikuta akipaishwa juu na kujibwaga kama mzigo sakafuni tayari damu ilikuwa ikimtoka kama bomba. Amata alishuhudia hilo kwa haraka sana hakuelewa nini kinatokea.

Wamegeukana? Akajiuliza.

“Upo salama Kamanda Jitokeze!” sauti ya Gina ilimrudishia matuamaini. Kamanda Amata akajitokeza mzima mzima, lo! Domo la shot gun lilikuwa likimtazama umbali wa mita tatu tu kutoka pale alipo.

“Umeharibu utaratibu, nilikwambia usifanye makeke yoyote sasa wewe umekiuka kanuni, namuua huyu Malaya wako kasha naondoka na wewe,” sauti ya mtekaji ilisikika. Kamanda Amata akaona sasa mchezo usio rasmi unaanza kwani hakuwa na taarifa yoyote juu ya hii hatari.

“Umeshasema Malaya, we muue tu, hana thamani kwangu!” Kamanda akajibu.

“Leo hana thamani kwako wakati kila siku unamlala nyumbani kwako!” Yule mtekaji akaendele kuropoka, maneno ambayo yalimtia hasira Gina, akajaribu kukukuruka lakini hakuweza kutoka kwani kono la mtekaji lilimbana koo na akajihisi kukosa pumzi. Kamanda Amata alaimtazama Gina anavyoteseka, akawasiliana naye kwa macho, gina alielewa kitendo alichokifanya Kamanda.

Gina aliachia mkono wake kutoka kwenye ule wa Mtekaji lakini bado alikuwa kabanwa kwa kabala, akajizungusha na kukamata uume wa mtekaji huyo, akaubana kwa nguvu na kuuzungusha ghafla. Yule mtekaji akapiga kelele za maumivu, akamwachia Gina akabaki katoa macho ya kutisha, Gina akaendelea kuuzungusha huku amezikamata na korodani zake, Yule mtekaji akaanguka chini, Gina hakumwachia mpaka alipohakikisha kamtoa roho.

“Asante Gina!” Kamanda akamshukuru wakakumbatiana.

“Kompyuta Gina,” Kamanda akamwambia.

“Usiwe na shaka, nimekwishaitoa muda mrefu, wakati naondoka ndipo nilipoona hiyo gari inakuja, nikajibana hapo kwenye kochi kubwa upande wa nyuma hamkuniona. Niliposikia kile kishindo huko chumbani mlipo, nikajua kumekucha, nikamwona huyu wa sebuleni akija kwa kasi huko ndani, name nikajitokeza kumwahi kabla hajaleta madhara, ndipo nikamfumua bichwa lake, lakini sikujua kama kuna mwingine huku nje ndo huyu mpumbavu akanibana kabala. Pole sana Kamanda, nafurahi kukuona, Idara imetikiswa!” Gina alieleza kinachojiri.

“Gina haina haja ya kukaa hapa, twende tukajipange juu ya hili,” Kamanda akamwambia huku wakitoka. Walipofika karibu na geti, Gina akauchukua begi kubwa alilokuwa amelificha hapo wakatoka nje.

“We ulikujaje hapa?” kamanda akamwuliza.

“Shiiit!” Gina aling’aka baada ya kugeuka na kutoiona gari aliyokuja nayo. Akageuka kwa Kamanda na kumtazama usoni.

“Dr. Jasmine!” akamwambia huku chozi likimtoka. Amata akamtazama na kisha akaliendea lile gari walilokuja nalo na wale watekaji, akaingia, bahati nzuri halikuhitaji ufunguo, lilikuwa ni la kubonya tu nalo likawaka, wakaingia barabarani kuondoka.

 

KUZIMU – shimo la mauti

Kilikuwa chumba kikubwa chenye vijichumba vingi vidogo kwa vikubwa, kwa ujumla kilitisha kwani mafuvu ya vichwa vya binadamu yalipambwa ukutani kama mapambo ya kawaida, taa nyekundu kwa buluu ndizo zilizong’aza eneo hilo la kutisha, kulikuwa na friji kubwa mithiri ya chumba cha kuhifadhia maiti. Sehemu nyingine kulikuwa na stoo iliyohifadhi kila aina ya vikorokoro vya kutisha maalumu kwa ajili ya kutesea, kunyongea, na hata kuulia kabisa.

Chumba hiki kilijengwa chini kabisa ya jumba la kifahari la Mhindi Pancho Panchilio eneo la Kerege njia ya kwenda Bagamoyo, hakuna aiyejua kinachoendelea. Kwa nje lilikuwa ni jumba linalovutia kuliangalia, asilimia kubwa ya wananchi wa eneo hilo hawakuwahi kumjua wala kumwona mmiliki wa kasri hilo, ni watoto tu waliopenda kusemajumba lile ni la wanyonya damu kutokana na mambo kadhaa waliyokuwa wakiyaona, mara watu wameletwa huku nyuso zao zimefungwa vitambaa vyeusi na mambo kadha wa kadha kiasi kwamba ilipelekea watoto wa kitongoji hicho kukaa mbali na jumba hilo.

Lakini tofauti na watu wazima, wao waliwachapa fimbo watoto wao waliokuwa wakisema maneno hayo kutokana na kwamba kutoka ndani ya jumba hilo waliweza kupelekewa maji safi kwa mabomba maalum yaliyounganishwa na pampu kubwa na yenye nguvu, hivyo waliondokana na kero ya maji ya kunywa.

Mwili wa Madam S ulibwagwa chini kama roba la chumvi, haukuwa na uzima wowote.

Kibosho, akaangalia hali ya chumba kizima walichouhifadhi mwili huo, aliporidhika nacho akatikisa kichwa juu chini na kuwageukia watu wake.

“Ulinzi wa nguvu zaidi ya ule wa Ikulu, sawa?” akaagiza.

“Sawa Mkuu!” wakajibu. Akawaacha na kutoka, akaelekea chumba kingine, akakuta vijana wakimsulubu vikali Chiba wa Chiba huku akiwa ananing’inia kwenye minyororo, mwili wote ulitota damu, hakutamanika, hakuangalika. Kibosho alisimama mlangoni.

“Karibu sana kuzimu!” akamwambia Chiba aliyekuwa hawezi hata kuinua uso, “Wewe ndiye kinara wa kuvuruga mitandao ya watu sivyo, sasa utakuwa binadamu wa kwanza kushuhudia kifo chako mwenyewe baada ya kuwaona wenzako wote wako hapa, mbuzi nyie, nani aliwadanganya kuwa mna uwezo wa Kijasusi wa kuitisha Dunia? Sasa leo mtapambana na Shetani nah ii ndiyo himaya yake,” akaongeza kusema kisha akageuka kando akawatazama vijana wake walioonekana wana uchu wa kuua.

“Na Yule bibi, mfungeni kama huyu, lakini msimtese mpaka azinduke kama bado hajafa ili mateso yote ayashuhudie kwa akili na ufahamu wake, nimekuja hapa kwa kazi moja tu,” akamgeukia Chiba “Kuua!” akamaliza na kutoka huku akifuatiwa na vijana watatu wenye misuli ya ajabu. Chiba akiwa katika ile minyororo hakufanya lolote zaidi ya kutulia tu na kusubiri kuona nini kinaendelea.

§§§§§

Kamanda Amata waliitelekeza ile gari eneo la Hoteli ya Sheratoni na kisha wao kutembea kwa miguu mpaka ilipo ofisi ya Madam S. ilikuwa tayari imepita saa tano usiku, walinzi wakawapokea na kuwaruhusu kupita kwani walishazoea kuwa muda wowote watu hao huwa wanaingia ofisini. Moja kwa moja jicho la Kamanda Amata likaenda kwenye maegesho na hakuliona gari la Madam S, wakaingia ofisini na kuketi katika viti vyao kwa namba zao, kwani katika ofisi hiyo kila moja alikuwa na kiti chake kadiri ya namba zao za kikazi. Ukimya ulichukua nafasi kati yao, hakuna aliyeongea kwa sababu wakiwa hapo ni Madam S huwa anasema alichowaitia.

Kamanda Amata akamgeukia Gina.

“Gina, hili eneo si salama kwa sasa!” akamwambia.

“Yaani mi sina amani na eneo lolote, hata kitanda change nakiogopa, natamani kutoroka,” akajibu.

“Kutoroka! Sio suluhisho,” Kamanda akamwambia huku akinyanyuka na kufungua jokofu lililowekwa vinywaji vya kila aina, akatoa Konyagi ndogo na kuketi kitini, akachanganya na Sprite kisha akanywa taratibu. Gina alionekana kuwa mwenye mawazo mengi sana. Wakiwa katka ukimya huo mara simu ya mezani ikaita kwa fujo. Kila mmoja aliitazama hakuna aliyeipokea, baada ya kukerwa na kelele ya chombo hicho Kamanda Amata akaiinua na kuiweka sikioni bila kuongea.

“Kamanda Amata”, kisha cheko zito na la dharau likafuata, “…leo mtaishi kama digidigi, na nitawafuata popote mlipo mpaka nihakikishe nawamaliza, kwa taarifa yako, kibibi chako ninacho hapa nusu mfu, na wengine wawili, mmoja tayari ni marehemu kama unataka kumwona nenda kwenye vichaka vya Gongo la Mboto njia panda ya kwenda kwenye makaburi ya Wachina… tuachane na hilo, naihitaji hiyo kompyuta usiku huu… nipe kompyuta nikupe marehemu wako ukazike…”

Hasira ya Kamanda Amata ikawaka juu ya huyo asiyemwona, “…kama unaitaka hii kompyuta njoo uichukue!” akamjibu.

“…Nataka uniletee wewe mwenyewe kwa mkono wako au huyo Malaya wako ambaye pamoja nawe mmeshanipotezea watu wangu watatu, kama hamtaki basi nitaichukua mwenyewe…” ile sauti ikaendelea.

“Acha uoga wewe! Kama unajiamini jitokeze tupambane, atakayeshinda atachukua kompyuta!” Kamanda akaongea kwa jazba, tayari konyagi ilishaanza kufanya kazi ichwani.

Yule mtu wa upande wa pili akacheka sana kisha akaendelea “…sifanyi hiyo michezo ya kitoto, lakini nakuhakikishia kuwa nitaipata hiyo kompyuta, na nitazichukua roho zenu wote sita kabla ya jua kuchomoza,” akapiga mkwara.

“Na mimi nakuhakikishia kuwa nitakuwa nimekwisha kutoa roho yako na vibaraka wako kabla ya jua kuchomoza, shetani wewe!” alipomaliza kusema hayo, akainuka kitini.

“Unaenda wapi Kamanda?” Gina akauliza.

“Huyu mshenzi keshanitia wazimu, nitahakikisha namjua usiku huu huu na namng’oa koromeo lake, hawezi kufanya dharau na kitengo nyeti kama hiki, huyu hafai kuishi,” Amata aliongea kwa hasira.

Gina naye akasimama wima na lile begi lenye kompyuta mkononi, “Na hii je? Maana inaonekana wana uchu nayo,” akamwambia Amata.

“Tia kwenye sefu salama hapo hata uje na kifaru huwezi kuitoa,” akamweleza.

“Sijui namba za kufungulia,”

“Oh, sorry!” Kamanda akaichukua ile kompyuta na kuingia kwenye kijichumba kidogo kisha akaiweka mahala salama na kutoka na lile begi, akafungua kabati linguine na kutoa kompyuta iliyofanana na ile lakini ilikuwa mbovu siku nyingi, akaipachua hard disk na kulichukua lile ganda tupu akalitia kwenye begi, kisha wakatoka na kuchukua gari mojawapo iliyo kwenye maegesho.

“Gina, upo vizuri? Akili ipo sawa?” Kamanda akamwuliza. Gina hakujibu, alionekana kujawa na hofu kuu, Kamanda akamwangalia na kumwuliza tena.

“Gina, unajua kitu kinaitwa The Art f War?” akamwuliza.

“Hapana Kamanda!” akajibu. Kamanda Amata akatikisa kichwa baada ya jibu hilo.

“Sikiliza Sun Tzu aliandika ‘Jifanye mchovu unapokuwa na nguvu na jifanye una nguvu unapokuwa mchovu’, hata mimi Gina ninaogopa maana simjui adui yangu kasimama wapi, lakini lazima na mimi nimtishe hiyo ndiyo Art Of War,” Kamanda alimtoa hofu Gina.

“Nimekuelewa Kamanda, sasa tunapambana vipi na huyu hayawani?” Gina akauliza. Kamanda akabaki kimya kwa muda, kisha akamgeukia Gina.

“Gina, naomba nisikujibu, na wala usinambie unachofikiria, unajua kwa nini?” akamuuliza.

“Hapana!” akajibu.

“Art of War inasema ‘Ifanye mipango yako iwe siri, isipenyeke kama giza la usiku, na unapojitokeza jitokeze kwa nguvu kama radi’ sio maneno yangu nia Sun Tzu na daima huwa napenda kufuata maneno yake ndiyo maana unaona hapa nilipo,” alipotaka kupachika ufunguo kwenye switchi ya gari Gina akamdaka mkono.

“Kamanda! Hayo uliyosema si ajabu hata adui anayajua,” akafungua mlango na kumvuta Kamanda nje, kisha wakaelekea getini na kutoka nje mpaka barabarani.

“Naona sasa umeanza kujua unalotakiwa kufanya, vizuri sana Gina!” Kamanda akampongeza kisha wakaingia kwenye tax na kutokomea.

Breki ya kwanza ilikuwa mje ya ukumbi wa Jiji mkabala na bandari ya boti za Zanzibar, wakalipa na kisha wakapotelea gizani.

§§§§§§

Katika kaunta ya kituo cha Polisi cha Kati, kulikuwa na PC wawili na WP mmoja, Kamanda Amata na Gina walikwea ngazi na kusimama mbele yao. Wale Polisi mara moja walimtambua Gina na kusimama imara kwa kumpa heshima yake ya kijeshi.

“Inspekta Simbeye, ameonakana tena huku?” Gina akauliza.

“Yupo afande, amekuja muda si mrefu,” Yule WP akajibu.

“Naomba tumwone!” Gina akasema hayo huku tayari ameshaanza safari ya kuifuata ofisi hiyo.

Inspekta Simbeye alionekana kuzeeka ghafla kwani mashavu yake yalikuwa yameshuka kiasi kwamba Kamanda Amata alitamani kucheka.

“Shikamoo mzee!” Amata alianza kwa kuamkia kama kawaida akikutana na Inspekta huyo.

“Sina haja ya shikamoo yako, nakupigia simu Amata hupatikani kwa nini?” akauliza kwa hasira.

“Inspekta, kama ulivyowakosa wengine wote na mimi pia usingeshangaa, hata mimi sina mji wa kupokea, hali ni mbaya, nilikutafuta ulikuwa umetoka,” kamanda akajibu.

“Kamanda Amata! Ni nani huyu anayetufanya sisi wapumbavu kiasi hiki, Mheshimiwa Mbunge wa Miroroso ameuawa usiku wa leo, ni masaa mawili tu yalopita,” kabla hajaendelea Kamanda akamkatisha.

“Na hilo hasa ndilo limenileta kwako, nilitaka kujua ni nani aliyeuawa maana nimesikia tua lakini sikujua ni nani aliyeuawa!”

“Ni Mbunge wa Miroroso,” Simbeye akajibu.

“Ok, nimeelewa Inspekta, sasa picha inaanza kujijenga taratibu na itakamilika tu,” Kamanda akajibu.

“Huu umekuwa usiku mbaya sana, siwezi kulala kwa kuwa kifo cha huyu Mbunge kimekuja wakati mambo haya ya vita vya Ufisadi mliyopambana nayo huko Uswizz bado hayajapoa, na huyu Mbunge ndiye alikuwa mstari wa mbele kabisa katika kuyafichua, je huu si mnyororo mmoja?” Inspekta akaonesha wazi hofu yake.

“Nimekupata Inspekta, naomba niondoke kisha tuwasiliane dakika arobaini na tano zijazo,” Kamanda akajibu kisha akaondoka na kufuatiwa na Gina.

 

HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI- SAA 6:47 USIKU

KAMANDA Amata akifuatana na Gina waliingia moja kwa moja chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo, wakamkuta Daktari akiendelea na uchunguzi. Wakiwa wanaongozwa na muuguzi waliingia ndani ya chumba hicho. Walipofika wakaonesha vitambulisho vyao kwa Yule daktari, hivyo hakuwatilia shaka.

“Karibuni sana!” akawakaribisha.

“Asante!” Gina akawa wa kwanza kujibu.

“Sijui niwasaidie nini? Maana nimechoshwa na maswali yenu yanayofanana,” Yule daktari akauliza huku akiwa amesitisha kuendelea kufanya uchunguzi.

“Nataka kujua maraehemu amekufaje?” Kamanda akauliza.

“Amepigwa risasi,” akajibu daktari.

“Ngapi?” Gina akawahi.

“Mbili za kifuani,” akajibu.

Kamanda Amata akasogea jirani na kutazama yale majeraha yalivyojipanga, moyo wake ukapiga chogo chemba, yalikuwa mithiri ya yale ya Frederick Masawe na Petit kule Uswizz, akatazama kwenye paji la uso la marehemu akaona alama ndogo ya risasi nyembamba iliyopenye bila uharibifu.

“Daktari, nah ii je?” akauliza. Yule Daktari akasogea na kwa kutumia kurunzi yake maalumu akagundua tundu hilo, wakamgeuza marehemu na kisogozi wakakuta matone machache ya damu.

“Amepigwa risasi tatu,” Kamanda akaeleza, “Asante Daktari, tulitaka kujua hilo tu,” wakamwacha na kuondoka zao.

“Kamanda hii kazi nyingine sasa,” Gina akamwambia Amata.

“Usijali Gina, hii kazi lazima imalizike usiku huu, kimya kimya mpaka kitaeleweka, leo nataka tufanye kazi hii ngumu mi na wewe tu, jua likichomoza tujue nini tumefanya na dunia ya pili isijue nini kimefanyika, usiogope, Art Of War iliyoandikwa na Sun Tzu inasema ‘Nenda taratibu kama upepo na muwe karibu kama miti. Shambulia kama moto na uwe imara kama Mlima’” Kamanda akamwambia Gina huku wakitoka nje ya chumba hicho.

“Twende nyumbani kwanza tukachukue dhana za kutosha kisha tuingie rasmi kwenye mpambano, tufanye haraka kabla watu wetu hawajapata madhara zaidi, Gina, piga simu Polisi Mabatini waambie kuna mwili wa marehemu kule Gongo la Mboto ili waende kutazama, na kama adui alitegemea kutunasa huko atapambana na vijana wa khaki,” Kamanda alimwambia Gina na mara baada ya Gina kufanya hivyo, wakaingia kwenye Tax.

“Kinondoni makaburini tafadhali!” Kamanda akamwambia dereva tax, kisha wakaondoka eneo hilo. Baada ya kuuacha Mtaa wa Mindu na kuchukua barabara ya Umoja wa Mataifa ndipo kamanda alipogundua kuwa kuna gari ikiwafuata, akamtazama dereva ambaye alionekana hajui chochote, walipopita shule ya Sekondari Tambaza ile gari ikawapita kwa kasi na kuwazuia kwa mbele.

Watu watatu walishuka kwa kasi kwenye ile gari, mikononi wakiwa na Shot Gun, waliishambulia ile tax kwa risasi na kuichakaza vibaya.

Kamanda Amata alimvuta dereva na kumsweka chini, mtawanyiko wa vyoo uliwafanya kushindwa kufanaya lolote, Gina alishuhudia lile begi likinyakuliwa na alipotaka kulitetea alipigwa na kitako cha bunduki akarudi chini, wale jamaa wakaondoka kwa kasi na gari yao wakapotelea katika mitaa ya Upanga.

Kamanda Amata akajinyanyua na kutoka nje, akamtoa Gina kisha Yule dereva ambaye alikuwa katika hali mbaya, hakuguswa na risasi lakini hofu ya milio ya zile mashine ilimfanya kuachia mkojo bila kujijua.

Kamanda Amata akachomoa kadi moja ya kibiashara na kumpatia Yule kijana, “Kesho jioni unitafute!” kisha yeye na Gina wakapotea eneo lile kabla Polisi hawajafika.

Walipokuwa wakikimbia, Gina alikuwa akiishiwa nguvu kila muda ukienda.

“Kamanda, Kamanda! Nakufa!” alilalamika.

“Jikaze Gina!” akamhimiza lakini hali haikuwa nzuri, Gina akaanguka chini. Kamanda akamtazama vizuri akaona mchaniko mkubwa a kichwani na damu zikimvuja eneo moja la mgongo karibu na nyonga, ilikuwa ni risasi iliyompata barabara katika eneo hilo.

“Shiiitttt!”

Akatazama huku na kule, akaona gari ikija kwa mbali, akamweka Gina chini na kuizuia kwa kuingia barabarani, hakuuliza, alimbeba Gina haraka na kumwingiza kwenye gari.

“Nifikishe Mtaa wa Upanga Seaview haraka!” akaamuru.

“Aliyekwambia hii tax ni nani?” Yule deeva akajibu kijeuri huku akizima gari na kuchomoa ufunguo. Kamanda Amata hakuwa na muda wa kupoteza, alfungua mlango akazunguka upande wa dereva, akafyatu lock na kumvuta nje, akamtupia barabarani kisha akakaa kwenye usukani, akachomoa kadi yake ya benki na kuivunja katikati, akaislaidi, katikati yake pakatokea ufunguo mdogo wenye meno mawili akaupachika kwenye swichi ya gari n kuiwasha kisha akaingia barabarani na kumwacha Yule mmiliki wa gari akipiga kelele.

§§§§§

SAA saba na nusu usiku ilimkuta Kamanda Amata katika jumba kubwa lililojengwa kandokando ya bahari ya Hindi huko Upanga, akaegesha gari mahala pake kisha akamtoa Gina ambaye tayari alikuwa amekwishapoteza fahamu.

“Usife Gina, usife tafadhali, subiri kidogo Gina!” kamanda alikuwa akiongea kama aliyechanganyikiwa huku kambeba Gina katika mikono yake akielekea ndani ya jumba hilo.

Dr. Khadrai alikuwa mlangoni akimwangalia kijana huyo ambaye wamekutana mara chache sana katika harakati za maisha yao.

“Karibu Amata, pole sana!” akamkaribisha na kumwongoza moja kwa moja mpaka kwenye chumba maalum ambacho kilishehenu kila aina ya kifaa tiba unachokijua, akamwonesha kitanda pa kumlaza Gina. Dr. Khadrai akamtazama Gina harakaharaka kisha akamtazama kamanda Amata. Akavuta mashine yake kubwa na kuchukua trei iliyojaa vikorokoro kisha akaanza kazi yake ya kitabibu, kwa kumsafisha Gina majeraha na kumtoa risasi iliyokuwa imenasa ndani. Kamanda Amata hakuwa na muda wa kusubiri.

“Daktari, maadam yuko mikononi mwako, naomba niende, kama kuna shida yoyote naomba unitaarifu kwa namba hizi,” akampa namba za Gina, kisha yeye akachukua simu mbili za Gina, akachukua saa na kumwachia simu moja ndogo ambayo si rahisi kwa mtu mwingine kuitumia kwa jinsi ilivyo.

“Amata usiwe na wasiwasi, huyu hajadhurika sana, akiamka tu nitakwambia,” kisha akaendelea na kazi yake.

 

KEREGE – saa 7:35 usiku.

PANCHO Panchilio alishusha siga alilokuwa amelipachika kinywani mwake na kulibana kwenye kibompoli maalumu cha kuzimia dubwasha hilo. Akainua macho yake na kutega masikio akisikiliza michakacho ya miguu ya mtu aliyekuwa akitembea sebuleni. Kwa jinsi alivyoijenga nyumba yake hiyo, yeye aliweza kumwona kila mtu lakini wale watu hawakuweza kumwona yeye nah ii iliwafanya kusikia sauti daima na kutokuona sura ya bosi wao.

“Karibu sana!” sauti yake ikaijaza sebule yote.

“Mkuu tumefanikiwa kuipata kompyuta uliyotuagiza Mkuu!,” Yule mtu akasema.

“Vizuri sana, sikufanya kosa kabisa kuwachagua ninyi watu makini katka kazi hii, je wale hayawani wawili mmewapata?” akauliza.

“Hapana hatujawapata lakini bila shaka wamefia kwenye gari waliyokuwa wakiitumia kwani tumeishambulia kwa risasi za kutosha,” akajibu, mara hakusikia kitu zaidi ya ukimya uliofuwatiwa na sonyo refu.

“Fanculato!” akatukana, “Kwa nini msihakikishe kama amekufa? Yule bwana ni hatari sana, hakikisheni mnapata habari zake usiku huu, naitaka roho yake kabla hakujapambazuka, potea!” akamukuza.

Pancho Panchilio alikuwa amekodi vikosi viatatu kwa nyakati tofauti na vyote kuvipa kazi moja tu ya kukisambaratisha kikosi cha TSA kuanzia Madam S mpaka wa mwisho. Mipango ya kazi hiyo ilipangwa kitaalamu sana na ilitumia mbinu za hali ya juu, mpaka dakika hiyo alikuwa tayari amefanikisha kwa asilimia sitini ya kile alichokidhamiria, nab ado muda wake bado ulikuwa unaruhusu kumalizia asilimia zilizobaki. Alihakikisha vikosi vyake hivyo havijuani na wala havikutani lakini vyote alikuwa amevipa kazi ileile kwa saa zilezile za kutekeleza lakini muda tofauti wa kufanya kazi.

Hakuona hasara sana kwa kupoteza vijana watatu usiku ule yeye aliishupalia dhamira yake tu ndio maana alikodi watu hao.

Kikosi cha kwanza kiliongozwa na Kibosho, Kanali wa jeshi aliyehasi na kupotea pasikojulikana, sasa alirudi baada ya kuitwa na Mhinidi huyo kwa kufanya kazi kama hizo. Kikosi cha pili kiliongozwa na mtu mmoja hatari kutoka nchi jirani aiyejulikana kama Kaburu na kikosi cha tatu kiliongozwa na mpiganaji aliyebobea kwenye taaluma ya kuua bila kukusidia huyu alikuwa ni mtaalmu wa kucheza na kifo mbele ya binadamu yeyote Yule, ni jambazi la kimataifa kutoka Kigoma, alijulikana kama Naima.

Hawa wote walipewa kazi kwa nyakati tofauti na wenyewe hawakujuana kama wana kazi moja kwa maana kila mtu hiyo ilikuwa ni siri kwake. Walipewa saa kumi na mbili za usiku tu kukamilisha kazi hiyo ngumu. Nao waliwasaka wabaya wao kwa hali na mali kuhakikisha wanamfurahisha bosi wao, malipo waliyopewa ni makubwa na yaliwapa jeuri ya kufanya hivyo.

Usiku huo kwao, ulikuwa usiku wa kazi.

 

 

 

SURA YA 3

KAMANDA Amata alikuwa kachanganyikiwa akili kwa namna moja au nyingine, alikuwa akiona kama ndoto inayotokea mbele yake, hakuamini kama wamewahiwa namna hiyo na kwa kasi ya ajabu, alijiuliza kila wakati ni nani mwenye uwezo wa kuwanasa namna hiyo, hakupata jibu zaidi ya hapo aligundua kuwa kwa vyovyote ni watu hatari wanaojua nini wanafanya na kwa wakati pia alielewa watu hao wamepewa kazi kwa muda maalumu hivyo nay eye kama ilimpasa kuwa saidia wenzake alitakiwa ajipe muda maalum na muda wa kazi yake uwe mdogo kuiko muda wa adui zake pia ucheze ndani ya muda wa adui zake. Alitikisa kichwa kana kwamba kuna mdudu akimtembea kwenye ubongo wake, akaitazama saa yake, saa zinayoyoma kwelikweli.

Ilikuwa inakaribia saa nane usiku alipokuwa akifungua geti la nyumbani kwake, akaingia na kulifunga nyuma yake, kisha akasimama kidogo kuangalia nini kinaendelea huku na kule, kwa macho yake makali aliweza kuona ua moja kubwa likitikisika kidogo, akaelewa wazi kuwa mtikiso huo lazima kuna kitu na si wa upepo kwani hali yah ewe ilikuwa imetulia sana na haikuwa na upepo. Damu ikamtembe haraka mwilini, hakufanya lolote, akauendea mlango wa nyumba kubwa na alipoufikia alikuta karatasi iliyoning’inizwa mlangoni, kisu chembamba chenye makali kuwili kilitumika kuishikia hiyo karatasi pale mlango.

Mwisho wa zama zenu umekwisha, mtaongea na Ngurumo.

Ulikuwa ujumbe uliosomeka katika karatasi hiyo pale juu. Akakikamata kile kisu na kukichomoa kwa nguvu, akakibusu, akaiokota ile karatasi na kuishika mkononi kisha akaingia ndani na kuuacha mlango wa nyumba yake bila kuufunga makusudi tu. Moja kwa moja akakiendea chumba chake na kufungua kabati kubwa lililokuwa mbele yake. Akavuta fulana yake nyeusi kaba shingo ya mikono mirefu akaivaa ikitanguliwa na vesti nyeusi pia. Kizibao cheusi chenye mifuko mingi ya kuwekea zana mbalimbali kikafuata juu yake, na zana zake zikapachikwa, bastola nne zilizosheheni risasi zikakaa mahala pake, visu vidogodogo vikawekwa mahala pake, paketi za risasi zikawekwa mahala pake, Shotgun mbili zikabanwa mahala pake nazo zikiwa zimetimia. Akakusanya vikolokolo vya kutosha kwa pambano hilo ambalo hakujua ni nani haswa anakwenda kupambana naye.

Akiwa kasimama kwenye kioo, anajiweka sawa, akahisi vinyweleo vyake vikisimama, mwili ukamsisimka, akajua kuna jambo, akalisubiri huku akijifanya hajui lolote.

Palepale kwenye kioo alimuona mtu akiingia kwa minyato kumfuata, Kamanda alitamani kucheka kwa sababu hata kama alikuwa akinyata wakati yeye alikuwa akimuona kwenye kioo ni kazi bure. Akamsubiri amkaribie ili ajue nini cha kumfanya. Yule mtu akajiandaa kwa waya aliokuwa kaufunga kutoka mkono hu mpaka ule mwingine.

Anataka kunikaba, Kamanda akawaza. Kisha kwa kasi ya ajabu akageuka na guu lake lenye nguvu likatua kichwani mwa Yule mtu, akajibwaga na kujibamiza kwenye mwamba wa kitanda, yowe la maumivu likamtoka, kabla hajafanya lolote akamnyanyua na kumpa kichapo kikali, alipohakikisha kuwa hali aliyokuwa nayo hawezi fanya lolote akamkalisha chini na kumwegemeza ukutani, akamtikisa na kumtazama  usoni.

“Nani bosi wako?” akamwuliza.

“Si-si-simjui!” akajibu kwa tabu.

“Unaniletea utani siyo?” akamwuliza kwa ukali.

“Kweli simjui, mi natumwa tu na kulipwa ujira mkubwa wa kunitosha, kwa hali ya nchi yetu nakubali kufanya kazi yoyote kwa malipo yoyote,” akajieleza.

“Nafikiri hunijui sawa sawa sasa utanijua!” Kamanda akamwambia kisha akamkamata korodani zake na kuziminya kwa nguvu.

“Aaaaaiiiiggggghhhh…. Niache, niache nitasema,” akalia kwa uchungu.

“Sema, nani bosi wako, nani aliyekutuma kuja hapa?” kamanda akauliza sasa kwa ukali zaidi.

“Kweli kaka sim-ju-jui…” akajibu huku akijigeuza geuza.

Kabla Kamanda hajauliza linguine, akashuhudia povu jeupe likitoka kinywani mwa Yule mtu.

“Shiiit! Limejiua,” akang’aka kwa sauti, akaanza kumpekua.

Katika moja ya mfuko wa suruali yake akatoa simu ya mkononi, zaidi ya hapo hakuona chochote cha maana. Akaitazama ile simu, akaenda kwenye kitabu cha majina akakuta majina matano tu, la kwanza kabisa likamvutia, lilikuwa limeandikwa kwa jina moja tu ‘Naima’, kisha akaliangalia la pili na la tatu. Akaamua kuanza kampeni na jina hilo la kwanza.

Akaperuzi upande wa ujumbe mfupi, akakutana na ujumbe kutoka kwa Naima uliotumwa ndani ya dakika kumi zilizopita lakini ulionekana kutojibiwa.

‘…Akifika nijulishe nije nimalize kazi…’ ujumbe ulisema hivyo.

Lilifikiri litaniweza, sasa naanza na Naima, kawaza na kuamua kuujibu ule ujumbe.

Kamanda Amata akaujibu ule ujumbe, kisha akaburuza mwili wa Yule mtu na kuubwaga katika mlango wan je kisha yeye akalitoa pikipiki lake na kuliegesha nje kabisa, akisubiri kuona kinachoendelea.

Akiwa nje ya nyumba yake, juu yapikipiki lake kubwa akasubiri kimya nje kabisa ya nyumba yake.

Dakika tano hazikupita, mwanga wa taa za gari ukaonekana ukijitokeza katika kona ya barabara na kuelekea mtaa huo ilipo nyumba ya Kamanda Amata. Ilikuwa Ford Ranger nyeusi, haikuwa na namba za usajili, ikasoge polepole na kuegeshwa karibu kabisa na lango la nyumba hiyo, watu watatu wakashuka, mmoaj kati yao alikuwa mwanamke, alionekana ndiye akiongoza wengine, aliwapanga, mmoja alimwamuru abaki langoni, yeye na mwingine aliyeonekana pande la jitu waliingia ndani.

§§§§§

Naima na lile jitu moja kwa moja waliingia getini na kutembea kwa mainyato huku silaha zikiwa mikononi mwao. Wakiwa wanajigawa kiufundi zaidi kuuelekea mlango, walishangazwa na ukimya uliotawala, lakini hawakujali. Lilikuwa ni lile pande la mtu lililotangulia kuuendea mlango, kabla halijafika likajikwaa kwenye kitu kama gogo.

“Aah!” likajivuta na kujibwaga mbele. Lilipogeuka nyuma likaona mwili wa binadamu, “Shiit! Amemuua,” akasema kwa sauti.

“Nani amemuua?” Naima akauliza, kisha akashusha silaha yake na kusogea pale ulipo ule mwili, akaugeuza, na kuchomoa kijikaratasi kilichopachikwa kinywani mwa marehemu.

…Naanza na wewe…

Naima akageuka huku na kule asione mtu, anaanza na mimi! Hata kama Naima alikuwa ni muuaji mzuri kitaaluma lakini alijikuta akishikwa na ubaridi wa ghafla. Wakaingia ndani wakatafuta huku na kule hawakuona mtu zaidi ya redio kubwa iliyokuwa ikipiga muziki laini wa ‘Killing me softly’ akasonya na kutoka nje. Wakabeba mwili wa mwenzao na kutoka nao.Wakaubwaga katika nyuma ya pikap yao na kufungia. Kisha nao wakaingia garini na kuondoka.

§§§§§§

Kamanda Amata akawasha pikipiki lake, bila kuwasha taa, akaingia barabarani na kuwafuata taratibu, wakaikamata barabara ya Kinondoni na kuvuka daraja la Salenda kisha wakaelekea mjini, moja kwa moja mpaka Mbowe Club, wakaegesha gari na kuteremka kisha wakapotelea ndani.

Kamanda Amata akaingia baada yao na kuhakikisha hawapotezi katika himaya ya macho yake, akaketi katika moja ya viti vya kaunta na kuagiza glass moja ya Whisky akachanganya na sprite baridi kisha akawa anakunywa taratibu.

Wale jamaa wakaketi mahala Fulani wakijadiliana jambo lakini wakionekana kuwa na wasiwasi, kila mara Naima alionekana kuisoma ile karatasi na kuiweka tena mfukoni. Mara lile jitu la miraba mine likanyanyuka na kutoka mahala pale likamwacha Naima na mwingine mmoja. Kamanda Amata alipogeuka hakuliona lile jitu limeingilia kona gani, akili yake ikazunguka mara mbili, akateremka katika kile kiti na kujichanganya katikati ya watu waliokuwa wakiburudika na uziki katika ukumbi huo. Dakika kadhaa baadae akaliona lile jitu pale kaunta likinga’aang’aa macho, likabeba vinywaji na kuelekea kule lilikokaa tangu mwanzo, yote hayo Kamanda Amata alikuwa akiyatazama kutoka katika kundi la watu wale. Alipoona kuwa hakuna aliye na yeye alirudi tena kaunta na kuagiza kinywaji, lakini hakuweza kukimaliza baada ya kumwona Naima akinyanyuka kitini na kuelekea nje, Kamanda Amata naye akatoka na kumfuatilia mwanadada huyo.

Naima alisimama kati ya magari na kuweka simu yake sikioni kisha akaendelea kuongea na aliyekuwa upande wa pili.

Naima akiwa anaendelea kuongea na simu alihisi ubaridi ukimgusa maeneo ya shingoni, akashtuka akataka kugeuka.

“Tulia!” sauti nzito ya Kamanda Amata ikapenya sikioni mwake. Naima akatulia kama alivyoamuriwa, “Nilikwambia nitaanza na wewe, na ndiyo sasa naanza,” akaongeza.

“Weweni nani?” Naima akauliza kwa sauti yake nyororo inayoweza kumnyong’onyesha mwanaume yeyote Yule rijali.

“Mimi ni Yule mnayenitafuta, Kamanda Amata, na nataka unambie watu wangu wako wapi?” Kamanda akaongeza swali kisha akatulia. Naima naye alitulia bila kujibu, akitafakari la kufanya. Baada ya sekunde kadhaa, uamuzi aliofuanya haukuwa mzuri hata kidogo. Aligeuka na pigo kali kwa Kamanda Amata, lakini Kamanda aliliepa kiufundi huku bastola yake ikimtoka mikononi. Naima aliruka sarakasi kwa minajiri ya kuiwahi le bastola lakini kabla hajafika alijikuta akipokea teka la nguvu mbavuni na kutupwa upande wa pili, akajiinua haraka na kusimama wima kumkabili Amata. Amata alijiweka sawa mwili wake na kumwendea kama mbogo, Naima alijiweka sawa na kuvamiana na Amata, kama Kamanda alifikiri mwanamke huyo anapigika kirahisi alikosea, mapigo matatu ya haraka yalimwingia Kamanda akajikuta anapoteza netweki, akajaribu kujitutumua lakini akajikuta amedhibitiwa ka mikono imara ya mwanamama huyo.

Naima alijirusha hewani kama jani la mkorosho na kuachia dabo kiki za maana zilizotua sawia kifuani mwake na kumpeleka chini.

Kisha Naima akatua chini kwa miguu miwilia akimtazama Kamanda Amata akigalagala chini.

“Ha ha ha ha niliambiwa kuwa Amata ni mwanamume wa chuma kaa mbali naye! Chuma kiko wapi hapa? Na sasa nakuua kwa mkono wangu kwani nimeahidiwa pesa nyingi sana kama roho yako nikiipeleka kwa bosi wangu,” Naima aliongea kwa kujiamini huku akiiweka sawa mikono yake tayari kumshushia pigo la mwisho kijana huyo. Alipomjia kumvamia alimshuhudia Kamanda Amata akijirusha kutoka chini kwa mtindo wa ajabu na guu lake la kulia likatua chini ya kidevu cha Naima, akanyanyuliwa na kubwagwa upande wa pili meno kadhaa yakimtoka.

“Mpo chini ya ulinzi!” sauti kali ikasikika upande mwingine. Kamanda alipotupa jicho akaona polisi eneo hilo, akaruka sarakasi na kutua upande wa pili wa gari, akajibana sehemu ambayo kutokana na nguo zake hakuweza kuonekana, akitazama linaloendelea.

Amata alishuhudia wale polisi wawili wakichezea kichapo cha maana kutoka kwa Naima, wakishindwa kujitetea hata kwa ngumi moja kwani kipigo kilikuwa cha sekunde kadhaa lakini kikali.

Huyu mwanamke ni balaa! Akajisemea, upo muda wake nitamtia mkononi tu, akajisemeana kusonya.

 

KEREGE – saa 8 usiku.

KIKAO cha dharula kiliitishwa ndani ya kasri la Pancho Panchilio, watu watatu walingia ndani ya jumba hilo kupitia milango tofauti kiasi kwamba hata walinzi tu hawakuweza kuwaona wageni hao. Walijikuta ndani wakiwa waneketi katika mtindo wa duara na Yule kinara wao akiwa mbele pa si na kuonekana. Wote waliketi kimya kabisa wakisubiri mkuu wao aongee.

Akajikohoza kidogo kutengeneza koo lake, kisha akafungua kikao hicho kisicho rasmi.

“Wajumbe mtashangaa nimewaita ghafla usiku huu, lakini lengo ni kuwapa taarifa ya kile kinachoendelea mpaka sasa,” Pancho alianza.

“Ndio tunakusikiliza,” mjumbe mmoja akaitikia.

“Vikundi vyetu vimefanya kazi kubwa sana na vimefanikiwa kuwakamata watu watatu, yaani namba moja, namba tatu na namba nne, na hali zao ni kifo muda wowote,” akaendelea.

“Ndiyo hata mimi nilikwishasema kuwa, hawa wakikamatwa ni kuwaua tu na maiti zao tunateketeza kwa moto ili kupoteza ushahidi,” Mjumbe mwingine akaongeza.

“Lakini sasa kuna kikwazo kimoja,” Pancho akatulia hapo.

“Kikwazo gani tena?” akauliza mjumbe.

“Namba moja wao ndiyo anyelete shida na kati ya watu wetu tuliowapa kazi kumbukeni ni vikosi vitatu mashuhuri, watu wane wameshapoteza maisha kwa mkono wake,” akawapa ujumbe uliowashtua kidogo.

“Unasema!” Mjumbe mmoja akaonekana kuanza kuchanganyikiwa.

“Habari ndiyo hiyo! Hivi sasa vijana wapo mtaani wanamsaka mshenzi huyo, mmoja kati ya hao tumemuua yupo katika machaka ya Gongo la Mboto ambako huko pia tumemkosakosa Amata ijapokuwa vijana wetu walilishambulia vikali gari lake lakini alitoweka.”

“Huyo siyo binadamu ni shetani, kwanza mi siku zote sijawahi kumwona japo nimefanya juu chini nimwone japo kwa sekunde moja, namsoma tu vitabuni,” mjumbe ambaye ni mzee kuliko wote aliongeza na wote wakacheka.

“Sasa tunafanyaje?”

“Vikosi vyetu vipo kazini, bado vinasakana na huyo Amata, hwa tulio nao nafikiri ni kuwamaliza kuwaweka hapa ni hatari kwani wakipata nguvu madhara yake ni makubwa,” Pancho akashusha pumzi, “Ila hapa kuna habari njema,” aliposema hayo wote wakakaa sawa.

“Tumeipata kompyuta mama, ile ambayo anatumia boss wao Yule bibi,” akawaambia.

“Eewaaaa hilo nalo neon asee!”

“Sasa ina neno fungushi ndiyo tatizo (password), maana humu ndimo kuna siri zote za hawa jamaa, nilikuwa nawasubiri kwa pamoja tuamue la kufanya,” akaeleza.

“Ni kutumia nguvu tu kupata hiyo password, wenyewe wanaijua, sasa wape kazi vijana watumie nguvu ili kupata hiyo password tujue kilichomo, hawawezi kutupanda kichwani,” Mjumbe mzee akatoa wazo.

§§§§§

Taarifa za kupatikana kwa mwili wa Scoba zilimfikia Kamanda Amata, nguvu zilimwishia kabisa hakuwa hata na la kufanya. Aliitazama saa yake mkononi ilikuwa saa nane na uchafu wake, muda unayoyoma, hakujali aliliwasha pikipiki lake na kuelekea hospitali ya jeshi Ukonga ambako aiambiwa mwili huo umehfadhiwa kwenye chumba maalum.

Hakuamini alipomkuta Scoba kalala kimya huku madaktari wakijaribu kupigania uhai wake wa mwisho. Kamanda Amata alisimama mlangoni na kisha akarudi nje, akajinaamia kwenye ukuta machozi yakimtoka.

Akachomoa mfukoni simu yake na kuiweka sikioni, akamsubiri mtu wa upande wa pili ajibu.

“Ndiyo konokono vipi?” sauti ile ikauliza.

“Konokono anahitaji miguu ya kutembea!” kamanda akaeleza kwa lugha waliyoelewa wenyewe.

“Mwambie aje kuchukua!” akajibiwa na simu ikakatika.

Kamanda Amata akapiga namba nyingine na kuisikiliza.

“Hello!” sauti ikaita.

“TSA namba moja anaongea!” akajibu lile itikio.

“Unasema nani a-a-naonge-a” kigugumizi kilimshika mtu wa upande wa pili.

“TSA namba moja ninaongea, Mkuu naomba tuonane ofisini kwako usiku huu, haraka sana,” Kamanda akatoa amri.

“Kuna nini Namba moja?” akauliza Mkuu wa Usalama wa Taifa Bwana Hosea.

“We naomba tuonane tutajua hapohapo kuna nini…”

“Ok! Copy and paste,” Hosea akajibu huku akikiacha kitanda na kumbusu mkewe Techla aliyekuwa kazama usingizini, kalala fofofo.

 

USALAMA WA TAIFA – saa 8:40 usiku.

MKUU wa kitengo cha Usalama wa Taifa, Bwana Hosea aliwasili katika jengo hilo na kupokelewa na walinzi, kila mmoja alishangaa kumwona mtu huyo usiku mnene kama huo, kuja kwake halikuwa tatizo, tatizo ni kuja ghafa na bila taarifa. Hakuongea na mtu, alipita moja kwamoja katia sebule kubwa ya kupokelea wageni.

“Mkuu mbona hivyo vipi?” Avanti alimtupia swali walipokutana koridoni.

“Salama tu, upo nani ofisini?” akamuuliza.

“Nipo na Muba,” akajibu.

“Ok, kuna lolote la ajabu mliloliona? Au taarifa mliyoipata?” akamwuliza.

“Ni ajlia iliyotokea Salenda, lakini tumeishaianyia kazi, na mauaji ya Mheshimiwa Mbunge wa Miroroso,” Avant akamweleza.

“Ok, nitawaona baadae kama nitawahitaji,” akamwambia huku akiiendea ofisi yake.

Dakika moja tu baada ya yeye kuingia katika jingo hilo, pikipiki kubwa la Kamanda Amata lilifika getini.

“Jitambulishe!” ilikuwa sauti ya mlinzi.

Kamanda Amata, akataja namba yake ya siri inayomtambulisha kikazi badala ya kitambulisho. Ukimya ukachukua nafasi kisha geti likafunguliwa naye akaingia. Akaegesha pikipiki lake na kuuendea mlango mkubwa, moja kwa moja ofisini kwa Hosea. Akamkuta Mkuu huyo akiwa ametulia kitini na bastola yake kaiweka uchi mezani.

“Karibu Namba moja!” akamkaribisha kwa hofu sana.

“Asante Mkuu! Samahani kwa kukusumbua maana imebidi umwache shemeji,” akamtania.

“Usijali, ndiyo kazi zetu hata yeye anajua, niambie Namba moja, vipi usiku huu, maana hujawahi fika ofini kwangu zaidi ya mwaka mmoja sasa,” akaanza kumhoji.

“Mkuu hali ni mbaya! Ni Kitisho!” kamanda akaanza namna hiyo.

“Unasema?” akauliza.

“Nasema idara ina hali mbaya!” akakazia.

“Kamanda Amata, TSA 1, nini tatizo?” Hosea akauliza.

“Mkuu, Madam S hajulikani alipo, Chiba, Dr. Jasmine wote hawajulikani walipo, Gina yuko mahututi kwa Dr. Khadrai, Scoba naye habari yoyote inaweza kutokea,” Kamanda akaeleza na kuangusha chozi.

“Kamanda Amata…!” Hosea akanyanyuka kitini na kuliendea dirisha kubwa la ofisi yake, alionekana wazi kuchanganyikiwa na taarifa hiyo, akajishika kiuno, akatikisa kichwa, akajipigapiga kichwani mara kadhaa kana kwamba analazimisha kukumbuka kitu, akasonya na kugeuka alipo Kamanda Amata.

“Eti unasemeje? Ina maana wametekwa au wameuawa?” akauliza tena kama hakusikia aliloambiwa.

“Siwezi kujua kama wametekwa au wameuawa! Ila wametoweka, na hapa unaponiona ninatafutwa kwa ubani na uvumba,” Kamanda akaeleza.

Mara hodi katika mlango wa ofisi hiyo ikabishwa.

“Ingia!” Hosea akaitikia, “Vipi, usiku huu sasa!”

“Samahani Mkuu, kuna taarifa hapa ambayo ungeikuta asubuhi lakini maadam upo ni muhimu kuiona tena haraka iwekanavyo,” Mubah akakabidhi karatasi ndogo kwa Hosea kisha yeye akaondoka. Hosea akaitazama kwa makini, akairudiarudia kuisoma kama haielewi.

“Japokuwa si kazi yako lakini tazama hii taarifa,” akampa Kamanda Amata, akaipokea na kuisoma, moyo ukamlipuka, akaanza kuhema kwa nguvu.

…Moja ya gari zenu imepata ajali leo wakato wa mvua kubwa katika daraja la Salenda, ndani ya gari hajapatikana majeruhi wala maiti, tunaomba ushirikiano wenu…

Ilikuwa ni sehemu ya taarifa hiyo, Kamanda Amata akashusha ile karatasi na kuiweka mezani.

“Naomba niwe na haraka!” akamwambia Hosea.

“Bila shaka kamanda!” akamjibu. Amata akachukua simu ya ofisini kwa Hosea na kuzungusha tarakimu kadhaa kisha akaweka sikioni.

Akaongea na mtu aliyemtaka kisha akaishusha simu na kuiweka mahala pake.

“Kamanda, njoo huku!” Hosea akamwambia kisha wakatoka na kuelekea chumba cha mawasiliano.

Wakaingia katika chumba kipana ambacho kilikuwa na kila aina ya mawasiliano ikiwe zile kamera za mabarabarani na sehemu nyeti Dar es salaam.

“Nyie, hii ajali imetokea saa ngapi?” Hosea akauliza.

“Saa moja kama na nusu hivi Mkuu!” Mubah akajibu.

“Sasa, saa moja mpaka sasa nane, na mnajua gari iliyopata ajali ni ya kwetu, eh! Mubah, Avant mlikuwa mnafanya nini humu ndani…?” Hosea aliongea kwa hasira, Mubah na Avant wakabaki kimya huku Mubah akimtazama Avant kwa chini.

“Hebu rudisha nyuma nione hiyo picha kwanza!” Kamanada akaomba. Avant akafanya hivyo na ile picha ikafika mahala pake, Kamanda Amata akashuhudia ile gari ikiacha njia na kupanda tuta la katikati kisha ikajipiga mwambani na kupinduka vibaya kabla ya kutumbukia kwenye mikoko chini ya daraja. Akairudiarudia kama mara tano hivi, kisha akamgeukia Hosea.

“Vipi?”

“Hii ni gari pekee ya Madam S japo siioni vizuri kutokana na mvua lakini bila shaka, tazama hapa, hapa, hii ni BMW umeona ee?” akamwonesha vizuri Hosea.

“Nyie vijana muwe makini nyie! Siku nyingine nitawafaya, sasa unajua kwa kuchelewa kupata hii taarifa meshaliweka pabaya Taifa na ninyi kazi yenu ni kuangalia usalama wa Taifa, nipigieni simu wakati wowote ule nitakuja kazini,” Hosea alilalama.

“Samahani boss, siku niliyopiga simu mkeo Techla alinitukana eti mi ni hawara wako,” Avant alilalamika.

“Avant haya ni mambo ya kazi achana na mke wangu! Sawa?” akafoka na kutoka ofisini. Wakasimama kwenye korido yeye na Kamanda Amata wakijadilia jambo.

“Sasa Mkuu, yaani hapa muda hautoshi, lazima kwanza niione hiyo gari kisha nijue la kufanya, na mimi nahusisha matukio haya na lile la mauaji ya Mbunge,” Kamanda akaeleza.

“Hapo umenichanganya kidogo!” Hosea akamwambia Kamanda.

“Nilikwenda kukagua maiti ya Mheshimiwa, mauaji yake yamefanana kabisa nay a wale waliouawa Uswizz, mlenga shabaha alifanya vile vile, kumbuka huyu Mbunge ni Yule mwenye kelele za kuibua mambo bungeni hasa sakata hili la kutorosha mapesa nje ya nchi,” kamanda akaeleza kwa undani mambo mbalimbai anayoyatilia mashaka.

Hosea, Mkuu wa idara ya Usalama wa Taifa wa nchi akabaki kinywa wazi, akajishika kidevuni hasijue la kufanya.

“Ok Kamanda, sasa ulikuwa unasemaje?” Hosea akarudisha mazungumzo nyuma.

“Mkuu kwanza nilikuwa nakupa hiyo taarifa na unajua taarifa zetu huwa ni salama kwa kuziongea ana kwa ana,” akamweleza.

“Idara, imepata taarifa kama ulivyoileta, sasa wewe endelea na harakati zako, na mi hapa nawaita vijana wangu usiku huu, ili kuanza uchunguzi wa kina nitakutaarifu muda wowote nikipata lolote, nawe unitaarifu muda wowote ukipata lolote, kama kuna mahala utahitaji nguvu nafikiri una kibali cha kuomba jeshi la polisi muda wowote sivyo?” Hosea akunguruma.

“Ndivyo!” Kamanda akajibu.

“All the best!”

 

KITUO CHA POLISI SALENDA – saa 9:11 usiku

GARI ya Madam S haikutazamika mara mbili, kwa ujumla ukiitazama ni kama imegeuzwa nje ndani; ndani nje, vyoo vyote hakuna, injini iko nje na mengine mengi. Kamanda Amata akaitazama kwa kina, akaikagua hapa na pale kwa utaratibu maalum sio kama ule wa polisi wa haraka haraka, yeye aliangalia kimoja kwa kingine. Akakagua magurudumu na kisha akatulia kimya.

Akiwa katika kuangalia ndani ya gari hiyo ndipo alipoona kitu cha pekee kabisa, heleni, heleni ambayo yeye anaifahamu sana, akaiokota akaitia mfukoni mwake. Kisha akamgeukia polisi aliyekuwa naye mahala hapo.

“Twende eneo la tukio!” akamwamuru.

Yule WP aliyekuwa zamu akajiweka tayari kwa safari fupi ya usiku huo, wakapiga hatu mbili.kamanda akamsimamaisha.

“We WP! Tunakoenda huko unafikiri kupo salama? Hata kama hamruhusiwi kubeba silaha, mimi nakwambia kachukue silaha,” akamwambia kwa ukali.

Dakika mbili baadae Yule WP alikuwa na SMJ iliyoshiba vyema, wote wakakaa juu ya pikipiki kubwa aina ya BMW wakaelekea darajani.

Mikoko mingi ilikuwa imekatika huku na kule, kwa ujumla palisambaratika.

“Mlikuja wangapi?” Kamanda akamwuliza.

“Tulikuja watatu,” Yule WP akajibu.

“Hamkukuta mtu hapa, majeruhi wala maiti?” akauliza.

“Hatukukuta,” akajibu.

“Njoo hapa!” Kamanda akamwita, kisha akamwonesha alama za miburuzo.

“Unaona hii, huyu ni mtu kaburuzwa kutoka hapa ilipoangukia gari mpaka kule juu labda, na hizi ni alama za viatu vya huyo aliyemburuza,” akamweleza. “Tazama hiki kioo cha mbele, hii ni risasi, kioo cha ajali hakiwezi kupasuka namna hii, kwa hiyo ajalia hii kabla haijatokea dereva alipigwa risasi,” akaendelea kumjuza.

Baada ya kuridhika na hapo wakarudi kituoni.

“Wote mlilikuwepo ajalini?” akauliza tena.

“Hapana walikuwapo watatu tu,” akajibiwa.

“Naomba wote waliokuwepo wafike hapa haraka!” akaamuru. Sekunde tu. Askari watatu wakasimama mbele ya Kamanda Amata akiwemo Yule WP.

“Vueni viatu!” akawaamuru. Nao wakavua na kuviweka pembeni.

Akavichukua kimoja kimoja na kuvigeuza chini kuangali soli za viatu hivyo, akawarudishia. Kisha akawashukuru na kuondoka kituoni hapo, alipovuka tu daraja la Salenda, mbele ya ubalozi wa Ufaransa akasimamisha pikipiki lake, akaichukua ile heleni na kuipachua katikati kisha akaipachika sikioni kama earphone.

Kwanza akasikia miruzi mikali, kisha utulivu ukafuata na sauti ya Madam S ikasikika kwa mabli kidogo.

…Nataka wote tukutane ofisini, Shamba, Chiba na mimi tumepata ujumbe wa kitisho, hili sio la kupuuzia, (ukimya ukatawala) nimetoka nyumbani, naelekea shamba, ofisi za Ubalozi, Daraja la Salenda…

Kisha ikasikika sauti ya maumivu, na kelele ya kishindo kikubwa kilichojirudia mara kadhaa.

…Angalieni kwa chini, ndani ya gari, fanyeni haraka. Atakuwa amekufa huyu! Sawa tu, mchukueni hivyo hivyo…

Akasikia sauti ya kitu kama kijiwe kikianguka kisha ukimya ukatawala. Kamanda Amata akashusha pumzi ndefu, akaitoa ile earphone na kuiweka tena kama heleni kisha akaiweka mfukoni, pepo wa hasira akampanda, akapiga kiki moja na pikipiki lile likakubali sheria, akaingiza barabarani na kuchukua barabara ya Kinodoni, kisha akakunja ile ya Kawawa akaambaa nayo mpaka Kigogo akatobolea Tabata akasonga mbele.

 

GEREZA LA UKONGA- saa 10:01 alfajiri.

MBELE ya Kamanda Amata kulikuwa askari Magereza mmoja aliyekuwa zamu usiku huo, baada ya kuwasiliana na Mkuu wa gereza na kuwasili pale, wote kwa pamoja wakakaa ndani ya chumba kidogo kwa mazungumzo ya kikazi.

“Ndio bwana!” Yule Mkuu wa gereza akaanzisha mazungumzo.

“Asee Mkuu, nahitaji kuona rekodi ya wageni wanaomtembelea Kanayo O. Kanayo na Mahmoud Zebaki, hilo tu!” Kamanda akatoa ombi lake.

Punde si punde ikaletwa rekodi karibu ya mwezi mzima, kila mtu alitembelewa mara nyingi na mkewe isipokuwa tu kwa Mahmoud Zebaki, huyu zaidi ya mkewe alikuwa akitembelewa na mtu mwingine aliyejiandikisha kwa jina la Ravi Kumar, Amata akatikisa kichwa. Akatazama juu huku na kule.

“Mna kamera za usalama hapa gerezani?” akauliza.

“Ndiyo zipo,” Mkuu wa gereza akajibu.

“Naomba nione rekodi yake ya tarehe 21 May mwaka huu,” wakanyanyuka wote na kupita kwenye ujia mrefu mpaka ofisi nyingine ndogo ambako walimkuta kijana mmoja mwenye cheo cha koplo, akafanya hivyo walivyoomba.

Tarehe ile mwezi ule saa ile, akaonekana mtu mwenye asili ya Kihindi akiingia katika chumba cha kuongelea, kisha Mahmoud Zebaki akaja pale wakafanya mazungumzo mafupi kama dakika tano tu. Kamanda Amata alikuwa akiangalia midomo yao na matendo yao, walipokuwa wakiagana. Mahmoud aliiweka mikono yake juu ya mbao iliyokaa kama meza katikati yao ijapokuwa walitenganisha na nondo, na Yule Mhindi akaweka juu yake na kuiondoa. Kamanda Amata akatazama sana kitu hicho na kukirudisha nyuma mara kadhaa akagundua kuwa kabla ya Ravi kuweka mikono juu ya mikono ya Mahmoud kuna kitu alikuwa akikisoma au kukiangalia kwa makini. Kisha akaondoka na kumwacha Mahmoud akiwa na tabasamu pana.

Walipoangalia tukio la siku nyingine walimuona Ravi akifuatana na mke wa Mahmoud na mazungumzo yao yalikuwa yalionekana wazi hayakuwa ya Kiswahili bali lugha Fulani kama si Kihindi basi ni Kibangla.

“Asante Mkuu!” Kamanda akashukuru.

“Umeridhika? Ni wajibu wetu kulinda Taifa, mimi na wewe,” Yule Mkuu wa gereza akamweleza Kamanda Amata.

“Ni kweli, nikiwa na shida yoyote juu ya haya nitakutaarifu,” akamjibu.

“Bila shaka, muda wowote karibu sana,” wakaagana na Kamanda Amata akaondoka. Kamanda Amata akashika njia na pikipiki lake kuelekea mitaa ya Msasani ambako nyumba ya Mahmoud Zebaki ndiko iliko na familia yake yote iko huko, akiwa njiani akapiga simu kwa kutumia simu ileile ya Gina kwa Inspekta Simbeye, akaomba askari watatu wenye kibali cha upekuzi na gari haraka sana, akapatiwa.

Saa kumi na moja alfajiri alikuwa tayari amewasili Msasani Peninsula na ile gari ilikuwa tayari iko pale.

“Mko kamili?” akawauliza.

“Ndio afande!” wakajibu.

Wakagonga na kuingia ndani ya jumba hilo, walinzi hawakuwa na tatizo baada ya kuona serikali imefika hapo. Wakagonga mlango mkubwa na mfanyakazi wa ndani akatoka.

Walipouliza kuhusu mama mwenye nyumba wakajibiwa hayupo lakini kwa kuwa walikuwa na kibali cha upekuzi na walipita kwa Mjumbe wa shina ambaye alifuatana nao upekuzi ukaanza, nusu saa iliwachukua polisi wale kupekuwa nyumba huku wote waliobaki wakiwa wameanyang’anywa simu zao za mikononi, hakuna kibaya walichokipata isipokuwa kitabu cha kumbukumbu kilichoonesha kuwa Yule mama amekwenda Zanzibar likizo yeye na watoto wake. Ndani ya kijitabu hicho pia baada ya kupekuwa sana wakakuta namba za simu za watu mbalimbali ikiwemo Ravi Kumar, na namba hiyo iliandikwa tarehe 21 May. Kamanda Amata aaliendea likitabu likubwa la TTCL linaloitwa Yellow Page na kutafuta jina hilo mpaka akalipata, na kugundua mtu huyo anakoishi, Mtaa wa India kitalu namba 453RF, wakaagana na Mjumbe wa shina na kuondoka zao mpaka mtaa huo, haikuwa tabu kufika ghorofa ya tatu na kumkuta bwana huyo akiwa hoi kwa usingizi.

“Nyie taka nni kwagu, usiku hii bana!” Ravi alalamika. Kamanda Amata hakuwa na shaka naye kwani picha aliyoiona ni ilele iliyosimama mbele yake.

“Mchukueni huyo, tuondoke naye,” Kamanda akaamuru.

“Jamani mmi nafanya nini nyinyi? Manonea sana raia nyie bana, acheni mimi tawapa pesa jingi sana mfungue maduka!” akalalama.

“Kelele!” Kamanda akamkoromea kisha wakampakia kwenye gari ya polisi mpaka kituo cha kati. Wakamwifadhi chumba maalum.

§§§§§

KEREGE

“SASA mtataja password au hamtaji? Tunajua kama ninyi mnaijua ofisi nzima na sisi tunataka kuwasha hii kompyuta,” John the Killer ‘JoKi’ akiwa na mjeledi mkononi mwake alikuwa akimuhoji Chiba aliyekuwa hoi kwa kipigo huku mikono na miguu yake ikiwa imefungwa kwa minyororo imara. Kila alipoiangalia ile kompyuta Chiba alshikwa na woga wa kutaja password, kwa maana alijua wazi kuwa akitaja tu basi siri za za idara zimemwagika.

Upande wa pili Madam S alikuwa amerudiwa na fahamu lakini bado akajifanya amepoteza fahamu akiskiliza kila kinachoendelea, damu iliyoganda usoni kwa majeraha ya vioo, maumivu makali ya mkono na mguu yalimfanya ajikute anashindwa kustahimili hali ile, aliwaza sana alipogundua kuwa wale jamaa wameikamata ile kompyuta na vijana wake wote alishawaambia ni heri kufa kuliko kutaja hiyo password.

“Anhaaa! Bibi ameamka, verygood!” JoKi akavuta hatua mpaka kwa Madam S, akatikisa kichwa chake, kisha akamkanyaga kwa nguvu kwenye mguu wake ulioonesha kila dalili ya kuwa umevunjika kwa jinsi ulivyovimba.

“Aaaaaiiiiggghhhh! Ms**ge wewe!” Madam akapiga yowe la uchungu na kutoa tusi, JoKi akamtandika teke la usoni, Madam S akajigonga ukutani kwa kisogo na kutulia bado kwenye ile minyororo, kwa kuwa alikuwa hajafungwa miguu yake na alijiinua kwa kutumia nguvu ya mikono kwa kujiegemeza na ile minyororo, alijisungusha hewani na kumtandika teke JoKi, lililomsukuma na ye akajibamiza ukutani na kupasuka kwenye paji la uso.

Mtesi mwingine akampiga na shoti ya umeme Madam S akapiga kelele na kutulia.

JoKi akajipapasa usoni na kukuta damu zikimwagika, akamtazama Madam S kwa hasira sana, “Umefanya jambo baya sana mwanamke! Utajuta leo nakwambia!” JoKi akauzungusha mjeledi wake na kumcharaza vibaya Madam. Chiba alishindwa la kufanya.

“Mwachee!” akapiga kelele kutoka pale chini. Wale jamaa wakaanza kucheka kwa kejeli, “Ipo saa yenu, na haiku mbali, mtajuta kuiona siku ya leo,” akaongea huku akiuma meno.

“Tutajuta saa ngapi ilhali alfajiri hii nyote mnauawa?” mmoja wao akasema.

“Hata kama mkituua, nawaapia mtajuta kuiona siku ya leo!” Chiba aliendelea kusisitiza.

“Kelele wewe, nguruwe jike we!” JoKi akafoka. Na wakati huo huo watu wane wakaingia ndani ya chumba kile wote wakiwa wamevaa maguo meusi na soksi usoni; ni macho tu yaliyokuwa yakionekana.

“Karibuni wazee!” JoKi akakaribisha.

“Madam S, na kikosi chako, serikali ilkutuma kufuatilia nyendo za watu au kulinda usalama wa Taifa dhidi ya hila za Mabeberu?” mmoja wao akauliza.

“Beberu lenyewe ndio wewe!” Madam S akajibu kwa taabu kidogo lakini waliayaelewa maneno yake.

“Unajibu utumbo! Madam ! unakitaka kifo kabla ya wakati wake sio, subiri subiri bado nusu saa ya kukuua kwanza utimize haja yetu moja tu kisha tunakuua ili upumzike na mateso haya,” mwingine akadakia.

“Inaonekana mnanifahamu vema sio? Mimi siogopi kifo, nishakutana na kifo zaidi ya mara mia tano sasa hicho unachosema wewe wala sikiogopi, lakini naomba mniue kabla sijawaua ninyi,” akaongea kijeuri.

Kosi kali likatua shavuni, la pili, la tatu, la nne, kisha sonyo kali likafuata, “Acha ujeuri, usibishane na Mkuu!” Yule mtu wa pili akamaliza alilolifanya.

“Yote yatarudi kama usiponiua sasa!” madam akamwambia Yule bwana.

Jasmine akaletwa ndani akiwa na kamba mikononi na tambala chafu lililoshindiliwa kinywani, akasukumiziwa mle chumbani.

“Wawili wameshakufa,” Yule bwana aliyezungumza mwanzo akamwonesha picha ya mwili wa Scoba. Madam S akaangusha chozi, “Hakika mtalipa roho ya huyo mtu kwa gharama kubwa!” akalalama.

“Never!” Yule bwana akajibu.

Madam S akamtemea mate usoni, “Never say never again!”.

“Huyu mwanamke jeuri mpeni disprini kwanza!” amri ikatolewa, umeme ukawashwa na shoti zikamchapa Madam S takriban sekunde thelethini.

“Stop!” ikatolewa amri ya pili, umeme ukazimwa, “Nilishawaambia, ukifuata nyayo zap aka utapotea, sasa ninyi ni manunda na sasa mtapotea hakika,” sauti yenye lafudhi ya kihindi kwa mbali ikasikika kutoka kwenye soksi jeusi lililomfunika mtu huyo.

“Haya nataka password ya hii kompyuta!” ile sauti ya kihindi ikaendelea. Alipoichukua ile kompyuta kutoka kwa kijana mmoja ndipo Chiba alipoiona kwa uvunguni na kugundua kuwa kompyuta ile si yenyewe, akamtazama Madam S, akajikohoza mara tatu kwa mtindo wa pekee, Madam akaelewa kuwa ule ni wito akamtazama Chiba, Chiba akayazungusha macho yake kwa namna ya ajabu huku akibana na kuachia kope zake, Madam S akaelewa anachoambiwa kuwa kompyuta ile ni feki.

Akawatajia password ya hiyo kompyuta, wale jamaa wakaanza kuifungua, ilipoanza kufunguka wakafurahi sana na kuondoka zao.

“Tunarudi muda si mrefu kuwaua!” mmoja wao akasema.

Wakaondoka zao.

KITUO CHA POLISI KATI –saa 11 alfajiri.

KIPIGO alichokipata Ravi Kumar kutoka katika mikono ya vijana wataalam wa kazi hiyo alitapika kila alichokijua juu ya sakata hilo, ingawaje alionekana vingi hafahamu lakini alimtaja mshirika wake mkubwa aliyekuwa akimpa maagizo ya kupeleka Gerezani au kuchukua na kuleta kwake, huyu hakuwa mwingine ni Pancho Panchilio.

“Kwa hiyo Pancho ndiye alikuwa anakutuma?” kamanda akauliza.

“Ndiyo kabisa yaani, ni jeje huyo, lakini mimi sijui nini alikuwa anaadika,” akajieleza.

“Pancho anaishi wapi?” akauliza Kamanda.

“Mimi mtaniua, sijui naishi wapi najua ofisi yake tu,” Ravi akajibu huku akilia na damu zikimtoka kinywani na puani.

“Na huyu Mke wa Mahmoud umemjuaje?” kamanda akauliza.

“Huyu manamuke bana, nilikutanishwa na jeje tu,” akaeleza.

“Sasa yuko wapi?” swali linguine.

“Aliniaga anaenda Zanzibar na atarudi jumamosi hii,” akajibu.

“Zanziba sehemu gani?”

“Mimi hapana jua jamani, mambo ya familia hayo!” akaanza kulia.

Kamanda Amata akaanza kupekuwa simu moja baada ya nyingine za wale wafanyakazi, ndipo katika simu ya msichana wa kazi alipokuta ujumbe mfupi wenye maagizo Fulani kuwa mtu yeyote akiuliza aseme mama huyo kaenda Zanzibar lakini alipochunguza haraka kwa makampuni ya simu aliambiwa namba hiyo mara ya mwisho ilikuwa ikisoma eneo la Laskazoni Tanga.

Kamanda Amata akaagiza kwa Inspekta Simbeye kuwa huyo mama akamatwe mara moja, simu ikapigwa Tanga, kituo kikuucha polisi, masako wa panya wa kimya kimya ukaanza.

“Kamanda Amata,” Simbeye akaita, kisha akampa ishara ya mkono kumwita pembeni.

“Vijana wangu wawili wameuawa eneo la Klabu ya Mbowe! Masaa matatu yaliyopita,” akamnong’oneza.

“Pole sana Inspekta, walikuwa kazini, wamekufa kishujaa, na muuaji atapatikana tu!” kamanda Amata akajibu na kutoka kituoni hapo.

 

 

 

SURA YA 4

JOKI alitulia mezani kupokea taarifa zote za vikosi kazi walivyovituma kuwasaka watu hao, vikosi vinavyoongozwa na wapiganaji hodari kuanzia makabiliano ya ana kwa ana na hata yale ya silaha za kila aina. Alishangaa tu kuwa muda unakwenda lakini hapati jibu lolote juu ya kupatikana au kuonekana kwa Kamanda Amata ambaye nguvu zote walikuwa wameelekeza kwake, isitoshe ilikwisha amuriwa kuwa akipatikana wala haina haja kumleta na uhai wake bali ni kumuua kwa vyovyote vile.

Aliitazama saa yake, pambazuko lilikuwa kwenye miimo ya mlango ulio mbele yake. Wamepatwa nini hawa? Mbona muda umetutupa mkono! Alijisemea kwa sauti ndogo iliyotosha kujisikia yeye mwenyewe. Kichwa kilikuwa kikimzunguka kila mara alitamanai kuinua simu awapigie kuliza lakini alikumbuka kuwa makubaliano yao hayakuwa hivyo bai wao wakikamilisha kazi watampigia simu kama walivyofanya kwa wengine wote.

Akiwa katika kuwaza, simu yake iliita, akaiinua na kuiweka sikioni akiwa na shauku ya kujua nini kimetokea katika msakao huo.

“JoKi !” sauti iliita kisha ikakata.

“Sema, mmekamlisha kazi?” akauliza.

“Hapana JoKi, muda tulioupanga kukamilisha kazi umepita, lakini hatujafanikiwa kumpata Yule hayawani, tufanyeje?” Mkuu wa kikosi cha kwanza akajieleza.

JoKi akatulia kimya kwa fungu la sekunde, akashusha pumzi na kuitoa simu sikioni; tayari alikuwa amesahau anaongea na nani, akakumbuka, akajicheka na kurudisha simu sikioni.

“Subiri kidogo, nitakupa jibu,” JoKi akajibu. Akaitua simu chini na kuhisi kuchanganyikiwa, akabofya namba Fulani na kusikiliza. Naima alikuwa upande wa pili.

“Yes JoKi!” akaitikia.

“Niambie mmefikia wapi na harakati?” JoKi akauliza.

“Bad! Very bad! Huyu jamaa kwanza keshaua mtu mmoja, nimepambana naye lakini Polisi wameharibu muvi, kanitoroka,” akaeleza.

JoKi akapiga ngumi mezani baada ya kujua uwa keshapoteza watu wane katika harakati zake.

“Shiit!” akang’aka, “Unamwonaje?” akauliza.

“Mtepetevu, simshindwi hata kidogo, nab ado namsaka kwani amenijeruhi,” Naima akajigamba. Baada ya kuongea na Naima akapigia kikosi cha tatu nacho majibu ni yaleyale kuwa mtu huyo hajaonekana. Ni Naima peke yake aliweza kumwona na kupambana naye japo kwa sekunde chache. JoKi akatoa maagizo kuwa vikosi viwili vibaki kazini na kikosi kimoja kirudi kambini kwa ajili ya kutekeleza majukumu mengine. Kati ya vikosi viwili vilivyobaki kumsaka Amata kikosi cha Naima nacho kilikuwamo.

Tayari giza lilianza kuuachia mwanga nafasi ya utawala, kwa pande zote mbili huo haukuwa muda rafiki kufanya makeke yoyote lakini haikuwa na jinsi. Pande zote mbili zilikuwa kazini kwa umakini zaidi.

JoKi aliwapanga watu wake vyema katika jiji la Dar es salaam kuwa popote watakapomuona Kamanda Amata wasifanye lolote bali waitaarifu ofisi nayo itajua nini cha kufanya ili kumaliza kijana huyo shababi.

§§§§§

KATIKATI YA JIJI LA DAR ES SALAAM

saa 1:02 asubuhi.

MITEGO MIWILI ilitegwa mahsusi kwa ajili ya Kamanda Amata, wakati huu wa jua hawakutakiwa kumuua ila walipewa amri moja tu ya kutoa taarifa kwamba kaonekana sehemu Fulani kisha kazi ya kummaliza ifanyike bila tabu.

Kikosi cha kwanza chenye watu wane kilikuwa jirani kabisa na jingo la JM Mall ambapo ndani yake, juu; ghorofa ya sita kuna ofisi ya AGI Investiment inayomilikiwa na Kamanda Amata kama Mkurugenza huku Gina akiwa kama Katibu wake, hapo ndipo hupangia mipango yote migumu na kuigeuza kuwa myepesi, nani afe na nani hasife, nani aokolewe na nani atoswe yote yalijadiliwa hapo kwa usiri mkubwa wakati leseni ya kampuni hiyo ni ya ufaulishaji mizigo bandarini.

Watu waliaanza kulijaza jiji, mishemishe za hapa na pale zilianza kuzikumba kona za jiji la Dar es salaam, jua nalo lilipanda angani taratibu likitokea pande zile za Kigamboni. Naima alikuwa ametulia katika moja ya mbao za magazeti akitazama habari nzito iliyobeba magazeti mengi ya siku hiyo.

…Mbunge wa Miroroso auawa kikatili nyumbani kwake Msasani…

Moja ya gazeti liliandika hivyo kwa wino mzito, watu walijazana kusoma habari hiyo, kila kona ya jiji liliongelewa hilo.

“Washamuua huyo! Nchi hii utaiweza!” mmoja wa madereva Tax aliropoka

“Ndiyo hivyo, hii nchi ya wenyewe hii, alikuwa anaongea sana huyu, washamtengeneza!” mwingine alidakia.

“Badala msikitike wapigania haki wanapotezwa nyie mnashabikia kwa maneno ya ajabu,” mara hii mshona viatu alimalizia.

Mazungumzo juu ya hilo yakatawala kila kona ya eneo lile, kufumba na kufumbua gazeti la Mbiu ya Mnyonge likapotea mbaoni, likaisha kabisa kwa kuwa liliandika vizuri habari hiyo.

Naima alisikiliza yote hayo, akakitazama kidole chake cha shahada cha mkono wa kuume akatabasamu na kusogea pembeni ya eneo hilo, aliwatazama vijana wake wawili aliobaki nao katika kikosi chake akawapa ishara kuwa mambo yako sawa.

Kamanda Amata alikuwa akisubiriwa katika maeneo yake muhimu ya kujidai, yeye hakuwa na habari ya lolote katika kuwindwa huko. Asubuhi hiyo alirudi nyumbani kwake japo kujiweka sawa na kuanza awamu mpya ya mapambano ya mchana, muda ulimpiga kikumbo, alipenda kuibuka kidedea kabla ya jogoo kuwika lakini akajikuta akikabiliwa na mambo mengi ya kiupelelzi ili kuwajua adui zake walivyo, lakini hakujuwa bado wamejipanga vipi, kitu kilichompa ujasiri siku hiyo, ni kule kuwa peke yake katika uwanja wa mapambano, kumbe hakuhitaji kutumia akili ya pili kumlinda mwingine; lakini pia alijua wazi kuwa nalo ni hatari ubwa kwani macho ya adui yake yatakuwa na kazi moja tu ya kumtazama yeye kila anaponyanyua wayo wa mguu wake. Aliegesha pikipiki lake mahala pake na kulizima, akatulia kusikiliza lolote kama lipo, ukimya ulitawala, hakuna jipya, akavua kofia lake na kulipachika juu ya kioo cha pikipiki hilo kisha yeye kujitoma ndani huku mkono mmoja ukiwa ndani ya jaketi lake.

Alipohakikisha kila kitu ni salama, akaingia chumbani mwake na kujiweka sawa kivingine. Alipotoka ndani; alikuwa ndani ya suti ya kijivu iliyotanguliwa na shati la buluu bahari, akalielekea jokofu na kuchukua dumu la maziwa, akamimina kwenye kikombe kikubwa, soseji tatu nene pamoja na slesi kadhaa za mkate, vikapashwa kwa microwave na toaster.

Nje ya nyumba ya Amata kulikuwa na pub ya kisasa ambayo iliendesha shughuli zake saa saa ishirini na nne, asubuhi hiyo iliyokuwa na hali ya mawingu, bado watu wachache walionekana kuwapo eneo hilo ama wakiongea hiki na kile au wakipata supu ya kongolo. Hilo halikuwa tatizo kwa Amata, aliitoa gari yake nje na kuiweka sawa tayari kwa safari, akafunga geti lake kwa kutumia rimoti maalum kwa kazi hiyo.

Huku macho yake yakifanya kazi ya ziada ya kuatzama huku na kule akili yake ilipisha uamuzi wa kuhamisha tiba za Gina na Scoba kwenda shamba ili kuepusha lolote ambalo adui yake anaweza kulifanya, kwa maana kama ni watu aliyoawategemea basi ni hao tu. Aliingia kwenye gari yake aina ya Volks Wagen, au wengi mngependa kuiita Golf, akashusha kioo taratibu na kumtazama binti aliyekuwa akipita mbele ya gari yake. “Duniani kuna viumbe mwe!” akajisemea na kisha akaingiza gia namba moja na kuondoka taratibu, alipoumaliza wigo wa ile Pub, akatupa jicho kutazama kijia kile alichoingilia Yule mwanadada, akalisanifu umbo la msichana huyo kwa nyuma, lo; akashindwa afanye nini, akaodoa gari yake na kuikamata barabara ya KInondoni kuelekea daraja la Salenda, alipoikanyaga tu barabara ile na kwenda mwendo wa mita kama 200 hivi, akatazama kioo chake cha ndani na kuona gari nyingine nyeupe ikiingia barabarani kutokea njia ileile. Hakuitilia shaka lakini alitaka kupata uhakika kama gari hiyo ana nasaba nayo au la.

Kabla hajafika kwenye makutano, akakunja kulia na kuingia ofisi za ubalozi wa Uswizz, akaweka gari katika maegesho yake, hakushuka. Akaiona ile gari ikipitiliza, hapo nay eye akatoa gari yake na kurudi barabarani, alipokunja kulia hakuiona ile gari, akajua hisia zake hazikuwa sawasawa, akaingia barabarani na kuifuata barabara ya Bagamoyo mpaka Salenda na kukunja kushoto kuingia barabara ya Ocean kisha akaegesha gari yake kwa mbele kidogo akitazama kama kunayeyote anayefuatilia nyendo hizo. Alipohakikisha hakuna jipya, akakodi Tax na kuelekea Sea View.

“Nishushe hapa!” akamwamuru dereva Tax kisha akamtupia not ya 5000 na kutokomea zake.

§§§§§

DR. KHADRAI ALIKUWA BIZE NA MGONJWA WAKE, kama Mzuka Kamanda Amata akasimama katika mlango wa chumba hicho.

“Karibu Amata,” akamkaribisha kitini.

“Asante nimekaribia, anaendeleaje huyo?” akauliza mara baada ya kuketi kitini.

“Anaendelea vyema, ameamka ila bado fahamu hazijamrudia, lakini si muda mrefu atakuwa sawa, lakini, Amata, huyu atatakiwa kupumzika kama miezi mitatu hivi asifanye shughuli za mikiki mikiki,” akaeleza.

“Ok, umeeleweka kabisa. Sasa Khadrai ipo hivi, hali ya kiusalama sio nzuri sana, na nimekuja hapa kwa jambo moja tu,” Kamanda akainuka kitini, na kuliendea dirisha kubwa la aluminium na kuchungulia nje, akaiona ile gari ikiegeshwa mahala Fulani jirani kabisa na lile jumba la Khadrai, akarudi na kusimama karibu kabisa na daktari huyo, “Sikiliza, wewe na huyu Gina nitawapeleka Safe House, leo hii, kila kitu kipo kule utatumia ofisi ya Dr. Jasmine”.

“Ni wapi huko?” Khadrai akauliza.

“We jua ni Safe House, iko wapi hilo sio swali kwa sasa, haya mwandae mgonjwa wako kwa safari, ukiwa tayari unambie, nitatumia gari yako pia,” akamwambia huku akitokea sebuleni, ukimya wa jumba hilo ulibaki hivyo hivyo, akatzama huku na huko, akachomoa bastola yake ndogo kabisa na kuiweka sawa, akavuta hatua kuuelekea mlango wa kutokea nje, akabana dirishani kutazama.

Mlinzi wa geti aliliendea kufungua baada ya kusikia mbisho, Kamanda akatulia palepale akitazama huku bastola yake ikiwa tayari kutekeleza itakaloamuriwa. Yule mlinzi akafungua geti, mtu mmoja akaingia ndani akifuatiwa na wengine wawili, alikuwa amevalia suti nyeupe kabisa na wale wenzake vivyo hivyo, hakuwa Mtanzania, wala hakuwa Mwafrika, kutoka pale dirishani Kamanda Amata akajihisi kupata ubaridi wa ghafla. “Smart Killer!” akajisemea, kisha akarudi ndani kwa Daktari Khadrai.

“Kaeni humu, msitoke nje wala kuchungulia,” akarudi sebuleni, na kukuta wageni wake wakiujia mlango mkubwa wa nyumba ilhali mlinzi anagalagala chini pale getini.

“Haina haja ya kutukaribisha,” Yule mtu aliongea kwa Kifaransa safi huku wale wenzake wakiwa kimya na mikono yao wameifumbata ndani ya makoti yao, Yule bwana mkubwa alijishika kiuno na kuyaachia mabastola yake waziwazi yakining’inia.

“Karibuni, karibuni viti,” akawakaribisha huku yeye akikiendea kimoja ya viti hivyo.

“Hatuna haja ya kukaa! Tumeshakaa sana kwenye ndege tuliyokuja nayo!” tunataka kitu kimoja tu hapa na tunaondoka na ndege ya saa tano,” Yule bwana akajibu kijeuri huku akichomoa bastola moja na kuifunga kiwambo cha sauti.

“Kitu gani?” Amata akauliza.

“Roho, roho yako inayokutia ujeuri ndiyo tunayoitaka sisi!” Yule bwana akaeleza, huku akiwa tayari kainua bastola yake na kuielekezea katika paji la uso la Amata. Uongo wa Amata ulikuwa ukifanya kazi kwa kasi ya ajabu kuliko kawaida yake akitazama huku na kule kwa kuzungusha macho, akiwatazama wote watatu na kuuona kwa haraka haraka uhatari wa viumbe hao waliovalia sare mpaka mtindo wa viatu vyao ulikuwa wa kipiganaji kabisa. “Kazi ipo, hapa ni kufa nakupona,” Kamanda akawaza.

§§§§§

 

 

 

 

SURA YA 5

KANAYO O. KANAYO ALIKETI KATIKA NUSU UKUTA akiangali mechi ya mpira wa miguu kati ya afungwa mashabiki wa Yanga na Simba. Nywele zilianza kupoteza mng’ao wake, ndevu zilizokosa mnyoaji mzuri anayeijua kazi yake nazo zilikuwa hoi, uzee ulinyemelea mwili huo ambao ulikuwa wa kupendeza kwa mafuta na unyunyu wa gharama. Akiwa ametingwa katika kutazama mechi hiyo ambayo upande wa Yanga ulishinda 3-0 kama kawaida, alihisi kitu kikipenyeshwa kwenye kiganja cha mkono wake.

Ilikuwa kijikaratasi kidogo, akamtazama huyo aliyeifanya kazi hiyo, akamwona na kumbania jicho kisha akaifungua ile karatasi na kuisoma, alipomaliza, akaikunja na kuondoka zake.

Ndani ya chumba chao cha kulala chake cha kulala kilichokuwa na kitanda kimoja kidogo chenye tandiko tu bila godoro, aliketi kwa utulivu na kuingiza mkono uvunguni akachomoa bahasha ndogo na kuifungua ndani.

“…Kazi imeanza mtaani, tumekamata watatu, tumewaweka kwenye hali mbaya wawili, bado mmoja, Kamanda Amata.

Tumeleta Smart Killer kama mlivyoagiza, tukimmaliza yeye ndipo tutafanya plan B, kaa tayari kwa taarifa ya mapinduzi.

Mafisadi; kama wanavyotuita, tutaendelea kuwapo tu na tutaiburuza nchi kwa noti zetu.

Cheers!…”

Akaikunja ile karatasi na kuitia kinywani huku akitabasamu.

§§§§§

MAHMOUD ZEBAKI alitema karatasi iliyokuwa kinywani mwake na kuipachika uvunguni mwa kitanda chake, akatabasamu kwa tabasamu pana. Ijapokua ngozi yake ilikuwa kavu kwa kukosa japo Vaseline lakini bado ilionesha afya kwa mbali, jela ni jela tu. “Hawatuwezi hawa, tutaendelea kutafuna pesa tu, fisadi sio peke yangu kuna Magurubembe huko nje hawayajui, na kesi yetu tutashinda,” akajipa moyo huku akisimama na kutembea hapa na pale.

Kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na pesa za umma waliyoshitakiwa Mahmoud Zebaki, aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uswizz na Kanayo O. Kanayo aliyekuwa Waziri katia Wizara nyeti ya Serikali ilikuwa ikiunguruma katika Mahakama ya Kisutu, kila mara iliposomwa iliahirishwa na watu hao kurudisha lumande. Wananchi wengi walilalamika kwani hawakuelewa kwanini kesi hiyo inapigwa danadana kiasi hicho, wakati Wananchi wakilalama kuwa watu hao ‘wasulibiwe’, walioshika mpini wanasema ‘uchunguzi unaendelea’.

§§§§§§

Kama kuna kitu kilimuuzi Pancho Panchilio alipokuwa ofisini kwake ni kitendo cha kudanganywa juu ya ile kompyuta, alipoifungua akiwa ofisini mwake ilifunguka na kumuonesha picha moja tu ya fuvu lenye ujumbe chini yake ‘Ni zamu yako kufa’. “Kama wao ni wajanja basi mimi ni zaidi, na ile kompyuta lazima niipate leo hii,” akajiwazia huku mwili wake ukitetemeka kwa hasira. Aliinuka na kuliendea dirisha kubwa la kioo na kuitazama mandhari ya jiji la Dar es salaam, akasonya na kuichomoa bastola yake, alipogeuka alifyatua na kuisambaratisha ile kompyuta pale mezani, akairudisha bastola yake na kurudi kitini. “Fanya nililokuagiza, kumbuka sisi ndiyo tunaokulinda hapa nchini na hata nchi yako haijui kama upo hapa kutokana na makosa uliyoyafanya huko,” aliyakumbuka maneno ya Kanayo O. kanayo siku alipokwenda kumtembelea gerezani. “Lazima ufe leo Kamanda,” akajisemea na kujibwaga kitini. Aliinamisha kichwa chake mezani huku mikono yake ikizitimua nywele zake za Kihindi kama anayetafuta kitu Fulani humo, kisha akakiinua ghafla na kutazama mlangoni. Akapiga ngumi mezani, akanyanyuka na kuibeba briefcase yake, akatoka mpaka kwenye ofisi ndogo ya katibu wake.

“Boss, mbona mapema?” Yule binti akauliza.

“Usijali, natoka, kuna kazi naenda kuifanya, nitarudi hapa kesho, aaah no hapana, naweza kuchukua hata siku mbili nje ya ofisi, nitakupigia baadaye,” alikuwa akiongea huku akibabaika hapa na pale. Akatoka ofisini na kuiendea gari yake kabla hajapotelea mjini.

 

KITUO CHA POLISI CHA KATI- muda huohuo

INSPEKTA SIMBEYE hakujua nini la kufanya asubuhi hiyo, wingu jeusi lilikuwa limekigubika kichwa chake, alijua la kufanya lakini alishindwa kulifanya. Hapo ndipo moyo wake uliporudisha uamuzi wa kustahafu kazi hiyo, uamuzi ambao ulikataliwa pindi ulipowafikia wakubwa, ulikataliwa kwa sababu ya utendaji kazi wa kiumbe huyo alijulikana kwa cheo kama jina, Inspekta. Aliipenda kazi yake sana, hata baadaye akafanya kazi nyingi kwa kushirikiana na Idara nyeti za Usalama wa Taifa, alikuwa mpole, mnyeyekevu, msiri, mwenye huruma, lakini makini katika kazi na hakufanya makosa. Hakupenda kukumbatia ujinga wala upumbavu. Alikuwa mkufunzi wa mafunzo ya polisi wapya pale CCP na ndipo alipokuatana na Kijana Amata alipoingia mafunzoni.

Mara kwa mara alikuwa akimtazama kijana huyo mchangamfu kwa jicho la pekee, “Anafaa,” alijisemea huku akitikisa kichwa alipokuwa akishuhudia shabaha ya aina yake iliyokuwa ikilengwa mazoezini, wepesi wa kufanya michezo ya karate na kungfu, alivutiwa. Alimjua vema, vema sana na alimwamini kuliko unavyofikiria.

Alijiinua kichwa chake na kuitazama picha kubwa ya Mwl. Nyerere iliyokuwa imening’inia ukutani, “Tutakumbatia waovu mpaka lini ilhali wanajulikana walipo?” alijikuta akiiuliza ile picha bila kujua kuwa haiwezi kumjibu, akatikisa kichwa. “Usifanye lolote juu ya mtu huyo! Mwache kama alivyo mpaka oda ya juu itakapotoka,” aliikumbuka sauti hiyo iliyomfikia kupitia simu yake ya ofisini pale alipoomba kumkamata bwanyenye huyo aliyezaliwa India na kutarajia kufia Tanganyika.

Akasonya, akaisogeza kofia yake pembeni na kuinyanyua simu yake, akabofya zile namba unazozifahamu, akaiweka sikioni, tayari moyo wake ulipitisha maamuzi, kifua chake kilikuwa kikipanda na kushuka, “Nitajua la kumfanya!” alijiambia.

§§§§§

NYUMBANI KWA DR. KHADRAI

SIMU ya Kamanda Amata ikaita kutoka mfukoni mwake, Yule bwana aliyekuwa amemlenga sawia Kamanda Amata akijiongelesha kwa Kifaransa chake safi, akayumbisha jicho kidogo. Kama kuna kosa ambalo Kamanda Amata alikuwa akilisubiri lifanyike basi hilo lilikuwa haswa, ndilo lenyewe.

Aliipiga ile bastola kwa pigo la nguvu, ikachomoka mikononi mwa Yule bwana, kisha akamsukuma kwa nguvu na kuwapamia wale wawili wa nyuma, wakati huo Kamanda tayari hakuwepo eneo lile, alijirusha na kuviringika na kochi kubwa. Risasi takribani tano zilifumua kochi lile kisha utulivu ukafuata. Wale mabwana wakiwa na bastola zao mikononi mwao walitulia kama masanamu, hawakutikisika, Yule kiongozi wao alikuwa akihema, hakuamini anachokiona. Ni sekunde mbili hadi tatu tukio hilo lilikuwa limekamilika, akawapa ishara vijana wake waende kuangali upande wa pili wa kochi kama mtu huyo yuko hai au la.

Walitawanyika mmoja upande huu na mwingine upande wa kule, wakaenda mbali na kochi lile huku wakitembea bila kufanya ukelele wowote kwa miguu yao kutokana na viatu walivyovivaa.

Kamanda Amata alikuwa ametulia kimya huku lile kochi likiwa limemfunika nusu na miguu yake ikiwa nje ya kochi lile, lakini kiwiliwili kilifunikwa ndani yake, hakujitikisa alitulia tuli kabisa. Wale mabwana walipoona hali ile wakasimama kila mmoja upande wake, mmoja akashusha bastola yake na kuipachika mahala pake, kisha akachomoa kisu kidogo na kukirusha sawia kwenye mguu wa Amata, kikachoma kwenye ‘kigimbi’ kikatulia palepale. Kamanda hakutikisika japo maumivu makali yalimwingia moyoni. Akatulia tuli akiwacheza shere akisubiri wasogee kabisa eneo lile.

“Amekufa huyo!” Yule aliyerusha kisu aliwaambia wenzake kisha kila mmoja aliteremsha bastola yake na kukaribia eneo hilo. Ni nukta hiyo hiyo Kamanda alitumia nguvu zake zote akanyanyuka kwa kasi na aliuzungusha mguu na kumchapa ngwala mmoja wao, naye akajibwaga kama gunia la chumvi ya Uvinza, chali sakafuni, alipotaka kujiinua kiufundi alichelewa, kwani kwa jinsi alivyojizungusha Amata aliipiga tena mikono yake Yule bwana akarudi chini.

Yule kiongozi wao aliruka sarakasi ‘back’ baada ya kuona lile kochi likija kwake, kabla hajajipanga alisuhudia kijana wake aliyebaki akijishika koromeo, tayari kisu kikali kilichomolewa na Amata katika mguu wake na kurushwa kwa ustadi. Yule Kiongozi alipandwa na hasira, akaichomoa tena bastola yake na kuiweka sawa kuua. Kama umeme Amata alijirusha na kuinuka kumuwahi Yule aliyeanguka, alipoona ile bastola inafyatuliwa alijikusanya chini na Yule jamaa kisha akamweka ngao na risasi tatu zilimfumua mgongo wake akabaki hana uhai.

Kitendo hicho kilimchukiza Yule Kiongozi wao, kwani alijiona bwege kwa kuuawa mbele ya macho yake watu wake anaowategemea kwenye kazi kama hizi. Aliilegeza tai yake na kuruka hewani kumwendea Kamanda Amata. Amata akajiweka sawa na kuandaa pigo la maana ambalo kusudio lake lilikuwa ni kupasua korodani lakini Yule bwana alikuwa mjuvi wa mambo, alijigeuza hewani na kutanguliza mikono, pigo alilolitoa hapo, lilimpeleka Kamanda Amata kwenye kabati la vioo na kujibamizapo. Vioo vilitawanyika eneo lote na vingine vilimwachia michuno ya hapa na pale. Hakupotea muda alijichomoa na kujiweka sawa. Yule mjinga alikuwa hafai, alitembeza kichapo kwa Amata na kuhakikisha kamnyongonyesha katika kila kona ya mwili.

“Shenzi sana, umeniulia watu wangu!” aliongea kwa ukali kwa lugha ya Kifaransa.

“Hata wewe utakufa!” Kamanda Amata aliongea kwa shida huku akijivuta kujiinua kutoka pale alipojibwaga.

“Nani wa kuniua? Nimetumwa kukuua wewe tu!” akaendelea kuongea kwa sauti lake baya la kukwaruza.

§§§§§

Dr. Khadrai aliposikia kishindo cha kabati kuvunjika na vyombo vyake kumwagika, alijikunyata kwenye moja ya kona ya chumba hicho, kisha vishindo vya kipigo kizito vilifuatia. Kishindo kile cha kabati ndicho kilichomshtua Gina na fahamu zake zikamrudia upya, akatzama huku na kule kwa mshangao.

Alipomtupia jicho Yule daktari hakuwa anamfahamu.

“Kuna nini? Hapa ni wapi?” akauliza haraka haraka, akajaribu kujinyanyua lakini maumivu yake makali yakamrudisha kitandani.

Dr. Khadrai akasimama huku machozi yakimtoka.

“Amata anauawa!” akajibu.

“What?” Gina akauliza kwa mshangao. Akatazama huku na kule kwenye trey ya daktari huyo akaona vikorokoro kadhaa vimejaa. Akateremka kitandani huku mkono wake mmoja ukiwa umejishika eneo lile alilopigwa risasi.

“Ah aaaaa! Tulia kitandani, wewe hali yako hii haitaki mikiki mikiki, utajiumiza Gina!” Dr. Khadrai alimsihi Gina huku akijaribu kumrudisha kitandani. Gina hakukubali.

“Wacha nife, lakini bosi wangu hawezi kufa ndani ya mita tano toka kwangu,” akajivuta mpaka kwenye kabati kubwa.

“Gina unataka kufanya nini?” Dr. Khadrai akauliza alipomwona Gina akipekua boksi na kutoa bomba la sindano, kisha akasogeza sogeza vitu vingine na kulifumania boksi lililokuwa na dawa za ganzi.

“Gina acha!” Khadrai alimwambia kwa sauti ya chini lakini ya ukali. Gina akamchana lile bomba la sindano, akaipachika sindano bombani na kuchoma kile kizibo cha ile dawa akafyonza yote na bomba likajaa, kisha akamkabidhi Khadrai.

“Nichome haraka sana!” aliamuru.

Dr. Khadrai hakujua la kufanya.

“Nyingi hii tuipunguze!” akasihi.

“We! Nataka yote hiyo, choma, muda unakwenda!” Gina aliamuru, Dr. Khadrai huku akijua kuwa afanyacho si sahihi kwani ile dawa ilikuwa nyingi sana, lakini afanye nini, akamdunga Gina katika eneo la jirani kabisa na lile jeraha lililokuwa limefunikwa kwa bandeji. Gina alitulia kama dakika moja tu na kuhisi eneo la jereha lake ni pazito na hapaeleweki, hakusikia maumivu tena.

Kishindo kikubwa cha mtu kujibamiza ukutani kilimshtua Gina, akachukua forceps na kuufungua mlango kwa nguvu, akajitokeza msambweni, kwa mbali alimuona Kamanda Amata akigalagala chini huku lile jamaa likiwa linajinadi kummaliza. Kishindo cha mlango kufunguliwa kilimgutusha mtu huyo, lakini alipogeuka tu forceps ilizama kwenye shavu lake. Kwa hasira, alimpiga ngumi mbili Gina na kumtupa upande wa pili, alimwendea alimnyayua na kumtupa chini, Gina hakuweza kujitetea, aliruka kiutaalamu na kusimama, pigo la kwanza alilipangua vizuri, la pili na la tatu, lakini la nne lilimchanganya na kupata kipigo cha mbwa mwizi.

Kamanda Amata akanyanyuka kwa hasira na kumwendea mtu huyo.

“Geuka huku mjinga wewe unaonea wanawake sio!” Kamanda akampa maneno ya kejeli. Yule bwana akageuka na kukumbana na makonde mazito ya Amata yasiyo na idadi, Yule bwana alijitahidi kuyapangua mapigo hayo lakini alijikuta anaelemewa. akaanguka sakafuni na mara akajiinua na kwa wepesi w ajabu akajirusha hewani akatawanya miguu yake kwa kufanya shambulio a ghafla lakini Kamanda Amata alikwisha iona hiyo, naye akajirusha juu kisha wote wawili wakakutana hewani. Guu la Amata likatua tumboni kwa Yule jamaa alipoanguka akafikia juu ya meza ya kioo na kuitawanya vipande vipande, Kamanda Amata akasimama kwa miguu yake miwili huku tayari akijipanga kimapigano, akavua koti lake na kulitupa pembeni, Yule bwana naye akafanya vivyo hivyo. Kamanda akafyatua vifungo vya mikono ya shati, na Yule bwana akafanya vivyo hivyo, Amata akajiweka sawa kwa Karate na yyule bwana naye akajiweka tayari, wakabaki wakitazamana.

Mchezo ukaanza, mapigo takribani kumi na tano kutoka kwa Kamanda Amata yalipanguliwa kitaalamu na hakuna hata pigo moja lililomfikia Yule muuaji. “Napambana na mjuvi,” akajisemea. Akajiweka tena sawa na kupeleka mashambulizi ya kasi na haraka, Yule bwana alikuwa mwepesi ajabu, aliyakinga kwa kasi ileile na kumnyima Kamanda hata nafasi ya pigo moja, wakatulia tena kimya.

“Come baby, sasa namaliza kazi yangu!” Yule muuaji alijigamba kwa KIfaransa chake, kisha akajitutumua na kumfuata Kamanda Amata kwa namna ya ajabu, pigo moja lilitua lilitua kifuani mwa Kamanda Amata, akayumba nyuma na kujibamiza ukutani, nukta hiyohiyo Yule bwana alikuwa akileta wayo wa guu lake kukanyaga ama kifua au koromeo, Amata akasubiri kucheza na sekunde ya mwisho, akabonyea chini na kupiga kujizungusha, akamchota ngwala moja maridadi, Yule muuaji badala ya kuanguka akaruka sarakasi na kusimama tena lakini kabla hajatulia alikutana na mapigo matatu ya karate kutoka kwa Gina yaliyotua sawia tumboni, Gina akaruka shufan na kutua nyuma yake, pigo linguine maridadi likatua kweny uti wa mgongo. Yule bwana akasukumwa kwenda mbele na akajikuta akikumbana na Kamanda Amata kwa kichapo cha maana, shughuli nzito.

Alipoona anazidiwa kwa mapigo na mbinu aliamua uamuzi wa ajabu kidogo, “Llive today fight tomorrow!” alijisemea na kujirusha kwenye dirisha la kioo, akatua nje na kuruka sarakasi akauruka ukuta mrefu na kutua nje yake, akapotea.

Amata akatoka kasi ndani ya ile nyumba, akasikia gari ikiwashwa na kupigwa norinda, akatazama huku na kule, akaona Toyota Duet iliyokuwa pembeni, akaingia haraka kisha akampigia kelele Gina aliyekuwa nje hapo afungue geti, akatoka kasi na kukunja kulia kuifuata ile gari.

§§§§§

JoKi alichanganyikiwa kwa maana kila alipopiga simu kwa wageni wake simu yake haikujibiwa kabisa, alikuwa akizunguka huku na kule na simu yake mkononi. Baadae akapiga kwa Naima na kumpa taarifa ya watu hao, akamwomba Naima akae tayari kwa lolote litakaloamuriwa. “Kazi hii iishe mapema kabla serikali haijaamka,” aliyakumbuka maneno ya bosi wake, akajikuta akiuma meno kwa hasira na uchungu.

Akiwa kasimama nje, akitazama walinzi waliokuwa wakiendelea kuweka ulinzi wa ngome hiyo, alijikuta hana uamuzi, “Ina mana huyu mshenzi katuzidi kete? Maana muda wa kuwasiliana umefika lakini kimya,” aliwasiwasika moyoni mwake, moyo wake ukapiga kite kwa ukimya huo.

Kutoka katka mitego yake hakukuwa na taarifa ya Kamanda kuonekana mjini, taarifa alokuwa nayo ilikuwa ni kamanda kuonekana nyumbani kwake na kisha maeneo ya Sea View, akaelekeza nguvu huko kwa kukituma kikosi namba mbili kikiambatana na Smart Killer aliyekodiwa kutoka nchi za mbali akakamilishe kazi hiyo pa si na fujo.

Mara simu yake ikaita, akainyanyua na moja kwa moja alijua ni huyo jamaa yake akaiteguwa na kuitia sikioni huku akiingia ndani.

“Hello!” akaita.

“Hey JoKi, ile kazi imekuwa ngumu, vijana wangu wawili wameuawa na Yule mjinga ndani ya sekunde tatu tu, nimebaki peke yangu,” Yule muuaji akaongea harakaharaka akihema.

“Sasa uko wapi?” JoKi akauliza.

“Nimetoroka na gari nipo barabara ya Ocean, Yule jamaa hafai ni shetani,” akaeleza.

“Jitahidi umpotee urudi kisha tujipange kummaliza kwa shambulio moja hata kama itabidi kukodi B-52 itabidi,” JoKi aliongea kwa hasira na kuiendea simu ya mezani.

§§§§§

CHIBA aliendelea kulala palepale chini, fahamu zake zilikuwa zimerudi sawasawa lakini alijikuta nguvu za kufanya lolote hana, alimtazama Madam S, bado mnyororo uliotumika kumfunga ulimshika sawasawa, alionekana kachoka sana na mwili wake ulikuwa umetona damu hapa na pale. Chumba kilifungwa, lakini kwa nje kulikuwa na ulinzi mkali bila shaka. Alijaribu kujigeuza; bado alikuwa na hali mbaya alishindwa, akaendelea kulala pale chini huku akili yake ikianza kufanya mapambano na kufikiri jinsi ya kujiokoa kwani mpaka muda huo hakujua Kamanda ana hali gani na yuko wapi, kitendawili.

Ndani ya chumba hicho kulikuwa na kamera moja ya usalama iliyokuwa inaonesha matukio yote ya ndani ya chumba hicho na kusafirisha picha hizo moja kwa moja kwenye chumba cha usalama chenye luninga zinazoonesha jumba lote ndani na nje, hata sisimizi akipita wanajua na moja kwa moja mlinzi wa eneo husika hupigiwa simu ya upepo kuulizwa juu ya hilo. Kiujumla kulikuwa na ulinzi wa uhakika si wa kubabaisha.

Chiba aliitazama ile kamera kwa jicho upande, ilikuwa imetazama upande mmoja kwa muda mrefu, upande ambao Madam S alikuwa amefungwa. Mara nyingi kamera hiyo ilikuwa ikizunguka huku na kule kutazama chumba kizima. “Au opereta amelala?” akajiuliza moyoni na kutokuwa na jibu.

Aliitazama minyororo aliyofungwa nayo Madam S, akabaki kusonya kwa maana ilikuwa imefungwa kwa kufuli madhubuti kabisa, linalofungwa kwa tarakimu maalum; ujanja hakuna. Aliuma meno kwa hasira na uchungu, aliona wazi watu hao jinsi walivyowadhalilisha kwa kuwanyanyasa namna hiyo.

Mara akasikia mlango ukifunguliwa na vijana wawili wenye silaha wakaingia huku nyuso zao zikiwa zimefichwa kwa soksi nyeusi, kisha akafuatia mtu mwingine, yeye hakuwa na silaha yoyote lakini mwili wake uliositiriwa na fulana iliyombana ulionekana wazi jinsi gani mtu huyo alivyokuwa mwanamazoezi. Hakuongea, alionesha ishara ya kidole kwa Chiba, wale vijana wawili wakaweka silaha zao migongoni na kumfunika kwa mfuko mweusi kisha kumnyanyua Chiba kumtowa nje ya chumba kile huku wakimwacha Madam S akiwatazama bila kusema neno.

§§§§§

Kilikuwa ni chumba kingine chini ya ardhi, chumba ambacho kilikuwa kikitisha zaidi ya kile cha kuhifadhia maiti, damu zilikuwa zimefanya maua ya ajabu kwenye kuta zake nyeupe na hakuna aliyezisafisha, vitu kama vining’inizio na vitanzi vilikuwepo upande mmoja wa chumba kile. Chiba akatolewa ule mfuko usoni mwake na macho yake yakapambana na hali hiyo ya kuogofya ya chumba hicho.

Hewa nzito ilikijaza chumba hicho kilichokuwa na kila dalili za umauti.

“Karibu sana Kuzimu,” JoKi alimwambia Chiba mara tu walipomfunua lile limfuko, “Unaweza kukitalii chumba hiki ambacho kamwe huwezi kukiona mahala pengine zaidi ya hapa ulipo,” akamwonesha kwa mkono chumba hicho, “Na sasa utaona demo ya kazi ya chumba hichi kama ifuatavyo,” kisha akapiga kidole chake hewani.

Watu wengine wawili wakaingia na mtu aliyefungwa mithili ileile ya Chiba, akafungwa katika moja ya zile kamba karibu na ukuta, nyuma tu ya kichwa chake, ukutani, kulikuwa na damu iliyoganda, Yule mtu akavuliwa lile limfuko kama ilivyokuwa kwa Chiba, Chiba akamwona, akashtuka na kukodoa macho, hakuamini anachokiona.

“Usishangae! Na demo yetu itaanzia hapa!” JoKi akamwambia Chiba aliyekuwa kabaki kimya akitetemeka kwa hasira lakini bado kamba zilimdhibiti na hakujua la kufanya.

§§§§§

SCOBA alifumbua macho, akili ikamrudia na kujikuta kwenye kitanda cha hospitalini, linga ikiwa pembeni na chupa ya maji ikiyatiririsha kwa matone madogo madogo yaliyokuwa yakitembea ndani ya mrija mrefu wa plastiki na kuingia mwilini mwake kupitia sindano iliyochomwa kwa ufundi kabisa katika mshipa wa mkono wake. Macho yake yakanyanyuka na kutamtazama huyo aliyesimama jirani yake ambaye alimwona miguu tu pindi alipokuwa akiangalia ule mrija wa maji ulioingia mwilini mwake.

Mubah alikuwa amesimama akiwa ndani ya suti yake nyeusi ya mikono mifupi au mimi hupenda kuziita ‘suti za mbao’.

“Scoba!” Mubah akaita. Muba akamtazama usoni hakuwa anamjua mtu huyo, “Usihofu, akampoza na kumwonesha kitambulisho chake, “Niko upande wako, nimekuja kukuchukua, vipi una nguvu za kutosha?”

“Yeah! Niko fiti, hawa washenzi hawajaniumiza ila tu walinipiga na kitu gani sijui kichwani wakanipotezea network,” Scoba akajibu. Mara muuguzi mmoja waliyevalia mavazi rasmi ya kiuguzi akiongozana na daktari aliyevalia kijeshi na juu yake kujitupia koti kubwa jeupe, walikifikia kitanda cha Scoba.

“Hauna majeraha, wala hakuna mfupa wako uliovunjika, hatuna budi kukuruhusu ila unatakiwa utumie dawa kali za maumivu,” Yule daktari akamwambia Scoba huku akiwa anaandika andika vitu Fulani, kisha akararua ile karatasi kutoka kwenye faili lake na kumpa Mubah. Muuguzi akaondoa ile sindano mkononi mwa Scoba.

“Simama!” akamwambia.

Scoba akasimama kwa tabu kidogo alipokuwa wima, akashika kichwa, akayumba kidogo kisha akasimama imara, akajinyoosha mwili; uko fiti. Akapiga push up kama kumi na tano hivi kisha akasimama imara, akachukua vidonge viwili kutoka kwa Yule Muuguzi na kuvimeza.

“Baada ya dakika thelethini waweza kufanya lolote, utakuwa poa!” Yule Muuguzi akamwambia huku akiondoka.

“Asante kwa ukarimu wako mrembo,” akamshukuru huku akimwangalia na jicho lake kutua kwenye nyama za nyuma za binti huyo aliyejaliwa shepu, “Mwe!” akajikuna kichwa, kisha wakaondoka.

 

OFISI ZA USALAMA WA TAIFA-

Saa 3:20 asubuhi

KIKAO KIZITO CHA IDARA ya Usalama wa Taifa kilikuwa kikiendelea ndani ya ofisi hizo, kila mtu alipigwa na butwaa kwa taarifa alizokuwa akizipata kutoka kwa Hosea. Ilikuwa ni asubuhi na mapema tu walipoitwa kutoka kwenye kona zao tofauti za kazi zao na kukutana hapo. Mara hii Scoba aliungana nao katika kikao hicho.

“Mpaka sasa ni huyu ambaye anaweza kutujuza juu ya watu hao! Kamanda Amata alikuwa hapa lakini na yeye haelewi watu hawa ni akina nani, anajaribu kupambana kiume kutegua kitendawili hiki, labda Scoba mwenyewe atueleze kilichompata kwa kifupi, kisha tuchukue hatua ya haraka,” Hosea akalieleza jopo.

Scoba akajikohoza kusafisha koo kisha akafungua kinywa kueleza mkasa uliomkuta.

 SAA 16 ZILIZOPITA –

Mtaa wa SHABAN ROBERT

Scoba aliegesha gari yake kandokando ya barabara hiyo mahala ambapo Tax nyingi huegeshwa, akateremka na kuliendea benchi ambalo madereva wa kijiwe hicho hukaa kusubiria wateja huku wakinywa kahawa na kupiga soga kama kawaida yao.

Akiwa ametingwa na mchezo wa draft aliyokuwa akiucheza na mwenzake huku wengine wakishangilia. Mara karibu kabisa ya mguu wake aliona mguu mwingine uliovikwa kiatu cha kike ukisimama na kumkanyaga kidogo, linguine lililomshtua ni ukimya uliofika ghafla.

“Aaa mrembo huyo! Karibu bibie,” sauti ya mmoja wa madereva ilisikika. Scoba akainua uso wake na kukutana na uso wa mwanadada, uso laini husio na chunusi, akashusha jicho mpaka kifuani, lo; kifua kilijaa sawia, matiti madogo yaliyobanwa na sidiria ya kisasa yaliongeza utamu na kusisimua mwanaume yeyote rijali.

“Twende!” Yule mrembo akamwambia Scoba.

“Na mimi?” Scoba akauliza.

“Ndiyo na wewe, nataka gari yako mie, maana we wajua kuendesha vile nitakavyo,” Yule mrembo akamwambia.

Scuba akanyanyuka na kujipukuta vumbi katika makalio yake, “Haya mama twende kama wanitaka mimi,” wakaondoka na kuingia kwenye gari.

“Waitwa nani mrembo?” Scoba akaanza uchokozi.

“Naima,”

“Waoh, una jina zuri sana,”

“Kwa nini?” Naima akauliza.

“We huoni? Hata maana yake tu, mtu mwenye nguvu na uwezo mkubwa wa fikra ndiyo maana ya jina Naima, so sweet!” Scoba aliendelea kuonge huku akiingiza gari barabarani.

“Asante; twende Magomeni kuna watu wangu pale kisha utupeleke Kijiwe Samli tuna shughuli kule, leo nitakukodi siku nzima, shing’ ngapi?” Naima akauliza huku akiuvuta mkoba wake na kufungua zipu, maburungutu ya noti yalikuwa yamelala kimya.

“Kwa wewe mrembo sikuumizi, nipe Laki moja tu,” akamwambia.

“Haina tabu, nitakuongezea na hamsini,”

Wakakamata barabara ya Samora mpaka kwenye mzunguko wa Picha ya Askari, moja kwa moja wakapita Maktaba na kuikamata ile ya Morogoro mpaka Magomeni.

“Ingia Mapipa, mtaa wa tatu!” Naima akamwelekeza, Scoba akafanya hivyo, mbele ya nyumba moja iliyokwisha kwisha hivi akaegesha gari, Naima akateremka na kumwacha Scoba, akaingia kwenye ile nyumba. Baada ya dakika kama tano hivi akatoka yeye na vijana watatu, wakaingia garini, wale vijana wakaketi nyuma na Naima akaketi mbele.

“Kijiwe Samli,” akamwambia Scoba. Scoba aliwatazama kwenye kioo cha ndani wale vijana ambao hata kusalimia hawakusalimia, nywele zikamsisimka, akaihisi hatari mbele yake, akawasha gari na kuondoka zake. Wakiwa barabara ya Nyerere kuelekea maeneo ya Vingunguti mmoja wa wale vijana akawaambia wenzake kuwa kabla ya kwenda kwenye shughuli yao basi wapiti japo wapate mbili mbili, wakafanya hivyo, wakakunja kulia na kuchukua barabara ya Kiembe Mbuzi.

Kizota Pub.

“Egesha gari hapo,” mmoja wao akaamuru na Scoba akafanya hivyo. wakateremka na kuingia kwenye Pub hiyo, wakachagua viti na kuketi.

“Mwambie Angel kama kawaida,” kijana mwingine akamwagiza Mhudumu wa Bar na baada ya hapo vinywaji vikaletwa wakaanza kuburudika.

Iiwachukua dakika kama kumi natano hivi na kilamtu alikuwa kapata mbili, wakanyanyuka kuondoka.

Scuba alipokuwa katika usukani aliana kuahisi macho mazito, alijaribu kuyafungua lakini yalimuwia mazito, akaanza kupoteza umakini barabarani, aliendelea kupambana na hali ile lakini ikawa ngumu, akaegesha gari pembeni.

“Vipi?” Naima akamwuliza.

“Mmenipa nini nyie? Nyie majambazi ee?” akaongea kwa shida sana kwani kinywa chote kilimuwia kizito. Mlango wa nyuma ukafunguliwa, kijana mmoja akashuka na kumtoa Scoba kwenye usukani akaketi yeye, Scoba akawekwa nyuma mtu kati.

“Tueleze Madam S anaishi wapi?” swali hilo lilimrudishia akili Scoba ghafla, akawatazama wale vijana huyu kisha Yule.

“Ninyi mnamjua Madam S?” akawauliza.

“Hatuna muda wa kujibu swali lako, jibu swali letu,” Sauti ya mwingine ikasisitiza.

“Siwezi kuwajibu swali lenu,” Scoba alijibu kwa dharau.

“Unajifanya nunda siyo, kumbuka tuko wane hapa, tutakumaliza,”

“Hata mkiwa kumi au ishirini, siwezi kuwaambia,” akaendelea kuwadindia zaidi. Tayari ile gari ilikuwa ikiuwacha mji na kuelekea Gongo la Mboto. Domo la bastola likatua kwenye ubavu wa Scoba.

“Tulia, ukileta ujeuri wako tu nakumaliza,” akaambiwa. Scoba hakusubiri, alimshindilia kichwa Yule mwenye bastola, akamtindika ngumi huyu wa pili, vurugu ikaamka kwenye gari. Yule jamaa aliinua bastola lakini kabla hajafanya lolote mkono wake ukadakwa na bastola ilipofyatuka ikapita sentimeta chache kutoka kwa Naima ambaye ilibidi alalie upande wa dirisha, na ile risasi ikapasua kioo cha mbele. Dereva akayumba barabarani na kuitoa gari nje akasimama.

Naima aliachia pigo moja kali la ‘pigo la kifo’ lililotua sawia katika uso wa Scoba, akageuka huku akipiga yowe la uchungu, pigo la pili likatua shingoni na kumfanya Scoba kutepeta. Yule mwenye bastola alamshindilia pigo la kisogoni kwa bastola yake Scoba akazimika.

Kila mmoja alikuwa anathema kwa shughuli hiyo ya sekunde chache.

“Amekufa?” mmoja aliuliza.

“Akaongee na babu zake, mtupeni vichakani huko,” Naima akaamuru na Scoba akashushwa na kutupwa katika chaka.

§§§§§

SCOBA alimaliza kusimulia mkasa uliyompata, kila mmoja alisikitika sana na hali hiyo, minong’ono ikachukua nafasi kati yao.

Hosea akajikohoza na kurudisha ukimya kwa namna hiyo, “Ok, sasa nataka tuingie kazini ili kuwapata hao watu laeo kabla jua halijazama,” akatoa amri. Wakiwa bado katika kikao icho mara simu ya mezani katika chumba cha mikutano ikachukua uhai. Hosea akaipokea na kuiweka sikioni.

“Mkuu, katika barabara ya Ocean kuelekea Ikulu – Magogoni kuna gari zinafanya fujo,” ilikuwa sauti ya Avanti aliyekuwa katika chumba cha mawasiliano cha Teknohama. Baada tu ya taarifa hiyo jopo zaima likanyanyuka likimfuata Bwana Hosea na kuelekea kwenye chumba hicho kutazma hicho walichoambiwa.

Katika luninga kubwa kulikuwa kukionesha ramani ya jiji la Dar es salaam na kuonesha maeneo yote muhimu kwa ajili ya usalama wa Taifa. Zilionekana gari mbili zikielekea Upande wa Ikulu kutokea Hospitali ya Ocean Road.

“Zuia haraka, point namba mbili ifanye kazi tafadhali!” Hosea aling’aka na muda huo huo Avant aliinua kitu kama simu na kukiweka sikioni kisha akaboinyeza tufe Fulani na kuongea maneno machache, akatulia.

Bado macho hayo yote yalikodoa bila kufumba yakiangalia tukio hilo, hakuna aliyejua ni nini kinaendelea. Scoba alitulia akitazama kwa makini, akapenya katikati ya watu na kusogea karibu na Avant.

“Naomba nione picha inayowezekana tafadhari,” akamwambia Avant, naye akafanya manuva Fulani kwenye mashine yake wakaweza kuona vipande vya picha za magari hayo, Scoba alitazama kwa makini.

“Unaitambua hiyo gari?” Hosea akamwuliza.

“Yeah, kama sikosei hii Toyota Duet ni ya dada mmoja hivi ana uhusiano na Kamanda Amata, huyu dada ni daktari pale Agha Khan na huwa wakati mwingine tunamtumia kwa hili na lile, anaishi Upanga Sea View,” Scoba alieleza.

“Kamanda Amata,” Hosea akanong’ona, kisha akawaangalia watu wake, “Namtaka huyo anayefukuzana na Amata sasa hivi!!” akatoa amri na kuondoka mle ndani huku akiweka sawa miwani yake. Maafisa wale wakatazamana kisha mmoja akawapa ishara ya kutoka katika chumba kile.

“Ili tufike haraka eneo lile kwa foleni za Dar lazima tutumie njia ya anga, Chopa tafadhali, Scoba twende zetu,” afisa mmoja aliyeonekana kuwa na cheo cha juu kati yao alitoa amri hiyo, Scoba akakabidhiwa nafasi ya kuliongoza dude hilo, pamoja naye watu wengine wawili walikwea ndani yake wakiwa wamekamilika, bunduki ndogo na kubwa zilihusika, mashine ikanyanyuka.

§§§§§

Barabara ya Ocean ilikuwa imekumbwa na taharuki, Kamanda Amata, mwili wake ukiwa unavuja damu hapa na pale alikuwa akiendesha Toyota Duet kwa mwendo wa hatari akiifukuza gari ya mbele yake ambayo ilionekana wazi kuendeshwa na mtu anayeijua kazi yake. Ovateki zilizokuwa zikifanywa na huyo jamaa ni za hatari mpaka kila mtu alikuwa akishika kichwa kuhofia maisha ya hao walio ndani ya vyombo hivyo.

Walipokaribia njia panda ya Gymkhana na Ocean Road; Kamanda Amata akazipita gari mbili na kuingia upande wa kulia, baada ya kuisoma akili ya adui yake kuwa atapinda upande huo, hakuwa mbali na mawazo ya mtu huyo, gari zile zikakutana katikati ya njia panda na kusababisha ajali mbaya iliyohusisha gari kama nne hivi. Gari ya Kamanda Amata kutokana na udogo wake ilijifinya chini ya Land Cruiser Hard Top.

Gari aliyokuwa akiitumia Yule jamaa baada ya kukutana na ile ya Amata, alijaribu kuikwepa akajikuta akiingia katika ukuta wa Hospitali na ukuta ule kuvunjika vibaya. Mguu wake ulikuwa umenasa chini kwenye pedo, alijitahidi kuutoa na kufanikiwa. Akajivuta na kutoka nje kwa kupitia dirishani.

Kamanda Amata naye akajitoa taratibu huku mwili wake ukivuja damu. Kama kawaida ya Watanzania kama kawaida yao wakaanza kujazana, vibaka nao wakitafuta bahati yao, Kamanda Amata alijitupa nje na kudondokea barabarani.

Yule bwana alitazama huku na kule na kuona kundi la watu likija kwenye eneo la tukio, sura yote ilijaa damu, nguo alizovaa hazikutamanika. Mngurumo wa helkopta ndiyo uliomfanya aamue aliloamua, alitazama juu na kuona helkopta hiyo ikisogea eneo hilo, katika mlango wake mtu mmoja aliyevalia suti nyeusi akiwa kakamata bunduki yenye nguvu, “Nimekwisha!” akajiwazia. Kitendo bila kuchelewa alichomoa bastola yake na kupiga tanko ya mafuta ile gari yake.

Mlipuko mkubwa ukatokea na gari kadhaa zilizokuwa eneo hilo zilishika moto, moshi ulitanda eneo lote, kelele za watu zikasikika huku na kule. Kamanda Amata akaenda pembeni kabisa na kuanza kutazama wapi adui yake alipo. Haikumchukua muda kumwona mtu huyo akiwa anatoroka kwa kujichanganya na watu.

“Shabash! Huwezi kunitoroka,” akasema kwa sauti ndogo, akavuta hatua na kuyapita magari matatu yaliyokuwa yamejibana hapo, akatokea upande wa pili na kumwona adui yake akipotelea katika kundi la watu. Kutokana na wingi wa watu ilikuwa ngumu kupenya eneo lile, akafikiri kwa haraka kuwa hapo ni kutumia plan B ili kumpata, lakini kabla hajatekeleza hilo. Gari ya polisi ilifika eneo hilo kwa mbwembwe na walipofika tu waliteremka haraka wakiwa na bunduki zao mikononi, mara moja walimwona Yule mtu aliyekuwa akijichanganya na watu.

Inspekta Simbeye akiwa na bastola yake mkononi, akatoa amri mtu huyo akamatwe mara moja, lakini mtu Yule naye hakuwa tayari kukamatwa namna hiyo, alichomoa bastola yake na kupiga risasi mbili hewani na kufanya hali ya taharuki mahala pale, baada ya kupiga hewani ile risasi, akashusha mkono na kufyatua tena, risasi ile ilimkosa mlengwa ikampata mmoja wa raia aliyekuwa eneo lile na kumjeruhi, hapo ndipo hasira za wananchi zilipopanda, walimvamia Yule bwana bila hata kujali polisi waliopo, walipiga na kupiga mpaka mtu Yule akapoteza uhai.

Ile Chopa ikateremka taratibu na kujiegesha pembezoni mwa ufukwe wa bahari, vijana watatu Smart Guys wakateremka na kuifikia ile maiti iliyopigwa vibaya na wananchi, Scoba aliteremka pia huku akiacha dude lile likiunguruma kwa hasira, Inspekta Simbeye na vijana wake wakawasili.

“Shiit!” akafoka Simbeye, “Siyo Mtanzania huyu!” akamalizia.

Akainua uso na kuangaza huku na kule wakatia huo tayari utepe wa polisi ulikuwa umezunguka eneo hilo na kuzuia Wananchi kufika hapo. Gari za zima moto tayari zilikuwa zikizima moto uliounguza gari takribani tano eneo hilo.

Kamanda Amata akatazama hali iliyokuwa hapo, akafikiria kama ajitokeze au la, lakini hiyo huwa si kawaida yake, alipigwa na bumbuwazi alipomuona Scoba, “Ni yeye au nimechanganyikiwa?” akajiuliza, kisha taratibu akaondoka eneo hilo huku akijiweka sawa uso wake. Akapotea eneo hilo.

 

 

 

 

SURA YA 6

CHIBA alimtambua mara moja Yule mtu pale mbele, ni mtu a;iyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu, kutoweka kwake kulisababisha maandamano makubwa ya waandishi wa habari, alikuwa mwandishi nguli wa habari nchini. Wananchi waliongea, katuni zikachorwa ikasemekana watu wa Usalama wa Taifa wamemteka na siku yoyote angeonekana akiwa hana macho, au meno. Au kucha. “Kwa nini? Kwa nini walimteka na kumleta huku?” akajiuliza bila majibu.

“Unamjua huyu?” JoKi akamuuliza.

“Ndiyo namjua, na kwa nini mmemfanya hivi?” akamuuliza.

“Aaaaa ha ha ha ha, hii ni serikali kaka, ina Rais, Mawaziri, Wabunge, Wanausalam kama sisi na kadhalika, na ina maadui kama wewe. Nusu saa ijayo nawe nitakufanya hivi,” alipomaliza kusema hayo, risasi moja ilikipasua kichwa cha Yule mwandishi na kutawanya damu iliyonganyika na ubongo. Chiba alitetemeka kwa hasira.

“Jiandae, nitawapanga wote hapa na kuwa fumua mmoja mmoja huku nikitengeneza filamu ya kumbukumbu kama za wadi ya kusherehekea miaka mingapi sijui ya uhuru wa nchi yako,” akaongea kwa kebehi.

“Hicho ni kitisho!” Chiba akaunguruma kwa hasira.

“Kitisho! Kitisho ee,” JoKi alipomaliza hiyo sentensi, aliinua mkono kwa minajiri ya kumchapa kofi Chiba. Chiba aliigundua hiyo dhamira yake akasubiri kitendo hicho, kiganja cha mkono wa JoKi kilipolifikia shavu Chiba aligeuka ghafla na kukidaka kidole kimoja kwa kinya chake, akakibana barabara kwa meno yake imara.

“Aaaaaaiiiigggghhh!” JoKi alipiga kelele za maumivu, alijitahidi kuuchomoa mkono wake kinywani mwa Chiba lakini ilikuwa kazi bure, alitumia mkono mwingine kumpiga ngumi za tumboni na kwingine lakini Chiba hakukiacha. Wenzake walijaribu kumnasua lakini wapi.

“Mwache au la nakupiga risasi,” mmoja wao alimwambia Chiba. Lakini Chiba hakujali alizidi kung’ata na kung’ata, mishipa ya hasira ikiwa imedinda usoni na shingoni. Yule mlinzi alitumia kitako cha bunduki kumpiga Chiba mbavuni lakini Chiba hakuachia. Wakati JoKi akijitutumua kujinasua alimpiga kichwa kizito Chiba, Chiba akayumba na kuanguka chini kama mzigo kutokana na kamba alizofungwa.

JoKi akamtazama Chiba kinywani akona damu zikitiririka, mara chiba akatema kidole kutoka kinywani mwake, JoKi akajitazama mkono wake, hakuna kidole kimoja, hasira ikawaka huku akipiga kelele kama mtoto.

“Na bado ukiniua mimi wapo watakaokata miguu yako kwa meno!” Chiba akazungumza kwa gadhabu.

“Jeuri sana wewe, si ndiyo?” mlinzi mwingine akauliza huku akimpa bunduki mwenzake ili amwadhibu.

“Mtieni adabu Mwanaharamu huyo nakuja sasa hivi,” JoKi aliagiza kisha yeye akatoka huku damu zikimmwagika. Yule mlinzi alivuta teke kali kumpiga Chiba pale chini, Chiba akajizungusha na kumchota ngwala ya maana, Yule mlinzi alipiga mweleka na kudondoka chini akitanguliza kisogo, akatoa yowe la uchungu, Chiba akainua miguu yake iliyofungwa na kuitua kwa nguvu katika koromeo la mtu huyo.

“We mwache mwenzio! Mi nakuua!” mlinzi wa pili alimpiga Chiba kwa kitako cha bunduki aina ya Rifle na Chiba akatulia kimya, huku akimwacha Yule mlinzi akiwa hana uhai.

§§§§§§

Hali ya Gina ilibadilika baada ya jeraha lake kumwaga damu nyingi, Dkt. Khadrai alijitahidi kuona namna ya kumsaidia, hakuna na damu ya akiba nyumbani kwake kwani ni ni kinyume cha sheria. Akiwa bado hajui la kufanya, mlango ukafunguliwa, Kamanda Amata akaingia ndani, moja kwa moja akafikia katika chumba hicho cha matibabu na kumkuta Gina akiwa tena kitandani.

“Vipi dokta?” akauliza.

“Hali imebadilika, damu nyingi imetoka katika jeraha lake,” akajibu.

“Oh Come on Gina. Sasa tunafanyaje?”

“Hapa nikupata damu nyingine kumwongezea, haraka,” Khadrai akajibu huku bado akiwa hai hai kumsaidia Gina.

“Ita gari yenu ya wagonjwa!”

“Oh, nilisahau kabisa, asante Amata kunikumbusha,” akachukua simu yake ya upepo ambayo madaktari wote wanazo kwa ajaili ya mawasiliano ya karibu kama inahitajika. Akaita gari na na kuagiza ije na damu kabisa.

Dakika kumi hazikupita gari ya wagonjwa ilifika eneo hilo, Gina, Amata na Dr. Khadrai waliingia na safari ya kuelekea Agha Khan ilianza kwa mbwembwe kama kawaida ya madereva wa gari hizo.

Gina alilazwa katika hospitali hiyo chumba maalum ambacho hakuruhusiwa mtu yeyote kuingia zaidi ya Dr. Khadrai na Kamanda Amata tu.

§§§§§§

Kamanda Amata aliiacha hospitali ya Agha Khan na kuingia mtaani, akatembea mpaka barabara ya Ally Hassan Mwinyi, alipoona hali ya hewa ni ya utulivu, akachukua simu yake na kupiga namba ya Mkuu wa Usalama wa Taifa, Bwana Hosea na kumwuliza juu ya Scoba, akajibiwa kuwa Scoba yupo salama na anaendelea vyema.

“Ok, ninamwitaji sasa tuingie kazini kwa nguvu zote,” akamwambia Hosea.

“Haina tabu kwani huyu ni wa kwenu, mkutano wapi?” Hosea akauliza.

“Kanisa kuu la Mtakatifu Joseph dakika kumi baadae,” kisha simu ikakatika. Amata aliingia kwenye tax iliyoegeshwa jirani kabisa, na kuitaka impeleke mpaka JM Mall ilipo ofisi yake ya siri au tuiite ofisi binafsi.

Aliwasili katika jengo hilo mida ya kama saa sita hivi, moja kwa moja akaiendea mbao ya magazeti na kutazama nini kilichoandikwa. Habari zilikuwa zile zile za jana yake ila zilikolezwa wino tu. Akapita taratibu na kuuendea mlango mkubwa wa jengo hilo. Akasimama kidogo karibu na mashine za kutolea pesa, akatzama huku na kule, kila mtu alikuwa akiendelea na hamsini zake, akasogea pembeni na kubonya kidubwasha cha lifti, ilipofika akaingia na kuiamuru imfikishe ghorofa ya nne.

Alipofika ghorofa ya nne aliteremka na kwa kutumia ngazi alipanda kwenda ghorofa ya sita ambako ofisi yake ndipo ilipo. Akaufikia mlango na kusita kidogo, jicho lake likatua chini ya mlango, kulikuwa na ncha ya bahasha ikichungulia nje, akaivuta kwa vidole vyake na kuitazama. Ilikuwa bahasha nyeupe, ndani ilikuwa na kitu kama kadi ya kibiashara, akaitazama kwa makini sana, akataka kuichana, akasita, akafungua mlango wake na kuucha wazi, akatulia kidogo, kisha akaingia ndani na kutembea taratibu. Kila kitu kilikuwa kama alivyokiacha mara ya mwisho, hakuna kilichoguswa wala kusogezwa. Moja kwa moja akaiendea jokofu ndogo iliyokuwa hapo akafungua, akatazama chupa zake za kinywaji, akacheka kidogo kisha akafunga, ijapokuwa alikuwa na kiu lakini hakuchukua chochote baada ya kuona mpangilio wa zile chupa umegeuzwa kwani yeye na Gina walikuwa na mpangilio wao maalum. “Kama mmeweka sumu mtakunywa wenyewe,” akawaza kisha akavuta droo yake na kupekua hapa na pale, akachukua saa yake ya mkononi na kuivaa, akachukua miwani yake yenye uwezo wa kurekodi picha mjongeo, kuona nyuma bila kugeuka, bastola yake ndogo kuliko zote inayotosha kwenye kiganja cha mkono akaipachika mahala pake.

Akalivua koti lake na kulitupia huko, akavua shati na kuvaa fulana nyeupe inayobana mwili kisha akarudishia kila kinachohitajika, akafungua kijikabati kidogo na kutoa kikoti cha Kodroy akakivaa juu yake, pesa kama shilingi za Kitanzania laki tano akazitia kibindoni. Akaiinua bastola yake na kuisukuma slide mbele nyuma, “Iko fiti,” akawaza na kuikubali, kisha akafyatua magazine na kuiweka mezani, akapanga risasi zake nane na kuirudishia mahala pake, akaislide tena na risasi moja ikatumbukia chemba, akailoki na kuitia mkandani.

Akatulia kwa sekunde kadhaa kisha akaamua kutoka kwa nguvu zote kwenda kumsaka mbaya wake ambaye mpaka nukta hiyo hakujua yuko wapi. Alitoka na kuufunga mlango nyuma yake, akaingia kwenye lifti kwa minajiri ya kuteremka chini, kabla mlango haujajifunga, kijana mwingine akawahi kuingia na kusimama jirani na Amata lakini kwa nyuma. Kamanda Amata aliichomo miwani yake na kuivaa kisha kumtasama kupita vioo vidogo vilivyo kwenye miimo ya miwani hiyo.

Yule kijana alikuwa ametulia tuli hasemi lolote lakini kwa jinsi macho yake yalivyokuwa yakipepesa, Amata akajua kuwa huyo si mtu mwema, akajiweka tayari kwa lolote kwani mwili wake kw muda huo ulikuwa ukichemka damu ukizingatia bado ndugu zake hakujua wako wapi, kitendawili.

Aiendelea kumtizama huku akiangalia tarakimu zinazobadilika kutoka kumi na tano na kuteremka chini kwenda G, akamwona mtu huyo akiingiza mikono ndani ya kijaketi chake, akajua nini kinataka kutokea, akajiweka sawa.

Lakini alikuwa anatamani kucheka kila akimtazama kijana huyo aliyeonekana kujawa na wasiwasi. Ilionekana katika kazi hizo huyu atakuwa ni mwanafunzi tu kwa jinsi asivyojiamini, Amata akanyoosha mkono na kubofya tarakimu zile kwa kuingiza namba kama sita hivi na lifti ikasimama ghafla. Yule kijana alitoa waya kwenye koti lake na kutaka kumkaba Amata.

Kamanda Amata hakupoteza muda, alimjifanya anaudaka ule waya kumbe ilikuwa ni danganya toto, alipiga kiwiko cha mbavu dogo akalegea, alimnyanyua kwa kumshika mikono yake na kupigiza upande wa pili, akambwaga chini hoi. Kisha akapiga goti moja na kuondo amiwani yake  usoni.

“We ni nani?” akamuuliza.

“Mi-mi-mi ni-metu-mwa,” akajibu huku akijikinga mikono yake usoni.

“Najua umetumwa, wewe ni nani?”

“Jose,” akajibu.

“Nani aliyekutuma?” akamchapa swali linguine.

“Mdada mmoja, yuko hapo nje,”

“Kavaaje na anaitwa nani?” Yule kijana hakujibu hilo swali, akabaki akimwemwesa mwemwesa midomo, Amata akamwinua kichwa na kumpigiza chini kwa nguvu.

“Nasemaaaa!” akalia kwa uchungu.

“Haya sema!” akamlazimisha kusema, mara hii bastola ikiwa mkononi.

“Simjui jina, alinipa hiki, akaniahidi pesa,” akatoa kadi ya kibiashara na kumpatia.

Kamanda Amata akaitazama na kusoma jina na namba za simu zilizopo, lakini alishangaa kuona jina la mwenye kadi ni la kiume. “Haijalishi, ndiyo njia zao hizi,” akawaza, akamtazama Yule kijana, yuko hoi pale chini, akamwacha na kufyatua zile namba kisha akaiamuru ile lifti iende juu kabisa. Huko akatoka na kuiacha akatumia ngazi kuteremka mpaka ghorofa ya sita ilipo ofisi yake, akaichukua ile kadi, na kuandika zile tarakimu katika mashine maalumu ambayo ina uwezo wa kukupigia simu ukajua unaongea na binadamu kumbe kompyuta, unachokifanya ni kulisha maneno kisha kuyaoanisha na yale ya upande wa pili, kwamba huyu akisema hivi yenyewe iseme vile, kisha akaunganisha ile mashine na simu yake ndogo aliyoipachika kwa mkono huku kisikilizio chake kikiwa masikioni, akatoka na kuondoka zake.

§§§§§

NAIMA akiwa ndani ya gari yake pamoja na wenzake wawili, aliipachika darubini yake machoni na kutazama kwa makini kwenye lango kuu la JM Mall, alichokiona sicho alichokitegemea, alimwona Kamanda Amata akitokea pale mlangoni na kuivaa miwani yake, kisha akatembea kuielekea gari moja aina ya Toyota Carina Ti, Kafungua buti na kujifanya anatazama vitu Fulani Fulani.

Naima na kijana wake mmoja wakatoka na kuwahi pale kwenye ile gari, Yule jamaa akamwona bado Amata ameinama akifanya shughuli zake kwenye ile gari iliyokuwa katika maegesho pweke upande wa pili wa lile jingo.

Kamanda Amata akahisi tayari kuna hatari, akatazama kwenye kioo chake cha siri kwenye ile miwani na kuona watu wawili wakimsogelea kwa mwendo wa Mamba awindapo, akataka kufanya makeke lakini akilini akawaza kutumia Art of War, jifanye mnyonge unapokuwa una nguvu, akaendele na shughuli yake.

“Usilete makeke yako ya kitoto, bunduko mbili zenye nguvu ziko nyuma yako na nkyingine kubwa ipo ghorofa ya pili, tulia hivyohivyo,” sauti ya Naima ikaunguruma.

Kamanda Amata alishalitegemea hilo na alijua kuwa ahadi yake na Scoba ilikuwa imetimia kwani wanapoahidiana kukutana Kanisa kuu la St Joseph, basi ujue hapo JM Mall ndiyo Kanisa Kuu.

“Simama!” akamwamuru.

Kamanda akafanya hivyo, kisha lile jitu la miraba minne likaja na kumpekuwa likachukua bastola tu bila kuona silaha nyingine zilizotapakaa mwilini mwa Amata. Naima akiwa mkononi na Shot Gun akamwongoza Kamanda Amata ndani ya gari hiyohiyo, Yule jitu akaketi kwenye usukani, Amata akawekwa nyuma huku Naima akiwa kampachika domo la Shot Gun katika ubavu wake.

Kamanda Amata alipotoka pale nyuma ya gari aliacha buti bila kufunga ila alilipachika kwa namna anayoijua yeye. Scoba alikuwa akiona mambo yote hayo, alipoingia tu garini na kuiwasha, alinyata taratibu na kufungua buti kisha akaingia ndani yake na kujiweka humo, akarudisha lile funiko na kuliegesha kwa namna ya ajabu, ile gari ikaondoshwa mahala pale na kuelekea kusikojulikana.

§§§§§

Simu ya kukamatwa kwa Kamanda Amata ilipokelewa kwa furaha sana na JoKi, naye muda huo huo akaingia katika chumba cha mawasiliano na Boss wake asiyeonekana sura na kumpa habari hiyo njema.

Pancho Panchilio alitamani aruke angani lakini hakuweza, aliinua simu yakena kuwapa ujumbe huo wenzi wake na kuwa wakutane huko kwenye kasri lao ili wamalize kazi waliyoidhamiria.

Ilimchukua dakika kadhaa tu Pancho Panchilio kuingia katika kasri lake huko Kerege kwa njia ya siri ambayo ni yeye tu aiyekuwa akiijua na kuitumia, na kila Mjumbe wake naye alikuwa na njia tofauti ya kuingilia, wao walikutana tu ndani ya jengo hilo.

Haikupita muda Mjumbe mmoja mmoja aliingia katika kasri hilo na kukutana kwenye chumba chao ambacho kwacho siku zote hufanyia mazungumzo na mipango yao.

 

 

 

SURA YA 7

ZANZIBAR

NURU MUSABAHA alitulia tuli kwenye kochi kubwa huku jicho lake likiwa kwenye luninga kupata habari mbalimbali kutoka Bara, mara kwa mara moyo wake ulikuwa ukilipuka na kujawa hofu lakini baadae alitulia tena, hata aliposikia unyayo wa paka yeye alihisi kama sijui kitu gani, alijua kila kinachoendelea huko Bara na kusudi kitekelezeke, alitakiwa kutoroka namna hiyo na kusubiri hali itulie na mumewe Mahmoud Zebaki awe na matumaini ya kurudi uraiani.

Asubuhi hiyo majira kama ya saa nne hivi, kila alipojaribu kuwasiliana na Ravi, simu hakupatikana, nah ii ndiyo ilimfanya achanganyikiwe zaidi, “Kwa nini hapatikani?” alijiuliza pa si na majibu. Kabla ya kuja Zanzibar alimshauri Ravi waondoke pamoja baada ya kuusuka mpango huo na mtu wasiyemjua, lakini Ravi yeye alikataa katakata kuondoka, akiamini kuwa maadam watu hao watakamatwa kwa siri yeye watamjuaje ilhali ni raia wa kawaida tu.

Alikuwa akisoma gazeti juu ya habari ya marehemu Mbunge lakini alihisi haelewi akalitupa huko, akazima TV na kujinyanyua kitini akasimama wima. Akavuta hatua fupi kukielekea chumba cha kulala lakini akiwa humo bado akili yake haikumkaa sawa, akaamua kubadilisha nguo alizokuwa amevaa, akavalia suruali ya jeans nyeusi, fulana moja yenye picha ya Madonna na kubebwa na neno Holyday , akajiangalia kwenye kioo na kujiona yuko fiti ukizingatia na shepu aliyonayo ya mchanganyiko wa Kimanyema na Kipemba basi utamu mtupu.

Alipojiweka vizuri akachukua pesa kidogo na kujaza mfukoni, “Nikalale hotelini,” akawaza kisha akavuta juba lake na kujifunika mwilini akaacha macho tu kisha akanyanyua kijimkoba chake na kuanza safari ya kuondoka eneo hilo.

Alipoukaribia mlango tu, akasikia hodi ikibishwa, akasita kuuendea mlango, “Nani atanifuata huku?” akajipa moyo na kuuendea mlango, akaufungua.

“Karibu sana, nikusaidie nini?” Nuru akamwuliza huyo aliyegonga mlango.

§§§§§

Alikuwa kijana mtanashati, aliyeva suti yake nyeusi, miwani nyeusi akitazamana na Nuru pale mlangoni, Yule kijana alimwangalia Nuru chini mpaka juu na kulistaajabu umbo la mwanamke huyo, “Tangu lini Mpemba akawa na shepu ya maana kama hii?” akajiuliza.

“Mimi ni polisi Detective,” akajitambulisha na kumwonesha kitambulisho.

“Kwa hiyo mi nifanyeje, nikupandishe cheo au?” Nuru akauliza kijeuri lakini moyoni mwake alikuwa hoi, alihisi kijimkojo kwa mbali lakini akajikaza kikike.

“Hii ni barua ya wito wa kufika kituo cha polisi cha kati mara moja,” Yule kijana akamweleza. Nuru akaisoma pasi na kuishika kwai hakutakiwa kufanya hivyo. macho yake yakaonekana wazi kuwa na machozi.

“Nimefanya nini mimi mpaka michukue?” kauliza.

“Swali gumu mama, mi natekeleza wajibu, ukifika kituoni ndipo watakueleza yote,” akajibu Yule kijana.

“Ok, ngoja nijiandae,” Nuru akaomba.                

“Hapana, hivyo hvyo ulivyo, mbona utarudi sasa hivi tu!” Yule kijana akamwambia na mara hiyo akaja mwenzake mwanamke WP aliyevaa kiraia na kumchukua Nuru mpaka kwenye gari. Safari ikaanza mpaka kituoni. Alipofika pale danadana ilikuwa ile.

“Na sisi pia tumepewa oda hiyo kutoka juu, hivyo madai yako yote utapewa majibu kutoka Dar es salaam,” akajibiwa hivyo na mkuu wa kituo.

Nuru aliishiwa nguvu, mapigo ya moyo yakashuka, akawa wa kupepewa tu, wakamvua viatu, wakamlegeza mkanda, wakambeba kwenye gari ya polisi mpaka hospitali ya Mnazi Mmoja.

Nuru alijua linalomkabiri, akashindwa kuvumilia.

§§§§§

Akiwa ofisini kwake, Inspekta Simbeye aliishuhsa simu yake mezani na kuirudisha kwenye kitako chake. Akatikisa kichwa na kupiga ngumi mezani.

Taarifa iliyomfikia punde tu kupitia simu hiyo ilimwambia kuwa Nuru, Mke wa Mahmoud Zebaki amefariki dunia katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa Shinikizo la Damu.

“Nilikuwa namtaka sana huyu mama,” akajikuta akiongea peke yake.

Hbfliqebvoe v;            bfno3u

huku akijiangalia kidole chake na kushikwa na hasira kali juu ya Chiba, “Atanikoma huyu mshenzi!” aliongea mwenyewe: alipofika katika chumba kile, Kuzimu, alishamgaa kukuta mwili wa mlinzi umelala bila uhai, alipopepesa macho pembeni hakuona mtu mwingine.

“Shiit!” akang’aka kwa hasira na kuugeuza ule mwili, “Shetani huyu, kamuuaje huyu jamaa ilhali alikuwa na silaha mkononi?” akajiuliza kisha akaondoka kuelekea chumba kile alichomfungia kwanza. Akiwa njiani akakutana na Yule mlinzi wa pili.

“JoKi, huyu mateka ni hatari, kamuua Ngwabi kwa miguu yake,” Yule mlinzi akaeleza.

“Sasa yuko wapi?” JoKi akauliza.

“Nimemtupa huko kwenye chumba, sijui kafa au mzima maana nimempa kipigo cha maana,” akaendelea kueleza. Kisha wote wawili wakafuatana kwenda kumwangalia Chiba. Kweli hali yake ilikuwa mbaya, alilala mithili yam fu, damu zikimvuja kichwani baada ya kupigwa sana kwa kitako cha bunduki.

“Safi sana! Sasa njoo nikupe maagizo mengine,” wakafuatana mpaka chumba walichomwacha Madam S.

“Unamwona huyu Kibibi, huyu atauawa kwa kukatwa na msumeno wa umeme nusu saa ijayo, yule mrembo ambaye hatujamfanya chochote kibaya, tutafanya naye ngono mbele ya wenzake kabla ya kumuua, yeye lazima afe kwa kuingiliwa, huyo mpumbavu huko uliyemwka vibaya kwa kipigo, tutamchinja na huyo anayekuja anayejifanya ndiye mjuaji yeye atakufa kwa kulowekwa kwenye tindikali, ni hivyo tu. Kwa hiyo waambie wenzako muandae hivyo yote, nusu saa jopo lote litakuwa hapa kwa kazi hiyo,” akamaliza JoKi huku akicheka na ubaya wa sura yake kuonekana wazi mbele ya kila anayemtazama.

Sonyo kali likamtoka Madam S, “Mnajisumbua tu!” akaongea kwa shida sana huku akiwa bado kafungwa na ile minyororo.

“Unasemaje we Kibibi?” JoKi akamuuliza Madam S. kisa akatoka na kuufunga ule mlango nyuma yake huku akiwaacha wale walinzi wawili pale langoni wakiwa wamesimama kwa ukakamavu.

§§§§§

Scoba bado alitulia kimya ndani ya buti la gari, akichungulia mara kwa mara kujua ni wapi wanaelekea, mpaka wakati huo alishaanza kujua maana tayari waliiacha Bunju A na kuelekea mbele, “Kumbe ishu zote Bagamoyo!” alijisemea na kuendelea kutulia ndani ya lile buti kuona mwisho wa safari ni wapi na vipi ataweza kuanzisha msinambe, “Lazima wajue kama sisi ni T.S.A,” akajisemea huku bado akifungua kidogo lile buti ili kuona wapi wapo.

Scuba alifikiria kwanza kuanzisha msinambe huo kabla hawajafika katika ngome yao, lakini baadae akaona wazi kuwa siyo vyema kwani kuna wenzao ambao hawajui walipo, hivyo ni bora kufika katika ngome ya watu hao kisha kwa pamoja waweze kufanya kazi hiyo. Akiwa amezama katika mawazo hayo akahisi ile gari inakata kona, akafungua buti kidogo na kutazama nje, “Tumekata kushoto,” akajisemea, kisha akatulia tena.

Ndani ya gari hiyo hakuna aliyeonge wote walitulia kimya kana kwamba hakukuwa na mtu ndani yake. Ile gari ikasimama mahala Fulani, Scoba akajiweka tayari, akatega sikio kusikia nini kinaongelewa huko nje.

“Mpo wenyewe tu?” akasikia sauti kutoka nje ikiuliza.

“Kama unavyotuona,” Naima akajibu.

“Ok, ingizeni gari mpaka egesho namba sita mtakuta maagizo yenu,” ile sauti ikasema na kisha ile gari ikaingia taratibu na mara ikasimama tena.

“Vipi?” sauti ya Naima ikamfikia Scoba ndani ya buti.

“Hamjafunga buti, na mna bahati polisi hawakuwaona,” ile sauti ya mwanzo ikasema. Scuba akaona mtu kasimama nyuma ya buti, akatoa bastola yake na kuiweka tayari kwa lolote. Yule mtu akashika lile funiko la buti akalifunga kwa kulisukuma. “Aiyaaa!” Scoba alinung’unika kimoyomoyo akajaribu kulitikisa lile funiko lo, limefungwa, akatulia na kusukuti kuona nini cha kufanya na atatoka vipi. Ijapokuwa hilo kwake alikuwa tatizo lakini tatizo lilikuwa ni muda. Ile gari ikatoka pale na kuingia ndani kwa ni alihisi baada ya kusikia mlio wa geti lililokuwa likijitembeza kuruhusu gari hilo liingine ndani, kisha likasimama mahali.

Scoba alijua kutika getini mpaka hapo walipo ni kama mita ishirini na kwa jinsi mlio wa gari ulivyobadilika akajua wameingia ndani ya kitu au jingo. Akatulia kusikia kinachoendelea nje.

“Ha ha ha ha, Umekamatika paka wewe!” sauti ya JoKi ilisikika, “Naomba mumshushe kwa umakini sana, na silaha zenu ziwe tayari akileta ujanja muueni tu, hawezi kutusumbua akili sisi, kwanza mfikisheni Golgotha mkamtie adabu ila hakikisheni mmemfunga vizuri,” JoKi aliasa. Scoba alitulia kimya akisubiri kujua nini kitajiri, mpaka hapo alijua wazi kuwa ni yeye tu mwenye uwezo wa kuwakomboa wengine wote.

§§§§§

Naima aliwaomba wale jamaa kumtoa Kamanda ndani ya gari, “Hana fahamu huyo amenusa Mandrax kwa wingi sana,” akawaambia. Vijana wane wakasogea na kuweka bunduki zao migongoni kisha wakamteremsha Amata na kumsimamisha chini.

“Hana ujanja huyo!” JoKi akawaambia.

“Mpelekeni ndani nakuja mwenyewe kumpa adabu,” Naima akawaambia, na wale vijana wakamburuza mpaka mpaka ndani ya kile chumba walichoagizwa na kuanza utaratibu wa kumfunga.

Muda wote huo Kamanda Amata alijifanya kalala fo fo fo kutokana nay ale madawa kumbe la, alikuwa akiwavunga na kusubiri muda kuafaka wa kuwaonesha kama yeye ni T.S.A 1.

§§§§§

Scoba alipoona tayari utulivu umerejea na kuna lango limefungwa akaona sasa ni wakati wa kufanya makeke yake. Akafyatua mkanda wake wa kiuno na kuchomoa kitu kama pini hivi, akaipachika sehemu Fulani katika kile kitasa kwa upande wa ndani, kisha kwenye kiatu chake akachomoa kitu kama chipio na kukipachika upande wa pili wa ile loki, akajaribu kufanya anayojua na sekunde tatu zilikuwa nyingi, kikaachia. “Waohhh!!” akapumua kwa nguvu kisha aakachungulia nje na kuona giza tupu.

Akaichukua miwani yake na kuivaa akaibana vyema kabisa ili isije kuanguka akiwa kwenye harakati, miwani hii ilimpa uwezo wa kuona gizani. Alipoivaa tu akaanza kuona vyema ndani ya giza lililomo katika jengo lile. Akaangaza na kuona kuna kamera moja ya usalama upande ule ambao yeye anapaswa kutokea, kutokana na giza hilo hakujali, akafungua buti taratibu na kutoka akitanguliza mguu mmoja bila kufanya kelele yoyote. Akarudishia buti na kulibana tena. Alipokwisha kulibana akashtuka na kujishika kinywa, “Shit! Mi mpumbavu sana!” alijisemea maneno hayo alipogundua kuwa amesahau bastola kwenye buti. Sasa hakuwa na silaha yoyote, hakuna jinsi. Akajibana ukutani, kisha akajivuta taratibu mpaka karibu na mlango ambao bila shaka ndipo walipoingilia na Kamanda Amata, akashika kitasa na kukivuta chini taratibu, kisha akausukuma, ulikuwa wazi, “Missing in action!” akajisemea kisha akaingia ndani ya korido ndefu, akaivua miwani na kuruhusu ining’inie shingoni mwake.

Ndani ya korido hii kulikuwa na mwanga wa kutosha, hakukuwa na mlango wowote isipokuwa mbele yake umbaliwa kama mita mia moja aliona kuna kingo za chuma akajua kwa vyovyote kuna ngazi za kuteremka chini. Kikwazo kimoja kikawa mbele yake, katikati ya korido kulikuwa na kamera nyingine ya usalama, na ujia ule ulikuwa mwembamba kiasi kwamba huwezi kupita mbali na kamera hiyo, “Walijenga makusudi hivi,” akajisemea na kuanza kufikiri jinsi ya kuipita kamera ile.

 

 

 

 

SURA YA 8

HALI YA GINA ILIRUDI NA KUWA NZURI, ijapokuwa bado alikuwa wodini lakini huduma aliyoipata kutoka kwa Dr. Khadrai na jopo lake ilimfanya aweze hata kuongea. Kichwa kilimzunguka alipojaribu kufikiri ni wapi wenzake wote watakuwepo.

“Khadrai, hivi hauna dawa ya kuniondolea maumivu kabisa niingie kazini?” akauliza. Khadrai akabaki kucheka tu.

“Gina, naona akili yako haiku sawa, endelea kulala, hali yako ni mbaya sana usifanye lolote la mikikimikiki,” akajibiwa.

“Moyo unaniuma sana kuona siwezi kufanya lolote,” akamwambia Khadrai.

“We Gina tulia hapa, hakuna baya litalotokea kama unavyowaza,” Khadrai akampa matumaini. Alipotaka kuondoka, Gina akamzuia, “Khadrai, naomba mkoba wangu,” akamwambia na Khadrai akampa, Gina akapekua ndani na kutoa bastola moja aina ya Beretta, akaikagua ipo sawa akaitia ndani ya shuka mkono wa ke wa kulia.

“Ya nini Gina?” Khadrai akuliza.

“We nenda! Nenda!” akamwambia huku akimpa ishara ya mkono.

Kgadrai akatoka ndani ya kile chumba na mara akakutana na watu wawili waliosimama mbela yake, wakamwonesha vitambulisho, maafisa wa polisi.

“Tunahitaji kumwona WP Gina kikazi,” wakamwambia huku wakipita kuelekea ndani ya kile chumba. Wakafungua mlango na kukuta Gina amelala kimya, drip mkono ni mwake na mipira ya oksijeni puani mwake. Khadrai akapigwa na butwaa maana hakumwacha Gina na oksijeni isipokuwa drip tu.

“Gina, Gina!” akaita mmoja wao. Gina akabaki kimya kabisa kama hasikii ilhali alikuwa akisikia kila jambo, mkono wake wa kulia tayari ulikamata bastola iliyokuwa haina usalama na risasi moja ilikuwa tayari ndani ya chumba cha shughuli.

Baada ya kuona kimya cha Gina wakatazamana na kupeana ishara kwa kubaniana macho, mmoja wao akaurudisha mlango na Yule mwingine akaenda na kuondoa ule mpira wa oksijeni. Gina kama umeme, alichomoa bastola yake kwenye shuka na kuanza na Yule aliyekuwa akifunga mlango, alimlenga shabaha na kufumua bega lake kisha akajibiringisha na kudondokea upande wa pili wa kitanda akiicha sindano ya drip ikichomoka yenyewe. Kutoka uvunguni alimchapa risasi Yule mwingine na kuvunja mifupa ya ugoko, alipodondoka akammalizi risasi ya moyoni. Kisha akasimama na kumtazama Yule aliyekuwa akifunga mlango wakati huo akimwagika damu begani hana la kufanya.

Gina alizunguka kitanda na kusimama kando ya marehemu Yule na kumtazama huyo aliyemjeruhi.

“Nimekujeruhi makusudi fala we!” akamwambia kwa hasira, akafyatua risasi nyingine na kupiga bega la pili, “Niambie, watu wangu wako wapi?” akamwuliza.

Yule jamaa alibaki analia tu, “Umentia kilema cha maisha weweee!”

“Nini kilema nakuua kama usiposema,” akamwambia.

“Utanionea tu huyu uliyemuua ndiye anajua kila kitu,” akajibu huku akibuujikwa damu.

“Jeuri siyo?” Gina akamuliza na kumkanyaga kwa nguvu bega lake.

“Aaaaaaiiigghhh! Nasema, nasema, nasema!”

“Sema!”

“Wapo Kerege, Bagamoyo,” akajibu.

“Na wewe bosi wako nani?”

“Mtu mkubwa, mkubwa serikalini,” akajibu.

“Nani mtaje kwa jina!” Gina akang’aka.

“Kigogo, Ki-go-go,” akaongea kwa taabu. Gina akaelewa anachokifanya akamwahi na kumtandika ngumi ya shavu, Yule jamaa akatema kidonge cha manjano, kidoge cha sumu kali ambacho huficha kinywani wanapozidiwa kwa maswali huwa ni bora kujiuwa kuliko kutoa siri.

“Shenzi sana wewe, ulifikiri utaniwahi? Sasa utaenda kueleza yote kwa wanaojua cha kukufanya,” Gina alilalama, kisha akachukua simu ya Khadrai nakubofya namba Fulani Fulani.

“Ndiyo Inspekta Simbeye (…), Agha Khan hapa hospitali haraka,” akatoa ujumbe upate wa pili na kumwacha Yule jamaa akipewa huduma ya kwanza ili kuzuia damu zisiendelee kumtoka. Gina aliiweka vizuri bastola yake na kuirudisha kwenye pochi yake. Khadrai alikuwa hana amani kabisa, akamtazama Gina bila kumuuliza chochote, Gina akaweka vizuri kilichochake.

“Vipi Gina?” Khadrai akatupa swali.

“Hapa hakuna usalama, najua wapi nitakwenda, asante kwa msaada wako.”

“Lakini Gina hali yako bado mama,” Khadrai akamwambia.

“Najua, lakini kwa hali ilivyo ni hatari,” Gina akajibu huku akitembea kwa kuchechemea kidogo kutokana na lile jeraha lake.

Dakika kumi na tano baadae, Inspekta Simbeye akaingia katika ile hospitali akifuatana na vijana wake mahiri kabisa waliobeba silaha za kutosha, wakateremka na kupanda mpaka ghorofa ya tatu.

Baada ya kukamilisha mambo yao ya kiusalama waliondoka na ule mwili pamoja na Yule majeruhi kwa mahojiano zaidi.

“Gina, pole sana, unajisikiaje lakini?” Simbeye alimuuliza Gina.

“Maumivu makali sana, lakini hapa siwezi kulala, pia sina amani kwa kuwa sijui watu wangu wako wapi,” Gina akajibu huku amejilaza katika kitanda cha kitabibu.

“Pole, sasa itabidi upelekwe Lugalo mahali ambapo pana usalama zaidi,”

Wakakubaliana hilo na utaratibu wa kila kitu ukafanyika. Ijapokuwa Gina alikubali kwa shingo upande kwa kuwa yeye alipenda kuingia msambweni kuwasaka wenzi wake.

Inspekta Simbeye, aliyekuwa akilitumikia jeshi la Polisi kwa kofia mbili, moja kama Inspekta wa Polisi lakini ya pili ni ile ya Ukachero wa serikali, Usalama wa Taifa, aliwekwa pale kwa mpango maalumu wa kuchunguza maafisa wa Jeshi hilo kama kuna lolote baya wanalolifanya juu ya nchi hii.

 

 

 

 

 

SURA 9

Kerege – Bagamoyo

WAJUMBE WA KIKAO KILE CHA DHARULA walipiga makofi baada ya kupewa taarifa kuwa watu wao wote wamepatikana isipokuwa mmoja ambaye wao kama wao hawakuona kama anaweza kuwa na dhara lolote.

“Kazi imekwisha!” Pancho aliwaambia wenzi wake.

“Vijana wamefanya kazi ngumu na nzuri wanastahili pongezi,” mwingine aliongezea.

Baada ya furaha yao hiyo kukamilika na kugongeana bilauri kama ishara ya kupongezana,; Pancho Panchilio aliwataka watu wake kuteremka kuzimu ili kushuhudia kile kilichoitwa ‘Hukumu ya Mwisho’.

“Na tutawafuatilia mbali katika uso wa dunia,” Pancho aliwaambia wenzi wake. Kisha kila mmoja akavaa uso wake wa bandia akiwa sehemu yake ambayo mpaka hapo hawakuweza kuonana sawasawa. Wakavaa kisha Pancho akiwa katika guo jeusi akifuatiwa na wajumbe wake watatu wakatoka na kuteremka ngazi kuelekea bondeni walikopenda kukuita Kuzimu.

§§§§§

Scoba aliendlea kusukuti huku bado akiwa kasimama hakujua lipi lakufanya mbele ya kamera ile. Baada ya kuumiza sana kichwa akakumbuka kipande kimoja cha isa ambacho aliwahi kusimuliwa na Kamanda Amata jinsi anavyozipita kamera kama hizo, akatabasamu kisha akairusha kwa kutanua miguu na kunata ukutani, akiwa kataua miguu yake na kukanyaga huku na kule na mikono hivyo hivyo, akanata juu kabisa na kuanza kujivuta kwa namna ambayo wewe huwezi hata kidogo, ukimtazama unaweza kusema na mjusi au kenge.

Aliifikia ile kamera na kuushika waya wake kutoka nyuma akauchomoa, kisha akajiachia na kutua chini taratibu. Kisha akaenda kwa mwendo wa kasi mpaka katika zile ngazi, alipofika tu alikutana uso kwa uso na mtu mmoja aliyekuwa akipanda juu, Scoba akaruka na kutua juu ya ukingo wa ngazi uliotengenezwa kwa bomba la aluminiam akaseleleka na mguu mmoja akamtandika teke Yule mtu kisha akajiachi na kumshukia pale chini; kabla hajasema lolote akambana koo kwa goti lake.

“Wako wapi?” akamwuliza.

“Akina nani?” Yule bwana aliongea kwa taabu.

“Wako wapi watu wangu? Mmewaweka wapi?” akauliza kwa ukali lakini kwa sauti ambayo haiwezi kwenda popote.

“Hakuna watu wako huku aliyekwambia wapo ni nani?” Yule bwana akajibu kiujeuri. Scoba akamnyonga mkono na kuuvunja, Yule bwana akapiga yowe la uchungu, Scoba akaona itakuwa noma, akamkamata na kumvunja shingo kisha akaichukua bunduki yake aina ya S.M.G na kuteremka ngazi mpaka kwenye maboksi Fulani akajificha. Watu wawili wakapita eneo lile wakitangulizana, akatulia na kusubiri Yule wa pili ili amputeze lakini alighairi baada ya kusikia mazungumzo yao matamu.

“Wanauawa wote, tena sasa hivi,” mmoja akamweleza mwenzie.

“Yaani ni historia,” mwingine akamuunga mkono. Alipopita wa kwanza akamwacha wa pili akamkata na kabala moja matata sana kisha akamvuia kwenye maboksi taratibu na kumtuliza. Yule wa kwanza akajkuta kila akiongea hakuna kuungwa mkono akageuka kutazama kulikoni akakutana macho na Scoba. Bila kuchelewa Scoba alirusha kisu maridadi kabisa na kumchoma koromeo, akajibwaga chini.

§§§§§

Madam S alifunguliwa minyororo na kukokotwa kuelekea katika chumba cha mauaji, Chiba naye akachukuliwa kikondoo namna hiyo, Dr. Jasmin kwa kuwa yeye hakuteswa kama wengine alitembea mwenyewe mpaka ndani ya chumba kile cha kutisha.

“Wafunge pale huyo bibi na huyo kijana mtukutu, kisha mlete huyo rembo mbichi hapa,” JoKi alitoa amri nayo ikatekelezwa. Walipomaliza wakaambiwa wakamlete Kamanda Amata li kazi ya mauaji ianze kama ilivyopangwa. Amata akaletwa, na ye kama kawaida akatuliaa na kukokotwa mpaka ndani ya chumba kile kinachonuka damu mbichi na iliyoganda, macho yake yalikuwa yakiwatazama wote waliojipanga mle ndani wakiwa na silaha nzito nzito. Mara hiyo hiyo Pancho na watu wake waliingia ndani ya chumba kile na kusimama mahala Fulani.

“Sasa tunataka tuanze shughuli yetu, karamu ya damu, JoKi! Nataka ufanye kazi hii kama nilivyokuagiza, lakini kwanz ahuyo mrembo lazima aingiliwe nah ii ni motisha kwenu vijana wangu haya na muanze kazi sasa ya kumuingilia,” Pancho akatoa amri, vijana wawili walioshiba kimazoezi wakamvamia Jasmin, mmoja akaanza kumvua nguo kwa nguvu huku mwingine akishusha zipu yake kuuchomoa mshedede.

Yule jamaa aliyekuwa akimvua nguo Jasmine alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuchapwa makonde mawili matamu kabisa, akapepesuka pambeni na kujipanga upya, alipomwendea Jasmin ili ampe kibano alikutana na mapigo matano ya karate ya haraka haraka yaliyompeleka chini. Yule mwingine alitoa macho baada ya kujikuta dudu lake likikatika vipande viwili.

“Aaaaaaiiiggghhhh!!!” alipiga kelele huku akijiangalia, kila tu akashtuka waliposikia sauti ya kisu kikitua ardhini huku kikiwa kimekata dhakari ya Yule bwana.

“Shit! Muue huyo mwanamke haraka!” JoKi alitoa amri huku akiwakinga Pancho na wenzake.

“Nini JoKi?” Pancho akauliza.

“Tumevamiwa!” akatamka neno hilo na hapo hapo alishuhudia minyororo aliyofungwa Kamanda Amata ikikatika kwa shabaha maridhawa kutoka kwa Scoba, Kamanda Amata aliruka sarakasi maridadi na risasi nne zilichimba chini, alipotua tayari alikuwa na shingo ya mtu, alimkamata na kumzungusha kichwa Yule bwana akatoa macho na kuachama kinywa chake,kisha akambwaga chini. Alipogeuka huku na kule, JoKi hayupo, Pancho na watu wake hawapo.

“Soba fungua hao, fanya juu chini wafike kwenye gari, hii kazi niachie mimi niimaize, pumbavu zao,” Kamanda Amata akampa maagizo Scoba kisha yeye akajibana mahali na S.M.G kononi, akanyata kwa tahadari akiwa hajui wapi wale watu wamepotea ghafla namna hiyo. Mara taa zote zikazimika, giza likachukua nafasi ndani ya jingo hilo.

Scoba akaivaa miwani yake na kuendelea kuona vizuri kabisa, akawafungua Chiba na Madam S.

“Asante T.S.A 4, hakikisheni humu ndani hatoki mtu akiwa hai,” Madam S alitoa amri mara moja kama cheo chake kilivyo.

Mara sauti ikasikika kutoka katika vipaaza sauti vizivyoonekana.

“Ak! Ak!Ak! Ak! Hii ndiyo himaya ya Shetani, Taifa ndani ya nchi, hamjafanya lolote na hakika hamtatoka humu mkiwa hai, lazima muongee na bwana ngurumo,” ile sauti ikacheka tena kwa dhihaka.

“Usimsikilize huyo hanithi, Scoba ongoza mbele Jasmine linda nyuma ninyi ndio mna nguvu kwa sasa mi namaliza kazi,” Kamanda Amata akatoa maelekezo kisha kwa mwendo wa taratibu alipita kwenye ujia mrefu ulioonekana ukienda mahala Fulani. “Nitakukamata tu, na leo itajulikana mbivu na mbichi,” akajisemea. Mara nyuma yake akasikia kama mtu aiyetua ghafla kwa miguu laini, akageuka ghafla na kujikuta akipata pigo moja kali la kung fu, akayumba na kusimama tena, akajikuta akipigwa ngwala tamu, akapaa hewani na kujibwaga chini, akajikunja na kujiinua kwa ustadi. Alikuwa ni Naima aliyemtembezea mchezo huo.

“Malaya mkubwa wewe! Sasa umeingia mikononi mwangu!” Kamanda akaunguruma.

Mara ile sauti ikasikika tena ikicheka na cheko lake likifanya mwangwi, “Mtoto wa kike kutoka Kigoma lazima akuoneshe kazi”.

Mara taa zikawaka, Naima akajizungusha huku akipiga vijikelele kama nyau, akampelekea pigo la kwanza Kamanda akaliona, la pilia akaliona la tatu akaliona, la nne Kaliepa kwa chini na kujizungusha kwa kasi, aliupiga mguu wa Naima lakinia Naima aliruka sarakasi hiyo ile ngwala ikamkosa, Naima alitua sakafuni na kupiga teke kali huku akiruka tik tak; hilo lilimpata Amata na kumuinua juu juu na kumbwaga chini mzima mzima.

Naima alitua sakafuni na kusimama kwa madoido huku akimwonesha ishara ya mkono Amata akimwambia, “ Come to me boy, come to me boy”.

Dharau hizo Amata aizichoka, akajirusha kujiinua, Naima akataka kumwahi, akaruka teke ambalo lilikusudiwa kutua kidevuni mwa Amata lakini akaikinga mikono yake na kuudaka mguu wa Naima, akauzungusha kwa minajiri ya kuuvunja lakini Naima naye akaruka hewani na kujizungusha sambasamba na akili ya Amata na mguu wa pili akirusha teke linguine lakini Amata akaliepa na kumwachia, wote wakaanguka chini. Amata akawahi kuinuka na kujiweka sawa, Naima alipoinuka alikutana na mapigo kumi na mbili ya karate, kwa kazsi aliyoitumia Kamanda Amata , Naima aliwe kuyakinga mapigo manne tum na nane yaliyofuata yalimwacha hoi.

“Come to me bitch!” Kamanda Amata akamwita kwa dharau, Naima damu zilimtoka kinywani na puani, alijifuta bila mafanikio.

“Hesabu ushakufa Naima!” Amata alimwambia.

Naima akasonya na kujitutumua kumvamia Amata, akakutana na kono lenye nguvu lilimtandika ngumi moja ya maana katika ziwa lake la kushoto. Naima alisimama ghafla akiwa katoa macho, akijitahidi kuongea lolote lakini alijikuta hawezi. Alipotaka kuanguka Amata akamwahi, akamtazama husoni, akambusu kwenye paji la uso. Mara taa zikazimika akasikia sauti ya bastola inayoondolewa usalama, akawahi kuruka na kumwacha Naima akifumuliwa vibaya na risasi hizo.

“Tulia, fuata maelekezo yangu, sasa hivi sina masihara na kiumbe yoyote Yule, nipeleke walipo mabosi wako,” akaamuru.

JoKi akiwa mikono juu, akatulia kama alivyoamuriwa, akataka kugeuka, Kamanda akamzuia.

“Sijakwambia ugeuke, nimekwambia unipeleke walipo vinyamkera wako,” akamwambia tena. JoKi akatafakari jambo, “Sasa bila kugeuka nitakupelekaje walipo? Hivi ninyi mnachokifanya mnakijua? Mtajuta kuzaliwa ndani ya nchi hii,” JoKi akaongea.

“Funga domo lako kibaraka tu wewe, na sasa utatujua sisi ni nani, mlifikiri jaribio lenu litafika wapi? Haya nioneshe hao vinyamkera wako,” Amata akaamuru.

“Siwezi kukuonesha na huna la kunifanya,” alijibu JoKi huku akigeuka mzima mzima na kukutana na Amata aliyekuwa amefura kwa hasira.

“Ha ha ha ha, Kamanda Amata, nasikia tu unavyovuma katika visa vyako vya kubahatisha, safari hii maji yapo shingoni ee?” akaongea kwa ngebe zilizompandisha hasira Amata, akaiweka vizuri bunduki aliyoishika mkononi mwake.

“Amata, wanaume wakutanapo huweka silaha chini na kupambana kwa mikono,” akaongea kwa dharau huku mikono yake kaiweka kiunoni kana kwamba anaongea na mtu wa kawaida mbele yake.

“Najua hila zako, ichukue wewe utumie kunishambulia,” Amata akamwambia huku akimrushia ile bunduki. JoKi akainua mikono yake ili kuidaka na ndilo kosa alilolifanya. Konde moja la kilo nyingi lilitua sawia mbavuni, la pili na la tatu, JoKi akawa hoi, akajaribu kujipanga lakini Amata hakumpa nafasi kwani alimvurumishia makonde yasiyo na idadi mpaka akaenda chini na kuanza kubingirika kwenye ngazi, akafka chini akiwa hoi.

“Kelele zote mi nilijua unaweza mchezo kumbe hamna kitu, boya tu, haya simama sasa,” Amata akamwambia JoKi. Bado JoKi alikuwa pale chini, Kamanda Amata akamsogelea. Joki alifyatuka kasi na kumtia ngwala Amata, lakini hakukubali, aliruka beki na kusimama kwa miguu yake miwili, wakati huo tayari JoKi nae alikuwa wima. Kamanda Amata alirusha teke lililopanguliwa vyema na JoKi. JoKi alipeleka mashambulizi ya karate kwa Kamanda lakini mapigo yote yalikingwa kwa ufundi wa hali ya juu. Wakasimama pande ofauti wakitazamana kama majogoo hasimu, yenye uhasama wa kudhulumiana tetea.

JoKi alifyatuka na kucheza karate kadhaa kwa kumwelekezea mapigo ya hatari Amata, lakini alijikuta hapati kitu baada ya Kamanda Amata kuyacheza vizuri na kubaki imara akimtazama JoKi aliyeishiwa cha kufanya. JoKi akajikunja na kuanza upya mashambulizi, safari hii alikuja na ujanja mwingine ambao umakini kwa kamanda Amata ulihitajika. JoKi alipeleka mashambulizi makali ya mikono na wakati huo huo akibadilika na kutumia miguu yake. Kasi ya mashambulizi hayo ilimfanya kamanda Amata apate tabu kucheza na akili mtu huyo, lakini yote ya yote Kamanda Amata aliyakinga kwa ufundi. JoKi alimpiga ngwala ya nguvu na Amata .lirushwa juu, lakini akiwa hewani alijigeuza na kutumia mguu mwingine na kumzabua teke kali la shavu na kumvunja taya. JoKi akayumba na kujibamiza ukutani huku akijishika taya lake la chini lililohama mahala pake. Hakumjali, alimpa mapigo makali na kumwacha akiwa hoi sakafuni hajielewi, akamfuata na kumkamata kichwa chake akambamiza ukutani kwa nguvu kisha akamwinua mzima mzima.

“Nioneshe walipo,” akamwambia huku akiwa kamkunja vyema shati lake, damu zikimvuja.

“Wapo safe house,” akajibu huku mabonge ya damu yakimtoka kinywani.

“Safe house ndo wapi?” akamwuliza.

“Ipo chini kabisa ya jingo hili, lakini huwezi kufika kabla hujauawa,” akamjibu huku akitoa cheko la ajabu kisha akatokwa na uhai.

§§§§§

Kazi nzito ilikuwa upande wan je ambako Scoba na Jasmin walikuwa wakiwadhibiti walinzi wa jengo hilo. Watu wa kijiji hicho walikimbia mbali wakisema majambazi yamevamia jumba hilo.

Chiba alipita huu na kule na kutokea kwenye mlango mmoja ulioandikwa ‘Control Room’ akauchezea huo mlango kidogo tu na kujikuta ndani. Chumba kikubwa kilichojawa na mitambo ya mawasiliano, kompyuta na vitu vingine, kutoka pale ndipo alipoona kamera zote za usalama za eneo lile jinsi zilivyokuwa zikifanya kazi na kuangaza kila eneo, alitikisa kichwa baada ya kuona ugumu wa kazi yao ulikuwa wapi kwani walionekana kila walipokwenda, jambo la kwanza alizima tambo uliokuwa ukiwaunganisha watu wote wa jengo hilo kwa simu maalum za ndani ‘Voip’. Baada ya hapo akaelekea mahala palipokuwa na kitu kama kabati lenye switch mbalimbali, akaelewa ni switch za milango, akaibofya na kufungua milango yote ya jumba hilo kisha akaharibu mfumo mzima.

Akiwa katika shughuli hiyo akasikia mlio hafifu wa bastola inayoondolewa usalama.

“Nani alikwambia?” sauti ikatoka nyuma yake, “Haya mikono kichwani kisha geuka taratibu,” aliamuriwa. Chiba aliweka mikono kichwani na kugeuka kwa kasi na kuipiga teke ile bastola kisha akajirusha sarakasi na kuichukua mikononi mwake, Yule bwana alijikuta hana ujanja, macho yakamtoka. Kisha akamuongoza kwenye mitambo yake.

“Nioneshe mabosi wako walipo,” akamwamuru. Yule bwana hakuwa na aujanja aliwasha luninga mojawapo iliyowaonesha wale mabwanyenye kila mmoja akiwa katika harakati za kuiacha himaya hiyo, Chiba alibaki kinywa wazi, hakuamini kile anachokiona, aliwatambua watu wale kwa uwazi kabisa bila kificho akajikuta akiishiwa nguvu. Alipogeuka nyuma kumtazama Yule kijana hakumuona, katoweka. “Shiit!” akang’aka na kuiweka bastola yake vyema mkononi mwake kisha akaanza kuzunguka humo ndani kumtafuta.

Yule kijana alijificha kimya upande wa pili wa mashine zile, mkononi alikuwa na kisu akimvizia Chiba kufika upande huo ili amfanyie kweli, masikini, hakujua anacheza na kiumbe cha aina gani katika tasnia hiyo ya mchezo wa visu. Katika kupita akitafuta, Chiba alimwona Yule kijana akichungulia, akajifanya hamwoni kabisa na kuendelea kutafuta huku kampa mgongo. Yule kijana akaona hapo ndipo pa kumpata adui yake, akatoka mzima mzima na kisu mkononi kumpamia Chiba kwa nyuma. Chiba alimkwepa na kumdaka mkono, akauzungusha na kumnyanyua kisha kumbwaga chini na kumbana vyema.

“Nipe namba za milango!” akamwamuru.

“Sizijui,” akajibu huku akikunja sura kwa maumivu.

Chiba akaunyonga mkono kwa nguvu, “Taja, kabla sijakumaliza,” akamlazimisha huku akiunyonga ule mkono.

“Nataja, na-ta …” kabla hajamaliza, Chiba alishuhudia Yule kijana  akitoa macho na kisu kimedinda shingoni mwake, “Wamemuua!” akajisemea; kwa kasi ya ajabu alikichomoa kile kisu na kukirusha upande kilipotokea huku yeye mwenyewe akibiringika kuliacha eneo lile, akashuhudia risasi zikiufumua mwili wa Yule kijana ilhali mtu aliyemlenga akidondoka jirani na mlango bila uhai. Chiba akasimama chapchap na kuangaza macho huku na huko, chumba kilikuwa kimya, hakuna mtu zaidi yake na zile maiti mbili tu. Akahakikisha usalama kisha akazipekua zile maiti na kupata funguo moja ambayo hakujua hata ni ya kitu gani, akaitia mfukoni. Hakuzijali maiti akapanda juu ya kiti cha magurudumu kilichokuwa hapo na kuanza kucheza na zile kompyuta. Alishangaa kuona kuwa wale jamaa walikuwa wamejiunganisha na vitengo vyote muhimu vya serikali wakipata siri mbalimbali za vitengo hivyo.

Akaendelea kupekuwa na kukuta habari nyingi za Usalama wa Taifa zikiwa katika moja ya kompyuta hizo. “Ni nani hawa?” akajiuliza bila kupata jibu. Akasogeza kiti chake na kuelekea kwenye luninga kubwa iliyoonesha jingo lote ndani na nje na kuanza kukagua sehemu moja baada ya nyingine, akatazama vyumba mbalimbali vya jingo hilo na kugundua kuwa bado walikuwa hawajafika hata nusu ya hifadhi ya jingo hilo. “Shiit!” alijikuta aking’aka na kujisukuma kwa nguvu mpaka kwenye meza ndogo yenye simu na kuiyakua kisha akabofya namba fuklani na kuweka sikioni.

“…Inspekta Simbeye, Chiba anaongea hapa!” akaijibu sauti ya pili iliyoitikia simu hiyo.

“…Oh, Chiba, nafarijika kusikia sauti yako Kamanda wangu, nipe dondoo,” akamwambia.

“…Inspekta naomba haraka iweekanavyo uje na vijana wa kazi wasiopungua kumi na tano wenye silaha nzito zilizoshiba, eneo ni Kerege, Bagamoyo, plot namba KG/BY 1230p…” kisha akakata simu. Alipogeuka kwenye luninga hakuwaona wale Mabwanyenye kwenye vyumba vyao, wametoroka! Akazima swichi kubwa na umeme ukakatika kila kona ya jengo lile, akilenga kuwanasa kama walikuwa wakijaribu kutoroka na chombo chochote kitumiacho umeme, kisha akachukua silaha kutoka kwa mmoja wa maiti wale na kutaka kutoka kwenye kile chumba, akakumbuka kitu; akarudi.

Akaenda kwenye moja ya kisanduku na kutaka kufungua akashindwa, akagundua kuna funguo hutumika, akafikiri kidogo na kuchukua kale kafunguo alikochomoa ka Yule jamaa, akatumbukiza na kuzungusha kidogo tu, mlango ukafunguka. Ilikuwa na sisytem unity iliyounganisha kompyuta zote ikiwa na maana kuwa ilihifadhi data zote za wale jamaa. Kwa kutumia ile bunduki akavunja kufuli lililokuwako nyuma ya dubwasha hilo, akaondoa funiko lake na kutazama anachokitaka, akafyatua waya nene nene zilizojaa huko, akavuta dubwasha Fulani kubwa kubwa na kulichomoa kutoka kwenye system ile, akatikisa kichwa kwa ushindi, kisha akatokomea nalo.

§§§§§

“Hapana, lazima niende!” Gina alimsisitizia Inspekta Simbeye.

“Gina nimekuleta huku ili upumzike, sasa acha tupeleke kikosi katika eneo la tukio,” Inspekta Simbeye akambembeleza Gina lakini Gina hakukubaliani na bembelezo hilo. Mwisho alikubali kwa shingo upande kubaki Hospitali ya Lugalo chini ya uangalizi wa madaktari wa kijeshi.

Inspekta Simbeye alichukua vijana wachache wanaojua kazi, kikosi maalumu cha kukomesha ujambazi kilichoundwa na Kamanda Toss kikaingia kwenye Land Cruiser za Polisi. Kutoka kituo kikuu gari hizo zilichukua uelekeo wa Makongo mpaka Mwenge waipomchukua Inspekta huyo na kuongoza kwenda Kerege. Kwenye gari hizo hakuna aliyeongea, kila mmoja alikuwa kimya kabisa akiitafakari shughuli inayomkabili, bunduki zilikuwa tayari zimejazwa risasi na magazine za akiba zikipachikwa kwenye vikoba maalum tayari kupokea zile zilizopo chemba pale itakapobidi.

 

KEREGE  

KAMANDA AMATA BAADA YA KUHAKIKISHA JOKI AMEKATA ROHO, akaondoka upesi eneo lile, kila alipokuwa akipita kutazama tazama alikuwa safari hii milango iko wazi kabisa, hakuna tena milango ya siri, kazi ya Chiba ilisaidia. Akaiendea lifti ili aweze kushuka chini kabisa ya jengo hilo. Kwa mbali akiwa anasikia milio ya risasi za piga nikupige alijua wazi kuwa huko kazi inaendelea.

Ghafla akasimama kwenye moja ya kona za ndani ya jingo hilo baada ya kusikia michakacho ya viatu vya mtu anayekuja upande wake, akajiandaa kwa shambulizi la dharula, alipohisi mtu huyo amekaribia, alijitoa mzima mzima lakini pigo lake likakingwa kwa ustadi wa hali ya juu.

“Oh, sorry asee! Chiba vipi?” kumbe alikuwa Chiba.

“Yeah, hapa ni kujilinda muda wote, tuelekee chini, hawa jamaa wako huko,” Chiba akatoa maelekezo na kisha wote wakateremka kwa kutumia ngazi kwa maana Chiba alikuwa amezima umeme na kufanya lift zote zisifanye kazi. Haikuwachukua muda kuwasili chini kabisa ya jingo hilo kubwa na la kisasa, “Lilijengwa kwa miaka mingapi hili?” Kamanda akajiuliza, huku wakiufuata mlango mmoja baada ya mwingine, lakini vyumba vyote vilionekana tupu.

“Hawapo Chiba, laiti ningewapata!” Kamanda alimwambia Chiba huku akiiteremsha silaha yake kutoka mikononi na kuiweka mahala pake.

“Nimempa taarifa Inspekta, yuko njiani,” Chiba akatoa taarifa kwa Kamanda.

“Safi sana Chiba, kumbuka hapa sote hatuna mawasiliano na dunia ya nje,” kamanda akaitikia kisha wakaendelea kupekua chumba kimoja na kingine. Katika moja ya vyumba hivyo kulionekana kuna mlango wa siri lakini ulikuwa wazi ndani yake, akausogelea na kuchungulia ndani yake, ulikuwa ujia mrefu sana uliopotelea gizani.

“Hii ni njia ambayo kwa vyovyote wametorokea,” Kamanda akamwambia Chiba.

“Kila mmoja alikuwa na njia yake Kamanda, hapa alitumia mmoja wao,” Chiba akajibu. Kamanda Amata akageuka kumtazama kama akihoji kitu, lakini mwisho aliuliza.

“Umejuaje?” akamwuliza.

“Nimewaona katika dakika zao za mwisho kutoroka lakini mshenzi mmoja akanivamia; katika kupambana naye ndipo nilipowapoteza sikuona wametorokaje lakini walikuwa vyumba tofauti,” akaeleza.

“Umenikiwa kuona sura zao?” akauliza tena.

Chiba akatulia kwa nukta chache kwa maana aliwaona mara hii wakiwa hawana vinyago na aliwatambua kuwa ni vigogo wakubwa serikalini, “Je kama walitumia sura za bandia kutughilibu?” akawaza, kisha akamtazama Amata.

“Hapana, walificha sura zao kama kawaida,” akajibu.

“Ok, tutawajua tu, usiguse kitu watu wa Foresinc Bureau waje kufanya kazi yao ya kunasa alama za vidole na nyinginezo,” kamanda akamwambia Chiba huku wakitoka na kuelekea chumba kingine, nako wakakuta mambo hayo hayo, wakatoka na kupita vyumba vingine kama vitatu vilivyoonekana viko katika mtindo huohuo. Wakaviacha na kuendelea na uchunguzi wao zaidi na zaidi. Katika ghorofa ya chini wakagundua jambo ambalo liliwatia hofu, mioyo yao ikashtuka, kama wangekuwa na mioyo myepesi wangeziamia au hata kufa kabisa.

“Hawa ni mashetani!” Chiba akasema.

“Nin hiki?” Kamanda akauliza huku akivuta hatua ndani ya chumba hicho kikubwa, “Hawa jamaa hawastahili kuishi kabisa, ningewatia mkononi wangejuta kuzaliwa,” akaongeza.

“Kamanda, hapa msaada wa haraka unahitajika, nafikiri vijana watakuwa tayari nje,” akasema Chiba.

§§§§§

LAND CRUISER ZA POLISI ziliingia kwa fujo eneo lile na vijana wa kazi wakaruka tayari kuanza kudhibiti eneo hilo. Ilikuwa kama sinema ya kizungu vile. Inspekta Simbeye akawapanga vijana kuzunguka jingo hilo na wengine kuingia ndani kupitia lango kuu, haikuchukua dakika kumi tayari walizingira na risasi kadhaa zilirindima ndani ya wigo huo, kisha kundi la watu waliokuwa katikanulinzi wa jingo ilo waliwekwa chini ya ulinzi.

“Hivi hili jumba lina milikiwa na nani?” Simbeye akajiuliza bila kupata jibu. Vijana wake bado wakiwa katika sakasaka hiyo upande wa pili wa jingo walipomweka chini ya ulinzi Madam S na Jasmine. Kutii sheria bila shuruti, Madam S akiwa kachafuka damu zilizoganda, alisalimisha silaha yake na Jasmine akafanya hivyo kisha wakatiwa pingu. Inspekta Simbeye aliwaona wakiletwa kwake wakiwa na pingu mikononi, wakaamuriwa kukaa chini pembeni kidogo kwa wenzao.

Scoba alitokea pale ambapo gari ya Gina iliegeshwa baada ya kutekwa na kuletwa huku, moja kwa moja akaliendea lango na kulifungua na kuchungulia nje kwa minajiri ya kuwashambulia waliopo huko na apate jinsi ya kutoa gari hi;lo na kuwaokoa wengine kama walivyopanga, alishangaa alipoona vijana wenye silaha wakiwa wamewalaza chini vijana wengine kama kumi hivi tena kifudifudi, kwa jinsi alivyowaona tu akajua ni Polisi, akajitokeza mzima mzima na bunduki yake mkononi.

“Jisalimishe kama ulivyo, weka silaha chini,” amri ikatoka upande wa nyuma yake, Scoba akafanya hivyo na kuamuriwa asogee mbele, akafungwa pingu na kulazwa chini kama wenzake.

§§§§§

“Inspekta!” Kamanda Amata aliita wakati alipokutana na Simbeye katika uwanja wa himaya hiyo, huku akishangaa huku na kule kuwaona wenzake wote wamepigwa pingu isipokuwa yeye na Chiba ambaye bado alimwacha ndani.

“Kamanda Amata! Pole kwa kazi na janga hili,” akampa pole huku akimpa mkono.

“Asante Inspekta, tunafuga mashetani nchi hii Inspekta, naomba vijana kama watano hivi na wewe mwenyewe, pamoja na mama yangu muache huru hakuna baya hapa tupo kazini, tuingie ndani ya jengo hili, tupite na muone wenyewe mchezo wa kuwapa watu viwanja bila kujua nia na malengo yao,” Kamanda alilalama. Madam S na Jasmine wakafunguliwa pingu zao, Scoba naye alkadhalika.

“Usishangae hawa ni watu kama wewe!” Inspekta alimwambia mmoja wa polisi ambaye alishangaa amri anayopewa ya kuwaweka huru watu hao.

Muda si mrefu, vijana watatu wakaingia ndani ya himaya hiyo wakiwa na suti nadhifu, mach yao yakiwa yamezibwa na miwani nyeusi, hakika walikuwa watanashati na nyuma yao aliwafuata mzee wa makamo mwenye mvi kadhaa kichwani mwake.

“Karibu sana Bwana Hosea, nafurahi umefika,” Inspekta alimkaribisha wakapeana mikono kisha wote wakaongozana kuingia katika jingo hilo.

Hakuna aliyekuwa akiongea, kila mmoja alikuwa makini kutazama kila kilichopo ndani humo, hakuruhusiwa mtu yeyote kugusa chochote kwa mikono uchi.

Chiba aliliongoza jopo hilo baada ya kukutana nao humo ndani, akawaingiza chumba cha mawasiliano, jopo hilo likabaki hoi.

“Tazama huu mtambo, unanasa habari kutoka ofisi zote za serikali, simu zote za kiofisi kuanzia za Rais na watu wake zote zinanaswa hapa, ona hii kompyuta ni kubwa sana inafanya mambo mengi sana, inanasa picha kule Uwanja wa Ndege, nah ii kama unavyoona inaonehsa mazingira yote ya Ikulu,” Chiba alikuwa akieleza.

Hosea akabaki kajishika kiuno, taratibu jasho lilikuwa likimtiririka.

“Nani mmiliki wa jumba hili, na alikuwa na lengo gani na Taifa hili?” akauliza, lakini wote walikuwa hawana jibu.

“Hatujamaliza, twendeni huku chini, naomba muwe na roho kavu kwa unyama uliopo huku,” Chiba akawaambia kisha akawafikisha ‘Kuzimu’, “Hapa ndipo wanapotumia kuua wabaya wao, mnauona ule mwili, mnaweza kuutambua, Mkuu?” akauliza. Hosea na vijana wake wakauendea na kuuangalia vyema, wakaugeuza huku na huko.

“Hapana simfahamu huyu,” Hosea akajibu.

“Ni mwandishi anayetafutwa na jeshi la Polisi kwa miezi mingi sasa, ameuawa mbele ya macho yangu,” Chiba akawaeleza.

“Chilese Zuberi,” Inspekta Simbeye akataja jina la Mwamndishi huyo, akachuchumaa kumwangalia vizuri na jeraha baya la risasi likiwa limeharibu kabisa sehemu ya nyuma ya kichwa chake.

Walipotoka hapo wakaelekea kwenye chumba kingine, na kukuta miili ya watu watano iliyofungwa kwa kuning’inizwa. “Unyama gani huu?” akajiuliza Hosea. Wakatazama mwili mmoja baada ya mwingine na kuitambua miili ile kuwa ni ya watu ambao walipotea katika mazingira ya kutatanisha na hawakuonekana tena, mmoja wao akiwa Mwanasiasa machachari kabisa.

“Nimegundua kitu,” Simbeye akasema huku akiwageukia wenzake.

“Nini Inspekta,” Hosea akauliza.

“Kutokana na watu tuliowakuta humu wakiwa marehemu, na mikasa yao ambayo jeshi la polisi lilichukua kama vyanzo vya upotevu wao, kuna mtandao unaofanya kazi hii,” Simbeye akasema.

“Yeah, upo sahihi, siku zote wanalaumiwa Usalama wa Taifa pindi miili hii ikiokotwa haina kuchwa au meno, lakini hii nyumba ya nani? Lazima ukweli ujulikane,” Hosea akaongeza. Walipomaliza kukagua kila kona mle ndani wakatoka nje na kukuta tayari jeshi la Polisi limefika zaidi na waandishi wa habari kama kawaida yao walikuwa wametanda nje wakijaribu kupata habari hii na ile.

Madam S, Chiba, na Jasmine wakaingia kwenye gari maalum iliyokuja hapo, iliyofunikwa kwa vioo vyeusi, bila kupoteza muda ikaondoka eneo lile. Kamanda Amata na Scoba walibaki pamoja na vijana wa Polisi kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa. Akiwa kafuatana na vijana wawili wenye silaha waliingia vyumba vya chini na kupita ile milango iliyoonekana kama njia waliyotorokea wale mabwana, walitembea katika njia tofauti, moja ya njia hizo alipia Kamanda Amata na kijana mmoja wa Polisi mwenye silaha, njia nyingine aliingia Scoba na kijana mwingine nay a tatu aliingia Inspekta Simbeye na kijana wake. Cha kushangaza njia hizo tatu hazikukutana, kila moja ilikwenda kutokea mahala pake, na zilitokea kwenye nyumba tatu tofauti, utata. Mara tu baada ya hilo, uchunguzi mkali juu ya nyumba hizo, umiliki wake na uhalali wa kuwa hapo uliendelea; Mjumbe wa shina na Mwenyekiti wake walikuwa katika hali ngumu ya kuhojiwa  hili na lile. Walipopata majibu ambayo kwayo yaliridhisha wakawaacha na kuondoka zao.

 

SHAMBA –

baada ya siku 3

MADAM S, CHIBA, JASMINE, SCOBA, GINA NA KAMANDA AMATA wote walikuwa wameketi katika meza kubwa ya duara, kila mmoja mbele yake alikuwa na kabrasha lililojaa makaratasi. Walikuwa na majeraha ya hapa na pale, Gina bado alikuwa akiendelea kuuguza jeraha lake lakini sasa akiwa chini ya uangalizi wa Dkt. Jasmine.

Ukimya ulichukua nafasi kwa kila mmoja, walikutana tena katika meza hiyo ambayo daima wakikaa hapo basi ujue kuna maamuzi magumu ya kufanya. Gina alijigeuza na kujiweka vizuri kitini kwake huku mikono yake ikiwa juu ya meza na sura akiwa ameikunja kidogo.

“Pole sana Gina,” Madam S alimpa pole mwanadada huyo, akajikohoza, “Niliwaita siku tano zilizopita tuonane kwa kikao cha dharula lakini baadae nikagundua kosa nililolifanya, anyway, haina haja ya kuljadili bali tuangalie lile ambalo sasa ndio nimewaitia kabla ya kutazama lile nililotaka niwaeleze siku tano zilizopita ambalo litamhusu Kamanda zaidi,” akaongeza, alionekana wazi hata uongeaji wake haukuwa ule wa kawaida kwani bado alihisi maumivu ya hapa na pale na alihitaji mapumziko. Kipindi hicho cha siku tatu, T.S.A wote walikuwa pamoja Shamba, huko Gezaulole, wakipumzika na kuweka mikakati mipya, hakuna aliyejua walipo isipokuwa wao wenyewe.

“Kurasa ya kwanza kabisa kuna majibu kutoka kitengo cha utambuzi wa alama za mikono na vidole,” madam Sakawaambia na kila mtu akapekua jalada lake na macho kuyatumbulia hapo.

“Is it?” Gina alikuwa wa kwanza kupayuka.

“Yes It is,” Chiba akadakia. Wote wakamtazama kwa jicho kali.

“Una maana gani?” Madam akamuuliza.

“Nilikuwa nasubiri tu haya majibu kama yataoana na yangu, nilipozifanyia crossmatch hizi alama za vidole ambazo nilizipata kwenye vitasa vya milango ya mwisho ya vile vyumba vya chini, licha ya hivyo tu niliwahi kupata baadhi ya picha zao sekunde chache kabla hawajatoroka lakini sikuwa nauhakika nao kwani siku hizi teknolojia imekuwa; mtu anaweza kutengeneza sura ya Rais na kuivaa, hivyo sikuliweka wazi hili, lakini niliwaona na kila mmoja alikuwa mahala pake, bila kinyago cha usoni,” akawaeleza kisha akanyanyuka na kuiendea droo ndogo akatoa flash na kuipachika kwenye kompyuta mpakato, kisha akawasha chombo cha kutolea picha ukutani na dakika moja baadae picha zilianza kuonekana.

Pancho Panchilio, mfanyabiashara mkubwa nchini, mshawishi wa mambo mengi ya kisiasa, mwenye asili ya Kihindi, watu wengi walimjua kama si kwa jina basi kwa sura. Mhindi huyu alilindwa kwa jinsi zote, hagusiki. Alikuwa tajiri sana mwenye malori makubwa ya kusafirisha, aliwekeza kwenye sekta ya usafiri hasa sekta ya anga. Kwa ujumla alikuwa mwema mbele ya Watanzania, alitoa misaada mingi hapa na pale, alijenga mahospitali, mashule na kusaidia watoto yatima sehemu mbalimbali za nchi.

Picha ya pili nayo ilitia shaka kwa wote angu waliposoma katika lile jalada na sasa wakiona ushahdi ule wa Chiba kwa njia ya picha. Kigogo mkubwa serikalini, aliyepewa dhamana na Wasakatonge kisha anawazunguka na kuwafanyia mambo yasiyoelezeka kwa maandishi. Maisha yanakuwa magumu kila uchwao ilhali wengine wakitunisha matumbo yao kwa njia mbadala za unyonyaji na ukandamizaji.

Picha ya tatu nayo ilikuwa yaleyale, Kigogo mwingine kwenye wizara Fulani naye alikuwamo ndani ya jopo hilo la udhalimu.

Haikuishi hapo, Chiba kutoka katika Hard Disk aliyoichomoa katika ile kompyuta yao, alifumua majina mengine ya watu mbalimbali ambao kila mwezi huchukua mgawo wa pesa lukuki kwa mambo yao binafsi, wapo viongozi wa juu, wa kati na wa chini; si wanasiasa tu hata wafanyabiashara nao walikuwapo tena wengi.

“Inatosha!” Madam akamwambia Chiba, naye akazima ule mtambo wake.

“Sasa nataka operesheni ianze mara moja, taarifa tayari zipo panapohusika, lakini Pancho Panchilio akamatwe mara moja, pamoja na hawa vigogo wawili. Leo hii wanatakiwa kuwa pale kituo cha kati kwa mahojiano zaidi.

KATIKA JENGO NYETI LA SERIKALI

“Boss kuna mgeni anataka kukuona,” sauti nyororo ya Katibu Muhtas ilipenye kwenye sikio la Mheshimiwa Sikotu Sambwene, mmoja wa watu wazito na ‘vingunge’ katika Serikali.

“NIlikwambia sitaki kuonana na wageni au hukunielewa?” Sikotu akauliza kwa ukali, “Mwambie sina muda wa kuonana na watu sasa; aje mwezi ujao,” akaongeza kuongea kwa ukali uleule. Akiwa bado katika kumfokea huyo Katibu wake; mlango ulifunguliwa na Madam S akajitoma ndani mzima mzima na kusimama kando.

“Mgeni wako ni mimi,” akamwambia Mh. Sikotu. Mheshimiwa Yule alijkuta katika wakati mgumu, alijitupa kitini na kumtazama mwana mama huyo aliyeingia kibabe katika ofisi hiyo.

“We; nenda,” akamwambia Yule Katibu wa Mheshimiwa.

“Unafuata nini hapa?” Skotu akauliza.

“Sina jibu la kukwambia ninachokifuata, maana bila shaka unajua ninachokifuata kwako, nina swali moja tu ambalo ukinijibu shida yangu itakuwa imeisha,” Madam S aimwambia Sikotu huku akiwa kasimama mbali kwa tahadhari.

Mhesimiwa Sikotu akajifuta jasho ilhali mashine ya kupoza hewa iikuwa bize ikifanya kazi hiyo, akaweka kitambaa chake ndani ya koti lake na kumtazama mwanamama huyo aliyesimama mbele yake.

“Unasemaje?” akauliza.

“Unafahamu nini au kipi juu ya jumba kubwa la kifahari lililoko Kerege kitalu namba KG/BY 1230p?” akauliza Madam S. Sikotu akabaki kaduwaa, hakuwa na jibu. Madam S hata kabla hajapewa jibu hilo akatupa swali lingine.

“Unajua nini juu ya mwandishi wa habari mashuhuri aliyepotea miezi miwili nyuma?”

“Hivi we mwanamke una kichaa!” Sikotu akang’aka huku akiwa wima macho yamemtoka.

“Na ukichaa wangu ndio umenifikisha hapa leo, ulifikiri ukijiziba sura mbele yangu sintokujua? Kwa taarifa yako kutokana na kazi yangu, sauti zenu wote nyie nimezikariri, hukuweza kujificha mbele yangu ulipokuwa ukiongea, Sikotu, kiongozi mwenye dhamana, unajishusha hadhi kwa tama yako ya pesa mzee, utastahafu kwa fedheha baba, hebu jiangalie hapa,” Madam S akamtupia picha kumi na tano zinazomwonesha ndani ya jingo lile ambazo zilinaswa kwa kamera za usalama. Sikotu alizitupia jicho na machozi yakaanza kumtoka.

“Mwisho wa ubaya ni aibu, na mshahara wa dhambi mauti,” Madam S akainua akakusanya picha zake na kuzirudisha mkobani.

“Tutaonana mahakamani,” akageuka na kuondoka, akaufunga mlango nyuma yake na nukta hiyo hiyo vijana wawili waliovalia sare za jeshi la polisi waliingia ndani ya ofisi ile, pingu ikawekwa mezani.

“Siwezi kwenda popote, kwanza ni ninyi ni nani? Nani kawatuma? Ninyi mna kibali cha kunikamata mimi? Mnaitaka kazi yenu au?” Sikotu alikuwa kama akiweweseka, akavua koti na kulitupaa kando, mwili wote ulikuwa umelowa kwa jasho kana kwamba kamwagiwa maji.

Mmoja wa wale askari akatoa waraka ulioidhinishwa kukamatwa kwake, akamwonesha kwa mbali huku akimkatalia kuushika kwa mikono yake. Sikotu hakuwa na la kufanya aliahangaika, Yule askari kijana akamsogezea pigu ikiwa wazi ajipachike mikono yeye mwenyewe. Sikotu akavuta saraka katika meza yake akaitoa bastola iliyokuwamo ndani yake, wale askari wakaweka silaha zao tayari wakimwamuru kuweka chini bastola yake. Akaitumbukiza kinywani kwa minajiri ya kujilipua.

“Weweeee aaacchhhaaaaa!!!” mmoja wa askari akapiga kelele na wakati huo huo mlio wa risasi ulisikika na Mheshimiwa Sikotu akabwaga chini huku damu zikicafua vibaya shati lake, bastola yake ikitupwa mbali.

“Ha ha ha ha haujafa kiongozi lazima ufike mahakamani,” Sauti ya Chiba ilisikika nyuma ya wale askari, wakageuka na kumwona kijana huyo aliyekuwa ndani ya suti nadhifu akiiteremsha bastola yake. Chiba alipiga mkono wa Sikotu kwa risasi yake na kuumiza vibaya kiganja chake kabla hajajilipua.

WAKATI HUO HUO –

Ofisi nyingine ya serikali

“Una la kujitetea hapo?” Scoba na Gina walisimama mbele ya meza kubwa wakimtupia swali hilo mtu mkubwa mwenye tumbo la maana akilikuna kwa mbali. Alionekana wazi kuchanganyikiwa kwa hilo, hakuwa na la kujitetea.

“Gina, mtie pingu!” Scoba alitoa amri na Gina akaitekeleza. Gavana wa benki kuu ya Tanzania, Dkt. Shekibindu akavikwa pingu na kutolewa ofisini mpaka nje kwenye gari ya polisi, na moja kwa moja akapelekwa kituo cha kati kwa mahojiano zaidi.

WAKATI HAYO YOTE YAKITUKIA…

Kamanda Amata alisimama mikono yake akiwa kaikutanisha nyuma ikining’iniza bastola yake ndogo ya Kiitaliano ijulikanayo kama Beretta, huku usoni kajivika miwani safi nyeusi, suti yake ilimkaa vyema mwilini, kiatu chake kilichong’azwa kwa kiwi hakikuongopa kuonesha taswira ya kila kilichokaribu.

“Hajaonekana kabisa ofisini,” Msichana aliyeonekana kama Katibu wa Pancho Panchilio alimjibu Amata kwa swali aliloulizwa sekunde chache zilizopita.

“Tangu lini?” akauliza tena.

“Ana siku nne sasa, mara ya mwisho aliondoka hapa majuzi akiwa kama aliyechanganyikiwa, sikujua anakwenda wapi na wala hakusema, tangu hapo hakurudi tena,” Yule msichana akaendelea kueleza.

“Unapajua nyumbani kwake?”

“Hapana, mimi ni mfanyakazi tu huwa tunaonana hapa ofisini bas,” akajibu.

“Ok, naomba niingie ofisini kwake,” Kamanda akaomba.

“Pamefungwa, na funguo ni moja tu anayo mwenyewe,”

“We niruhusu au nikataze,” Kamanda akasisitiza.

“Sawa ingia, mi nakwambia hayupo,” Yule mwanadada akaendelea kujibu.

“Usihofu, mimi ni afisa wa polisi,” akamwonesha kitambulisho bandia cha upolisi. Akauendea mlango na kuufuangua kwa jinsi zake zilezile. Ilikuwa ofisi pana yenye kila kitu ndani yake, hakukuwa na mtu, akaiendea simu na kuitazma kisha akabonyeza kitufe cha kuiruhusu itoe ujumbe wowote uliopo.

“…Mheshimiwa booking yako imekamilika na tiketi yako tutakutumia soon katika email yako… enjoy your flight…”

Akili ya Kamanda ilisimama ghafla, “Katoroka?” akajikuta anajiuliza bila kupata jibu, akaiendea kompyuta ya mezani na kuipekua hapa na pale mpka alipopata email ya Panchilio ambayo ilikuwa wazi bila kufungwa akapekua e mail zilizoingia saa sabini na mbili zilizopita. Ilikuwa ni hiyo email ya tiketi ya ndege iliyoondoka saa arobaini zilizopita na ndege moja ya shirika la huko Uarabuni, safari yake ilionekana kuishia Bangalore, India.

“Hayawani huyu kaniwahi,” akawaza huku akitoka na nakala ya ile ytiketi aliyoitoa kwenye mashine kule ndani.

“Unaitwa nani?” akmwuliza Yule binti alipokuwa akitoka.

“Naitwa Ruth,”

“Mwenyeji wa wapi?” akamwuliza.

“Wa Arusha,” akajibu.

Kamanda Amata akamtupia jicho la wizi huku akiiondoa miwani yake usoni na kutuza muono wake juu ya kifua cha binti huyo kilichojaa vyema, matiti yaliyowekwa ndani ya sidiria yakitamanisha kila lijari. Kamanda akameza mate, akajikohoza, akaingiza mkono mfukoni na kutoa kadi ndogo ya kibiashara akampatia.

“Tuonane jioni ya leo, Hotel ya Land Mark, saa mbili kamili usiku,”

Ruth akamtupia jicho kijana huyo aliyekuwa akiipachika tena miwani usoni mwake, akaibetua midomo yake na kuuma chanda chake kwa meno ya mbele.

“Ok!” akaitikia. Kamanda Amata akauona mshtuko wa wazi mbele yake kutoka usoni mwa Yule dada, akageuka nyuma na ndipo alipogundua kuwa hawako peke yao, watu wawili walisimama nyuma yake, waliojazia kimazoezi. Akageuka na kupita katikati yao akaondoka na kuwaacha. Alipolifikia gari lake akasimama na kugeuka nyuma, akawaona wale vijana wamesimama mlangoni wakimwangalia. Akasimamisha tax na kuondoka huku akiliacha gari lake palepale.

 HATIMA

“Pancho Panchilio ametoroka,” kamanda alimwambia Madam S walipokutana katika mgahawa wa Steers.

“Atapatikana tu, na lazima tumpate iwe kwa mvua iwe kwa jua,” Madam akajibu.

GEREZA LA UKONGA

Saa tatu baadae

“Mmefurahi sasa sio? Maana rafiki zenu wamekuja kuungana nanyi, msijali tunamleta na Yule Gabacholi, tunamfuata hukohuko India,” Madam S akamwambia Kanayo na Mahmoud Zebaki waliokuwa wakitumikia kifungo chao.

“Tunakata rufaa!” Kanayo akajibu.

“Kateni tu kwani nimewafunga kamba, hiyo ni haki yenu kimsingi na kikatiba,” Madam S aliwajibu huku akinyanyuka na kuondoka.

Kanayo akasonya kwa gadhabu, “Our day will come!”(Siku yetu inakuja) akamwambia Madam S. akageuka kumtazama Kanayo O Kanayo, “Yes, will come soon, we shall face each other in the battle field,” (ndiyo inakuja punde tu, tutaonana kwenye uwanja wa mapambano)

§§§§§

Aiwa chumbani kwake, alimtazama Gina aliyekuwa mbele yake na vazi jepesi la usiku, Amata alijikuta akipata shida maeneo ya kati kwajinsi mwili wa mrembo huyo ulivyokuwa ukiita. Gina akageuka na kumtazama.

“Vipi? Arts of War ni ipi kwa mi na wewe sasa?” alimuuliza huku akijilaza ktandani na kuruhusu sehemu kubwa ya mwili wake kujiachia wazi.

“…mwili huo uliookotwa kando kando ya pwani ya Coco ni wa msichana wa kati ya miaka 25 na 30. Kamanda wa Polisi mkoa wa Dar es salaam Ndugu Sekuru, amethibitusha kutokea tukio hilo na uchunguzi unaendelea kuwabaini waliofanya mauaji hayo…”

Sauti ya Mtangazaji wa TV ilimtoa Kamanda Amata katika kifua cha Gina na kutupia macho katika kioo hicho.

“Shittt!” akang’aka, “Wamemuua Ruth!” akaongeza huku akisimama.

“Ndio tatizo lako, ukisikia mwanamke kauawa unahuzunika lakini mwanume unapotezea, mwanaume Malaya wewe!” Gina akalalamika huku akikaa kitandani.

“Gina, huyu ni sekretari wa Pancho Panchilio,” akamweleza.

“What? Usinambie,” Gina naye akahamanika.

“Kwa nini wamemuua msichana mzuri kama Yule, masikini Ruth!”

 

 ∞ ∞ MWISHO ∞ ∞

Richard R. MWAMBE

jamvilasimulizi@gmail.com

 

NB

Riwaya hii ni namba 2 katika mfululizo wa NYAYO ZA PAKA, nunua sasa namba 1 na namba 3 uburudike kwa kuunganisha matukio.

Bado haijahaririwa
Share

Leave a Reply

Translate »
error: OPS! Content is protected !! Imezuiwa