MAGNUM 22 – official trailer

 

 

 

I

 

SEHEMU FULANI HUKO AFRIKA MAGAHARIBI

MACHO YANGU yalikuwa mazito sana kiasi kwamba iliniwia ngumu kuyafumbua. Haikuwa rahisi kwangu, nilijaribu kutumia nguvu ya mwisho niliyonayo kuona japo nuru, haikuwezekana. Fahamu zilipokaa sawa nikahisi maumivu makali sana kisogoni, nikajaribu kuinua mkono ili japo kushika eneo hilo la mwili. Damu! Damu iliyoanza kuganda na kufanya kama buja zito iligandamana na nywele zangu, nilipopapasa zaidi nikagundua kuwa nina mpasuko au niite mchaniko.

Bado giza nene liliyafanya macho yangu yashindwe kuona chochote, mboni zilifunguka na kufunguka lakini kuiona nuru ilikuwa ndoto.

Niko wapi? Nikajiuliza, hakukuwa na wa kunijibu zaidi ya mvumo wa giza kuyapa taabu masikio yangu. Maumivu ya jeraha langu la kisogoni yakaanza kuhisika kwa mbali, nikahisi kama moyo umehamia hapo kwa jinsi ulivyokuwa ukipwita. Kila nukta ya sekunde iliyopita, maumivu yake yalizidi nikaanza kuhisi kero, nikajaribu kujigeuza, kichwa kizito, nilipotumia nguvu zote kujigeuza nikahisi kugonga vitu vigumu kama kuni zilizorundikwa lakini kwa mpangilio maalumu. Nikatulia kwa sekunde chache huku nikijaribu kuvuta hisia kutambua ni nini nimekigonga. Nikainua mkono na kupapasa, sikujua kama nimeshika fimbo au kota la kutungulia embe. Nikapapasa ka sentimeta kadhaa, mara nikahisi kitu ambacho sikukitegemea, mwisho wa kile nilichokipapasa nikahisi nimeshika kitanga cha mkono wa mwanadamu, nikakipapasa vyema nikajiridhisha kuwa ndiyo ni kitanga cha mkono lakini kimebaki mifupa tupu.

Nikachezesha mguu wangu nao ukagonga vitu vingine kama hivyo, ndipo nikagundua kuwa hata maumivu mengine ninayoyasikia ni kwa sababu nimelalia mifupa ya binadamu iliyojaa katika eneo hilo.

“Shiiiit!!!!” nikang’aka kwa sauti, kisha nikajiinua kuketi, kiuno changu nacho kikagosha kwa nguvu. Hapo nikagundua kuwa hta kiuno nacho kimepata tabu kidogo. Nikavumilia na kufanikiwa kuketi, kila nilipogusa na kushika kulikuwa na mifupa tu, mafuvu nayo niliyapapasa kama vifuu vya nazi. Sikuweza kuona kwa macho yangu kutokana na giza nene katika eneo hilo. Kila sekunde iliyopita nilizidi kuipata hali halisi ya ndani humo, harufu ya mauti ilitapakaa.

Wakiua huwa wanatupa maiti humu! Nikawaza.

Ina maana hata mimi walijua nimekufa? Nikajiuliza. Zaidi ya hapo sikuwa na lingine la kufanya zaidi ya kuutafuta kama ni ukuta au ni kitu gani kinachofanya miimo ya eneo hilo. Maumivu yalinizidi katika kisogo change kiasi kwamba iliniwia ngumu kuvumilia. Nikatambaa kwa shida nikiparamia mifupa na skeleton za binadamu, na kwa sababu nilikuwa sioni niendako nikajikuta na jigonga kwenye ukuta. Nikatulia na kuanza kuupapasa huku nikiugulia kwa maumivu. Ukuta ulikuwa laini na wa kutereza, wenye vitu kama marumaru kwa jinsi vilivyounganishwa, nikaupapasa na kufanikiwa kusimama lakini sikufikia juu, parefu.

Kaburi! Nikawaza na hapo nikaanza kupata kizunguzungu kwa sababu sikuwahi kuingia kaburini tangu nizaliwe, lakini mara hii nimezikwa mzima mzima? Nikajikuta naanguka kwa nguvu na kufikia juu ya miili iliyooza zamani maumivu yake hasa sehemu za kisogo changu yalizidi lakini nikazidi kuidhihirishia hali hiyo kuwa mimi ni mwanaume.

“Chwaaaa!!!! Chwaaaa!!!!” nikasikia mtu akipiga chafya, hii sasa ikanifanya nishikwe na hofu kuu. Pamoja na ukakamavu wangu na ujuvi wa upiganaji na kujilinda, nilijikuta Napata woga wa ajabu uliotiririka kutoka utosini mpaka unyayoni, moyo wangu ulikwenda mpio kama saa mbovu, macho ya kanitoka pima maana sikujua kama ni maiti imepata uhai, au ndiyo moja ya vitisho vya humu ndani au inakuaje, maana kwa mtindo huu mtu unaweza kufa kihoro. Tatizo kubwa sikuwa namwona mtu huyo au kiumbe hicho maana giza lilikuwa nene sana, joto nalo lilikuwa kali mno, nikajiinua na kutafuta kona ya ukuta huo kwa taabu nikaipata na kujiegama hapo nikisubiri hatima yangu.

“Kheeeee!!!!!” ile sauti ikakoroma, nikajiweka sawa, sasa nilijua nipo kwenye kona ya kaburi hilo, hata kama nitashambuliwa, basi shambulizi litatoka ndani ya nyuzi arobaini na tano tu, ningeweza kukabiliana nalo hata kama ni giza. Nilianza kuvuta hisia ambazo nilifundishwa na Master wangu wakati nipo Japan kwenye mafunzo magumu sana ya Karate huku nikiwa nimefungwa kitambaa usoni, jinsi ya kumhisi adui yuko upande gani, kusikiliza mgongano wa hewa na kujua adui anatumia pigo gani, kumwona adui ndani ya hisia ya sita.

“Chwaaaa! Khaaaaa!!!!” chafya nikasisikia tena na mkhoromo ukafuatia, safari hii sikuogopa, ila nilikuwa nimelowa jasho na hewa nzito ndani humo ilianza kunishinda taratibu na kujihisi kuchoka. Njaa nayo ikaendelea kuleta upinzani mkubwa. Mara ule mkhoromo ukaendelea sasa ukaanza kuyasumbua masikio yangu, nikagundua huyo ni mwanadamu ambaye amefika dakika za mwisho za uhai wake.

Anakufa? Nikajiuliza, kwa kuwa nilishajua ni upande gani alipo huyo akoromaye, nikainuka haraka na kaukanyaga mifupa na miili mikavu mpaka pale nilipohisi, naam ndipo. Nikajikuta nimepiga magoti na kuanza kumtikisa huyo mtu, mikono yangu nikahisi imeshika kitu kama koti la suti, nikamtikisa na kumtikisa, yeye akazidi kukoroma tu. Nikampapasa usoni nikahisi kuwa ana majeraha mengi na ya kutisha kani nilihisi nashika mtu asiye na macho. Yule mtu aliye kufani akanishika mkono kwa nguvu zake zote na kuupachika katika mkanda wa suruali yake kisha yeye mwenyewe akatulia kimya kabisa, mkono wake ukalegea, nikajua tayari andipela.

Hapo nikajikuta kwenye hofu kuu, hofu ya kifo, nikajikuta nimesahahu mateso yangu yote, na mawazo yangu yakawa juu ya mtu huyo. Akili iliporudi, nikaanza kumsachi kuanzia mifuko ya koti, shati lake na suruali. Katika mfuko wa ndani wa shati nikatoa kijitabu kidogo sana, sikuweza kukisoma kwani hapa nilikuwa natumia hisia tu kutambua vitu, katika viatu vyake baada ya kumvua nikatoa karatasi ambayo sikuweza kujua ni karatasi ya nini au gani. Nikakumbuka kuwa mtu huyu alipoushika mkono wangu kwa nguvu aliuweka kwenye mkanda wa kiunoni.

Inawezekana kuna ujumbe katika mkanda huo! Nikawaza na kuanza kuufungua kiunoni mwake nikautoa na kuushika mkononi. Ni mkanda tu wa ngozi wenye chuma kikubwa cha kuufungia kutoka upande huu kwenda huu.

Ujumbe gani upon a mkanda huu? Nikajiuliza, sikuwa na jibu, ambaye ningemuuliza, ameshakufa, sasa nafanyaje. Maumivu niliyoyasahau ghafla nikaanza kuyahisi upya kwa nguvu, joto kali, shati lote likawa chapachapa kwa jasho na suruali pia ikaanza kuwa katika hali hiyo. Nikatia kile kijitabu mfukoni na ile karatasi.

Vitanisaidia nini sasa, labda kama ningepata nuru ya kusoma au kuona ni vitu gani… nikajiambia kwa sauti ya moyoni kisha nikajiegemeza katika ukuta upande mwingine. Hapo nikahisi naishiwa nguvu kabisa, pumzi nazipata kwa taabu sana nikajua sasa muda wangu umekwisha, nikafunga mikono na kuanza kusali sala zangu za mwisho. Nikaomba kwa Mungu wangu, msamaha kwa yote niliyoyakosa, lakini nikamwachia kila kitu aamue yeye kwani yeye anajua kuwa yepi nimeyafanya kimakosa na yepi nilikuwa kazini. Japokuwa sikuwa nawaona wengine, kupitia sala zangu hizi nikawaomba msamaha wote.

Joto lilizidi kuwa kali, harufu nzito ya mauti ikaanza kuzisumbua upya pua zangu, giza nalo likawa adui mkubwa. Nikatulia kimya nikiwa nimejikunyata huku mikononi nikiwa nimeukamata mkanda wa yule marehemu aliyenitangulia. Kutoka moyoni nikahisi sauti ikinitaka kuufunga mkanda ule kiunoni, nikaipuuzia lakini baadae ikazidi kunisumbua, nikaamua kuitii hisia hii kwani ni moja ya kazi yetu kutii hisia ya sita na ndiyo intelijensia yenyewe. Nilikuwa naishiwa nguvu, nikaupachika kiunoni tu bila kuuweka kwenye lupsi za suruali kwani sikuwa na muda na nguvu hizo. Nikachuku mwisho huu na huu na kuukutanisha kisha nikaupachika kwa nguvu ili meno yake yaumane. Sekunde ileile nilipoupachika na yale meno kuumana, nikasikia mlipuko kutoka upande mmoja wa ukuta, vumbi likatawala ndani ya kaburi hilo, nikakohoa kwa nguvu sana, hali ilipotulia nikaona tundu la ukubwa wa mdomo wa pipa katika ukuta wa kushoto kwangu. Mwanga hafifu ukapenya ndani nikajua kuwa kwa hapo ningeweza kujiokoa, sasa ndani humu kulikuwa na mwanga ambao haukuweza kunionesha kila kilichomo bali angalau nilijuwa kuwa ukuta ni wa marumaru nyeupe kama za chooni, kwa shida niliona kweli miili mingi iliyokauka na mifupa isiyohesabika, sikuijali bali nilijijali mwenyewe kwa wakati huo. Nikajivuta mpaka kwenye lile tundu, lilikuwa refu kwenda chini. Na chini kabisa lilionekana kuelekea upande mwingine.

Ina maana hapa nipo juu au wapi? Nikajiuliza na kisha nikakamata bomba moja ndani ya mfereji au bomba hilo nikajitoa na kujitumbukiza, bahati mbaya lile bomba halikuwa na imara likakatika.

“Aaaaaaaaiiiiiiigggghhhhh!!!!” nikajikuta napiga kelele, nikajibamiza katika kuta za shimo hilo na kujigonga vibaya kisogoni. Giza kuu likanifunika, huku nikihisi upepo mkali ukipita masikioni mwangu kisha ukimya mkuu ukanitawala.

 

 

II

 

 

SHAMBA – SAFE HOUSE

HALI YA SINTOFAHAMU ilitanda ndani ya afisi hii ya siri, kila mmoja kichwani alikuwa anawaza lake, hakuna aliyekuwa akiongea na mwenzake. Meza, ambayo daima huwa imejawa na watu hawa sita leo ilikuwa tupu, ni taa inayoning’inia juu yake na makabrasha kadhaa ndivyo vilibakia mezani hapo, hakukuwa na mtu. Katika chumba kimojawapo ndani ya jengo hilo, Madam S alikuwa ameketi kimya kabisa, peke yake, meza ilikuwa na kabrasha moja tu na kiti cha mbele yake hakikuwa na mtu yeyote. Kalamu ilikuwa ikizungushwa katika vidole vya mikono yake huku macho yake yakiwa yamefumbwa kwa utulivu. Mwanamama huyu, mzoefu katika maswala ya intelijensia hupenda kujifungia ndani ya chumba hiki pindi mambo yakiwa magumu. Nywele zake zilionekana wazi kujawa mvi chwe! Ngozi ya uso wake nayo ilionesha wazi kuwa uzee umebisha hodi, kama si pesa basi tayari tungemwita mzee ila kwa sasa tumwite ‘mama mtu mzima’, alijua kujitunza.

Akiwa katika ukimya huo akagutushwa na simu iliyokuwa ikiunguruma kwa fujo kwenye meza yake, akainyakuwa na kuitazama kwenye kioo.

‘Unknown Caller ID’

Ilijiandika namna hiyo, kabla hajaipokea akatuliza moyo kwanza maana ulikuwa ukienda mbiyo. Simu hii ni ile ambayo huwa haipigwi ovyo, ni watu wachache sana hupiga, lakini kila apigaye namba yake huonekana, ni mara hii tu ilijiandika neno hili. Akabonya kitufe fulani pembeni ya simu hiyo na kisha akaiweka sikioni, bila kuongea.

“Selina!” upande wa pili ukaita, kwa sauti hiyo tu akatambua kuwa anayepiga si mwingine ni Inspekta Simbeye.

“Mzee vipi? Mbona unaniweka roho juu kwa kuficha ID yako?” akamuuliza.

“Oh sorry!”

“Enhe nambie…. Kuna lingine mtaani?” Madam S akauliza.

“Hakuna lingine, nilitaka kujua kama umepata lolote kuhusu kazi yetu,” Simbeye akamwambia Madam S.

“Hapana! Bado tumechanganyikiwa, ni saa la 120 sasa hatujajua kinachoendelea,” Madam S akajibu.

“Nimepata ujumbe mwingine hapa…”

“Unasemaje…”

“Ataendelea kuua viongozi wa Afrika mpaka AU isalimu amri,”

“Kichaa… kichaa! Si bure… bado tunamfanyia kazi tutamnasa tu!” akaongea kwa jazba huku mwili wake ukitetemeka kwa mbali.

“Kwa lolote tutakuwa tukiwasiliana,” Inspekta Simbeye kutakamaliza na kukata simu. Madam S hakukata simu haraka badala yake akasubiri kidogo na hapo akasikia ‘kliki’ nyingine mbili za kukata simu hiyo. Hapo Madam akaju moja kwa moja kuwa simu hiyo imesikilizwa na watu wawili zaidi yake, ni akina nani hao? Akatoka ndani ya chumba hicho na kuelekea kile cha mawasiliano ambako alimkuta Chiba na Jasmini wakiwa wametingwa na kufanya hili na lile kwenye kompyuta ndani ya chumba hicho.

“Chiba!” akaita.

“Yes Mom!” Kijana huyo akaitika na kuacha kile alichokuwa akifanya.

“Umesikiliza simu niliyokuwa napigiwa sasa hivi?” akamuuliza.

“Yes, na nimeirekodi, nimekosea?” akauliza.

“Hujakosea, vipi hujagundua uwa simu hiyo imesikilizwa na watu watatu yaani mimi, wewe na mwingine zaidi?” Madam akauliza.

“Hapana!”

“Usiwe unawahi kukata simu, daima subiri sekunde kadhaa baada ya mpigaji kukata unaweza kugundua kuwa kuna mwingine anakusikiliza…” akamwambia.

“Shiiiit! So?”

“Hatuna budi kumtracy!”

“Sawa mama!” Chiba akajibu na kurudi kitini tena.

Madam S kutoka pale aliposimama, akavuta hatua na kuingia ndani kabisa ya chumba hicho, akavuta kiti cha akiba kilichokuwapo, akaketi.

“Gina yuko wapi?” akauliza.

“Ametoka, kaenda Uwanja wa ndege mara moja,” Jasmini akawa wa kwanza kujibu.

“Kuna la maana huko?”

“Aaaaannn naweza kusema yes au no ila ni maswala ya kikazi,” Jasmini akajibu tena.

“Ok! Tetesi yoyote Chiba…”

“Hakuna tetesi mama, nimejaribu mbinu zote nimeshindwa kumpata alipo, sipati signal ya GPS wala nini, hakuna kitu na sasa ni siku ya tano, huwa si kawaida….”

“Inamaanisha…”

“Man Down!” Chiba akamalizia.

“No! napingana na mawazo hayo, kinadharia ndiyo, ila kiuhalisia najua yule mwanaume ni mjanja anaweza akafufuka hata baada ya siku kumi, naomba tusiamini mpaka tutakapoupata mwili wake,” Madam akawaambia na kusimama.

“Call ya mwisho alikwambia nini na alikuwa wapi?” Madam akamuuliza.

“Alikuwa Freetown, na aliafikia katika hoteli ya kawaida sana ya Swiss Spirit,” Chiba akamwambia Madam.

“Inabidi kwenda kufuatilia Chiba, jiandae…” Madam akamwambia kijana wake.

“Mimi?”

“Ndiyo, wewe si ndiyo TSA 2?” Madam akamwambia huku akikiacha chumba kile.

“Come on!” Chiba akapiga kite na kuinuka, moja kwa moja akaingia chumba cha mazoezi na kuvua suruali yake na shati akavaa Karategi lake na kuanza mazoenzi makali kama kichaa. Alikuwa akijikunja na kupiga mapigo ya hatari huku akitoa kelele zenye mirindimo tofauti.

*   *   *

OFISI ZA MUDA ZA USALAMA ZA AU

Madam S alikunja kona kutoka barabara ya Haile Selassie na kuingi ile ndogo ya Ruvu, mwendo kama wa mita hamsini hivi akakunja kushoto na kuingia moja kwa moja kwenye geti lililokuwa wazi. Akaegesha gari katikati ya magari mengine ambayo yalikuwa hapo, akashuka na kuufunga mlango. Hatua zake fupifupi zikamfikisha kwenye mlango wa kawaida tu, akausukuma na kuingia ndani, hapo akakutana na mwanadada mrembo aliyekuwa nyuma ya kompyuta akiendelea na kazi.

Baada ya kusalimiana, mwanadada huyo akamwongoza mgeni mpaka chumba namba tano.

“Ni wewe tu unasubiriwa!” yule mwanadada akamwambia huku akimfungulia mlango na Madam S akaingia na kuchukua kiti chake. Ulikuwa ukumbi mdogo wenye viti sita na kati ya viti hivyo palikuwa na meza kubwa yenye umbo la yai. Nyumba hii iliyo chini ya Shirika la Nyumba la Taifa ilibadilishwa matumizi ghafla baada ya mkutano wa Baraza la Usalama la nchi huru za Afrika kuamua iwe hivyo kufuatia matukio ya kutisha yaliyokuwa yakiwakumba viongozi wan chi hizo katika maeneo tofauti ya bara hilo. Baraza la usalama katika kikao chake cha mwisho likaiomba Tanzania kuiweka ofisi hiyo nchini kwake kwa muda mpaka tatizo hilo litakapopatiwa ufumbuzi.

“Karibu sana Sellina!” Rais wa baraza hilo alimkaribisha.

“Asante nimefika!” akajibu na kuketi.

Kilikuwa ni kikao cha watu sita tu, na Madam S alikuwa ni mwanamama pekee katika jopo hili la wanaintelijensia hatari wa Afrika ambao kila mmoja kama si kustaafu basi alikuwa akiendesha Secret Services katika taifa lake kama ilivyo kwa Madam S.

“Karibuni wajumbe! Naomba kila mmoja afungue kabrasha lake na kupitia kilichomo humo ndani…” Rais wa baraza hilo ambaye pia aliteuliwa kama mwenyekiti wa tume hiyo ya usalama aliwataka wajumbe kufanya hivyo. Kila mmoja alichukua kama dakika kumi hivi kusoma kabrasha lake kisha wakafunga kwa nyakati tofauti.

“Ina maana haya mauaji yanaendeshwa na kikundi hiki au na mtu huyu?” Madam S akawa wa kwanza kuuliza.

“Ndiyo!” akajibiwa.

“Sasa kama mpaka picha yake tunayo tunashndwa nini kumkamata au kumuulia mbali?” akauliza tena.

“Swali zuri, baada ya uchunguzi wa awali kufanyika huyu amekuwa mtuhumiwa wa kwanza anaitwa Bwana Fadicky Al Habib, picha hii ilipigwa Mogadishu na askari wa jeshi la kulinda amani la AU baada ya kumshuku kutokana na mzungumzo yake…”

“Sina uhakika mwenyekiti,” Madam S akapinga, “kwanza tuangalie chanzo hasa cha mauaji haya na kwa nini yanafanyika, pia tutazama ujumbe ambao muuaji amekuwa akituma siku au saa chache kabla ya kutekeleza takwa lake…” akaunguruma na wanaume wote ndani ya kikao hicho wakabaki kimya.

“Hatutakiwi kuchukulia mambo haya kirahisi namna hii, maadam mmetaka taasisi ya intelijensi ya Tanzania ifanye kazi basi naomba msipokee taarifa nyingine kutoka upande wowote wa dunia, unless otherwise tutakuwa tunayumbishwa na kila anayetaka kufanya hivyo…” Madam S akaendelea.

“Cool down Madam Seline Mwenyekiti akamwambia na wajumbe wengine wakatikisa vichwa kukubali, “ipo hivi, katika siku saba hizi ambazo hatujapata taarifa yoyote kutoka kwako, utaratibu wa siri ulifanyika na ndipo tukapata taarifa hii, hivyo hatuna budi kufanyia kazi hii na siyo nyingine yoyote. Kumbuka kikao chetu cha mwisho tulikubaliana kuwa kila siku tatu tupeane taarifa, lakini mpaka sasa hatujapata zaidi ya zile tatu za kwanza…” Mwenyekiti akasema na kutulia kidogo.

“Naunga mkono asemalo mwenyekiti, mi’ nafikiri kama tulivyofikiri, tuunde timu nyingine ya wapelelezi watakaofikisha suala hili mwisho, maana wapelelezi wa Tanzania wapo kimya…”

“Si kwamba tupo kimya, tunafanya kazi, na hizi taarifa si ‘confidencial’, wala si ‘secret’ bali ni ‘top secret’ hivyo hatuwezi kuzitoa ovyo isipokuwa kwa mtu mmoja tu, sasa tunaziweka pamoja na mtazipata as soon as possible!” Madam S akaliambia jopo la watu hao kutoka nchi tofauti za Afrika.

Ukimya ukatawala kwa nukta kadhaa kati ya wote sita, baadae kidogo mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ndiye rais wa Baraza la Usalama la AU akajikohoza na kuuvunja ukimya huo.

“Kwa hiyo unataka kutuambiaje?” akamuuliza mwanamke huyo.

“Mtapata taarifa kwani tumefikia hatua nzuri tu…”

“…No! imetosha, lazima tuunde jopo lingine la kufanya upelelezi huu…”

“Sawa, undeni, ni sawa tu! Maadam hata sisi kiongozi wetu mmoja ameuawa na watu hao, tutafanya upelelezi kama serikali kumsaka muuaji na ninyi muendelee, asante!” Madam S akazungumza huku amesimama, akafunga kabrasha lake na kuliinua tayari kwa safari.

“Unaenda wapi?” Mwenyekiti akamzuia.

“Kikao hakina maana kwangu, wacha niende nanyi muendelee na kazi yenu, mkiihitaji msaada mtatutafuta,” akamjibu.

“Kwa hiyo umesusa?” Mkuu wa idara ya usalama wa taifa ya Afrika Kusini akauliza.

“Yes! Naenda kuabort mission, hata nikikaa hapa nina machango gani?”

“Tunakuhitaji wewe, ila hatuihitaji timu yako…”

“Impossible!!!” akajibu kwa neno moja tu.

“Kaa chini, kikao kiingie awamu ya pili,” Mwenyekiti akaamuru.

“Awamu ya pili!” Madam akashangaa.

“Yes! Awamu ya pili, kuunda kikosi kazi kingine…” Mwenyekiti akajibu.

Kikao kile kikaingia awamu ya pili kama ilivyotamkwa na katika hii ajenda ilikuwa ni kuunda kikosi kipya cha upelelezi kitakachofanya kazi zake moja kwa moja chini ya baraza hili. Wapelelezi mashuhuri kadhaa kutoka nchi za Maghalibi na Kasakzini na Kusini wakawekwa pamoja, wengine hata walikuwa tayari wamestahafu, lakini kwa hili wakatakiwa kurudi kazini mara moja. Watu hao kwa idadi walikuwa watano wakatakiwa kufika Dar es salaam mara moja kila mtu kwa wakati wake na kupangiwa kazi.

“Nataka tukomeshe kabisa uhuni huu, tumeshapoteza viongozi watatu wakubwa Afrika ndani ya miezi sita, hatutaki hali hii iendelee hata kidogo, yoyote anayehusika ashughurikiwe tukianza na huyu kwenye hii picha!” Mwenyekiti akaliambia jopo baada ya kuwa tayari kikosi kimepatikana. Madam S akabaki kimya, hakutaka hata kuchangia neno kwa jinsi alivyoshikwa na hasira na maamuzi hayo. Hasira yake ilikuja mara mbili; kwanza kwa kusitisha operesheni nyingine, na pili mpaka dakika hiyo bado hajui kijana wake yuko wapi na katika hali gani.

“Selina unasemaje katika hilo?” Mwenyekiti akauliza baada ya kuwauliza wengine wote.

“Naunga mkono hoja!” akajibu.

Baada ya mazungumzo marefu, kikao kikafungwa na wajumbe wakatawanyika kwa miadi ya kukutana kesho yake ambapo mtu wa kwanza atakuwa amewasili kwa ajili ya kugewa majukumu yake.

Mara baada ya kumalza kikao hicho, Madam S alikanyaga mafuta moja kwa moja mpaka makazi binafsi ya Mheshimiwa Rais huko Oysterbay. Alipowasili tu, akafunguliwa geti na kuingia mpaka maegeshoni ambako alimkuta Rais akimsubiri hapo.

“Karibu sana Selina!” akamkaribisha huku akimfungulia mlango wa gari hilo.

“Asante,”

“Kikao kimekwenda vizuri?”

“Hapana kwa sababu wametaka tuabbort mission, wameunda kikosi kingine kwa ajili ya kazi hii,” Madam akajibu.

“Mmmmhhh!!! Ina maana hawana imani na sisi?” akauliza tena.

“Hawana imani, wanasema hatujawapa majibu kwa siku tatu hizi, so hawajui nini kinaendelea, ukimya umewafanya wao wajue tumeshindwa. Wanasema una mmoja wa vijana wao wa siri kawatumia picha hii na kumhisi mtu huyu kuwa ndiye mhusika wa mambo haya,” akamwambia huku akimpa ile bahasha. Mheshimiwa Rais, akaitazama ile picha kwa makini sana.

“Anaitwa Fadicky Al-Habib,” Madam S akamtajia jina hilo.

“Kwa hiyo tunasitisha operesheni?” akauliza.

“Kamwe! Kwanza mpaka sasa kijana wangu sijajua nini kimempata maana sina mawasiliano naye, hatuwezi kusitisha zoezi kwa sababu tumefika mahali pazuri sana katika upelelezi huu…” akaeleza.

“Ulimtuma nani kule?”

“Namba moja!” akashangaa. Ilimchukua kama sekunde kumi na tano akili kumkaa sawa, akamshika bega Madam S na kuingia ndani katika varanda ndogo, akamkaribisha kiti na kuletewa kinywaji kikali, akaamuru walinzi watoke na yeye abaki na Madam S pekee.

“Unataka kunambia kuna habari mbaya kwa TSA 1?” akauliza.

“Bado hatujafikia kusema hivyo, na tunaamini kuwa anaweza kufanya lolote huko aliko,” Madam akamjibu, “hata hivyo kesho TSA 2 ataondoka kuelekea Sierra Leone kwa ajili ya kumtafuta mwenzake…”

“Come on!” Mheshimiwa akatulia kwa nukta kadhaa, akainua bilauri na kupiga mafunda kadhaa ya kinywaji, kisha akaitua, “hakikisha habari zote unanipatia, kama unavyojua, idara yako ni kama moyo wa Ikulu na utendaji mzima wa Rais, kama kunahitajika msaada wowote, fanay kama ufanyavyo kawaida,” akamaliza na kuagana na mwanamke huyo. Walinzi wa Rais daima walimwona mwanamke huyu mara kwa mara akija na kila alipotaka kuzungumza naye faragha aliwaondsha; wapo walioamini kuwa ni demu wake, wapo waliojua kuwa alikuwa ni classmate na mengine mengi, lakini hawakuwahi kujua kama ana cheo kikubwa katika idara nyeti ya usalama wa taifa hili.

*   *   *

KITONGOJI CHA WATERLOO

SIERRA LEONE

MARTIN Gupter akafunga pazia la dirisha na kurudi tena mezani ambapo aliwaacha wenzake.

“Vipi?” mwanamke pekee katika jopo hilo akamtupia swali.

“Ni yeye! Anapita na watu wake, anajivunia kuukwaa urais wa nchi hii…” Martin akamjibu huku akiketi tena mahala pake.

“Wamempa tu, si swahiba wao, lakini wataona kile ambacho tutakifanya, safari hii lazima niishangaze Afrika kama nilichokifanya pale Lusaka! Na watasaka mpaka wakome hawatanipata…” Yule mwanamke aliyejulikana kama Amanda akawaambia wenzake.

“Mpango upoje?” kijana mwingine akauliza.

“Kama kawaida, ni keshokutwa tu, lazima tuangushe wa nne, hii itawapa kiwewe, watakubali tu tunachotaka,” yule mwanamke akajibu huku akismama.

“Kama kuna mpelelezi ambaye nilikwishapewa jina lake kuwa ni wakumwogopa ndiye huyo tayari yupo kwenye kaburi la halaiki, hajawahi kutoka mtu mle…”

“Zaidi ya hapo hakuna mwingine… hawa wengine watoto tu,” Frederick Garincha, kijana mpole asiye na mawaa akawaambia wenzake.

“Timu imetimia hatujawahi kuharibu, na hatutaharibu kamwe…”

Vijana hawa watatu ndani ya nyumba hii kubwa ya ghorofa walikuwa wamepiga kambi kwa muda, mambo yao na mipango yao ilikuwa ikipangwa kwenye majumba ya siri ambayo yalitapakaa miji tafauti Afrika. Walikuwa wamebobea kwenye kazi mbalimbali za kigaidi, mauaji, wizi na kadhalika, mara hii walikuwa wamepata kazi katika Bara la Afrika. Mkataba mnono, wenye pesa za kutosha, hawakukataa bali waliifanya kazi hiyo kwa umakini usioelezeka. Afrika ilihaha pale Rais wa nchi ya Angola alipotunguliwa kwa risasi akiwa katika gari lake. Liikuwa ni tukio ambalo wanausalama hawakulitegemea kabisa, na baada ya hapo hawakufanikiwa kumpata muuaji wala nyayo zake.

 

…MIEZI SITA ILIYOPITA

LUANDA – ANGOLA

            ASUBUHI ya siku hii kulikuwa na hali ya mawingu kiasi, ukizingatia ni mwisho wa juma hakukuwa na kashkash za wapita njia kama ilivyo siku za kazi. Utulivu ulishika hatamu kila kiunga cha jiji hilo, zaidi ya wafanya biashara kufungua maduka ni watu wachache sana walioonekana kwenda huku na kule hasa akinamama kwa kuwa walihitaji chochote kwa siku hiyo, wao na familia zao.

Askari maalumu wa usalama barabarani katika jiji hilo walianza kuonekana kwenye barabara nyeti ambayo kiongozi wa nchi huitumia mara nyingi kutoka makao yake kuelekea Uwanja wa ndege kama anakuwa na safari ya kutumia usafiri wa anga. Hakuna aliyekuwa anajua nini ambacho kitatukia siku hiyo na kuitikisa nchi hiyo kwa mapana na marefu. Watu wenye fikra mbili tofauti walikuwa ndani ya jiji moja. Upande huu wanausalama walioakikisha Rais na watu wake wanakuwa salama muda wote katika safari hiyo walikuwa wanawasiliana kujiridhisha hali halisi ya siku hiyo. Mambo kadhaa yalikuwa yakiwekwa sawa, huwa tunaita itifaki, barabara ya kupitia msafar huo tayari ilikuwa chini ya ulinzi mkali, ikiwa imeshafungwa mitambo yote kuhakikisha usalama. Katika jiji hilohilo kulikuwa na kundi lingine la watu watatu nao walikuwa wakiweka mambo sawa kwa upande wa kazi yake. Hawa hawakuwa wengine zaidi ya Amanda Keller, Martin Gupter na Frederick Garincha. Jamaa hawa waliingia nchini humo kwa usafiri wa barabara wakitokea nchi ya Jamhuri ya Congo yaani Zaire ya zamani.

Kadiri ya mipango yao hawakutaka kuingia nchini humo kwa ndege kwani ingeweza kuhatarisha usalma wao. Ni Amanda pekee aliyeingie kwa njia hiyo kwa kuwa alitakiwa kuwahi angalau juma moaj kabla ili kuweza kufanya udukuzi wa mipango na maisha ya mheshimiwa ili kujua ni jinsi gani wataweza kufanikisha azma ya mteja wao.

Ndani ya jumba hili kubwa wawili yaani Frederick na Martin walikuwa tayari kwa kazi asubuhi hii wakati Amanda akiwa nje akifanya mazoezi ya kukimbia. Kiujumla haikuwa mazoezi kama mazoezi bali ni moja ya kukusanya taarifa kama watu wa usalama wamegundua chochote katika njama hiyo.

Martin Gupter aliijua vyema kazi yake, aliitazama saa yake ya mkononi na mara moja akaliendea dirisha la upande wa barabara kuu ya Avenue Revolucao de Outubro ambayo inaelekea moja kwa moja katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro. Mbinu chafu iliyofanywa na Amanda ni kupandikiza kifaa cha mawasiliano kwa mmoja wa watu wa usalama waliokuwa barabarani huko nje alipojifanya ameumia na kijana huyo kutaka kumsaidia.

“Time is now!” Frederick alimwambia Martin na wawili hao wakagawana. Fred akateremka chini kutoka ghorofani na kuingia garini huku akimwacha Martin kijana wa Ki-Holland akiwa tayari kweka bunduki yake kwa kificho dirishani na jicho lake likiwa kwenye lensi iliyofungwa vyema juu ya bunduki hiyo ya kawaida kabisa.

Alipojiridhisha, akaikunja katikati na kuchukua risasi moja tu, kubwa yeney nguvu, akaitumbukiza mahala pake na kuirudishia bunduki hiyo kama kwanza, akaipachika tena kwenye stendi yake na kuiweka dirishani kwa mtindo uleule.

“Wanakuja!” akasikia sauti kutoka kwenye kifaa chae cha sikioni, sauti hiyo ya Amanda ilimpa taarifa.

“Ok!” akaitikia. Sekunde chache tu, akasikia king’ora cha gari la polisi huku nyuma yake kukifuata gari kama sita hivi zilizojipanga katika mtindo wa kupendeza.

“Gari ya tatu kushoto, ameketi katika kiti cha nyuma katikati!” Amanda akamwambia tena Martin.

Kijana huyo akapata kama ganzi hivi kwa kuwa alijua wazi kwa shabaha hapo patakuwa pagumu, hawakutegemea kwa kiongozi huyo kukaa katikati labda kama na wao wangekuwa chini.

“Hard Target!” akatamka.

“Tumia akili ya ziada!” Frederic akamwambia katika chombo kilekile. Martin alikuwa mzoefu sana katika kudungua, alijua kila aina ya shabaha katika kazi hiyo, kwa ujumla yeye alikuwa ni muuaji mwenye taaluma ya juu sana. Alijua wazi kuwa akikose shabaha tu basi atakuwa katika wakati mgumu kwani kanuni za mauaji ya namna hiyo ni hizo, risasi moja tu uwe umemaliza mchezo, hutakiwi kupiga risasi mbili kwa maana risasi mbili huzidi kufanya usalama wako kuwa matatani asilimia za kukamatwa au kugundulika zinapungua. Akiwa katika kuwaza hivyo, tayari ule msafara ulikuwa umekaribia umbali ambao shabaha yake ingeweza kufanya kazi.

Kutoka pale alipo, alifyatu usalama wa bunduki yake, na ile risasi ikingia chemba, kwa shabaha ya ajabu, akavuta trigger nyuma na kuiruhusu risasi ile iende ilikokusudiwa, hakujali kama imepata au imekosa, aliinuka haraka, akakunja miguu ya ile bunduki, kuifungua mtutu wake, akatia kwenye mkoba na kutoka haraka. Huku chini Frederick tayari alikuwa amewasha gari na hakupita muda, akamwona Martin akiingia garini naye akaondosha.

*   *   *

Ghafla, dereva wa gari la rais, aliyumba baada ya kusikia yowe moja tu la mheshimiwa. Magari mengine nayo haraka yakalizunguka lile la rais ambalo kidogo litoe nje ya barabara kama si umahiri wa dereva. Askari wenye silaha tayari walikuwa nje na bunduki zao. Dakika chache baadae helkopta ya serikali iliwasili ikiwa na madaktari, wakamchukua rais na kumpakia kisha wakaondoka eneo hilo kuwahi matibabu.

Jiji la Luanda lilikuwa kwenye hali mbaya siku hiyo, askari kaznu walimwagwa haraka kila kona na mshikemshike ulikuwa si wa kawaida.

Amanda aliwasili katika eneo la tukia kama dakika tano baadae na kukuta rais akiondolewa eneo lile huku askari wakiranda huku na kule. Akasimama mbali kidogo na ghafla akatakiwa kupita njia nyingine na si pale kwa kuwa tayari kuliwekwa utepe wa zuio.

“Nini kimetokea?” mkuu wa polisi wa jiji hilo aliwasili na kutaka kujua kutoka kwa vijana wake kilichotokea, lakini kabla hata hajapoke jibu akapigiwa simu na kutakiwa kufika Ikulu ya nchi hiyo haraka sana kwa kikao cha dharula.

Katika ukumbi wa mikutano ndani ya jingo la Ikulu ya nchi hiyo, viongozi wa juu wa maswala ya usalama walitangaziwa kuwa rais wan chi hiyo amefarika dunia kwa kupigwa risasi iliyomuumiza vibaya kichwani. Ilikuwa ni taarifa ya masikitiko si kwao tu bali kwa taifa zima.

Mara baada ya kuondoka pale, Fredric na Martin waliwasili Mbuga ya wanyama ya Kissama pembezoni kidogo mwa jiji hilo maana walijua mpaka dakika hiyo wasingeweza kutoka nje ya mpaka kwa njia yoyote ile.

 

 

 

III

 

 

 

 

ADDIS ABABA

TAARIFA ZA KIFO cha rais huyo zikafika Makao Makuu ya AU siku hiyohiyo na kuleta mtafaruku mkubwa miongoni mwa marais wan a wawakilishi mbalimbali waliofika kuwakilisha nchi zao katika mkutano mkuu. Rais wa Angol alikuwa ni mmoja wa wajumbe muhimu sana na mwenye hoja nzito ya kuwasilisha.

Nako kikao cha dharula kikakaliwa kuijadili hali hiyo, haikuingia akilini, swali kubwa lilikuwa ni; kwa nini na nani aliyemuua kiongozi. Vichwa viliuma akili ikasinyaa, hakukuwa na jibu, mkutano huo ukaahirishwa ili kwanza upishwe uchunguzi juu ya mauaji yale. Ilikuwa ngumu sana kujua kiini cha mauji hayo kwa sababu hakukuwa na taarifa ya madai wala uhasama. Kilichowekwa mezani na kujadiliwa ni ugaidi, kwamba ‘lilikuwa tukio la kigaidi’ basi hakukuwa na kingine. Baada ya wachunguzi waliobobea kwenye mambo ya kiuchunguzi kama haya walijiuliza sana ni vipi wataita ugadidi kama hakuna mkwaruzano wowote wa kisiasa kati ya nchi hiyo na magaidi, hawakupata picha ya moja kwa moja bali hata wao walibaki kuanza kutengeneza jibu kisha walifanyie kazi.

 

DAR ES SALAAM

Nchi zote za Afrika zilipata taarifa hiyo haraka sana ikiwamo Tanzania. Habari hii ilimkuta Madam S akiwa ametingwa afisini kwake, na ilipenyezwa kwake moja kwa moja kutoka Ikulu ya Magogoni. Akabaki amebutwaika pasi na kujua nini hasa kimetokea. Ni tatizo ililotokea nchi nyingine lakini yeye kama mwanausalama alitakiwa kufanya chochote katika hilo. Na yeye hakusita aliwataka vijana wake kufika katika ofisi ndogo na kuwapa taarifa hiyo ambayo wote waliipokea kwa mshangao na fikra tafauti. Lakii baada ya mazungumzo nao wakatakiwa kuhakikisha usalama kwa nchi yao.

“Nashindwa kuelewa huyo mdunguaji wanyemwacha anajinywea bia kwa raha zake wana mpango naye gani?” Amata akasema.

“Umeshaanza kuingilia kazi isiyokuhusu…” Madam S akamuonya.

“Ingekuwa hapa huyo hayawani asingepona, yaani mpaka sasa angekuwa anapumulia mipira…” akasema na jopo zima likacheka sana.

“Kwa hiyo sasa safari ya ya mheshimiwa Rais imeahirishwa, na haitakuwepo kwa sasa,” Madam S akawapa taarifa hiyo nao wakaafiki kabisa bila kuipinga.

 

MIEZI MINNE ILIYOPITA

ABIDJAN – IVORY COAST

WAKATI BADO Waafrika hawajasahau shambulizi lililotokea Angola, wakashitushwa tena na hili la Abidjan. Hili lilimlenga moja kwa moja Waziri Mkuu wa nchi hiyo. Siku alipokuwa akiandhimisha sikukuu ya Mtoto wa Afrika katika uwanja mkubwa wa michezo katika jiji hilo unaojulikana kama Stade Felix Houphouet. Siku hii ni siku kubwa sana Afrika ambayo husherehekewa karibu barani kote hukusanya watoto na viongozi mbalimbali wa serikali. Waziri Mkuu wa Ivory Coast alikuwa miongoni mwa watu ambao wangehudhuria sherehe hizo katika nchi yake.

“Tutamwondoa siku hiyo!” walipanga wakiwa mafichoni kwao katika mji wa Anyama ambako waliingia kama wiki tatu kabla ya tukio. Kama kawaida Amanda alitangulia kuiangia Abidjan kwa ajili ya kulichunguza windo lake na kujua ratiba na taratiu zte za maisha ya mtu huyo ili kujua ni wakati gani wa kutekeleza. Kilichofanyika ni kuwa wao walikuwa wakipewa picha tu kuwa ni nani anatakiwa aondolewe, hata sababu ya watu hao kuuawa hawakuijua, wao walitekeleza tu matakwa ya mteja wao, basi.

“Unafikiri hapo ni pazuri?” Martini akauliza.

“Kwa upande wangu, ndiyo, pazuri na panafaa sana, cha muhimu ni kujua tu ni vipi tutamaliza kazi na vipi tutaondoka.

“No! hapo si pazuri kwa upande wangu!” Martin akaeleza wasiwasi wake, “hujapata ratiba yake nyingine baada ya hapo?”

“Of coz baada ya hapo kuna tafrija fupi, imeandaliwa katika Hoteli ya Leopard, pembezoni mwa Bahari ya Atlantiki….”

“Baaassss hapo sasa mi nitamaliza kazi yangu kwa sekunde chache sana,” Martin akamkatisha Amanda, “tena ni muda mzuri sana, usiku, muda wa giza, unajua tofauti na kule Luanda ile nilipiga jiwe kichakani….”

“Lakini kwa shabaha ileile!” Frederick akamalizia.

Mipango yote ilisukwa ndani ya nyumba hii ndogo na kazi ikabaki tu utekelezaji, Amanda na Fred walienda zao mapema sana katika Jiji la Abidjan kwa ajili ya maandalizi ya shambulio wakimwacha Martin nyuma akiendelea kujifua tayari kwa kazi hiyo. Martin alikuwa muuaji ‘assassin’ aliyebobea katika kazi yake na aliijua vyema. Alipitia mafunzo ya ujasusi hasahasa katika edani hii ya kuetekeleza mauaji, hivyo alijua jinsi ya kuua kwa silaha, kwa mikono, kwa kutenegneza ajali au njia nyingine yoyote ile. Alipoachana na ofisi yake huko Ughaibuni akaamua kujificha kwa miaka mingi sana na hapa ndipo akaunda kikosi hiki maalum kwa kazi hii, kilichokodiwa na watu wenye mahitaji kama haya.

*   *   *

USIKU WA SIKUKUU YA MTOTO WA AFRIKA

KATIKA hoteli kubwa na ya kisasa yaani ya nyota tano ndani ya Jiji la Abidjan, iliyojulikana kama Leopard. Usiku wa siku hiyo, viongozi wa taasisi mbalimbali na mashirika yasiyo ya kiserikali walikusanyika kwa tafrija ndani ya ukumbi wa hoteli hiyo.

Saa tatu usiku, Waziri Mkuu wan chi hiyo Bwana Ayatou Al Assad aliwasili na wapambe wake huiku ulinzi ukiwa umewekwa nje ya hoteli hiyo na ndani pia. Baada ya kusalimiana na wale waliompokea nje ya jingo hilo, akaingia ndani kwa kusindikizwa. Yote haya Amanda alikuwa anayaona kutoka ndani ya gari lake alilokuwa akitumia ndani ya jiji hilo.

“Umeona?” akamwambia Martin

“Nimeona!” Martin akajibu.

“Mi nilikwambia, mchana ingekuwa muda muafaka sana kwa kazi hii,” akalalama mwanamke huyu.

“Sikia Amanda, najua nini unahofia, sasa kwa taarifa yako huu ni muda muafaka sana kwa mimi kumaiza kazi hii, utashangaa mwenyewe, tena nafikiri sihitaji kabisa hata silaha ya moto ni mikono yangu tu itakayoshughulika naye…” Martin akawaeleza wenzake.

“Sawa, sasa sisi tutakusubiri pale tulipokubaliana, sivyo?” Fred akamwambia swahiba wake naye akajibu kwa kutikisa kichwa.

Martin akashuka kwenye lile gari na kuwaacha wenzi wake wakiwa bado ndani yake.

“Kazi njema!” Amanda akamwambia huku Fred akimpa mkono. Wawili hao wakatia gari moto na kuondoka katika viwanja vya hoteli hiyo huku wakimwacha Martin akiwasindikiza kwa macho. Baada ya kuhakikisha kuwa lile gari limeondoka, Martin akachukua simu yake na kupachika vifaa vya kusikilizia, kisha taratibu akavuka barabara na kuelekea katika hoteli ile, akuufuata mlango mkubwa bali alifanya kama anapita njia na kuzunguka upande wa nyuma wa hoteli hiyo.

“Hey! Hey! Simama!” Martin akasikia sauti ikimwita nyuma yake, hakusimama akaendelea kutembea huku mikono yake ikiwa mifukoni, bado ile sauti ikazidi kumsimamisha, akasimama. Martin kutokana na ugeni wake hakujua kama upande anaokwenda kupita hauruhusiwi ndiyo maana alitakiwa kusimama.

“Njia imefungwa upande huo!” akaambiwa.

“Sasa tunapita wapi?” akauliza huku akiwa amejiandaa kwa lolote maana hakujau ni nini kitatokea kwa kusimamishwa huko.

“Oh samahani, sikujua kabisa juu ya hilo,” Martin akajibu na kugeuza njia kuufuata upande wa pili. Yule askari aliyekuwa anaongea akamwangalia kijana huyo akitembea kuelekea upande mwingine, akamtilia shaka. Akavuta hatua za haraka na kumnong’oneza mwenzake kisha wote wawili wakaanza kumfuata kwa nyuma kujua hasa ni wapi anakokwenda. Martin akajua hila zao, akaendelea kutembea kana kwamba hajui kama wanamfuata. Akafika kwenye kona na kukunja, kisha akajibana katika ya kuta mbili zilizoacha nafasi katikati, hakuonekana.

Wale askari wakafika kwenye ile kona nao wakakunja, hawakuona mtu, wakjikuta peke yao, si kwamba upande huo hakukuwa na mwanga, la, taa kubwa zilikuwa zikiangaza upande huo kwa usalama zaidi lakini askrai hao hawakuweza kumwona mtu huyo.

“Ghost!” mmoja akamwambia mwingine ambaye tayari alikuwa na bastola mkononi akirandaranda huku na huko.

“Kapotelea wapi huyu mtu?” yule wa pili akauliza lakini hakupewa jibu kwani hata wa kwanza alishazani kuwa huyo si binadamu bali ni mzuka tu. Kutoka kwenye pachipachi za kuta zile, Martin alikuwa akiwaona na kuwasikia kila walichokuwa wakizungumza. Utulivu na jinsi alivyojiranda na kuta zile isingekuwa rahisi kumgundua kwani hiyo ilikuwa ni moja ya mafunzo yake aliyopitia jinsi ya kujificha katika mazingira tofauti na kumpoteza adui yake. Kama dakika kumi hivi wale walinzi wakaondoka wakisikika kusema kuwa wankwenda kuchukua wengine zaidi kwani hata wao walionekana kwamba wana munkari ya kumtia mkononi. Walipotoka tu, Martin akajitokeza na kuwahi bomba kubwa la maji taka litokalo chooni, bomba hilo lilikuwa limeunganishwa kutoka vyoo vya ghorofa ya juu mpaka chini kabisa. Kwa kasi ya ajabu akakamata na kukwea kwenda juu kwa kutumia bomba hilo. Na alipofika kama ghorofa ya sita hivi akasikia huko chini sauti za watu wakizungumza, akatazama na kugundua kuwa ni wale askari sasa wamekuja wane zaidi jumla sita, akatulia na kujibana tena sambamba na bomba hilo. Hata wale askari walipoangaza macho yao juu hawakuweza kugundua kama kuna binadamu. Baada ya kujiridhisha kuwa hakuna mtu wakaondoka zao na kurudi kwenye malindo yao ya kawaida. Martin akaendelea mpaka ghorofa ya saba na kufika katika moja ya chumba ambacho kilimfurahisha, dirisha lilikuwa wazi. Kutoka katika bomba hilo mpaka kufikia dirisha hapakuwa mbali sana, alijivuta na kujifyatua mara moja mikono yake ikawahi kudaka kingo za chini za dirisha hilo, akatulia akining’inia kama sekunde arobaini hivi akaisikiliza kama kunamtu atakayekuja upande huo.

Zaidi ya sauti za mahaba zilizotoka ndani ya chumba hicho hakukuwa na mtu kuja dirishani wala nini, Martin akajivuta juu taratibu na kichwa chake kikavuka ukingo wa dirisha lile, naam juu ya kitanda kikubwa ni binadamu wawili ambao walikuwa juu yake wakipeana mambo ya kwenye video. Martin alijivuta na kuingia mzima mzima, akatua sakafuni taratibu, mita moja tu kutoka katika kitanda kile.

“Who are youuu!!!” yule mwanamke juu ya kitanda kile akapiga ukelele huku akimsukuma kwa nguvu mwanaume aliyekuwa naye akimchomoa mwilini mwake. Martin tayari alikwishachomoa bastola yake lakini hii haikuwa ya mauaji, akafyatua mara kadhaa na vijishale vidogo vikawaingia wawili hao nao haikuwa pa hata dakika moja wakakumba na usingizi mzito.

Nimefika! Martin akajisemea ndani ya ubongo wake kisha akajiweka sawa, akachukua nguo za mwanaume huyo zilizokuwa kando tu, akazivaa juu ya zile za kwake, zikamkaa vyema, akavua begi lake la mgongoni na kuliweka kando, ndani yake katoa waya wa piano ‘piano wire’, waya hatari sana katika kuvunjia shingo. Akaueka katika mfuko wake na bastola yenye risasi akaiweka vyema kabisa katika koti lake la suti. Akajitazama kiooni na kujiweka nywele sawia, tayari kuingia ndani ya tafrija ile.

“Tunasubiri taarifa kutoka kwako!” sauti ta Amanda ikayafikia masikio ya Martin kupitia earphone zile.

“Wait! The patient dog will eat a big bone! I am in!!” akawajibu kupitia njia hiyo hiyo. Martin tayari alikuwa amebadilika mwonekano wake, akafungua mlango na kupita kwenye korido ndefu mpaka kwenye lifti, akaingia na kuamuru irudi tena mpaka chini, akateremka na kuingia katika ukumbi huo wa waalikwa alipoulizwa mlangoni, akaonesha kadi ndogo aliyoikuta katika shati lile akaruhusiwa kuingia.

Hakukuwa na watu wengi, isipokuwa wachache wenye heshima zao na wazito, akazungusha macho kwa haraka na kuona mchezo gani anastahili kuucheza ili amalize alilotumwa. Kabla hajakaa kitini akavuta hatua na kuingia kwenye ujia ambao wahudumu walikuwa wakitokea kama wanaleta vinywaji. Mara moja alimkariri sura mhudumu wa kike ambaye alikuwa akimhudumia mheshimiwa waziri. Ndani ya chumba kidogo msichana yule aliingia tayari kuchukua chano ya vinywaji na kuipeleka, Martin alijua wazi kuwa chano hiyo kwa vyovyote inaeenda meza kuu, akajifanya anapita kuendelea na safari lakini haikuwa nia yake, mara yule msichana alipotoka akamjia kwa nyuma taratibu sana kwa mwendo ambao hauna kelele. Akiwa mkononi ana kinywaji kilichoshahabiana kabisa na kile ndani ya chano. Akakibadili taratibu bila yeye kujua kisha akamwambia.

“Samahani, heti maliwato ni wapi?”

Yule mwanadada akashtuka na kugeuka nyuma akakutana macho na kijana huyo wa kizungu.

“Oh sorry, huku umekosea njia, ni upande ule wa pili korido kama hii utaona milango,” akamwelekeza na kumwacha apite. Martin alipita pasi na kujulikana kama amebadili kinywaji kile.

Hatua kadhaa zikamfikisha upande ule, akaingia kama alivyoelekezwa, naama kulikuwa na milango miwili. Mmoja uliandikwa V.I.P akaupita na kuingia unaofuatia ambao kwa ndani umegawanyika mara mbii aani kushoto wanawake na kuume wanaume, akasimama na kutafakari kidogo. Akaingia choo kimoja cha wanawake kwani ndicho hasa kimepakana na kile cha VIP, ndani ya choo hicho akajifungia. Akajaribu kuugonga ukuta huo, akagundua kuwa si ukuta kama ukuta bali ni mbao laini zilitenganisha. Martin akatafakari jinsi gani atatekeleza azma yake hiyo, akili yake ikamwambia ‘umecheza pata potea’ lakini hakukubaliana nayo. Juu ya darai kulikuwa na taa kubwa imefungwa kwa mtindo wa pekee.

“Yes!” akasema kwa sauti ndogo na kupanda juu ya sinki la choo cha kukaa na kuing’oa taa ile kwa urahisi nayo ikamwachia tundu kubwa la kutosha, akakwea kwa ustadi na kuingia ndaani ya dari kisha akaivuta taa ile taratibu na kuirudishia. Ndani ya dari ile kulikuwa na uwazi ambao mtu angeweza kutambaa, akafanya hivyo mpaka kwa uangalifu na kusubiri pale alipoona kuwa patakuwa ni choo cha VIP. Akatazama saa yake ikamwambi kuwa ni saa tano za usiku.

Vipi kama asipokuja chooni? Akajiuliza.

Atakuja tu! Akajijibu.

====================

SOMA RIWAYA HII KWA Tsh 6000 tu za Kitanzania

Lipia sasa kwa

Mpesa – 0766974865       Richard Mwambe

Tigopesa – 0713948437    Richard Mwambe

Ukishafanya muamala, wasiliana na mwandishi kwa namba yoyote hapo, kisha utatumia password itakayokuwezesha kusoma mpaka mwisho riwaya hiyo.

Karibu sana!

===========================

 

Share

Leave a Reply

Translate »
error: OPS! Content is protected !! Imezuiwa