RIWAYA: JIUE MWENYEWE

 

 

 

 

 JIUE  MWENYEWE

©Richard R. MWAMBE

 

1

Mwaka 2003…

DURBAN – AFRIKA KUSINI-Saa 3:21 asubuhi

NDANI YA JENGO REFU KULIKO YOTE, Monte Blanc, lililopo katika jiji la Durban, jimbo la KwaZulu Natal, Afrika ya Kusini, ni mtu mmoja aliyekuwa akiwindwa kwa udi na uvumba. Ni mara ya sita kama si tano mtu huyo kukoswakoswa na muuaji hatari wa kike kutoka Marekani, Tracy Tasha. Mara hii akamfuata hukohuko katika ardhi ya nchi yake, Afrika ya Kusini.

Lamborghini Veneno, gari ya gharama kabisa duniani iliegeshwa taratibu katika maegesho Monte Blanc, nyuma yake ikasimama gari nyingine, BMW nyeusi, vijana wanne wakakamavu waliovalia suti nyeusi zilizotanguliwa na mashati meupe na shingoni mwao kila mmoja alining’iniza tai ndefu nyeusi. Walikuwa kikazi zaidi, macho yao yakitazama kila upande kwa umakini, mmoja wao aliiendea ile gari, Lamborghini, akaufungua mlango na kuukinga upande wa juu kwa kiganja cha mkono wake wa kushoto ili atokaye ndani hasidhurike kwa kujigonga. Kwa mtindo huu ilionekana atokaye ndani ya gari hiyo ni Mheshimiwa sana.

The Great Khumalo, kama alivyojiita, alitoka nje ya gari ile, akajiweka vizuri suti yake ya gharama, huku mkono wake wa kulia ukiwa kwenye kifundo cha tai kuirekebisha, alianza kuvuta hatua ndogo ndogo na mwamvuli ukiwa umeshikiliwa juu yake kuyakinga manyunyu ya mvua yaliyokuwa yakinyurunyuta asubuhi hiyo yasimletee tabu. Vijana wake walifuata, nyuma wawili na mbele wawili, yeye alikuwa katikati. Ilikuwa ni ngumu kumgusa mtu huyu, tajiri sana katika jiji la Durban, nani asiyemjua Khumalo? Hakuna shule ambayo hajawahi kuifadhili katika jiji hilo, alijulikana, alipendwa, alitazamwa kama almasi. Anaitwa Gervas Khumalo aliyezaliwa na kukulia katika kitongoji cha Berea, alizaliwa katika familia yenye maisha ya kati, lakini iliyoweza kumlipia masomo yake ndani na nje ya nchi mpaka akawa mtu mkubwa.

Jengo la Monte Blanc, katika Jiji la Durban. Ndani yake, ndimo Mr Khumalo alipouawa…

Hatua zake zilimfikisha katika mlango mkubwa wa jengo hilo, ukafunguliwa kwani yeye hakutakiwa kushika sehemu yoyote, kila mtu alimhusudu, lakini hakukuwa na nafasi ya kumpa hata mkono kwani alikuwa akilindwa vilivyo, moja kwa moja wakaingia katika lifti ili kupanda juu katika ofisi mojawapo ya jengo hilo. Monte Blanc, jengo lenye urefu wa mita 133, sakafu (ghorofa) 40, lililojengwa hapo mwaka 1985 lilisifika kama kitivo cha biashara katika jiji la Durban. Ndani ya lifti hiyo alizungukwa pande zote na vijana wake waliosheheni silaha ndani ya makoti yao.

Ishirini na tatu: Mmoja wao alibofya kitufe kilicho katika kuta ya dude hilo na mara tu likaanza kupanda juu. Lilipofika mahala lilipoamrishwa likasimama kitu kama kengele kikagonga kwa pigo moja laini, mlango ukafunguka, wakateremka na kutembea kuelekea mahala fulani, wakaipita milango kadhaa. Kila mtu alipisha tajiri huyo apite.

KwaZULU Beauty and Massage, wakasimama hapo, mlango wa kioo ukafunguka wawili wakaingia na tajiri wao na wawili wakabaki mlangoni kuhakikisha ulinzi. Khumalo moja kwa moja alienda katika kochi kubwa na kulikalia mara baada ya vijana wake kulihakikisha kuwa lina usalama wa kutosha. Muda huo huo mwanamke mrembo mwenye weupe wa Kiafrika alijitokeza kwenye mapazia yaliyokuwa na nakshi za mmemeto. Ndani ya ofisi hiyo pana na nzuri kulikuwa na wasichana wanne waliokuwa katika kazi zao za kila siku; mmoja mapokezi, mwingine kupokea pesa na kutoa risiti, anayefuata wa usafi na mwisho kuongoza wageni kule wanakotakiwa kwenda.

“You are welcome Sir,” (karibu sana mheshimiwa) yule mwanamke akamsalimu. Ukimwangalia alivyo, utasema ni Malaika kashushwa kutoka Mbinguni lakini alikuwa ni Binadamu kama wengine.

“Thank you so much,” (asante sana) Mr. Khumalo akaitikia karibisho hilo, yule Mwanamke akampa ishara ya kumfuata naye akafanya hivyo.

Haikuwa mara ya kwanza kwa tajiri huyo na matajiri wengine wengi kufika sehemu hiyo, wote walifika hapa kwa minajiri ya kupata huduma ya kukandwa mwili, ili kuirudisha miili yao katika hali nzuri ya kiafya. Bwana Khumalo alikwishazoea mara nyingi kuja mahala hapo kwa ajili ya huduma hiyo, alikuwa amejipangia ratiba kabisa ya tendo hilo. Akainuka na kumfuata yule mwanamke huku walinzi wake nao wakiwa nyuma yake, wakaingia katika mlango ule wa mapazia na kufuata korido ndefu, waliipita milango mingi ya vioo ambayo ndani yake kulikuwa na wanawake waliokuwa wakifanyiwa urembo wa mwili na nywele, vyumba vingine vilikuwa ni vya mazoezi ya viungo, kulikuwa na mabafu mvuke kwa ajili ya wanaotaka kuusafisha mwili kwa kuuvukisha.

Wakafika kwenye moja ya milango ambayo daima huingia hapo, wale walinzi wakasimama nje ya mlango na bosi wao akaingia ndani pamoja na yule mwanamke kwa ajili ya kumpa huduma hiyo. Juu ya mlango ule kuliandikwa V.I.P.

 

 

SAA I6 ZILIZOPITA

UWANJA WA NDEGE WA LOUIS BOTHA

Uwanja wa ndege wa Louis Botha – Durban

 

BOEING 747 YA SHIRIKA LA NDEGE LA AMERICA (American Airlines) ilikanyaga barabara za uwanja huo na kwa mwendo wa maringo iliegeshwa kandokando ya jengo kubwa na zuri. Ngazi zilisogezwa, abiria wakashuka mmoja baada ya mwingine. Katikati ya abiria hao alikuwapo  mwanamke mmoja wa Kizungu, aliyezifunga nywele zake kwa mpira kisogoni mwake, miwani myeusi ya kumkinga jua ilitulia sawia usoni ijapokuwa jua halikuwa kali sana kwani ilikuwa jioni tayari. Kwa hatua za hesabu na mwendo wa maringo aliiacha ngazi hiyo na kutembea kwa haraka kidogo kuingia ndani ya jengo kubwa la kupokelea wageni. Hakuwa na mizigo zaidi ya kibegi kidogo kilichotulia mgongoni mwake, akafanya itifaki za uhamiaji kisha akatoka nje ya jengo hilo. Moja kwa moja akaziendea gari za kukodi zilizosimama nje hapo, akafungua mlango wa mojawapo na kuingia kuingiamo.

“Hard Rock Café,” akamwambia dereva, naye hakuuliza mara mbili aliwasha gari na kuifuata barabara kuu, akakaza mguu mpaka katikati ya jiji, mbele ya mgahawa huo maarufu kabisa katika miji mingi mikubwa duniani.

Tracy Tasha, akamlipa yule kijana na kumuomba kadi yake ya kibiashara, bila kinyongo yule dereva akampatia. Mwanadada huyo akazikwea ngazi na kuingia kwenye mgahawa huo uliosheheni Wazungu, hakuona mtu mweusi zaidi ya wafanyakazi wachache waliokuwa hapo, alipotupa macho upande wa pili aliona kumejaa watu weusi wengi sana wake kwa waume pamoja na familia zao. Ubaguzi hauwezi kwisha nchi hii, alijiwazia huku akitoa noti ya Randi 50 na kuagiza kinywaji cha matunda. Kwa jinsi alivyokaa jioni hiyo katika mgahawa huo, alikuwa akitazama upande wa barabara, na ng’ambo ya barabara hiyo kulikuwa na jengo kubwa la takribani ghorofa kumi hivi, likipambwa na maandishi makubwa meusi yaliyobandikwa kwenye ukuta wa njano, KHUMALO TOWER, yalisomeka namna hiyo.

…Saa 2:00 usiku milango yote hujifunga kwa mitambo maalum ya kiusalama, ukisogelae mita kumi na tano tu taarifa hupelekwa panapohusika…

Aliikumbuka sauti ya mteja wake bwana Robinson kutoka Canada alipokuwa akimpa maagizo akimwelekeza eneo ambalo atampata mbaya wake. Tracy, alishajaribu sana kumuua Khumalo kwa kulipwa kitita cha pesa lakini ni mara tano au zaidi alimkosa, alipompiga kwa risasi pale Uingereza miaka miwili iliyopita, alikuwa amevaa vazi lisilopitisha risasi, hakumpata, akajilaumu kwa hilo, mteja wake hakukata tama kwa maana aliamini ni mwanmke huyo tu anayeweza kuifanya kazi hiyo. Miezi kumi na moja baadae alimvizia tena katika hoteli kubwa huko Ethiopia akamtilia sumu kwenye chai, lakini kabla ya kunywa kulikuwa na mtu maalumu wa kuonja chakula au kinywaji chake, yule mtu akadhurika na kufa lakini bwana Khumalo akabaki hai. Kwa mara nyingine alimkosa tena mtu huyo. Tracy hakuwa mtu wa kufanya makosa, alipokabidhiwa kazi kama hiyo ni saa kumi tu angekwishakutoa uhai lakini kwa Bwana Khumalo ilikuwa ngumu, alitumia mbinu zote lakini alishindwa.

“Haiwezekani!” alijisemea na kupiga ngumi meza.

Safari hii alimhakikishia mteja wake, kuwa ahesabu kazi imekamilika kwani hakuna njia nyingine zaidi ya kutumia mikono yake.

…Utaweza?… 

Swali lililompa utata sana ambalo mteja wake alimuuliza. Nitaweza tu, kama nilivyoweza kwa wengine, akajijibu mwenyewe ndani ya moyo wake. Punde si punde giza likaikabili Durban, Tracy akainua macho yake na kuona taa za barabarani zimeupendezesha mji huo, akanyanyuka taratibu na kutoka nje, akavuka barabara kubwa na kufika upande ule wenye lile jengo alilolikusudia, watu walikuwa wakitoka ndani yake kwani muda wa kazi ulikuwa umekwisha, mwanamke huyo alifika mlangoni na kuingia ndani akipishana na wafanyakazi wa maofisi mbalimbali ambao walitakiwa kuliacha jengo hilo kabla ya saa mbili kamili usiku.

“Fanya haraka uwahi kutoka bado dakika ishirini tu,” sauti ya mlinzi ilimwambia Tracy ambaye tayari alikuwa ameifikia lifti ya jengo hilo na kuingia, akabonya kitufe namba kumi, lakini lengo lake lilikuwa ni kufika ghorofa ya saba ambapo ndipo zilipo ofisi za tajiri, mmiliki wa jengo hilo, The Great Khumalo. Akili yake ilicheza haraka sana, alijua wazi akibofya kitufe namba saba walinzi wangemshtukia kwa kuwa ghorofa hiyo mtu huenda kwa miadi maalum, hivyo akaenda gholofa ya  kumi kisha akashika ngazi kuruidi ghorofa ya saba. Akiwa katika ngazi hizo akachukua gloves zake na kuzivaa. Mbele ya ofisi aliyoidhamiria, akakutana na mlango wa kioo uliofungwa, akajaribu kuugusa na kuutikisa, haukutikisika, kitasa chake kilifungwa kwa ndani, akashusha begi lake chini akafungua na kutoa kifaa chemye uwezo wa kukata kioo kilichopachikwa ncha ya almasi kinachojulikana kama Circular Glass Cutter.  Akakibandika upande mmoja katika ule mlango na ile ncha akaizungusha vizuri kabisa alipotoa kile kifaa chake akatoka na kipande cha kioo katika mtindo wa duara, kikaacha pale tundu, akapenyeza mkono na kufungua kile kitasa kisha akaingia ndani kwa mwendo wa polepole akiangalia kila upande, mpaka alipoufikia mlango wa ofisi iliyoandikwa kwa maansidhi ya dhahabu M.D Khumalo. Akachukua funguo yake kwa mikono, akaufungua taratibu nao wala haukumpa shida. Akaingia na moja kwa moja aliielekea meza kubwa iliyo tanguliwa na kiti kikubwa cha kuzunguka. Hakika ilikuwa ofisi ya kisasa mithili ya ile ya Rais. Akatupa jicho mezani na kuona kile alichotaka, kitabu kikubwa cha kumbukumbu, akakipekua mpaka tarehe ya siku hiyo, akatazama tazama na kuona vyote viliandikwa kwa lugha ya kwao Ki-zulu, katika tarehe inayofuata, akaona alichofikiri kingemfaa.

‘KwaZulu Natal Beauty and Massage, saa 3:30 asubuhi kesho’,

Ilikuwa ni miadi ya kila mwezi, Tracy akatikisa kichwa juu chini, akafunga kitabu hicho na kutoka ndani ya ofisi ile, akafunga ule mlango wa kioo na kukirudisha kile kipande cha kioo kwa gundi kali sana ambayo huwezi kugundua kirahisi kama palikatwa. Akatoka na kukwea ngazi mpaka ghorofa ya kumi akaingia kwenye lifti na kuteremka chini.

 

Rejea KwaZulu Natal Beauty and Massaging Point…

Mwanamke aliyekuwa ameandaliwa kwa ajili ya kazi ya kumkanda mwili Bwana Khumalo alikuwa akisubiri mteja wake kama alivyoelekezwa na bosi wake, na daima ni yeye tu aliyekuwa akimfanyia kazi hiyo kwa maana baada ya kumaliza zoezi hilo basi ndani ya vyumba hivyo Khumalo alipeana mapenzi mazito na mwanamke huyo.

Kabla tajiri huyo hajaingia katika chumba hicho walinzi wake walikikagua na kuhakikisha usalama, ndani kulikuwa na mwanamke mmoja tu kwa ajili ya kazi hiyo, wakatoka ili kumruhusu bosi wao aendelee na starehe zake. Bwana Khumalo akaingia ndani ya kile chumba na kuingia tena katika kijichumba kingine kwa ajili ya kutoa nguo zake na kuvaa taulo. Kishapo litoka na kulala kifudifudi kwenye kile kitanda maalumu kwa kazi hiyo, yule mwanadada akasogea na kibweta cha mafuta na kuanza kumpaka mgongoni.

“Yesss Beibi, fanya kama siku zote, mmmmmmhhh!” Khumalo alianza kuguna kwa ule mtomaso laini wa yule mwanadada, alianza kumpigapiga vijingumi kwenye sehemu zake za mbavu, mgongo akipanda mpaka karibu na mabega na kushuka mpaka katikati ya mgongo.

***

Tracy Tasha alikuwa kimya kabisa kajificha katika bafu la chumba hicho, hakuna aliyemwona akiingia ndani ya chumba hicho. Alipoona dakika kumi zimepita akajua sasa ndio wakati wa kutekeleza azma yake, kazi ya mteja wake.

Leo nimekupata, akajisemea kindanindani, akatoka taratibu kutoka katika lile bafu na kusogea mpaka pale kitandani nyuma ya yule mwanadada aliyekuwa akiendelea na kazi yake. Akamsogelea na kusimama pembeni yake, yule mwanamke akamuona Tracy, alipopigwa na bumbuazi, Tracy alimuoneshea ishara ya ‘kimya’ kwa kuweka kidole chake cha shahada juu ya midomo yake. Kabla yule mwana dada hajaondoa mkono wake pale mgongoni mwa Khumalo Tracy akauondoa mmoja na kuweka wake kisha akafanya hivyo kwa ule wa pili. Akamsogeza nyuma yule mwanamke, naye akasogea huku macho yamemtoka na hajui nini anataka kufanya Mzungu huyo.

“Ooh mrembo, vipi mbona umesita?” Khumalo akauliza.

“Hapana nipo naendelea na kazi we tulia tu,” Tracy alijibu.

The great Khumalo alishtuka kwa sauti ile ngeni akataka kugeuka kuona ni nani huyo, akachelewa, Tracy kwa nguvu zote za mkono wake wa kulia alipiga pigo la vidole kwenye uti wa mgongo (lumber vertebrae),vidole vyake viwili yaani gumba na cha kati, alikamata pingili ya uti wa mgongo na kuivuta juu, akazitenganisha. Khumalo, alikuwa kama kapigwa shoti ya umeme, aliganda macho yamemtoka na kinywa kimeachama. Mwanamke huyo alipohakikisha mtu huyo hana uhai, na zile pingili zilizoachana zimetokeza juu lakini bado ziko ndani ya ngozi, akapiga kapigo ka wastani kwa kutumia kiganja cha mkono zikarudi kama zilivyokuwa. Khumalo akalala kimya, Tracy alikuwa amevunja pingili za uti wake wa mgongo na kukata kabisa spinal cord upande wa juu kama unakuja shingoni, ganzi kali ikampanda Khumalo, uhai wake ukaondoka ndani ya sekunde kumi tu za shambulizi hilo.

Tracy akageuka na kumwona yule mwanamke akiwa amechanganyikiwa hajui afanye nini, akamchukua na kumfungia kwenye chumba cha kubadilishia nguo, akamfungia kwa nje, akakizungusha kitasa na kukivunja, kisha akakitumbukiza kwenye ndoo ya takataka,  akatoka na kuufungua mlango, akawakuta wale askari wawili pale nje, akajua akiondoka tu itakuwa soo, akawaita ndani akawaambia kuna shida, wakaingia, aliwakamata na kuwagonganisha vichwa kwa nguvu wakaanguka chini hawana fahamu, akatoka mlangoni na kuufunga kwa nje, taratibu akatoka mpaka mapokezi na mwisho nje wa jengo lile, ile taksi ilikuwa imefika, akapanda na moja kwa moja akaelekea Uwanja wa ndege, amemaliza kazi.

Akiwa ndani ya gari hiyo akachukua simu yake na kubofya namba kadhaa kasha akaiweka sikioni na kuongea na mtu wa pili.

“Boss, nimemaliza kazi kwa mkono wangu bila vurugu kabisa,” alimwambia Bwana Robinson kwa simu.

“…oh, hongera sana mwanamke, fika haraka Ontario, nakusubiri,” Robinson akamjibu.

Saa nne na nusu asubuhi ndege ya shirika la ndege la Amerika iliiacha ardhi ya Durban na kuondoka zake, Trace akiwa ndani yake.

 

 

 

 

 

2

Miezi miwili baadaye…

KAZI NYINGINE YA TRACY TASHA

PARIS – mwaka 2004

PARIS – Ufaransa

 

KILIKUWA KIKAO CHA WATU WANNE TU walioonekana kuwa na pesa sana mifukoni mwao na hata katika mabenki mbalimbali duniani.

Danford Touzony, mtu mwenye pesa za dhuluma, mwenye siri nzito kifuani mwake, siri isiyotakiwa kujulikana na mtu mwingine yoyote, alikuwa na rafiki zake hao wakiongea mawili matatu juu ya biashara zao na maisha kwa ujumla, hakuwa na hili wala lile kama hapo alipo kuna mtu aliyekuwa akimwinda mchana huo.

Walikuwa katika hoteli kubwa ya kisasa iliyojengwa katika mnara mkubwa wa Eiffel mjini Paris, Ufaransa.

Bwana Danford Touzony alipata pesa nyingi sana na kuanzisha mabiashara makubwa baada ya kutoa siri nzito za kijasusi ambazo zilikusanywa na mtandao wa KGB na kuhifadhiwa katika makao makuu ya taasisi hiyo kule Lubyanka, Moscow nchini Urusi.

Alikuwa mwenye cheo cha kawaida sana katika shirika hilo miaka kadhaa nyuma, ushawishi alioupata na watu asiyowajua waliokuwa wakitaka kupata baadhi ya habari za kijasusi kutoka ndani ya shirika hilo walimwinda Danford mpaka walipohakikisha wamemtia mkononi na kumuahidi maisha mapya ya kila fahari aliyokuwa akihitaji.

Baada ya kukamilisha zoezi hilo hatari kabisa na kukabidhi siri hizo kwa watu waliozihitaji; alilipwa pesa nyingi sana na akapewa hifadhi katika nchi hiyo ya Ufaransa kwa kuwa swahiba zake wa KGB walikuwa wanamsaka kwa udi na uvumba. Baada ya ugumu mkubwa ulioonekana katika kumpata mtu huyo ilibidi wataalamu hao wa KGB kukutana na kujadili jinsi ya kummaliza mtu huyo hata kama amehifadhiwa vipi.

Likaja wazo la wao kutumia mtu binafsi kwa kazi hiyo, mtu ambaye hatodhaniwa kama ana kazi maalum kwa kuwa wao mara nyingi walikuwa wakijulikana kila wanapojaribu kufanya lolote dhidi ya mtu yeyote. Waliumizwa kwa siri zilizoibwa, na waliyahitaji maisha ya Touzony ili wengine wasije kufanya hivyo huko mbeleni. Iliwashtua sana kwa kuwa Touzony mwenye asili mbili zinazojenga ya tatu, ile isiyojulikana. Alizaliwa na mama Mrusi na baba Mfaransa akakua na kusoma Urusi, alikadhalika hata kazi alifanya Urusi, alipojiunga na idara hii ya KGB aliaminika sana katika kitengo cha TEHAMA, alikuwa mtaalamu asiyefananishwa na mwingine katika kucheza na kompyuta, siri zote za idara hiyo zilipita mikononi mwake kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa Mtawala katika mfumo huo wa kompyuta. Kulikuwa na siri nzito iliyofichwa kwa miaka mingi sana, miongo mingi sana. Siri ya mambo mazito ya Patriotic War of 1812 au kule Ufaransa wao waliita siri hiyo kwa jina la French Invasion of Russia. Serikali ya Ufaransa ilifanya mbinu mbalimbali za kuinasa siri hiyo, mwishowe wakapata kumfahamu kijana huyu na kumfanyia hila, akwa mgumu sana lakini wakammezesha utaifa, uzalendo, uasili; akalainika, ikapenyezewa lupia, kijana hakuwa na chaguo, elimu ya ziada aliyopewa na wazee wa mikakati kutoka katika serikali ya Ufaransa, Danford alifanya alichoambiwa kwa umakini wa hali ya juu na kuitoa siri hiyo kwa wanaoitaka. Akagundulika; naye akatoroka, hakupatikana kwa miaka mingi. Alisakwa na kusakwa, KGB walifanya kazi kubwa kumsaka kila kona ya sayari hii, hawakumwona wala kusikia tetesi zake. Lakini baada ya kipindi kirefu walipata tetesi kuwa mtu huyo yupo Paris, hapo ndipo ari ya kumtia mkononi iliporudi, walishajua kumpata akiwa hai ni ngumu basi japo afe. Ndipo walipokutana kuliangalia kwa mapana na marefu.

***

“Nani anaweza kazi hiyo?” waliulizana.

“Hatuna budi kuwa wapole hapa,” mwingine alijibu, “Kwa sababu inatubidi tupitie orodha ya wauaji makini duniani na wengi ni wale ambao hata sisi tunawasaka kwa tukio moja au lingine, lakini sasa hatuna budi kufanya nao urafiki kwanza, je watatuamini?” utata ulianzia hapo.

Hayo yote yalijadiliwa miezi miwili kabla ya Bwana Touzony kukutana hapo katika mnara wa Eiffel na marafaiki zake hao.

Iliwashwa kompyuta yenye makabrasha ya siri, jina lililowadondokea wote ni la huyu mwanamke Tracy Tasha aliyeonekana kwenye picha akiwa mrembo aliyevaa bikini na kujilaza juu ya mchanga. Walipochambua rekodi yake waliona mauaji mbalimbali aliyowahi kuyafanya, ya kitaalamu zaidi, kati ya yote ni asilimia arobaini tu ya mauaji hayo alitumia bunduki lakini yaliyobaki alitumia mikono, sumu, kemikali na siraha ndogo ndogo, ndipo walipoona mauaji ya mwisho aliyoyafanya kule Durban miezi miwili iliyopita, wakamhusudu. Wazo likaja la kumtumia mwanamke huyo, kwa kuwa ni mwanamke basi labda ingekuwa rahisi kumnasa mbaya wao. Majadiliano yakaendelea kwa muda wakakubaliana la kufanya, Tracy atafutwe apewe kazi.

“Usimwambie kama umetumwa na hii idara, we mpe picha mwambie cha kufanya,” sauti nzito ya mkuu wa taasisi hiyo ya kijasusi ya KGB ilimpa maagizo kijana mmoja shababi ambaye ilibidi aonane na Tracy uso kwa uso.

 

ALKANSAS-U.S.A

Simu ya mezani ikaita katika nyumba iliyojengwa shambani kabisa na kuzungukwa na mahindi mengi yenye urefu wa ajabu. Mwanamke mmoja aliyekuwa kitandani na mwanaume wakipeana raha za dunia, aliinuka na kukiacha kitanda, akatembea kwa madaha kama mlimbwende akiwa kama alivyotoka tumboni mwa mama yake, akaiendea simu na kuinyakuwa akaiweka sikioni.

“Hellow!” aliita kwa sauti ya mahaba kiasi kwamba mtu wa upande wa pili alichelewa kujibu labda kwa ganzi iliyopenya mwilini mwake.

“Yeah, unaongea na Laurent McMiller kutoka Ujerumani,” sauti ilisema.

“Biashara au mapenzi?” Tracy aliuliza.

“Biashara,” akajibiwa.

“Wapi?” akauliza

“Paris, Ufaransa,”

“Tuonane baada ya saa saba zijazo kutoka sasa, nitakuwa kwenye Metro ya kutoka London kuelekea Paris unipe maelekezo, usisahau hundi ya Paundi za Kiingereza Milioni tano,” akakata simu. Tracy mara baada ya kukata simu, akatulia kidogo, kisha akairejesha simu hiyo mahala pake. Akatoka na kurudi kitandani, akaketi.

“What again?” (vipi?) Yule kijana akamwuliza.

“I’ve got a job!” (kuna kazi) akamjibu huku akichukua kompyuta yake na kutazama katika mtandao wa Internet kama angeweza kupata ndege ya kuondoka nayo muda huo. Bahati ilikuwa yake, Qatar Airways ilikuwa na nafasi, akalipia kwa mtandao kwa njia ya Master Card, akatazama muda wa kufika, akakuta ni ule muafaka kabisa, akakata tiketi ya treni kutoka London mpaka Paris.

Tracy aliijua vyema kazi yake, si kwamba hakuweza kusafiri mpaka Parisi, bali kwake ni njia aliyopenda kuitumia ya kupindisha safari.

 

SAA SABA BAADAE

London Metro – treni iendayo kasi

Ndani ya Metro

Treni ya kutumia umeme ilikuwa ikitoka London kuelekea Paris Ufaransa kwa kasi ya ajabu, treni hiyo ambayo wao huiita Metro iliondoka mchana wa siku hiyo kabisa kutoka London kuelekea Paris, Laurent akiwa ndani yake. Katika meza aliyoketi alikuwa peke yake, kiti cha mbele yake ambacho alitegemea kuketi na Tracy, hakikuwa na mtu. Akaitazama saa yake akajaribu kufananisha. Atoke Marekani afike London tuonane kwenye Metro ndani ya saa saba! alijiwazia huku akiendelea kunywa kinywaji chake taratibu. Akiwa katika mawazo huku akitazama kwenye dirisha akajikuta hayuko peke yake tena, akageuka na kukutana uso kwa uso na mtu asiyemjua, mwanaume mwenye sura ya kitoto. Mtu huyo hakuwa na maongezi marefu.

“Nipe mzigo,” akamwambia Laurenti, yeye akapigwa na butwaa akiwa hajui nini cha kufanya, Huyu ndo Tracy? Akajiuliza. Hakupata jibu.

“Muda unakwenda, nipe mzigo,” yule kijana akakazia kauli yake. Laurent akampa bahasha, yule kijana akaifungua na kutoa picha tano tofauti za Bwana Touzony, kisha hundi ya Paundi za Kiingereza Milioni tano.

“Ok!”.

Yule kijana akasimama na kuondoka kuelekea behewa la nyuma.

Laurent akaingiwa na wasiwasi, vipi kama huyu si Tracy?, akajiuliza, akainuka kumfuata, akamuona akiishia katika mlango wa behewa la nyuma yake, akamuwahi lakini alipofika kwenye lile behewa, hakuomuona yule mtu, kapotea. Lauretnt akajua kama sio jinni basi shetani, akarudi kitini kwake na kuketi.

Alijaribu kuyatauliza mawazo yake dhidi ya mtu huyo lakini haikuwezekana, alifikiria itakuwaje kama atakuwa kampa mtu mwingine pesa na picha ya mlengwa, ubongo wake ulisawajika kwa mawazo mapya. Aliamua kumsaka mtu huyo kabla treni ile haijasimama. Alizunguka kila behewa kuangalia lakini hakumuona hata wa kufanana naye. Laurent hakujua la kufanya aliinua simu yake na kupiga kwenda namba anayoijua yeye, simu ikapokelewa, ilikuwa ni ya mmoja wa watu waliompa kazi na alitakiwa atoe taarifa mara tu akionana na Tracy. Alijuwa kwa vyovyote atapata shida kueleweka kwa uzembe alioufanya. Lakini alishangaa alipoambiwa ‘well done’ na kisha simu kakatwa.

SIKU ILIYOFUATA

Akiwa ndani ya suti nyeusi iliyobeba umbo lake la kike lililovutia wanaume waliokuwa wakimwangalia wakati akishuka katika gari iliyomleta. Kila mtu alimwangalia mwanamke huyu wa kizungu lakini ngozi yake ilikuwa imepoa kwa rangi, ilikuwa kama aliyekaa juani muda mrefu, miwani nyeusi iliyaficha macho yake ya buluu, macho ya paka, viatu virefu vyeusi vilimbeba na kumfanya atembee kwa mwendo wa madaha. Alizivuta hatua za wastani kuelekea pale kwenye ule mnara mkubwa kabisa na maarufu duniani, mnara wa Eiffel uliopo Champ de Paris, mnara mkongwe uliojenga kati ya miaka ya 1887 na 1889, mnara uliojengwa kwa vyuma tupu, uliosanifiwa kitaalamu na Stephen Suvestre, wenye sakafu tatu na lifti tisa za kukupandisha juu na kukushusha chini.

Tracy, aliingia kwenye moja ya lifti hizo na kunyanyuliwa kuelekea juu kwenye sakafu ya tatu ambako ndiko liliko windo lake, alifika na kutoka ndani ya lifti hiyo. Ulikuwa mgahawa mkubwa uliokusanya watu mbalimbali wenye pesa, wakila na kunywa wanachotaka, pesa zilikuwa zikiteketea na kujaza matumbo yao yasiyoridhika.

Mnara wa Eiffel, katika Jiji la Paris. Tracy alipomfanyia kitu kibaya Bwana Touzony

Danford Touzony, pamoja na rafiki zake walikuwa wakiendelea kuburuka pasi na hili wala lile, walikunywa wakacheka, waliongea na kufurahi. Mwanadada mmoja mhudumu wa mgahawa huo, alikuja mpaka kwenye meza ya watu hao, meza aliyoketi Danford akamnong’oneza mmoja wa watu waliokuwa na Danford kwa kuwa haikuwa rahisi kumfikia mlengwa, ukimya ukachukua nafasi.

“Kuna simu ya mheshimiwa,” yule mwanadada alimwambia huyo kijana.

“Ok, nakuja kuisikiliza,” akajibu yule mtu.

“Hapana, simu imesisitiza kuongea moja kwa moja na Mr. Danford,” yule mwanadada alijibu. Kauli hiyo ilimfanya yule bwana kufungua macho ya akili yake, jukumu alilopewa ni kuhakikisha usalama wa mtu huyo, mtu aliyeitwa ‘muhimu’ na serikali ya Ufaransa. Danford Touzony alisimama na kuelekea kwenye kile chumba cha simu, na kama kawaida nyuma yake alifuatwa na yule bwana kwa ajili ya ulinzi.

Tracy Tasha, alikuwa katulia katika meza moja iliyojazwa vinywaji akinywa polepole huku jicho lake lililokuwa nyuma ya miwani yake lilikuwa likimwangalia Danford, mkononi mwake alikuwa amekamata kidubwasha kidogo kama rimoti ndogo kabisa ukubwa wa kidole gumba. Alikitumia kidubwasha hicho kutafuta namba ya simu ya moja ya vijichumba vya simu katika mgahawa huo, akapata, kwa kuunganisha na kipini kilichobanwa sawia katika pua yake chenye uwezo wa kunasa sauti na heleni iliyoweza kumfikishia ujumbe, alichanganyikiwa kidogo kuona badala ya mlengwa wake tu kuinuka aliinuka na mtu mwingine.

“Shiit!” aling’aka kwa sauti ya chini, akaibana vyema ile rimoti mkononi mwake kisha akasubiri kidogo. Alimtazama Touzony, aliyeukaribia mlango wa kile chumba na kisha akampa ishara yule bwana aliyekwenda naye, asubiri hapo nje ya mlango wakati yeye anapokea simu hiyo, lakini kabla hajaingia, yule bwana alitangulia kwanza akatazama ndani ya chumba kile, hakuna jipya, akampa ishara bwana Touzony ya kuendelea kuongea na simu yake, akaingia na kuuchukua mkono wa simu uliokuwa umeegeshwa juu ya kijimeza kidogo.

Tracy alimtazama kwa chati kwa mtindo wa kugeuka kiufundi, alikuwa akisubiri ainue mkono wa simu auweke kichwani, ili afanye yake.

Danford Touzony, aliingia ndani ya kile chumba na kuinua ule mkono wa simu, akauweka katika sikio na ile sehemu ya kuongea akaiweka kinywani.

“Oui,” alianza kwa kuitikia kana kwamba kuna kitu alikuwa ameambiwa.

“Tu es mort!” (umekufa) sauti ya kike ikapenya sikioni mwake. Akajisikia kama anapaliwa na kitu, akakohoa kusafisha koo, lakini bado, akakohoa na kukohoa, akaanza kuishiwa nguvu, akaanguka ndani ya chumba kile, akajishika shingoni huku akikohoa kwa nguvu. Mlango nulisukumwa na yule aliyekuwa nje akaingia na kumkuta Danford akigalagala chini, akaomba msaada na wengine wakaja, wakamsaidia kumbeba Danford, haraka haraka akawekwa kwenye machela, hekaheka zilikuwa kubwa, watu wa huduma ya kwanza walifika, na kumsaidia  kwa hili na lile. Kwa ujumla hali ilikuwa tete katika mgahawa huo. Danford alipakiwa kwenye helikopta ya shirika la Red Cross na kuondolewa kutoka hapo kukimbizwa hospitali huku akiendelea na matibabu akiwa angani.

“Est accompli!” (yamekwisha) akajisemea huku, akiirudisha rimoti yake katika mfuko wa suruali huku akitikisa kichwa kukubaliana na lililotukia, aliinuka kutoka pale alipoketi na kumalizia kinywaji chake kisha akateremka chini kwa kutumia lifti. Huko nje waandishi wa habari walijaa wakimbana maswali afisa mmoja wa polisi aliyeonekana kuwa ndiyo msemaji wa jeshi hilo. Tracy alipita taratibu na kutokea nyuma ya kundi lile, huku akiacha polisi wakipanda kule kwenye ule mgahawa wakiwa na uhakika wa kupata lolote.

***

Danford Touzony alifikishwa katika hospitali ya Taifa mjini Paris, harakaharaka huku akiwa amewekewa vifaa maalum vya kumsaidia kupumua huku chupa za maji zikifanya kazi yake ya kumuongezea maji mwilini hata kama hayakupungua. Machela iliyombeba ilikuwa ikisukumwa na vijana nanne waliokuwa wakikimbia nayo kupita kwenye korido ya hospitali hiyo kuelekea chumba maalum cha uchunguzi. Akiwa juu ya ile machela, mtu huyo alikuwa amelala kimya, hakuongea lolote, na macho yake akiwa ameyafumba. Sekunde ishirini zilitosha umfikisha katika chumba kilichokusudiwa, aliteremshwa na kuwekwa kitandani kisha waganga wenye vifaa vya kisasa walimzunguka, kila mmoja akiwa na kazi yake, kila mmoja akichukua kipimo anachokihitaji, mpishano wa humo ndani hakika ulionesha ni jinsi gani hospitali za wenzetu walivyo makini na kazi yao na jinsi walivyojali uhai wa mwanadamu.

“Je dois payer une visite pour mon patient!’ (nahitaji kumtembelea mgonjwa wangu),Tracy alijisemea huku akiipa milango kadhaa ya hospitali hiyo na kusimama katika mlango wa chumba hicho alicholazwa Danford Touzony, hakuna aliyeruhusiwa kuingia, vidirisha viwili vidogo vilivyotengenezwa katika mlango na kuwekwa kioo kinene vilimruhusu Tracy kutazama ndani na kumuona Danford aliyekuwa kimya kitandani akizungukwa na mitambo tiba pamoja na wauguzi wachache ambao walikuwa wametingwa na kutafsiri michoro na tarakimu mbalimbali zionekanazo katoka mitambo tiba hiyo. Alitaka kuhakikisha Danford amekufa kwani sumu mbaya aliyomtegea kwenye simu ile ilikuwa imefanya kazi yake.

Mara ghafla, moja ya mtambo tiba ilianza kutoa majibu ya ajabu kidogo, wale wauguzi walionekana kuchanganyikiwa, walishika hiki wakashika kile, mmoja akabofya kitufe fulani kilicho karibu na kichwa cha mgonjwa. Tracy aliona madaktari wengine kama wanne wakikimbia kwenye korido kuja pale kwenye kile chumba, akawapisha wakaingia na kuanza kushika hapa na pale, mmoja wao alionekana kujishika kichwani ilhali wengine walichukua vifaa maalum vya kutumia umeme na kujaribu kumwamsha Danford, walijaribu na kujaribu lakini haikuwezekana, kisha wote wakatazamana kwa huzuni, kifaa kimoja baada ya kingine kikaanza kuondolewa mwilini mwa mgonjwa na shuka jeupe likavutwa mpaka, hakukuwa na jambo jipya, Danford Touzony alifariki dunia.

“Au revoir,” (kwaheri) Tracy akaongea kwa sauti ya chini na kuondoka kwenye kile kidirisha bila kutiliwa shaka na mtu yoyote na kuketi katika mabenchi.

Watu watano wa makamo waliovalia suti nadhifu nyeusi waliingia kwenye kile chumba wakiongozwa na daktari mmojawapo, walimpita Tracy aliyekuwa ameketi kwenye viti vilivyojipanga kando ya ukuta wa korido hiyo pana, alimtambua mmoja wa wale watu, alikuwa ni ofisa katia maofisa wa juu wa idara ya usalama wa Taifa ya Ufaransa. Waliingia ndani ya kile chumba, hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuondoa shuka juu ya ule mwili na kuutazama kwa masikitiko huku wote wakiwa wameshika mikono yao kwa mbele. Baada ya dakika kumi hivi walitoka. Pale koridoni, mmoja wao alimuona Tasha akiwa ameketi kakunja nne akisoma gazeti kana kwamba kuna mtu anayemsubiri. Alipohakikisha watu wale wameondoka kabisa na kile chumba hakina mtu isipokuwa mwili wa marehemu tu, aliinuka taratibu na kwa kutumia funguo yake inayoweza kufungua vitasa asilimia 90 vya milango duniani, alifanikiwa kuingia ndani ya kile chumba, kwanza akasimama mlangoni pembeni kidogo, akatazama kwa umakini kisha akajivuta na kuuendea ule mwili, akakamata kidani alichovaa marehemu akakata na kukitia mfukoni. Mara akasikia watu wakiongea nje ya mlango, akainama na kujificha chini ya kile kitanda, walipokuwa wakifungua mlango, akajivuta na kujificha pembezoni mwa kabati, akaiziba kwa mapazia marefu ya dirisha. Wale watu wakafika na kitanda kingine, wakamtoa marehemu na kumweka kwenye kitanda kingine kisha wakatoka nae nje ya chumba hicho. Dakika moja baadae, Tracy akatoka na kuufunga mlango kisha akatokomea anakokujua yeye.

***

Tracy Tasha, binti yatima wa miaka ishirini na nane aliondokea kuwa muuaji mwenye uwezo mkubwa wa kuitekeleza kazi yake katika mazingira yoyote yale na jinsi yoyote ile. Alikuwa mkimya sana asiyependa kuongea, wazazi wake waliouawa miaka kadhaa nyuma katika tukio la ujambazi lililotokea ndani ya nyumba yao huku yeye mwenyewe akishuhudia, lilimfanya awe sugu wa kutoogopa kuua. Alitoroka akihofia kuuawa, akajiingiza kwenye makundi ya kihuni ya vijana wasio na adabu, akavuta sigara, bangi, ndiko huko akajifunza ukorofi, kupigana na vijana wa kiume, kupora, kuuza dawa za kulevya na mengine mengi.

Siku moja alipokuwa akipeleka mzigo wa dawa za kulevya gram 500 kwa tajiri mmoja wa Canada, aligoma kumkabidi mzigo huo kutokana na tajiri huyo kutaka kuuchukua kwa nguvu bila malipo ndipo Tracy alipokuwa Mbogo, yule tajiri akatuma vijana wake wawili wamshughulikie, lakini sivyo alivyotarajia, vijana wake walipata kichapo ambacho hawakutegemea kutoka kwa binti huyo. Bwana Robinson akampenda Tracy, akamchukua kama bidhaa ya bei ghali, akamfadhili na kumwingiza kwenye mafunzo ya upiganaji kwa kutumia mikono ‘Martial Art’, yaani mapambano bila silaha katika moja ya vyuo mahiri huko Marekani. Kutokana na juhudi zake hizo akapata heshima ya juu na kukabidhiwa Mkanda Mweusi, akawa mpiganaji mzuri sana. Miaka kadhaa mbele alikwenda huko Uchina, akaingia tena kwenye mafunzo ya sanaa hiyo na kuendelea kupata tuzo mbalimbali; alipohakikisha kuwa yuko vizuri katika hilo hakuishia hapo, kwa ufadhili wa tajiri yuyo huyo wa huko Tracy alipelekwa Japan kujipima uwezo, nako alifanya vizuri sana kabla ya kurudi Marekani na kujifunza matumizi ya silaha za aina aina.

Mwisho wa kila kitu, Robinson akamtumia Tracy katika kazi zake ngumu, hasa za kupambana na wabaya wake. Mwanamke huyo akaondokea kuwa mahili katika taaluma hiyo, taaluma ya uuaji. Alitumwa akaue, akaenda na akaua iwe kwa bunduki au mikono yake, au kwa sumu ya aina yoyote ile, aliijua kazi yake vizuri. Makachero wa FBI na mashirika ya nje ya Marekani walihangaika sana kumsaka, hawakuweza, kila walipofika katika tukio walizikuta nyayo zake tu, kama marehemu hakupigwa risasi ya kichwa, basi alivunjwa shingo, kama sivyo, basi alifyatuliwa pingili za mgongo, kama la basi alipewa sumu. Walichokifanya ni na kuoanisha tu ni mtindo wa muuaji; ama risasi iliyotumika, au aina ya sumu, pigo na kadhalika, lakini waliwiwa na utata, kitendawili kama muuaji alikuwa ni mtu mmoja au watu tofauti, uchunguzi unaendelea.

 

 

 

 

2

Dar es salaam – Tanzania.

MADAM S ALIIPOKEA NUKUSHI ILIYOINGIA punde tu kutoka katika mashine yake iliyopo pembeni mwa meza yake, ilipomaliza kuandika, aliivuta ile karatasi na kuichana, akaiweka mezani, kabla ya kuisoma akainuka na kuiendea meza ndogo iliyo pembezoni kabisa mwa ofisi hiyo, akawesha birika la umeme na kujitengenezea kahawa, akarudi tena mezani kwake na kikombe mkononi, akaketi na kunywa taratibu. Alikwishahau juu ya nukushi ile iliyoingia muda huo, uzee sasa ulimkabiri. Aliwasha runinga yake ya ofisini na kuendelea kutazama habari ya iliyokuwa ikirushwa na kituo cha Al-Jazeera.

Habari hii ilimvutia sana Madam S, ilikuwa ni juu ya mauaji ya Danford Touzony, mtangazaji aliipamba ikapambika. Lakini bado habari haikuelezwa kinagaubaga juu ya tukio hilo.

Madam S akainua simu yake, akabofya namba fulani na kuweka sikioni.

“Yeah! Kamanda Amata,” akaita.

“Niambie Madam…” akajibu.

“Washenzi wameshafanikiwa, hebu fungua Al-jazeera ujionee,” Madam S alimwambia.

***

Akiwa juu ya kiti chake cha kuzunguka, ndani ya ofisi ya AGI Investment, Kamanda Amata alibadilisha stesheni na kuweka ile aliyoambiwa na Madam. Alilakiwa na picha za Danford Touzony, zilizomuonesha enzi za uhai wake. Aliifuatilia kwa makini, na muda kidogo alimwita Gina wakaungana kutazama habari hiyo, ilyoonesha tukio lililotokea huko Paris saa chache zilizopita.

“Lazima muuaji ni mtaalam anayeijua kazi yake,” Amata alimwambia Gina.

“Kwa nini?” Gina akauliza.

“Kwa kuwa Touzony alikuwa anapewa ulinzi mkali sana, haikuwa rahisi kumpata, wamejaribu kila mbinu ya kumuua lakini wameshindwa, ila sasa mbinu waliyoitumia inanitia wazimu,” Kamanda Amata alieleza.

“Kwa nini wasema hivyo, unafikiri atakuwa ameuawa?” Gina alidadisi.

“Bila shaka ameuwa, kwa maelezo ya daktari pale waliposoma taarifa yake ameuawa kwa sumy mbaya kabisa iliyowekwa kitaalamu kwenye mkono wa simu, muuaji lazima awe mtaalamu sana,” Kamanda alisisitiza kauli yake.

“Sasa, kama simu iliwekwa sumu si wangekufa wengi Kamanda!” Gina alionesha kutoelewa katika kifo hicho.

“Usijali Gina, utajua tu wanavyofanya, yaani hapa muuaji anakusoma mwenendo wa maisha yako ili ajue wapi atakupata kirahisi, hainiingii akilini kuwa hawajamkamata au hata kumshuku, lazima alikuwa pale pale, tabia ya wauaji kama hawa hupenda kufuatilia kujua kama mtu wao amekufa au la, hivyo huyu kwa vyovyote hakutoka eneo lile sema tu kawazidi ujanja kwa namna moja au nyingine,” Kamanda alieleza. Gina alisikiliza kwa makini sana na akatingisha kichwa kuaonesha ameelewa.

Kelele ya simu ya mezani iliwakatisha mazungumzo yao, Gina akainyakuwa na kuiweka sikioni.

“Ufike hapa na Kamanda Amata mara moja,” ilikuwa ni sauti ya Madam S. Gina akarudisha simu mahala pake na kumpa ujumbe Kamanda Amata, mara moja wakanyanyuka na kuteremka chini kutoka katika ghorofa iliyobeba ofisi yao.

Dakika kumi baadae walikuwa katika ofisi ya Madam S, pamoja nao alikuwepo Chiba, Scoba na Dr. Jasmine.

“TSA 1 na wenzako, kuna hii fax hapa imefika, hebu muipitie kwanza kabla hatujaanza mazungumzo,” Madam S akamwambia Kamanda Amata. Akaichukua na kuipitishia macho, ilikuwa ni kurasa moja tu iliyoandikwa kwa mashine.

Ilikuwa ikieleza juu ya tukio la kifo cha Touzony, taarifa hiyo iliyotoka katika shirika la kijasusi la ndani ya Ufaransa ilikuwa ni kuomba msaada wa kupatikana muuaji huyo kutoka katika mashirika mengine makubwa duniani, kwa mara ya kwanza taarifa hizi zilifika katika shirika la kijasusi la Tanzania, TSA. Kulikuwa na picha kama kumi zilizoambatana na taarifa hiyo zikionesha yule anayesadikiwa ni muuaji, picha hizo ziligawanywa makundi matatu, na zilikuwa za watu watatu tofauti, ambao kwa maelezo ya taarifa hiyo ni kwamba watu hao waliingia katika chumba hicho na kutumia simu hiyo kwa tofauti ya dakika ishirini kwa wastani, kati yao mmoja alikuwa mwanamke.

Kamanda Amata alijikohoza na kumpa Chiba ile karatasi pamoja na picha zile. Akamtazama Madam S aliyekuwa bado anaangalia luninga yake iliyokuwa ikipeperusha habari za Mashariki ya kati. Aliposikia kikohozi cha uongo na kweli cha Amata aligeuka.

“Utatuambukiza bwana!” akamtania, “ Enhe sema,” akaongeza.

“Ina maana shirika lao la kipelelezi limeshindwa kumkamata mtu huyo mpaka waombe nje ya nchi haraka hivi?” kauliza.

“Sikia Kamanda, hawa wanaamini kabisa kuwa muuaji kama hayupo kati ya wale watatu basi tayari anaelea angani akitoroka nchi, ndiyo maana wameomba msaada huu,” Madam alitoa jibu.

“Ok, kazi yetu ni nini?” akauliza tena.

“Kuweka ulinzi na kubaini kama mtu huyu au mmoja wa hawa ataonekana hapa nchini tuwape taarifa,”  Madam S akamwambia Amata huku akimwangaliza usoni.

“Kwa hiyo tukiwapa taarifa watakuja kumkamata?”

“Ndiyo maana yake,”

“Kama walishindwa kumkamata pale pale wataweza huku? Ok, basi mi nafikiri hii kazi iko chini yetu, sio kiwango chetu, watawanyie hiyo taarifa idara ya usalama wa Taifa wa ndani ili waweke mitego yao uwanja wa ndege, bandarini, vituo vya mabasi na sehemu zozote zinazotumika kuingia au kutokea watu nje ya nchi,” Kamanda akajibu na kutroa maelekezo.

“Niliwaza hivyo,” Madam akaunga mkono. Baada ya hapo akatoa maelekezo mafupi kwa vijana wake kisha akafanya lile walilokubaliana.

MWAKA MMOJA BAADAE

KIKAO CHA SIRI

NDANI YA CHUMBA MAALUMU ambacho hakuna aliyekuwa akikijua zaidi ya watu hawa watatu, kulikuwa na kikao kizito kikiendelea, kikao cha siri kwa mambo ya siri. Walikuwa wakijadiliana swala zito kidogo lililoonesha kuwachanganya akili ghafla. Walikuwa watatu tu walioketi kwa kutazamana lakini ukiwaangalia hawakuwa kutoka sehemu moja, mmoja alionekana Mzungu kabisa, mwingine alikuwa Mweusi na wa mwisho alikuwa yupo yupo tu, Mwarabu si Mwarabu, Mchina si Mchina ilimradi alizaliwa na anaishi, ilitosha.

Yule Mzungu aliyeonekana kama kuchanganyikiwa, aliwatazama wenzi wake hao wawili waliongia hapo muda si mrefu.

“Tusipoangalia tutaingia mkenge,” aliwaambia wenzake hata bila ya salamu.

“Na mi nilijua tu, nilijua huyu jamaa si wa kumwamini sana, ni ndumilakuwili,” akadakia yule asiye na uraia wa maana.

“Anakiuka, utaratibu, kama mnavyojua tulikubaliana kugawana migodi, Mwadui, Buzwagi na Bulyanhulu ili tumfanikishie yeye mambo yake, sasa tumemuwezesha, na ameweza, mabillion ya dola tumetumia, leo hii anataka kuwapa mali watu wengine, huyu ana akili kweli huyu?” yule Mzungu aliyeonekana kama mwenyekiti wa kikao aliongea kwa hasira na uchungu, mara kwa mara alikuwa akifuta kamasi jembamba lililokuwa likitoka katika tundu za pua yake.

“Haina haja ya kupoteza muda, tuonane nae haraka atueleze kama inawezekana au la, baada ya hapo tutajua la kufanya, sisi sio watoto, tunajua tufanyalo,” alisema yule Mwafrika. Baada ya mazungumzo marefu kati yao waliamua kumtafuta mtu huyo ili wajue nini kinaendelea kati ya mikataba yao.

“Tukutane tena papa hapa baada ya saa tatu, najua tayari tutakuwa na jibu kamili, kazi hii nakupa Namba Tatu uonane na ndugu yetu, utuletee mustakabali, ili leo hii tuiache ardhi hii tukiwa na jibu,” yule Mzungu aliyejulikana kama Kinara kutokana na cheo chake katika jopo hilo alimaliza na kufunga kikao. Kila mmoja alipita kwenye mlango wake alioutumia kuingilia, hakuna aliyejua mwenzake kaenda wapi na anafanya nini.

Saa tatu baadae…

ILIKUWA KATIKA CHUMBA KILEKILE, kama walivyokubaliana, walikutana tena, sasa wakiwa na shauku ya kusikia habari za huyo waliyemtuma, Namba Tatu, kama wanavyomwita.

“Tuambie!” Kinara alifungua kikao kwa neno hilo.

“Nimeonana naye mwenyewe,” yule aliyetumwa akaeleza.

“Amesemaje, maana muda unazidi kwenda,” akadakia yule asiye na uraia wa maana.

“Nimeongea naye kwa muda wa dakika ishirini na tano, ana kwa ana, anasema ‘yeye kwa kuwa tumemsaidia hana budi kulipa fadhila, na katika kulipa fadhila ana mlolongo wa watu ambao wote wanahitaji malipo hayo tukiwamo sisi, hivyo amepanga mambo haya kwa awamu…”

“Kwa awamu!” alishtuka yule Kinara.

“Ndiyo, kwa awamu, na sisi ametuweka kundi la mwisho,” akamalizia kusema.

“Anatuchezea! Anatutania! Hajui tulilokubaliana au amesahau yale aliyotuahidi tulipukuwa pale East Java? Sina muda wa kusubiri, kilichobaki ni kutekeleza kurasa ya mwisho ya makubaliano yetu, basi,” alimaliza yule Kinara.

“Samahani Kinara, kabla ya kurasa ya mwisho kuna kurasa ya mkakati tuliyoifunga kwa pini za dhahabu,” yule mwenye uraia bubu alidakia pia.

“Oooh Shiit! Nilipitiwa, sasa tutamkumbusha baadae kadiri ya makubaliano na kisha tutaona la kufanya kama ni kutekeleza kurasa ya mwisho au tufungue kurasa za siri,” Kinara akaongeza.

“Ok, nafikiri tutekeleze mkataba, tumkumbushe, lakini kurasa yetu ya mwisho iwe ya mwisho, nikiwa na maana kuwa tufungue kurasa ya siri kisha tumalizie kurasa ya mwisho kwa kuwa hii ya siri ipo katikati ya mkataba wetu,” akamalizia yule Namba Tatu.

Kikao kikafungwa na utekelezaji wa hayo ambao ni wa siri zaidi ukasubiriwa. Walichotakiwa wao kufanya ni kutoa taarifa wasipopajua juu ya kile kinachoendelea.

Wakatawanyika.

MIEZI MIWILI BAADAE

MSAFARA WA MKUU WA NCHI ulikuwa ukipita kwa kasi katika barabara itokayo Bagamoyo kuja Dar es salaama mjini. Gari zipatazo sita zilizokuwa zikienda kwa mwendo mkali zikitanguliwa na pikipiki kubwa ya polisi iliyokuwa ikiendeshwa kwa madaha na kijana aliyekuwa juu yake. Baada ya pikipiki hiyo nyuma yake kulifuata gari ndogo ya polisi aina ya 506 Peugeot iliyokuwa ikiwasha vimulimuli juu yake, baada ya hiyo kulikuwa na Land Rover Defender ambayo juu kulikuwa na polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia wakiwa na bunduki zao tayari zikitazama kule wanakoelekea. Nyuma yao ilifuata Land Cruiser moja nyeusi modeli ya VX, iliyokuwa sambamba na gari mbili aina ya BMW nyuma yake kabla ya kumalizia ile ya mwisho ambayo hubeba watu mbalimbali wa usalama.

Ndani ya Toyota Land Cruiser VX alikuwamo Mkuu wa nchi, ametuna katika kiti cha nyuma hapa pembeni yake ameketi mkewe ‘First Lady’. Ilikuwa ni safari ya kutoka kwenye ziara huko Bagamoyo. Na sasa alikuwa akirejea Ikulu kwa ajili ya kuendelea na shughuli nyingine.

Kila mmoja alikuwa ametulia kwenye gari akifikiri hili na lile, mwendo kasi wa gari hizo ulifanya barabara yote kuachwa wazi na kuruhusuzo tu kupita kwa mwendo wautakao. Walikuwa wakikaribia kitongoji cha Bunju, wakiteremka kwenye daraja kubwa la Mto Mpiji, hapo ndipo kila mmoja alipopagawa kwa tukio la ghafla. Walinzi wa gari ya nyuma waliishuhudia ile Land Cruiser ya Mkuu wa nchi ikiyumba na kuacha njia, kisha ikagonga mwamba wa daraja. Dereva alikuwa akijitahidi kuiweka tena barabarani lakini ilikuwa ni ngumu. Ilijipiga tena na kunyanyuliwa juu kabla haijajibwaga chini nje ya barabara. Kitendo cha haraka, wale askari wa kutuliza ghasia walikwisharuka chini na wale wa Usalama wa Taifa walikwishateremka na kukimbilia eneo la tukio, ulinzi mkali ukawekwa ili wananchi wasivamie eneo. Haraka sana makachero waliokuwa katika gari za nyuma walishuka hai hai na kuvunja mlango wa ile gari ya Rais, wakamtoa salama lakini alikuwa akivuja damu nyingi mwilini, mkewe alikuwa amezimia. Dereva wa gari alikuwa hali mbaya baada ya paa la gari hiyo kupondeka na kumkandamiza kitini.

Lilikuwa ni tukio lililovuta hisia za walio wengi, haikuwahi kutokea.

“Mkuu upo salama usijali, sasa hivi tunaelekea Hospitali,” kiongozi wa Usalama wa Taifa mwenye jukumu la mwisho la kumwambia Mkuu ‘Twende’ au ‘Tusiende’ alimwakikishia usalama Mkuu wa nchi.

“Mke wangu yuko wapi?” akauliza.

“Yuko salama Mheshimiwa usijali,” akajibiwa.

Walihaha, walikimbia huku na huku, na muda huohuo helikopta ya serikali ilifika na kutua katikati ya barabara hiyo. Rais akaondolewa kutoka katika gari alimofichwa  na haraka kuwekwa katika Helkopta hiyo pamoja na mkewe ambaye alikuwa hana fahamu kabisa, na dereva ambaye naye halikuwa hajitambui, wakaondolewa mahala pale na kukimbizwa hospitali.

***

KIKAO CHA DHARULA

Idara ya Usalama wa Taifa ilikutana kwa dharula katika ofisi zao za makao makuu huko kandokando ya barabara ya Bagamoyo kujadili hali iliyotokea saa moja iliyopita katika barabara ya Bagamoyo eneo la Bunju Darajani.

“Haiwezekani, gari zote zilikuwa zimekaguliwa ipasavyo, mipira mipya na bora kabisa kutoka General Tyre, iweje mtuambie gari ya Rais inapasuka mpira?” aliuliza afisa mmoja.

“Hii bwana ni hujuma, baada ya ukaguzi wa kina tumegundua mpasuko wa tairi haukuwa wa kawaida ila ni kitu chenye ncha kali kilichosababisha hayo yote, lakini mimi kama mtaalamu wa magari, mipira isiyokuwa na tyubu ndani haichaniki namna ile, yenyewe ikitoboka huisha upepo pale gari inaposimama,” alijibu mtu aliyepewa kazi ya uchunguzi.

“Ok, Comrade, hebu tuambie nini mlikiona barabarani wakati mnapita eneo hilo?” akauliza yule afisa.

Akiwa na bandeji yake katika mkono wa kulia, akajibu kwa taabu kidogo, “Kwa kweli hata mimi nashangaa, maana Rider alipita bila tabu, na ile gari ya polisi ilipita eneo lilelile pamoja na ile ya asakari, lakini gari ya Mheshimiwa ikapata tatizo, tulishuka na kukagua eneo kwa haraka ikiwa ni pamoja na kuangalia katika nyumba za jirani na maduka kama kuna lolote la kutusaidia kupata jibu, hakukuwa na chochote, barabarani hakukuwa hata na chupa au kipande cha chupa,” akaeleza kinagaubaga.

Wakati kikao hicho kikiendelea mara mlango ukafunguliwa na faili moja dogo likaletwa mezani, msichana aliyelileta akamkabidhi yule afisa na kisha yeye kutoka nje. Yule afisa akalitazama na kulifungua ndani lilikuwa na kurasa mbili tu zilizoandikwa kwa mkono, ilionekana mwandishi alikuwa akiandika kwa taabu sana.

…Tumedunguliwa, nikiwa katika mwendo kasi wa kilomita 150 kwa saa mbele yangu upande wa kulia, umbali wa takribani mita 110 palikuwa na mtu mmoja aliyejipenyeza katikti ya vichaka vilivyo kando ya mto,  ghafla na kuinua kitu kama bunduki, sikuweza kujua haraka aina hiyo ya silaha, kabla sijafanya lolote nilihisi gari ikinivuta kulia, tairi ilikuwa imechanika na yule mtu akatoweka.

Nilijaribu kadiri ya uwezo wangu kumuokoa Mheshimiwa kwa adha ile kwa kuigongesha gari kwenye mwamba wa daraja ili kuizuia isilete madhara zaidi, nikafanikiwa (…)

Haikuwa ajali ya kawaida, tumedunguliwa, hakika ni hujuma…

Zaidi ya hapo kulikuwa na maelezo kadhaa ya liyoijaza taarifa hiyo ya dereva wa gari ya Rais. Kila mtu alibaki mdomo wazi, hakuna aliyeamini kinachosomwa hapo.

“Mtu kabisa kudungua gari ya Rais, anajitaka au la?” mmoja aling’aka huku akisimama.

“Lazima apatikane,” mwingine alidakia.

“Sasa hivi naomba kikosi cha watu wane kitumwe eno lile kufanya uchunguzi wa siri, wengine waende hospitali kumhoji zaidi dereva ili atumbie zaidi, kumbuka anadai kamwona mdunguaji, maana hapa kaandika kwa shida, wengine hakikisheni chumba alicholazwa Rais na Mkewe kinakuwa na usalama wa hali ya juu. Nitahitaji taarifa zote kila baada ya saa moja kwa redio zetu za siri,” yule afisa akafunga kikao na wajumbe wakatawanyika kila mmoja akiwa na jukumu la kufanya siku hiyo.

***

BUNJU DARAJANI, eneo lenye wakazi wengi na shughuli mbalimbali za kujitafutia maisha, maduka, magenge, mabaa, vilabu vya pombe za kienyeji vyote hapo palikuwa ni mahali pake. Siku hiyo ya tukio kila mmoja alikuwa kachanganyikiwa kwa namna yake, hawakuwahi kuona tukio kama lile katika maisha yao, hata kulisikia tu katika historia ya taifa lao lililojawa na wingi wa amani, likisifiwa kwa weledi wa hali ya juu wa usalama na upelelezi. Baada ya hali kuwa shwari kabisa, kila kitu kuondolewa mahala pale ikiwamo gari iliyombeba Rais, watu walirudi katika shughuli zao lakini mazungumzo katika vikundi yaliendelea kubaki, vilabuni na hata katika magenge ya bangi.

“Ile mi niliiona tangu inavyoanza kutokea, lakini yule dereva mi namsifu aisee, unajua angekuwa kama madereva wetu hawa, sasa hivi tunashusha bendera nusu mlingoti. Lakini jamaa alicheza nayo mpaka ikagonga ukuta wa daraja, lo!” kijana mmoja alisikika akipiga soga na wenzake wakimsikiliza kwa makini sana, huku wakionekana kushabikia yale anayowasimulia.

“Yaani ilikuwa kama muvi, kaka zile gari zinakimbia ni balaa, dakika moja tu hapa walitanda njagu wa kutosha, wote hatukusogea pale tulikodoa macho kwa mbali tu,” mwingine alieleza.

Wakati mazungumzo hayo marefu yakiendelea, kijana mmoja aliyekuwa kwenye kazi maalum alikuwa ameketi jirani na eneo hilo lakini aliweza kusikia yote kwa umakini kabisa huku akiyameza ili ayakumbuke baadae, alivaa ki-kawaida kabisa, jezi ya Taifa Stars na suruali ya jeans, hakuna ambaye angemzania kuwa ni mtu mwenye jukumu zito hapo alipo, waliendelea kuleta stori.

Upande mwingine wa eneo hilo kulikuwa na wazee waliokuwa wameketi wakinywa kahawa na wengine wakicheza bao, mchezo uliopendwa sana na wazee, huku wakitaniana na kuongea hili na lile. Wakiwa katika hali ile, alipita mzee mwingine wa makamo aliyevalia kanzu ya kawaida kabisa na baraghashia kichwani alisimama mahala pale na kuomba acheze kidogo bao kwa kuwa naye aliupenda mchezo huo. Watanzania hawana hiana siku zote, walimpa nafasi naye akawapa kikombe cha kahawa kila mmoja akafurahi, maisha yakaendelea. Mazungumzo ya wazee yakaendelea na kubwa lilikuwa lile lile la ajali ya msafara wa Rais, yule mzee mgeni alikuwa akisikiliza na kuwapa maneno ya hamasa ili waongee zaidi.

“Ile ajali bwana, hivi wewe kwa jinsi nchi hii ilivyokuwa na wana usalama wenye weledi wa juu kabisa unafikiri mtu anaweza kuhujumu msafara ule! Hata siku moja, kabla hawajapita hapa panakaguliwa pote, mnavyokaa kuwakodolea macho wengine mko nao hapo ni wanausalama,” mzee mmoja alikuwa akiongea kwa sauti ya juu huku akiendelea kucheza bao.

“Wewe mzee umesema, hii nchi kwa upelelezi hata F.B.I wanaiogopa, we ni wewe!” mzee mwingine akadakia.

“Lakini watu nao wajanja siku hizi wameendelea, unaweza kukuta mtu kaja hapahapa ili kuhujumu msafara, siku hizi kuna Boko Haram, Al-Qaeda, ISIS sijui na nani hawa wa Somalia… eee  Al- Shabab,” aliongeza kusema yule mzee mgeni akiwa na haja ya kuwachokonoa wabwabwaje zaidi.

“Yaani mzee mwenzangu umesema, na hawa wageni wageni wanaokuja kujifanya watalii sijui vidudu gani wengine wana mambo yao hawa, sasa we mzee Shomari yule mgeni aliyekuja juzi hapa yule mwanamke akapanga chumba pale Kibilisa Gesti Hausi, hivi kweli we mzungu unaweza kupanga pale chumba, Gesti chafu, inanuka maana ni uzinzi kila kukicha,” akadakia mzee mwingine.

Kwa habari hiyo yule mzee akatega masikio akijifanya yuko bize na bao kumbe alishtuka kidogo, kisha akadakia kusema, “Sasa we unashangaa yeye kukaa gesti kama hiyo wale hata juu ya miti wanakaa, wenzetu sio kama sisi wanajichanganya popote,” alisema.

“Wenzetu sio kama sisi mzee mwenzangu, yule mdada sijui mzungu alivyo pale au chotara, amekaa siku tatu hapa, yuko pale gesti ya Kibilisa,” mazungumzo yakapamba moto.

Baada ya muda huyu mzee mgeni akaaga akaahidi kurudi kesho yake kwani kapenda kile kijiwe, akawanunulia kahawa.

KIBILISA GESTI HAUSI

VIJANA WAWILI WA katika nyumba hiyo ya wageni majira ya saa nne usiku baada ya kuipeleleza na kuhakikisha hakuna mtu aliyetoka wala kuingia mwenye muonekano tofauti na Watanzania. Walipojiridhisha ndipo wakaijongelea gesti hiyo na kuingia mapokezi, walimkuta mwanadada mmoja aliyekuwa akifumua nywele kwa chanuo la mti.

“Habari dada!” wakamsabahi.

“Salama, niwasaidie nini? Kama vyumba vimejaa,” akawajibu huku akiendelea na kazi yake.

“Tunaomba kitabu chako cha wageni,” mmoja wao akamwambia.

“Cha nini? Kwani ninyi ni nani?” akauliza huku akisimama kutoka pale alipoketi kwenye kochi kuukuu. Wakamwonesha vitambulisho vya idara ya Uhamiaji. Bila kusita alitoa kile kitabu kwa maana alishazoea kutembelewa na watu hao mara kwa mara kukagua wahamiaji haramu lakini kilichomshangaza leo ni kuwa sura zilizokuja zilikuwa ni ngeni tupu. Wakachukua daftari na kuanza kulikagua, kila chumba kilichokuwa na shaka kikatiliwa alama.

“Mgeni wa chumba namba 23 yupo?” wakauliza.

“Hapana ametoka tangu asubuhi hajarudi mpaka sasa,” akajibu.

“Ni Mtanzania?” wakauliza.

“Hapana, kwa maana hajui hata Kiswahili vizuri zaidi ya kile cha kuombea maji,” akajibu yule mfanyakazi.

“Kwa nini hapa hukujaza namba ya passport yake?” wakatupa swali linguine.

Yule dada akabaki amebung’aa macho, hakuwahi kufikiri swali kama lile lingemjia.

“Tueleze kwa kina, alikuwa peke yake? Anajishughulisha na nini?”

“Yuko peke yake, ni mwanamke msichana tu, mwanafunzi wa chuo huko kwao Jamaica kwa jinsi alivyoniambia, kila siku alitoka na kurudi usiku, ila leo bado hajarudi,” yule dada akaeleza. Mara hiyo kengele za hatari zikalia kwa makachero wale.

“Tunaomba kukagua chumba chake,” wakasema.

Hatua zikachukuliwa, Mjumbe akafika na mlango wa chumba hicho ukafunguliwa kwa funguo ya akiba, wakaingia ndani ya chumba hicho, wakabaki wametumbua macho, hakukuwa na kitu wala mtu, walipekua hapa na pale mpaka juu ya dari lakini hakuna kilichoonekana, wakakifunga chumba hicho na kuongeza kufuli nyingine ili kisiguswe na mtu kisha wakamchukua yule mfanyakazi kwa mahojiano zaidi wakaondoka naye.

***

Mtaalamu wa kuchora picha aliketi mbele ya yule dada katika kituo cha Polisi Kati, akijaribu kueleza jinsi alivyokua akimuona yule mgeni katika sura tofauti, mara akivaa kofia, mara akitoka na kilemba na kadhalika. Mtaalamu yule wa uchoraji, aliendelea kuchora picha na baada ya maelezo hayo, alizinakshi kwa muonekano mzuri, akapata picha zipatazo kumi na tano tofauti tofauti, akamwonesha yule mfanyakazi wa gesti, hakika, alishtuka sana.

“Ni yeye, yaani kama umempiga picha vile,” akasema. Zile picha zikawekwa katika bahasha na kukabidhiwa afisa wa Usalama wa Taifa kwa muendelezo wa msako dhidi ya mtu huyo.

Picha za mtu huyo zilisambazwa kila kona ambayo ina uwezekano wa kupita kutoka nje ya nchi; Viwanja vya ndege vyote nchini, Bandari, Vituo vikuu vya mabasi, Vituo vya reli. Zaidi ya hapo mahoteli makubwa ya Dar es salaam nayo yalikuwa kwenye taabu siku hizo, kukaguliwa na kupekuliwa kila dakika, kila nanayeingia na kutoka alitathminiwa kikamilifu. Picha zilisambaa na siku chache baadae zilitoka magazetini. Kila mmoja aliziona, kila mwananchi alizitia machoni

***

MADAM S alishusha gazeti alilokuwa akisoma, ‘Mfanyakazi’ akaliweka mezani kabla ya kushusha pumzi ndefu. Juu ya gazeti hilo kulipambwa na picha ya huyo anayetafutwa ikiongozwa na maneno ‘ANATAFUTWA’ na maelezo mafupi yaliyoeleza hasa juu ya wajihi wake yalifuatia.

Watampata tu waongeze juhudi, alijiwazia huku akiendelea kutazama runinga yake ya ofisini. Mara ghafla mlango ukafunguliwa, Madam kwa kkasi isiyofikirika akainyakua bastola yake na kuiweka sawa. Kamanda Amata akaingia katika ofisi hiyo bila hodi, akaketi katika kiti akitazamana na Madam S.

“Vipi, mbona unakuja kwa shari?” Madam akamtupia swali huku akiirudisha bastola mahala pake.

“Hapana, ila kuna kitu kimenifurahisha leo,” akajibu.

“Kitu gani?” Madam akapenda kujua.

“Mdunguaji, anayefikiriwa, ninayo picha ya mchoro wa jana, na nikiitazama inafanana sana na ile tuliyoletewa miezi ya nyuma kutoka Ufaransa” akajibu.

Come on Kamanda, sikuwahi kufikiri hilo, hebu lete hapa,” akasema huku akionesha ishara ya mkono kuwa apewe picha zile.

Madam S akazitazama zilizochorwa Tanzania na zile zilizopigwa kwa CCTV kule Ufaransa, kweli alikuwa ni yuleyule jinsi alivyoonekana kwa  sura yake.

“Kamanda, unataka kunambia yupo hapa?” akanong’ona.

“Sijui, labda ni pacha wake,” akajibu huku akijiweka sawa kitini mwake. Madam S, akamtazama kijana huyu shababi, kisha akatikisa kichwa.

“Hivi unajua idara nzima ya Usalama wa Taifa itapanguliwa punde tu!” akamwambia Kamanda ambaye kwa hilo alikuwa hajui lolote.

“Uzembe?” Kamanda akajibu.

“Sikia Kamanda, sio uzembe, bali tulizidiwa kete, unajua hii hali ya kujiamini kuwa nchi yetu ina amani inatubwetesha sana,” akaelezal, “kuna wageni wengi sana nchi hii, hata hawajulikani kazi zao, wengine wanajifanya Watalii, Wengine sijui misaada ya kibinadamu, wanaitana tu wanajazana, ndivyo tunavyokaribisha magaidi na wauaji wa kimataifa kama hawa Kamanda, lazima vyombo vyetu vya usalama vibadilike sasa, hali ya kuaminiana imekwisha, huu ulimwengu mwingine huu, watu wako kazini, shauri yenu,” akavua miwani yake na kuiweka mezani.

“Madam, usemayo ni kweli kabisa, tunafanya mambo kwa mazoea lakini madhara yake ndiyo haya sasa, tusemeje, alitaka kumuua Rais akasindwa akapasua mpira wa gari?” Kamanda akauliza.

“Hapana,” akajibu Madam

“Kwa hiyo alidhamiria kufanya hivyo, hakukusudia kuua, unajua maana yake ni nini? Tunaamshwa usingizini Madam,” Kamanda akaongeza huku mara hii akiwa kaiegemea meza ya Madam S, baada ya nukta chache za kutazamana, akaendelea, “wao ndio walioshindwa, lakini maadam kafanya haya ndani ya ardhi ya Tanganyika nakuapia, atapatikana tu awe hai au mfu,” Amata alijibu kwa kujigamba.

Msako ulifanyika kila kona ya jiji la Dar es salaam, lakini ilikuwa ngumu kupatikana mtu anayefanana na picha ile. Siku tano zilipita hakuna jibu la matumaini zaidi ya kukamatwa tu wanawake wanaofanana kidogo na huyo lakini walipowahoji waliwaacha tu baada ya kugundua hata kushika manati hawawezi.

Ilipokamilika wiki moja baadae, idara ya Usalama wa Taifa ikapanguliwa na kufumwa upya, wengine wakiwajibishwa kwa kutokuwa makini na kazi yao kwa kubadilishiwa kitengo, Rais alibadilishiwa walinzi wake wa karibu na kupewa wengine, hapa na pale paligeuzwa hivi na vile ilimradi tu kujaribu kuweka mambo sawa. Wale waliokuwa Ikulu walibadilishwa na kupewa idara nyingine ikiwemo kuwapeleka mikoani na wapya kabisa walipewa kazi ya ulinzi wa karibu wa Rais.

***

MWEZI ULIPITA tangu msafara wa Rais ulipokoswakoswa, siku hii Mkuu huyu wa nchi alikuwa ofisini kwake kama ilivyo kawaida, ilikuwa ni Jumatatu na maana ya neno Jumatatu ni ‘bize’.

Mlango wa ofisi yake uligongwa mara mbili haraka haraka na kisha mara moja, akamruhusu mtu aliyekuwa akiingia.

“Karibu sana,” alimkaribisha bwana huyo aliyevalia suti nadhifu kabisa, alikuwa mkuu wa Usalama ambaye ni yeye tu aliweza kumruhusu Rais kufanya jambo fulani kila anaporidhishwa na hali ya usalama wa eneo husika.

“Wageni wako tayari wanakusubiri, waweza kwenda,” akazungumza. Mheshimiwa akanyanyuka na kutoka nje ya chumba cha ofisi na kuelekea ukumbi wa wageni. Alipofika walisalimiana na kuketi kwa mazungumzo mafupi, ulikuwa ni mkutano wa dakika ishirini tu lakini uliojitosheleza. Hazikuwa sura ngeni kwake, alizijua kwa maana alikutana nazo huku na kule duniani wakati akiwa waziri wa wizara nyeti iliyokuwa ikijenga mahusiano na nchi nyingine. Mazungumzo yalikuwa mafupi sana kisha wakamkabidhi bahasha ndogo nyeupe. Ulikuwa ni ujumbe uliotumwa kwake na mtu ambaye hakuweza kufika katika kikao hicho. Akaichana ile bahasha na kuisoma…

…Umetugeuka?

Kwa nini unashindwa kutekeleza upande wa pili wa makubaliano yetu? Sisi tumetekeleza yetu lakini wewe unashindwa kutekeleza yako.

Tunajua kuwa huwezi kuamua peke yako lakini kumbuka nguvu na amri ya dola unayo wewe, ukisema iwe na itakuwa tu.

Sina maneno mengi ila kumbuka kabrasha la makubaliano yetu lina kurasa thelathini na tano tu na sasa nenda ukasome uone tupo kurasa ya ngapi na nini kinafuata baada ya hapa.

Hatufanyi utani katika hili tupo makini …

Ilimaliza barua ile iliyoandikwa kwa wino wa dhahabu. Alikunja sura, akaikunjua, akabasilisha mkao, kijoto kilichochanganyika na kiubaridi kwa mbali kilimpitia kutoka utosini mpaka unyayoni. Baada ya hapo walipeana mikono wakaagana. Wale wageni wakondoka zao na kuliacha jengo la Ikulu. Mheshimiwa Rais aliikunja ile bahasha na kuitia mfukoni mwake, hakumpa yule mtu anayemshikia makabrasha yake, la, hii aliiweka mwenyewe. Akarudi ofisini, kila kitu kilikuwa hakiendi, akachukua dakika chache za kupumzika kwani kichwa chake kili-stuck kabisa.

 

 

3

MIAKA MITATU NYUMA

   WASHINGTON DC

“Sisi tutatimiza ombi lako. Kukufanya wewe ukae madarakani ndio kazi yetu, ukitazama kila kona ya Afrika tumeweka watu, jukumu letu ni kuwawezesha ninyi wenye sisa za mlengo wa pekee madarakani lakini baada ya utawala wako miaka miwili na nusu huna budi sasa kutuwezesha na sisi kadiri ya makubaliano yetu yaliyomo humu, je unakubali? Kama unakubali basi weka saini, maana kwa kusaini tu tayari umekuwa Rais na ukikiuka…” akafungua kurasa ya tano kutoka mwisho iliyoandikwa ‘JIUE MWENYEWE’

Mheshimiwa huyu alishusha pumzi na kusoma tena na tena kurasa hizo thelethini na tano zilizoandikwa kwa wino wa dhahabu, yalikuwa ni makubalino mepesi sana kutekeleza, hata ungekuwa wewe ni mepesi tu, hayakuhitaji damu ya mtu wala kiungo chake bali yalihitaji wewe kufanya watakalo wao.

“Na nikishindwa je?” akauliza yule Mheshimiwa.

“Huwezi kushindwa, sisi ndio tunaweka watu madarakani, uchaguzi wa Rais mwaka kesho ambao wewe unataka kugombea utaigharimu dola ngapi serikali ya Tanzania?” akaulizwa naye akajibu kwa ufasaha kabisa.

“Ok, sisi tutawafadhili pesa za kampeni na mambo yote, alikadhalika tutawatengenezea karatasi maalum, peni za kupigia kura na masanduku ya kuzihifadhi ambayo tunatumia teknolojia mpya inayoendana na karatasi hizo, karatsi ukiziona ni za kawaida kabisa, lakini tunavyowapa kama ni karatasi milioni thelethini basi ujue kura zako za NDIYO ni milioni ishirini na moja bila kuharibika,” akaambiwa, akafarijika.

“Hapo nimekuelewa Comrade,” akajibu Mheshimiwa.

“Basi ni hayo tu, lakini kumbuka, utatawala miaka miwili na nusu kwa manufaa yako na serikali yako, miaka miwili nanusu inayobaki ni kwa manufaa yetu, tutakuja kwa njia nzuri tu kama tulivyokwambia, uwekezaji,” yule Bwana akamweleza Mheshimiwa.

Kila Mheshimiwa alipojaribu kumtazama yule bwana aliyempachika jina la Comrade alishindwa kumuona sawasawa kwani kwa jinsi alivyoketi hakuonekana sawasawa sura yake, hivyo mpaka anamaliza kuongea naye hakumjua ni nani.

***

Kama alivyoahidiwa, aliukwaa uongozi wa nchi bila tabu kwa asilimia za kutosha, kura zilihesabiwa mara kadhaa kwa kushuku kuwa wamefanya utapeli lakini jibu lilikuwa ni lilelile. Ilikuwa miaka miwili na nusu ya neema kama ndoto aliyoiota Yusuph, alijitahidi kutimiza ahadi zake kwa wananchi kwa nguvu kubwa. Hakuna aliyegusa wala kumwuliza juu ya kubaliano lile, wafadhili wake walikuwa wakiangalia kutoka mbali kila linaloendela. Waliendelea kusubiri tu wakati wao ufike, nao waneemeke kwa kuitwaa migodi ya madini inayotoa madini kwa fujo bila kuchoka, walijuwa wazi kuwa ndani ya miaka miwili na nusu waliyokubaliana wangeweza kupata faida maradufu ya pesa waliyofadhili kwa kiongozi huyo.

Ulikuwa ni mkataba wa kitoto, kuwapatia mgodi au migodi kwa majina tofauti na kila mgodi serikali itapata 04% na wao watabeba zilizobaki. Mkataba wa kitoto, utakaowaumiza wananchi, wao walicheka sana huku wakijikuna matumbo yao.

Walijijenga, walikuwa na nguvu ya ushawishi, waliweza kufanya lolote katika dunia hii, walikuwa na uwezo wa kuleta migogoro isiyokwisha ninyi mkipigana wao wakibeba madini na rasilimali zenu kwa kuwapa bunduki na makombora ya kisasa ili muendelee kuuana, wakiwapa condom na dawa za uzazi wa majira ili msiendelee kuzaana, wakiwapa chanjo mbalimbali ambazo ni wao tu wanaojua kazi yake katika miili yenu, leo hii tunashuhudia dada zetu kati ya kumi wawili watazaa salama na wengine mimba zitaaribika au kunusurika kwa msaada wa madaktari wenye utu ambao ni wachache sana hasa kwa wewe usie na ‘njuruku’. Ukitazama kila kinachokuja kutoka ughaibuni kwetu ni ufahari kukinunua, kuwa nacho, lakini wenzetu ndio wanaojua nini walichokiweka ndani yake.  Wametusahaulisha kila kitu, wametuteka akili, tukiuza ng’ombe wetu mamia kwa mamia, tukifanya kazi kuchwa kutwa na kupata mshahara tunakimbilia dukani kununua simu kubwa na kurudi kwetu tukipiga miayo.

 

Rejea sasa….

Miezi mitatu baadae

MGODI WA ALMASI MWADUI

NDEGE ya serikali aina ya Bomberdier ilitua katika kiwanja kidogo cha ndege katika Mgodi huo mkoani Shinyanga. Walioshuka hawakuwa wageni sura zao, alikuwa ni Waziri wa madini na nishati, alishuka akifuatana na watu wengine kama wanne hivi, wakaliendea geti kuu la mgodi huo. Hakuna aliyewazuia, walifunguliwa lango na kuingia ndani yake, moja kwa moja wakasindikizwa kwa ulinzi mkali wa mbwa mpaka ndani ya jengo lenye ofisi za utawala, wakapokelewa na mwanadada mrembo, aliyekuwa katibu muhtasi wa ofisi hiyo.

Akawakaribisha  kwa heshima zote na kuwaruhusu kuonana na meneja wa Mgodi huo, wakapita ndani wakamkuta.

Dr. Justine McLean, alitulia akivuta mtemba wake, akawakaribisha na kuwapa sehemu za kuketi.

“Kama unavyotuona, hatuna muda wa kupoteza, ni dharula na ni lazima itekelezwe, tunahitaji almasi makasha yasiyopungua hamsini sasa hivi, ni amri ya serikali,” yule waziri akamwambia Dr. McLean. Mshtuko dhahir ukaonekana katika uso wa Meneja huyo.

“Kuna utaratibu mheshimiwa wa kufuata hata kama Mgodi ni wa serikali,” akajibu.

“Na mimi ndio waziri mwenye dhamana, na nina kibali cha Ikulu,” akasema huku akitoa karatasi zake na kumpatia. Ilikuwa barua kutoka Ikulu iliyosainiwa na Rais mwenyewe na kugongwa mhuri wa wake. Dr. McLean akarudisha karatasi ile kwa waziri huyo.

“Hapana, hii baki nayo wewe kwa faili lako kama utaletewa shida yoyote,” yule waziri akamkabidhi naye akaipokea na kumwita katibu muhtasi wake.

“Jenny, nenda kwa mkuu wa bohari mwambie atoe kasha hamsini kubwa za almasi ampatie mheshimiwa, serikali inazihitaji kwa shughuli za haraka”.

Jenny  hakuwa na lingine alitoka na kuiendea ofisi kama ya tatu hivi, akatoa maagizo aliyopewa na michakato ikafanyika. Wakiwa ofisini walipewa vinywaji huku mazungumzo ya kikazi yakiendelea. Wale waliofuatana na Waziri ambao waliipendezwa kwa mavazi ya kipolisi walikuwa wakisimamia zoezi la kupakia katika ile ndege.

Baada ya kama dakika kumi tu, binti yule alirudi na kumpa taarifa kuwa zoezi limekamilika kisha yeye akatoka na kuacha wakiagana.

Wakati wafanyakazi na walinzi wa mgodi huo wakiwa nje wakiitazama ndege ile ikipotelea mawinguni, Jenny alikuwa hana hili wala lile, aliendelea kuchapa kazi.

Zilipita dakika thelathini akiendelea na kazi zake, alipoitazama saa yake ilikuwa saa saba za mchana akagundua kuwa amechelewa kupeleka kahawa kwa meneja wake ambaye kila saa saba kamili lazima apate kinywaji hicho. Harakaharaka akandaa katika birika la umeme, alipokamilisha na kuweka katika chano vikombe viwili vya kahawa kwa boss wake Muingereza na mgeni wake, akauendea mlango wa Dr. McLean, akaususukuma kwa mgongo na kugeuka na chano yake kuingia ndani. Akasimama ghafla, ile chano ikamtoka mikononi mwake na kuanguka chini, vikombe vikatawanyika, hakuamini anachotazama mbele yake.

Dr. McLean alikuwa amelalia meza na damu nzito ikimtoka na kusambaa mezani, mgeni wake hakuwepo ofisini. Jenny alipiga kelele za msaada  hakuna aliyesikia ndipo alipokumbuka nobu ya hatari iliyopo chini ya meza yake, akaikimbilia huku mwili wake ukiwa umejaa hofu, akaibonyeza na dakika hizohizo walinzi waliingia kwa fujo na kumkuta binti yule akitetemeka, akiwaonesha ishara ya mkono kuwa waelekee ofisini kwa. Wote wakapigwa na bumbuwazi, wakashangaa kumkuta meneja wao katika hali hiyo.

Ilikuwa ni hali ya kuogofya sana, Jenny hakuweza kuielezea alibaki kimya muda wote huku chozi likimtoka. Nusu saa baadae polisi walifika na kufanya utaratibu wao ikiwamo na kuchukua maelezo kwa watu wawili watatu kuchukua alama za vidole kila ilipobidi na kuchukua picha za mwili wa marehemu kisha kuuondoa mwili wake.

“Mnafikiri nani atakuwa kafanya hivi?” wakauliza, lakini wafanyakazi wakabaki kutazamana,

“Mbona mnanitazama, haya nahitaji wafanyakazi wote hapa, haraka,” yule polisi mwenye cheo cha Inspekta akatoa amri na baada ya dakika tano wafanyakazi wote wakafika, lakini walipotazamana mmoja hakuwepo.

“Ndiyo wote ninyi?

“Hapa Boharia hayupo,” akasema fomeni wa mgodi baada ya kuwatazama wote.

“Yuko wapi? Na kwa nini hayupo? Naanza kumtilia mashaka, kamwangalieni ofisini mwake, mumlete hapa haraka, tunataka tufanye kazi,” akatoa amri. Lakini mtu aliyetumwa alirudi na jibu tata. Boharia naye alikutwa amekufa.

***

MADAM S alibaki kinywa wazi, hakuelewa mambo yanavyokwenda, likitoka hili linakuja lile na yote yamejawa utata, aliitua simu taratibu kutoka katika sikio lake na kuipachika katika kikalio chake kwa jinsi hiyohiyo. Akaurejesha mkono wake mezani lakini hakugundua kuwa hata ukope wa jicho lake haukuwa ukifumba, hakutabasamu wala hakukasirika alibaki yupoyupo tu.

Simu ilitoka Ikulu, ikimpa taarifa juu ya tukio la Mwadui.

“Haiwezekani, waziri! Waziri kabisa anaweza kufanya hivyo?” alijiuliza kwa sauti ya chini ambayo mtu wa pili hakuweza kusikia. Akainuka na kuiacha meza yake, kisha akakiendea kioo kikubwa kilicho pembeni ya ofisi yake, akajitazama na kujiona jinsi umri unavyomuacha.

Yanipasa kupumzika na kazi hizi zinazonipa msongo wa mawazo kila kukicha, akawaza huku. Akairudia meza yake, akainua simu na kubonyeza tarakimu kadhaa, akaitega sikioni.

“Uje sasa hivi, acha lolote unalofanya,” akakata simu mara tu alipomaliza kusema hilo. Akajibwaga kitini na kupitisha mkono wake kwenye mvi za kichwa chake zinazoongezeka kila kukicha.

Dakika kumi na mbili zikatim, mlango ukafunguliwa kwa pupa na kijana aliyemtarajia aliingia, Amata Ric au Kamanda Amata alisimama akimtazama mama huyu aliyeonekana kuchanganyikiwa kiasi fulani.

“Madam!” akaita.

Mwanamama huyo badala ya kujibu akamuonesha ishara ya kuketi kitini, naye akafanya hivyo.

“Kuna mambo yanayotokea kila kukicha katika serikali yetu, mi yananipa mashaka, kuanzi lile la msafara wa Rais miezi mitatu iliyopita kuna vitu sijui tuite vituko au tuiteje, vinanitia wasiwasi Kamanda,” Madam alieleza huku akionekana wazi kuchoshwa na kazi.

“Ndio Madam, lipi tena limetokea hata unite kwa haraka na ghafla namna hii?” kamanda akauliza.

“Kamanda!” akaita huku akisimama wima na kumatazama kijana huyo usoni. Kamanda Amata akajua wazi kuwa sasa kuna jambo lisilo la kawaida, maana alikwishazoea Madam S akikwambia jambo huku amesimama mkitazamana basi ujue hilo jambo ni siriasi sana na ulifanyie kazi kwa nguvu zote, lazima ujue kuwa anakutuma, hivyo Kamanda naye akasimama kwa heshima ya kikazi kumsikiliza mkuu wake.

“Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini, wiki hii yupo katika ziara ya kutembelea migodi yote inayoendeshwa na serikali, lakini jambo la kushangaza na kusikitisha limetokea, amefika katika mgodi wa almasi pale Mwadui dakika sabini na tano zilizopita na kuchukua makasha hamsini ya almasi na kuondoka nayo akisema kuwa katumwa kutoka Ikulu na ameonesha barua iliyosainiwa na kuwekwa muhuri wa Rais, Kamanda Amata naoma sasa hivi tunavyoongea uanze uchunguzi wa kina wa kadhia hii na unipe majibu kila baada ya dakika sitini za uchunguzi wako. Sawa?”

“Yes, Sir” kamanda akajibu kwa utani kama kawaida akikutana na Madam S.

“Ukihitaji msaada wowote unajua la kufanya! Haya ondoa mkia wako hapa!”

Kamanda Amata akatoka na kuchukua gari yake, kwanza aliona ni lazima afike nyumbani kwake, Kinondoni ili kuchukua zana zake za kazi zitakazomfaa kwa siku hiyo. Kichwani mwake alipanga kuwa pa kuanzia uchunguzi wa tukio hilo ni Mwadui palepale. Aliinua simu yake na kumpigia Gina aliyemwacha ofisini kwake akiendelea na majukumu mengine ya uongo na kweli.

“Naomba nitafutie chata ya kukodi, nina safari ya haraka kuelekea Mwadui mchana huu,” alipomaliza tu akakata simu, hakuwa na muda wa kuendelea kuzungumza.  Aliingia ndani na kuufunga mlango nyuma yake. Moja kwa moja akaelekea chumbani kwake, hakukuwa na jipya akajiandaa na kujitoma maliwato, akajiswafi na kurejea tena chumbani, akachagua silaha za kumfaa, akazipachika katika mkoba wake maalumu ambayo hata ukipekuwa vipi huwezi kuziona, akazipanga, zikapangika. Bastola mbili zilizojaa sawasawa zikawekwa kiunoni mwake, suti nadhifu ikafuata juu yake. Kamanda Amata akasimama mbele ya kioo akajitazama, waoh, akaonekana mithili ya mfanyabiashara maarufu duniani.

Kamwe hawatanijua kuwa mimi ni nani katika nchi, akajiwazia. Kisha akachukua kofia yake aina ya pama na kujitupia kichwani. Akainua mkoba wake na kutoka taratibu mpaka mlango mkubwa, akaminya nobu zake za siri na kuwasha mtambo wa usalama unaoruhisi kamera za siri kunasa picha zote ndani ya nyumba yake, kamera hizo ni yeye peke yake anayezijua hata Gina ambaye mara nyingi hulala katika nyumb a hiyo bado hakujua juu ya kamera hizo.

“Kamari wapi?” Scoba akamtupia swali Kamanda Amata wakati akiingia garini tayari kwa safari ya uwanja wa ndege.

“Mwadui Cassino, Shinyanga,” kwa jibu hilo wote wakacheka na kugonganisha viganja vya mikono yao, kisha ile gari ikaondolewa na kushika barabara ya Kinondoni makaburini kuelekea Ubalozi kabla ya kuikamata ile ya Ally Hassan Mwinyi mpaka Bibi Titi na kumalizia ya Pugu kupitia mpaka Uwanja wa ndege.

***

Gina alisimama kando ya ua kubwa lililokuwa nje tu ya mlang wa kuingilia Uwanja wa ndege wa jeshi, Terminal One, alipoona gari ya Scoba inaingia, akajitokeza na kuiendea, moja kwa moja alimwendea Kamanda Amata.

“Umependeza dear! Kama unaenda harusini,” Gina akamwambia Kamanda huku akimkumbatia na kumbusu.

“Yeah, ukipendeza namna hii kamwe adui zako hawatajua kama ni mtu wa hatari, watalegeza silaha zao na kukukaribisha kahawa,” akajibu huku akimtoa Gina kifuani mwake, akamtazama usoni,

“Gina, nitahitaji msaada wako wa hali na mali.”

“Sawa Boss!”

Kamanda akatoka na kuiendea ndege ndogo iliyokuwa tayari kwa ajili yake kumfikisha aendako, akafunguliwa mlango na kuingia ndani yake, akaketi na kufunga mkanda. Safari iaanza.

***

Saa tisa mchana Kamanda Amata alitua katika uwanja mdogo wa ndege wa Mwadui, uwanja uliojengwa pembezoni kidogo mwa mgodi huo. Kwa kuwa alikuwa peke yake, haikuchukua muda kutoka nje ya ndege hiyo na moja kwa moja kuelekea jengo lenye ofisi za utawala. Akapokelewa na Inspekta wa polisi aliyekuwa hapo akimsubiri baada ya kupewa taarifa ya ujio wake.

“Karibu Mwadui,” akamkaribisha.

“Asante sana Afande, nipe taarifa ya hapa na nini kimetokea,” Kamanda akamwambia yule Inspekta huku wakiongozana kuingia ndani ya jengo la utawala pamoja na wafanyakazi wachache wenye nyadhifa za juu katika Mgodi huo. Wakaketi kwenye ofisi ya Jenny.

“Kwanza poleni sana kwa matatizo, hebu niambieni vyema, ilikuwaje, nani amefanya mauaji haya na kuchukua hizo almasi?” akauliza.

“Alikuja Mheshimiwa Waziri wa Nisahati na Madini, akifuatana na vijana wa jeshi la polisi wawili waliovalia sare za jeshi hilo, walikuja kwa ndege ya Serikali…” Inspekta alieleza hali yote ilivyokuwa kadiri na yeye alivyoambiwa na kuandika kwenye kijidaftari chake.

“Mnaweza kunambia hiyo ndege ilifika hapa saa ngapi?” akauliza tena.

“Ndege ilitua hapa kati ya saa 5:20 na 5:40 hivi asubuhi ya leo.” Akajibu msemaji wa ofisi hiyo.

“Sawa, na ninyi mlikuwa mkimtegemea Waziri saa ngapi na kwa lipi?” Kamanda akatupa swali.

“Tulimtegemea muda uo huo, lakini alikuwa anakuja kwa ajili ya kukagua mgodi, badala yake tukapewa taarifa ameagizwa kuchukua almasi kwani zilihitajika serikalini kwa shughuli ya haraka, na alikuwa na uthibitisho ambao ni barua kutoka Ikulu,” akajibiwa.

Kamanda Amata akatikisa kichwa na kuuliza tena maswali kadhaa, kisha akaomba kukiona chumba cha Dr. McLean, akapelekwa. Alisimama mlangoni, akakiangalia jinsi kilivyo na kupangwa vilevile, kilichokosekana ni mhusika tu wa ofisi hiyo ambaye tayari muda huo alikuwa barafuni katika Hospitali ya Mkoa Shinyanga.

Alisogea na kuketi kwenye kiti cha mgeni akikitazama kile cha Dr. McLean, akazungusha macho yake huku na kule, akasimama na kuzunguka upande wa pili, akaangalia huku na kule kisha akafungua mlango wa chooni akatazama vizuri zaidi, akajifungia ndani ya choo hicho, alitazama kila kilichomo kwa makini kabisa, hakukuwa na kipya zaidi ya sinki la choo, sehemu ya kuogea, magazeti na majarida katika mfuko maalumu uliobanwa nyuma ya mlango. Akageuka huku na kule, kisha akatoka.

“Ok, sasa naomba nipeleke kwenye ofisi ya boharia,” akapelekwa na kuikagua kwa mtindo uleule, kisha wakarudi wote pamoja.

“Sawa, hakuna la zaidi, naomba niende lakini, ofisi hizo mbili zisiguswe na mtu yeyote mpaka mtakapopata taarifa nyingine,” akamgeukia yule afisa na kumuuliza, “Enhe ofisi hii ambayo ni mapokezi nani anahusika (…) nahitaji kuonana naye,” akasema.

“Aaa huyu dada tumemuhifadhi kituo cha polisi ili kuisaidia polisi,” akajibu Inspekta.

“Ok, nahitaji kumuona,” akasisitiza.

Kamanda Amata akatoka pamoja na Inspekta wa polisi na vijana wawili kutoka jeshi hilo, kwa kutumia gari ya polisi walielekea kituo kikuu cha wilaya ambako huko alihifadhiwa Katibu Muhtasi wa ofisi ile.

Mnamo saa kumi za jioni walifika katika kituo hicho na kukuta makundi ya watu pembeni mwa jengo hilo wakiongea hili na lile kama ilivyo kwa kituo chochote cha polisi, wapo waliokuja kuwaona ndugu zao, wapo waliokuja kuwawekea dhamana, wapo waliokuwa kwa hili na ile lakini pia wapo waliokuja kujaribu kuvunja sheria ya nchi, kupenyeza ‘Rupia’ ili kesi zao ziuawe kimazingara.

Kamanda Amata akifuatana na yule Inspekta moja kwa moja walielekea katika moja ya ofisi za kituo hicho, ofisi ilikuwa tupu isipokuwa meza moja ya mbao, viti viwili vya mbao upande huu na upande ule wa meza. Amata akakalia kiti kimoja kile ambacho kipo upande wa mlango, ambacho kwa vyovyote angetakiwa kukaa mgeni au mtuhumiwa kama inabidi wakati mwenyeji wake angekaa kwenye kile kinachoutazama mlango ili amuone mgeni wake au mtuhumiwa wake anapoingia, Amata alifanya tofauti. Mara mlango ukafunguliwa nyuma yake, akiwa anatazama simu yake kubwa aina ya Iphone, Kamanda Amata aliweza kuona yanayotukia nyuma yake, mwanadada aliye na nywele timu timu, alikuwa akiingizwa ndani ya chumba hicho akiwa na pingu mkononi mwake huku akiongozwa na WP mmoja.

“Mheshimiwa, ungekaa upande ule ili huyu akae huku,” yule WP alitoa maelekezo kwa Amata.

“Asante, lakini kwa leo nampa upendeleo wa pekee, muweke aketi kule mimi nitaketi hapa,” Kamanda akajibu. Yule WP akampeleka msichana yule katika kiti cha upande wa pili. Mara nyingi sana kosa hili hufanywa na wengi, kumuweka mtuhumiwa au mtu ambaye unajua kabisa anaweza kukusababishia hatari fulani upande wa mlango, kama ana silaha yoyote akikudhibiti huwezi kumkimbia, lakini kumbe ukikaa wewe mlangoni yeye upande usio na mlango basi unaweza kumkimbia au kumdhibiti asitoroke.

“Mfungue pingu, huyu sio mhalifu, mnafanya kosa,” Kamanda akatoa amri, “Kisha utupishe kidogo,” akaongeza kusema mara tu yule WP alipoanza kuzifungua pingu zile . Alipomaliza zoezi lile yule WP akatoka na kuwaacha wawili hao peke yao ofisini. Kamanda Amata akainua uso wake na kumtazama yule binti. Alikuwa mweupe wa wastani, nywele ndefu ambazo kabla ya mkasa huo ilionekana zilikuwa katika mtindo mzuri sana, macho yake yaliyokuwa yamelegea kidogo yalimfanya Amata kujua kuwa mwanadada huyu hutumia miwani kwa kuona na kusoma. Alimtazama kwa makini sana, akashusha macho yake taratibu, akasimama kifuani, kifua kilichokuwa kikipanda na kushuka kwa hofu, yote hayo Amata aliyang’amua kwa sekunde kadhaa, kwa jumla aligundua kuwa msichana huyo hajaolewa kwani alikuwa na kila dalili za kuwa ‘singo’.

“Naitwa Kamanda Amata,” alijitambulisha bila kificho mbele ya mrembo huyo. Na hapo aliuona mshtuko wa wazi kutoka kwa huyo binti aliye mbele yake, aligutuka na kuacha kinywa wazi kiasi kama mtu aliyeona Malaika aliyemtokea ghafla.

“Kamanda Amata!” akashangaa na kusema kwa sauti ndogo. Msichana huyo hakuamini kama mbele yake kakutana na mtu aliyekuwa akimsoma tu kwenye riwaya za magazeti na vitabuni, hakuwahi kufikiri kama yupo kiumbe hai mwenye aina na sifa hizo, hakuamini, alitikisa kichwa akakumbuka visa kadhaa vya kijasusi vilivyomhusisha kijana huyo kama mpelelezi namba moja wa serikali katika idara nyeti ‘invinsible’, anayetatua migogoro iliyogubikwa na siri nzito kwa siri vilevile. Hakuwahi kujua kama mtu huyo yupo au inawezekana kuwepo, mara nyingi alizoea kusikia tu watu hasa vijana wakijipa jina hilo kujionesha kuwa wao wana ndoto za kuwa kama mtu huyo. Hakuamini alijua wazi kuwa hata huyu ni mmoja wa hao wanaojipachika jina hilo. Lakini sasa alikuwa mbele yake, hata hivyo hakuamini, na mawazo yake yalishirikiana vyema na akili kuupinga moyo katika kile inachoamini.

“Naitwa Jenny,” naye akajitambulisha kwa kitetemeshi.

“Usiogope Jenny, nimekuja kukutoa na kukuacha huru kama mwanzo, lakini nataka kuongea na wewe mambo kadhaa yaliyojiri pale ofisini kwenu leo asubuhi,” akameza mate. Kwa kuanza alimtaka Jenny ajieleze juu ya maisha yake kwa kifupi, hapo Kamanda Amata alipata kujua kuwa Jenny ni binti wa Kichaga, aliyezaliwa huko Kiboloroni katika miaka kama ishirini na tatu iliyopita. Hakika Kamanda Amata hakuwa mbali na ukweli kwani alipomuona tu, muonekano wake ulijieleza, Mchaga wa Rombo.

“Niambie, juu ya kisa kilichotokea leo ofisini kwako,” Kamanda akamuomba, na Jenny akaeleza kila kitu kuanzia kufika kwa wale wageni, walikuwa wangapi na ni nani na ni nani kwa wale aliowajua. Kisha Amata akaanza kuuliza maswali ambayo kwayo labda yangempa mwanga katika kisa hicho tata.

“Mlikuwa mnategemea ugeni huo saa ngapi?”

“Tuliutegemea saa tano kama na nusu hivi.”

“Na ulikuwa unajua kuwa ugeni huo ulikuwa unakuja kufanya nini?”

“Kwa taarifa za wizara, tulijulishwa kuwa ugeni huo unakuja kwa ajili ya kutembelea na kukagua mgodi.”

“Umesema kuwa ulimgundua McLean akiwa ameuawa ofisini mwake wakati ulipokuwa ukipeleka kahawa, je ulitegemea kukuta watu wangapi ndani ya ofisi hiyo?”

“Kwa kweli nilitegemea watu wawili tu kwani wale polisi na wengine walikuwa wakishughulikia kupakia almasi ndegeni.”

“Na ulipomkuta Mc Lean ameuawa, je ulimkuta mtu mwingine ofisini?”

“Hapana, alikuwa peke yake.”

“Na huyo mgeni mwingine ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini uliuyetarajia kumkuta, ulimuona alipotoka?” Hapo Jenny akatulia kidogo, sekunde kadhaa zikapita, akashusha pumzi na kumeza mate, akajaribu kukumbuka jambo.

“Hapana, sikutazama kama alikuwepo maana akili yangu ilipaa baada ya kuona mwili wa Mc Lean.”

“Ok, kwa hiyo inawezekana alijificha nyuma ya mlango au kabatini?”

“Mh!” Jenny akaguna, “Labda lakini sina uhakika kwa kuwa milango ile ni ya aluminium, ile ya kuslide.

“Sasa unafikiri alikuwa wapi, au alipita na wewe hukumuona?” lilikuwa ni swali lingine ambalo lilimpa shida Jenny.

“Hapana, hapana, hakutoka kabisa na ofisini hakuwepo,” akajibu huku akipumua kwa nguvu.

“Je kuna mlango wowote wa siri kwenye ofisi ya Mc Lean ambao mtu anaweza kuutumia kutoka nje bila kujulikana?”

“Hapana, sidhani kama kuna kitu kama hicho,” akajibu.

“Basi hilo lilikua pepo, au we unasemaje?” Kamanda akauliza tena lakini mara hii akitoa cheko la mbali kidogo.

“Swali la mwisho,” akatamka, na Jenny akamtazama Kijana huyo usoni kidogo kisha akashusha macho yake chini.

“Unafikiri, waziri mwenye dhamana anaweza kuja na kuua bosi wako kisha vibaraka wake au yeye kuua mtu wa stoo, na kuchukua almasi ambazo ni mali ya serikali?”

“Hapana haiwezekani,” Jenny akajibu.

“Kwa hiyo unataka kunambia ni nani aliyeweza kuja na ndege ya serikali na kufanya hujuma hiyo, majambazi? Au magaidi?” akahoji huku akiwa ameikaza sura yake. Jenny akatulia kimya, hakuwa na jibu, alibaki kumwemwesa midomo tu.

“Jenny!” Kamanda akaita kwa kushtukiza. Jenny akashtuka na kunyanyua uso wake ghafla na kumtazama usoni huku akihema kwa mshtuko, machozi yalikuwa huku na huku, mashavu yake yaling’azwa kwayo, uzuri wake uliojificha nyuma ya vipodozi vya kisasa ulidhihirika wazi. Amata akatabasamu, akahisi moyo wake ukipiga harakaharaka, ikawa zamu yake kutazama chini, kisha akamtazama tena binti yule.

“Ok mrembo, kama kutakuwa na lolote ninalolihitaji nitakutafuta, kwa sasa utaachiliwa huru, lakini, usizungumze na mtu yeyote juu ya hili, hata mpenzi wako usimwambie lolote, ukikiuka ujue ndio mwisho wako,” Kamanda Amata akamaliza na kuinua simu ya mezani hapo akazungusha namba Fulani kisha akaita mtu wa upande wa pili.

WP yuleyule aliyemleta Jenny alikuja tena na ile pingu mkononi, nyuma yake akafuata yule Inspekta.

“Naomba mfanye utaratibu wenu, huyu aachiwe huru, aendelee na shughuli zake lakini kila baada ya siku aje hapa kuripoti, na asipoonekana atafutwe mara moja mpaka utata huu ukipatiwa ufumbuzi.

Baada ya dakika kadhaa Jenny aliachiwa huru na kupewa masharti hayo na polisi. Kamanda Amata aliagana na Inspekta na kumwambia kuwa muda wowote ataonana naye kama atahitaji msaada zaidi.

“Naweza kukusindikiza mpaka nyumbani kwako?” Kamanda akamuuliza Jenny, mara alipomkuta nje kaketi kivulini akifikiri hili na lile.

“Nitashukuru,” alijibu kwa unyonge. Kamanda Amata akakodi tax akaingia pamoja na Jenny, wakaondoka eneo lile.

 

DAR ES SALAAM saa 10:23 jioni

MADAM S ALIKUWA HAJANYANYUKA kutoka kitini kwake tangu alipoagana na kijana wake, zilikuwa zimepita saa takribani sita, hata hamu ya chakula hakuwa nayo, mawazo lukuki yalimtawala kichwani.

Simu ya mezani kwake ikaita, akainyakuwa na kuitega sikioni, upande wa pili sauti nzito ya kiume ikaita.

“Ndiyo Kamanda, tumesitisha kila aina ya uchunguzi mpaka tupate jibu kutoka kwako,” akaongea na mtu wa pili. Baada ya mazungumzo mafupi, Madam S alimwita Kamanda kurudi Dar es salaam mara moja kwa lengo la kujumuisha mambo kadhaa.

Usiku wa siku yiyo hiyo…

KAMANDA AMATA AKIWA NA MADAM S pamoja na Chiba walikuwa Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar es salaam kwa kikao cha kazi.

“Kwa hiyo, unasema ndege iliondoka hapa saa ngapi?” Kamanda Amata alimuuliza Mkuu wa Idara ya mambo ya anga anayeratibu safari za ndege kutoka na kuingia nchini.

“Ndege ya serikali, iliondoka saa moja kamili asubuhi, ikaelekea mgodi wa North Mara, taarifa tulizonazo ni kuwa, ilifika kule saa mbili asubuhi na wakaondoka tena saa nne kuelekea Mwadui ambako saa tano na dakika ishirini walitua pale,” Mkuu wa Idara akatoa ufafanuzi.

“Sawa, nimekuelewa, je; kwa sasa baada ya ile ndege kuruka pale Mwadui, mmeweza kuiona imeelekea wapi?” Madam S aliuliza.

“Ile ndege baada ya kuruka Mwadui, ilionekana kuelekea Kaskazini, na ikatupotea kwenye rada zikiwa zmebaki kilomita chache kufika mpakani na Uganda,” akaeleza.

“Ok, naomba muendelee kuitafuta popote ilipo, na mtupe taarifa pindi tu mkiiona,” Madam S akatoa amri. Wakanyanyuka na kutoka katika ofisi hiyo. Safari ilielekea kwa Katibu wa Wizara usiku huohuo.

Mikocheni B, Scoba alikunja kona kulia na kufuata  barabara inayoelekea katika afisi za The Guardian, baada ya kuipita mitaa miwili akakunja kushoto na kufuata barabara ya lami inayopita katika mtaa maarufu ambao umebeba majumba kadhaa ya mawaziri na watumishi wakubwa wa wizara. Nyumba ya kwanza, ya pili, ya tatu, akaegesha gari pembeni na kusimama. Wote wakashuka na kuliendea lango la jumba hilo la bei mbaya, mali ya serikali. Wakakaribishwa na mlinzi wa  kimasai aliyekuwa akilinda mlangoni, haikuwa tabu kwao kuruhusiwa kuingia katika kasri hilo.

Waliyemhitaji walimkuta sebuleni akiwa kajipumzisha huku kijana wake akiwa pembeni anamsomea kitabu cha Hujuma, alipowaona wageni hao, akamwambia yule mtoto akalale na angemwita baadae.

“Karibuni sana, karibuni ndani, mnanitisha usiku wote huu kutembelewa na watu nisiowafahamu,” akawakaribisha huku akiwapa mikono kwa zamu, kisha wote wakaketi chini, akashusha pumzi, “Ndio labda tufahamiane,” aliongea akionekana kuwa na hofu.

“Sisi ni watu wa wachunguzi, kutoka jeshi la polisi,” Madam S alitambulisha kwa ujumla wao, “samahani kwa kukuvamia usiku huu, lakini kwetu ulikuwa ni muda muafaka sana kuonana nawe, najua mpaka hapo umefahamu nini tunataka kuzungumza nawe,” akaongeza kusema.

“Yeah, ndiyo, nawasikiliza wakuu, lakini kabla hatujaendelea na mazungumzo, ningependa kuona vitambulisho vyenu,” akawaomba. Kila mmoja akatoa kitambulisho na kumuonesha, akajiridhisha navyo kwani alijua vitambulisho vya polisi vinafananaje, hivyo kungekuwa na kughushi kwa aina yoyote ile angetambua.

“Tuna jambo moja tu, Mheshimiwa kujua, kama ujuavyo tukio lililotokea leo asubuhi huko Mwadui, unaweza kunambia katika msafara wa Waziri ni nani na nani walifuatana nae?” Madam S akahoji.

“Ulikuwa ni msafara wa watu kumi na tano, wakiwemo Wabunge saba wa Kamati ya Madini, waziri kivuli wa wizara husika na wageni wanne kutoka mataifa ya Canada na Uingereza zaidi ya hapo ni watendaji wa wizara akiwamo katibu Muhtasi wa waziri mwenyewe,” akajibu kwa ufasaha.

Kwa jibu hilo Kamanda Amata, akili yake ikafanya kazi harakaharaka akamuuliza,

“Unafahamu lolote juu ya mpango wa wizi wa Almasi uliofanyika leo?”

“Mpango kama mpango, kiukweli siujui, labda kama Mheshimiwa alikuwa na mpango binafsi katika hilo, lakini mimi hakuna ninachojua kabisa,” akajibu.

“Ok, naomba kupata taarifa kamili za watu wote waliokuwa ndegeni, kuanzia walikozaliwa, wanakoishi na wanafanya nini, napenda kupata usiku huu, nikiwa na maana ama twende ofisini kwako sasa au unipatie kwa njia yoyote lakini usiku huu, kwa sababu kama ujuavyo, kumetokea wizi wa almasi, upotevu wa ndege ya serikali na watu wote waliopo ndani yake,” Kamanda akamaliza na kujiegemeza kitini, Madam S akatikisa kichwa juu chini kuashiria kuwa karidhika na hilo lililosemwa.

“Taarifa zao zote ninazo kwa sababu pia ni wajibu kuzihifadhi kwa dharula yoyote kwa mfano kama hii, niko tayari kuwapa ushirikiano wowote mtakao,” akajibu huku akinyanyuka na kuchukua fulana yake iliyokuwa kitini akaivaa, na saa yake nayo akaiandaa kuivaa mkononi mwake, lakini kabla hajaiweka mkononi, sauti ya Kamanda ikamshtua.

“Samahani, saa yako ni nzuri sana naweza kuiona?” akaomba.

“Bila shaka,” akampatia Kamanda Amata.

Kamanda Amata, akaitazama kidadisi sana saa ile na kuigeuza geuza huku na huko.

“Umeipenda?” akauliza

“Kwa kweli ni saa ya gharama sana kati ya saa za gharama,” Kamanda akajibu huku macho yake bado yakiitalii.

Wakati bado akiishangaa ile saa, mwenyeji wao akatoka pale sebuleni na kuelekea chumbani akiwataka kumsubiri kwa dakika kadhaa. Ni nafasi hiyo ambayo Chiba, mtaalamu wa mawasiliano na teknolojia ya kompyuta katika Idara ya Kijasusi ya Tanzania, alipomnyang’anya ile saa Amata, kwa haraka akaifungua pini yake ya pembeni, akaichomoa na kuichomeka kwa chini kwenye tundu dogo sana lililo katikati ya mfuniko, mfuniko wake ukaachia upande mmoja, akabana kitu fulani kwa ncha za kidole chake na kukivuta, kisha akairudishia kama ilivyokuwa na muda huohuo mwenyeji wao alikuwa akifika sebuleni. Akampa saa yake huku akimwuliza, “Mzee uko juu, hii saa uliipata duka gani?”

“Aaa nimepewa zawadi na hawa wageni wa Uingereza walioondoka na mheshimiwa, tulipokutana kule Michgan kwenye mkutano wa nchi zinazoongoza kwa uchimbaji wa madini duniani na ya kwetu ilikuwa mojawapo, ni saa nzuri sana kiukweli,” alijibu huku wakiwa wanatoka.

***

Usiku huo ndani ya ofisi ya katibu huyo wa wizara, TSA walipata taarifa za wote waliokuwa kwenye ndege ile pamoja na waziri. Walipoona zinatosha, wakaondoka na mwenyeji wao na kumsindikiza mpaka nyumbani kwake kisha wao wakageuza gari na kurudi.

Wakiwa ndani ya gari yao huku Scoba akiedelea kuwapeleka wanakokutaka, ukimya ulitawala kwa jozi ya dakika, kila mmoja mawazo yake yalipaa huku na kule.

“Mnajua!” Chiba aliwagutusha, wote wakamtazama isipokuwa Scoba, akajikohoza kidogo, ile saa ile, ina kifaa cha kunasa mawasiliano ya watu, hivi tulivyokuwa tunaongea pale, kuna watu wamenasa yote tuliyokuwa tukiyazungumza,” Chiba akawaeleza, Madam S akashtuka kidogo na kukodoa macho.

“Unajua, Chiba, mi ile saa niliistukia mapema kwa sababu, katika kioo pale juu katikati ya mishale kuna kajitaa kekundu kanawaka na kuzima na wakati tunaongea kakawa kanawaka harakaharaka, lakini kwa macho tupu huwezi kukaona kirahisi kutokana na rangi yake, ndiyo maana niliposhtukia ile saa nikatoa miwani yangu ambayo wengi hujua ya kusomea na kuivaa ndipo nilipouona ule mwanga kiurahisi zaidi,” Amata akawaeleza.

“Ndiyo, ulipoichukua, mimi nilishajua ni saa ya mtindo gani, ndio maana nikakunyang’anya nikijua nini nadhamiria kufanya na nikafanikiwa, nimeondoa chip ambayo inanasa na kutuma mawasiliano kwa wahusika lakini pia nimeondoa memory card ya simu, kwa kuwa bila memory card ile mic haiwezi kufanya kazi, sasa tutaujua ukweli ulivyo, tusikilize mazungumzo yote tangu mwanzo tukiwa na muda,” Chiba alieleza.

Muda huohuo, simu upepo iliyofungwa ndani ya gari ikakoroma kuashiria kuna taarifa inataka kuingia, Madam akampa ishara Scoba airuhusu. Kutoka katika ile simu ikasikika sauti ya mtu kama anayeongea kutoka mbali, mara moja walitambua ni mtaalamu wa mambo ya anga kutoka JWTZ ambako rada kubwa kabisa Afrika yenye uwezo wa kuona ndege yoyote inayoingia katika mpaka wa Afrika alikuwa akiongea. Madam S akaongeza sauti kidogo ili wote wasikie.

“(…) kwa vipimo vyetu vya chombo cha kunasa muelekeo wa ndege, ndege aina ya Bomberdier mali ya serikali, iliyoruka Mwadui saa tano na dakika hamsini na moja ilielekea Kaskazini Maghalibi, Latitud 23.76 Kaskazini na Longitude 85.01 Mashariki, lakini baada ya dakika arobaini, ndege hiyo ilishuka chini sana kitaalamu tunaita ‘low attitude’ hapo haikuonekana tena, sasa hatujui kama imeanguka au imetua mahali …

Ilimaliza taarifa ile.

Kamanda Amata akashusha pumzi, na kuwatazama wenzake, kisha akainua mkono na kuitazama saa yake, ilikuwa saa sita za usiku.

“Madam,” akaita.

“Kamanda,” Madam akajibu kisha wakatzamana.

“Naanza kupata wasiwasi, hapa hatujui nani hasa tunayemchunguza, au nini tunachokitafuta, nafikiri sasa tuanze kufanya chunguzi sambamba maana muda unaisha, kama inawezekana, hiyo ndege itafutwe kuanzia usiku huu kwa nguvu zote za angani, ardhini na majini, wakati sisi tunasaka watuhumiwa na usalama wa watu wetu, maana mwizi wetu anazidi kusonga mbele, tutamkosa,” Kamanda aliongea kwa hisia kali. Chiba akaunga mkono.

“Ok, naungana nanyi nyote, sasa naomba tuonane ofisi ndogo haraka usiku huu, mwite Dkt. Jasmine na Gina ndani ya dakika kumi,” Madam akatoa uamuzi. Kamanda Amata alimtazama mwanamama huyu ambaye daima aliamini vijana wake, hakupuuza hata siku moja mpango au hoja inayotolewa na mmoja wa vijana wake hasa katika kazi zao.

Amata alimpenda sana Madam S hasa kwa umakini wake wa kazi, na maamuzi yenye majibu chanya siku zote, hakuwa mtu wa dharau ila alithamini hata tone la maji ya mvua lidondokalo kutoka juu ya paa, alikuwa mwanamke wa chuma, aliyepitia mihangaiko, majanga, na mateso mengi katika kazi yake hiyo, mtu mzima, weusi wa nywele zake ulikuwa ukimezwa na weupe. Lakini ukali na umakini wa macho yake bado uling’aa daima, alikuwa na kipaji cha kujua unalotaka kusema kabla hujafungua kinywa chako. Alikuwa na IQ ya hali ya juu sana, aliaminiwa sana kwa usiri wa mambo na ndiyo ilikuwa nidhamu ya kazi yao, yupo tayari hata umkate kichwa lakini hawezi kukwambia chochote ambacho hataki wewe ukijue, alishafanya kazi anuai za kijasusi ndani ya mataifa rafiki na adui. Idara ya ujasusi ilipoanzishwa rasmi na Rais wa awamu ya kwanza hasa wakati wa lile sakata la Hujuma ambalo mwanausalama namba moja aliyekuwa akifanya kazi kwa siri sana na Mwalimu Nyerere, aliyetambulika kwa jina la uficho, The Chamelleone, alipopendekeza kuanzishwa idara hiyo, hakuna mtu aliyefaa kuiongoza zaidi ya mwanamke huyu, na mpaka sasa ilikuwa ngumu kwake kustahafu kwa jinsi alivyoaminiwa.

Ni idara ya siri sana ambayo kazi zake hufanywa kimya kimya lakini kwa umakini wa hali ya juu sana. Kila aliyefanya kazi katika idara hii alikuwa na utambulisho wake mbele ya jamii, tofauti na kazi yenyewe, hivyo ilikuwa ngumu kutambulikana kiurahisi, isipokuwa na watu wachache hasa wale walioko katika baraza la usalama la Taifa. Madam S alishastahafu kazi katika ofisi yake ya awali ya Usalama wa Taifa, na inajulikana hivyo. Lakini kumbe alihamishwa ofisi kwa siri na sasa alijulikana kama msatahafu isipokuwa tu huitwa kwa shughuli maalum ikibidi kuwa wazi.

Ukiachana na yeye, vijana wake wote walikuwa na shughuli mbalimbali za kufanya zinzowakutanisha na jamii kila siku. Chiba, yeye alikuwa ni mkufunzi wa muda katika idara ya TeHaMa pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam, wakati Kamanda Amata alikuwa akimiliki ofisi ya kufaulisha mizigo ya AGI Investiment akiwa na Gina kama katibu muhtasi wake. Dr Jasmine daima alipatikana Muhimbili kama daktari bingwa mpasuaji lakini pia alifanya kazi sana katika kitengo cha magonjwa ya akili ‘Psychiatric department’. Scoba, kama anavyojulikana alikuwa ni dereva Taksi na wengi walimjua kwa hilo. Taksi yake aina ya Toyota Carina iliyochoka kidogo, ilikuwa ikiegeshwa karibu kabisa na jengo la wizara ya Elimu ambao ni mitaa miwili tu unafika ofisi ya Madam S, ofisi ndogo iliyojulikana kuwa ni ya kusaidia Wazee hasa wale wanaofuatilia madai yao ya mafao ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

***

Usiku wa saa sita na dakika arobaini na sita, watu wote hawa sita walikuwa wamewasili katika ofisi ndogo, ofisi ya Madam S, kwanza kila mmoja alikuwa anapata kahawa ili kuchangamsha akili yake.

“Kiukweli hii ni kali ya mwaka, tangu nimeanza kazi hii sijawahi kupambana na janga kama hili,” Madam S alaianzisha mazungumzo, kila mmoja akajiweka sawa.

“Ee maana wengine huwa wanaiba mapesa kiufisadi lakini huyu safari hii kaamua kuchukua almasi kabisa na ndege ya serikali,” akadakia Dr. Jasmin.

“Katumiwa, kwa vyovyote vile, hakuna Mtanzania mwenye ujasiri kama huo endapo hakuna nguvu kubwa nyuma yake,” Scoba akaongeza.

“Ok, sasa tupo hapa kwa ajili ya kupanga mpango kazi, lazima hii kesi kesho asubuhi kwenye saa nne hivi tuwe tumepata mwanga kidogo maana kutakuwa na kikao cha Baraza la Usalama la Taifa saa tano ya asubuhi,” Madam S aliongea huku akijiweka katika kiti chake na wengine wote walikuwa tayari wakijiweka sawa, kusikiliza, hawakutakiwa kuandika popote ili walitakiwa kila kinachoongelewa kikae kichwani kwa kuwa ni siri.

“Chiba!” akaita, “kuna nini kwenye hiyo chip?” akamwuliza.

“Bado, nilikuwa nahangaika nayo hapa, inaonekana imefungwa kwa namba ambazo mpaka nijue kombinesheni yake ni kazi kubwa, lakini kabla ya hiyo saa nne kesho nakuhakikishia nitakuwa nimetegua kitendawili hata ikibidi niende America kwa kazi hii nitakwenda,” akajibu na wote wakacheka hasa kwa sentensi ya mwisho.

“Mpaka muda huo Madam, tutakuwa tumepata ufumbuzi,” Kamanda akamalizia.

“Ok, sasa nataka tufanye kazi katika mtindo wa pembetatu, siku zote mfumo wa pembetatu huwa unaleta mafanikio haraka sana,” Madam akawaambia. Wote wakaitika kwa kichwa kuashiria wako pamoja na mkuu wao.

“Rais amechanganyikiwa, haelewi kipi ni kipi, na hapa ni sisi tu tunaotegemewa, manaake mkijua polisi na wapelelezi wao, nao wanafanya upelelezi juu ya hili lakini sisi tupo mbele zaidi, sasa nimefakiria tufanye hivi, Chiba na Kamanda Amata mtakuwa shamba hakikisheni mnafungua hiyo chip na pia mnachambua taarifa zote za hao watu tuliopewa majina yao na katibu, hakikisheni mnajua mpaka saa ngapi huwa wanaenda haja, hiyo ni pembe ya kwanza. Gina na Dr Jasmine mtaondoka hapa usiku huu kwenda Shinyanga; Dr. Jasmine ukafanyie uchunguzi maiti ya Mc Lean na Boharia wake, ujue silaha iliyotumika kuua kama ni moja au mbili tafauti ili tuanze kuoanisha mambo maana muda unakimbia, mbili, Gina, kazi yako ni kuhakikisha usalama wa Dr. Jasmin, kunusa kila hatari inayozunguka na kuishughulikia, ukihitaji msaada unanitaarifu mara moja, hiyo ni pembe ya pili. Scoba utakuwa bega kwa bega na marubani wa jeshi ambao wanakusubiri muondoke, mkaitafute hiyo ndege pande hizo za Mwanza mpaka Uganda, wakati huo meli ya jeshi kikosi cha maji pale Mwanza nayo itakuwa kwenye doria, hiyo ni pembe ya tatu. Nafikiri tumeelewana, kuna swali?”

Ukimya ukatawala kati ya wote, majukumu waliyopewa yalikuwa yanajieleza kabisa, hakuna ambaye hakuelewa kilichosemwa na Madam. Kila mtu akajipapasa kiunoni mwake, na kujikuta yuko vizuri, bastola na chakara nyingine zilikuwa mahala pake. Gina alikuwa bado kamtumbulia macho Madam S.

“Gina, vipi mbona unashangaa?” Kamanda akauliza.

“Kazi niliyopewa, du! Mi nilijuwa ama Kamanda awe na mimi au awe na Dr. Jasmine, sasa wanawake tupu tutafanikiwa kweli endapo kutatokea ambush?” Gina akauliza.

“Gina, ingekuwa mwanamke hawezi kitu, Ikulu isingenipa hiki kitengo nyeti, na mimi ninsingekuteua wewe kukupa TSA 6. Kumbuka wewe na Amata mna taaluma moja, na taaluma yenu inatakiwa kila upande, sijataka ubaki hapa, nimetaka uende Shinyanga nina maana yangu, huo ni mtihani wako wa kwanza, mi nazeeka, nikistahafu au nikifa hii nafasi haina mtu zaidi ya Kamanda Amata je nani atashika kitengo cha Kamanda kama si wewe? Nimemaliza, wote mtawanyike”.

Usiku huo kila mtu aliondoka na kuingia katika jukumu alilopewa, Gina na Dr. Jasmine walifuatana mpaka Uwanja wa ndege ambapo walipata ndege ya kukodi kuelekea Shinyanga na Scoba aliingia Uwanja wa Jeshi ‘Air wing’ wa kikosi namba 603. Kamanda Amata, Chiba na Madam S walielekea Shamba.

 

04

 

SHINYANGA saa 8:15 usiku

NDEGE NDOGO ILITUA katika uwanja mdogo wa Shinyanga, Gina na Dr. Jasmine waliteremka na kuingia kwenye jengo la wageni.

“Karibuni sana,” wakakaribishwa na mwanadada aliyevalia nadhifu kabisa, alionekana wazi kuwa ni mfanyakazi wa hapo, wakakamilisha itifaki zote za uwanjani hapo ikiwa pamoja na kufanyiwa ukaguzi kisha wakaingia kwenye gari iliyoitwa na mwanadada yuyo huyo, wakaondoka zao.

Moja kwa moja walifika katika hospitali ya mkoa ya Shinyanga, wakakutana na mganga mfawidhi kwa kuwa tayari alipewa taarifa juu ya ujio wa wachunguzi hao. Walipokamilisha kila kitu wakaelekea chumba cha kuhifadhia maiti.

“Ndiyo sijui niwasaidie nini?” mhudumu wa chumba hicho akawauliza. Dr. Jasmine alikuwa amesimama jirani kabisa na yule mhudumu ilhali Gina alikuwa nyuma kama hatua tano hivi akichezea simu yake.

Jasmine akaonesha kitambulisho chake, “nahitaji kuuona mwili wa Mc Lean na Mr. Ngosha waliouwa Mwadui mapema jana”.

Yule mhudumu hakuwa na shaka kwani tayari alikwishapewa taarifa na bosi wake juu ya wageni hao. Akampa ishara ya kumfuata, akamfungua mlango mkubwa na kuingia ndani ya chumba hicho. Hakikuwa kikubwa sana, kulikuwa na jokofu lenye uwezo wa kuhifadi miili ishirini tu, hivyo mingine ilikuwa imehifadiwa kwenye vitanda vya chuma. Hewa nzito iliyochanganyika na baridi iliwalaki.

“Huu hapa ni wa Mc Lean,” alimuonesha Dr. Jasmine huku akivuta ile machela kutoka ndani ya jokofu na kuruhusu mwili huo uonekane nusu, “na huu huku wa Mr. Ngosha,” akamwambia na kumwonesha kwa kidole.

“Ok, sasa kokota hiyo miili, lete kwenye chumba cha uchunguzi, bila shaka ni hiki sivyo?” Jasmine akauliza. Yule Mhudumu akajibu kwa kichwa kuwa ‘ndicho’.

Dakika mbili baadae ile miili yote miwili ikawa ndani ya chumba kile alichokuwa Jasmine. Akavali vifaa vyake na kuweka vizuri barakoa usoni mwake na ile miwani kubwa inayomkinga macho, kisha akajivika joho la kijani na kuanza kazi yake.

“Sasa wewe kaendelee na kazi yako nyingine, hapo nje nimemweka mtu, naomba asiingie huku mtu yeyote nafanya kazi hii kwa dakika ishirini tu, sawa?” akamwambia Mhudumu.

“Sawa,” yule Mhudumu akajibu na kuondoka.

 

MWANZA saa 8:50 usiku

CHOPA YA JESHI ILIKATISHA ANGA la Mwanza kuelekea ziwani, ikiwa katika msako wa kuitafuta ndege ya serikali iliyopotea mchana wa siku iliyopita baada ya kutumiwa katika wizi wa almasi.

Katika ziwa Victoria kulikuwa na meli ya jeshi nayo ikitalii hapa na pale, wakitumia vyombo mbalimbali kutazama kama wanaweza kuona chochote kinachohusiana na ndge hiyo. Mawasiliano kati ya wale waliokuwa katika ndege na hawa walioko melini yaliunganishwa moja kwa moja na wale walio katika rada ya jeshi kule Ngelengele mkoani Morogoro.

“Elekea upande wa Magharibi nyuzi 121,” yalikuwa maelekezo kutoka kwa wale walioko Ngelengele. Scoba na yule Rubani wa Jeshi wailikiongoza chombo hicho kama walivyoelekezwa, hakika mtu aliyewaelekeza hakukosea hata kidogo, kwani walivyokuwa wakizunguka walikuwa wakiona kitu kisichoeleweka katikati ya misitu ndani ya Uganda kilomita chache sana kutoka ziwani.

“Kuna kitu tunachokiona katikati ya msitu, tuna wasiwasi nacho kama ni ndege kutokana na kinavyong’aa kwa mbalamwezi,” Scoba alitoa taarifa.

“Ok, Ok, nenda chini zaidi ili uone kwa ufasaha,” wakapewa maelekezo, “Kama kuna uwezekano wa kutua basi fanyeni hivyo,”

Ile chopa ilipita karibu kabisa na kuhakikisha kuwa walichokiona ni ndege iliyotua katika barabara finyu sana.

“Yeah, ni ndege ya serikali, tumeiona vizuri kabisa,” walitoa taarifa na kisha kurudi Mwanza, hawakuweza kutua hawakuwa na uhakika wa usalama katika eneo hilo, wangeweza kushambuliwa kirahisi tu kama adui angekuwa kawawekea mtego. Scoba alikumbuka maneno ya Chiba, alipowaambia kwenye kikao kuwa wote wawe na tahadhari kwani adui kwa vyovyote atakuwa amejua anatafutwa baada tu ya kuondoa ile chip ya mawasiliano kutoka kwenye saa ya katibu wa wizara.

 

 

 

 

SHAMBA saa 8:30 usiku

Taarifa zilifika mara moja kwa Madam S, kwani ndani ya jumba lao huko Gezaulole, Shamba, waliweza kunasa mawasiliano yote yaliyokuwa baina ya ile meli, Chopa  na mtaalam wa anga huko Ngelengele. Alikurupuka kitandani na kuwafata; Kamanda Amata na Chiba waliokuwa katika chumba maalum cha mawasiliano ili kujua kulikoni. Ilikuwa ni furaha kwa wote.

“Ehne, na ninyi kuhusu wale watu mmefikia wapi katika uchunguzi wenu?” Madam alimwuliza Amata.

“Aaaah, majibu sio mabaya, hawa Watanzania waliofuatana na Waziri taarifa zao hazina mashaka sana, ila hawa Wazungu wanne ndio bado tunachimba zaidi,” Kamanda alijibu.

“Mpaka ulipofikia…” Madama akamwulza Chiba.

“Mpaka nilipofikia kuna huyu Bwana Mark Steuben, tajiri mkubwa sana huko Uingereza, anafanya biashara ya madini na mataifa mbalimbali duniani, ana kampuni kubwa iitwayo Cunglia Gold Mines, ambayo ofisi zake zipo katika mji mdogo wa Cunglia, katikati ya Uingereza. Labda anaweza kumshawishi mtu yeyote kufanya wizi kama ule kwa kumpa pesa nyingi sana.” akajibu.

“Ok,” Madam S akaitikia huku akitikisa kichwa chake.

Halafu Chiba akaendelea, “halafu kuna huyu Bwana Dregen. Amewakilisha kampuni moja ya kuuza madini iliyoko huko Canada katika jiji la Ontario, nimejaribu kuingia kwa undani zaidi wa yeye na kampuni yenyewe, inaitwa Robinson Dia-Gold LTD. Kampuni hii ipo Ontario, na inamilikiwa na tajiri mkubwa wa huko Canada anaitwa Bwana Robinson Quebec,” akamalizia hapo.

“Very Good my boy, umeona hao wote wana makampuni ya madini kwa hiyo kuna uwezekano wa kushawishi au kufanya wizi huo, yote yanawezekana, endelea kuchambua zaidi, anagalia na wigo wa marafiki zao kibiashara duniani kote na Afrika ili tuone kama kuna muungano na popote panapoweza kutupa jibu,” Madam alitoa maelekezo. Chiba akamuonesha alama ya dole gumba.

“Chiba nipe ripoti nyingine,” Amata akamgeukia Chiba aliyekuwa bize na kompyuta zake mara tua baada ya kumaliza kuongea na bosi wake.

“Nimefanikiwa kufungua codes zilizowekwa, ila kazi ilikuwa ngumu sana, lakini hakuna cha maana sana isipokuwa chip hii ilikuwa inahifadhi kumbukumbu kwa njia ya sauti kutoka pande wa Mheshimiwa na kuzituma kwa hawa jamaa, sasa hapa ninachotaka kufanya ili tujue ilikuwa inapeleka wapi hasa, na nani alikuwa anazipokea, inabidi tuiunganishe tena, halafu ndio nijaribu kuona codes zake zinavyooana hapo tutajua upande gani na wapi inatuma taarifa, itakuwa rahisi kumpata mtu wetu au watu wetu,” Chiba alieleza kitaalamu kabisa.

“Ok, kama vipi fanya hivyo asubuhi, sijui utaipataje ile saa ya yule mzee na muda wote iko mkononi,” alionesha mashaka.

“Usijali, mimi ndio Chiba, huwa sishindwi kitu, nitaiunganisha hapahapa kwa kutumia vifaa vyangu na ninauhakika itafanya kazi.”

“All the best”.

SHINYANGA – Usiku uo huo

Dkt. JASMIN ALIMALIZA KAZI YAKE, ile miili ikarudishwa mahala pake, akavua maguo aliyokuwa amevaa na kuyaweka vizuri kwenye mfuko wa plastiki, kisha kwenye mkoba wake, akatoka akifuatana na yule mhudumu, nje walimkuta Gina akiwa anazungukazunguka huku na huko, akampaigia mruzi, Gina akarudi mara moja.

“Asante sana,” akamshukuru yule mhudumu na kumpa noti ya Sh. 10,000 za Kitanzania.

“Vipi, kuna lolote?” akamwuliza Gina.

“Nina wasiwasi, kuna gari imepita hapa kama mara mbili, imezunguka huku, ndio nilikuwa naitazama nijue inashughuli gani,” Gina alijibu.

“Vipi, umepata lolote?” Gina akamwuliza.

“Yeah, nimepata majibu yenye utata kabisa, lakini hata hivyo…” akasita kidogo, akampa Ishara Gina ya kutazama kwenye ua kubwa lililofanya kichaka cha kuogofya, Gina akageuka kwa chati na kuona kivuli cha mtu aliyetulia kama mti mkavu sambamba na mti wenyewe, akajiweka tayari kiakili na kimwili.

“Tutaongea baadae,” Jasmine akamwambia Gina huku wakiharakisha kulifuata lango la hospitali hiyo.

Hakukuwa na mtu kwenye vijia vya hospitali hiyo, isipokuwa wauguzi na madaktari waliokuwa wakipishana usiku huo kwa kazi mbalimbali. Gina alitazama nyuma na kuona watu wawili waliokuwa wakiwafuata taratibu ambao waliachana kama mita mbili katikati yao. Mbele yao kulikuwa na mtu mwingine aliyevalia kidaktari, Gina akili yake ikafanya kazi kwa haraka zaidi, mwili wake ukasisimka, akaiona hatari hiyo, akamgonga Jasmine kwa kiwiko, “una bastola?” akamwuliza.

“Ndiyo!” akajibu.

“Iweke tayari, funga kiwambo kwa siri, pale mbele kuna korido mbili wewe nenda kushoto mimi niende kulia tuone watagawanyika vipi kisha tuwashambulie, hakuna kubakisha kitu, muda mbaya huu,” Gina alimwambia Jasmine ambaye aliitikia kwa kichwa. Akatoa bastola yake kwa chati ndani ya mkoba wake huku mkono ukifunikwa na koti lake la kidaktari, alipoishika sawia, akaliweka juu koti lake la kidaktari hivyo hakuna aliyeona kama ana bastola mkononi mwake. Wale watu bado walikuwa wakiwafuata kwa nyuma.

Mara wakafika kwenye zile pacha za korido ambapo nyingine ilikatisha na kufanya alama ya ‘jumlisha’, Dr Jasmine akakunja kushoto na Gina akakunja kulia, kila mmoja akashika njia yake. Wale watu wawili walipofika pale, wakagawana njia mmoja kushoto na mwingine kulia, yule daktari naye alikunja upande wa Jasmine. Gina aliona tukio zima, alipofika mbele kidogo akasimama akajifanya anaweka kiatu chake vizuri. Yule mtu aliyekuja upande wa Gina akamkaribia huku mkono wake ukijishika kiunoni, alikuwa akitoa bastola, amechelewa, Gina alirusha teke moja kali la nyuma na kiatu alichovaa chenya kisigino kirefu kikamtoboa sehemu tumboni, akarudi tena wima, wakati yule mtu akijishika tumbo, tayari Gina alikuwa hewani akamtandika mateke mawili yaliyompeleka chini, yule jamaa akajiinua haraka ili akabiliane na mwanamke huyo, Gina aliona upande wa Jasimine, yule aliyevaa kidaktari akigeuka tayari na bastola mkononi kumlipua yeye.

Kwa haraka, alimkamata adui yake na kumuweka kati kisha akajirusha upande wa pili na ile risasi ikamfumua vibaya yule mtu akabwagwa chini kama kiroba.

***

Mara tu baada ya kuachana na Gina katika makutano ya korido zile, Jasmine, alisimama ghafla, na yule kijana akamwekea bastola mgongoni.

“Tembea vivyo hivyo, ongoza mpaka garini,” alimwamuru. Jasmine hakuonesha upinzani, akatembea lakini hatua tatu aliposikia ile sauti ya bastola ya yule aliyevaa kidaktari, akatumia nafasi yiyo hiyo, aligeuka ghafla na kuupiga mkono wa yule kijana kwa mkoba wake, bastola ikaanguka chini, yule mtu alijirusha kuiokota, ikapigwa teke na kwenda upande wa pili, kabla hajainuka, yule jamaa alikutana na teke kali la usoni, hakuna alichokiona zaidi ya vimulimuli. Akiwa katika hali hiyo, Jasmine alijiandaa kumpa shambulizi la pili, akachelewa, konde moja kali likatua sahavuni na kumpepesua mwanadada huyo mpaka kwenye ukingo wa ile korido, wakati huo yule aliyevaa kidaktari, bastola mkononi, alikuwa akimjia Jasmine kwa haraka, kabla hajafika, paji la uso wake likafumuka, risasi ya Gina iliyotoka upande wa nyuma ikafanya vitu vyake. Gina akakimbia na kujirusha hewani miguu yake miwili ikatua katika mgongo wa yule jamaa mmoja aliyempiga konde Jasmine, akamsukuma na kujibamiza katika ukuta wa jingo la karibu yake, akamfikia na kumkamata ukosi wa shati, akamdidimiza bastola kinywani mwake.

“Sema, nani kawatuma?” Gina akauliza.

“Si- si-mjui…” akajibu kwa kigugumizi huku macho yamemtoka.

“Sitaki kupoteza muda, sema haraka,” Gina akang’aka huku midomo ikimtetemeka, akatoa ile bastola kinywani mwa yule mtu na kuifyatua, akampiga gotini na kufumua mifupa.

“Aaaaaa, aaaaaa unaniua mimi! Iiiiiiii, mama weeee, ona damu sasa zinatoka,” yule mtu alilia kama mtoto.

“Utasema au husemi?” Gina aliuliza tena.

“Nasema, nasema, usiniue tena…”

“Haya sema,” Gina alimwamrisha

“Tumetumwa na Don Swa…” kabla hajamaliza kusema alitoa macho kama mjusi kabanwa na mlango.

“Ambushhhhhhh!!!!!”  Dr. Jasmine alipiga kelele, Gina akamwachia yule mtu na kuruka kinyumenyume akatua kwenye pipa la taka, akaanguka nalo, Dr. Jasmine akamshika mkono wakainuka na kutimua mbio, walijirusha kwa pamoja na kupenya dirishani wakaingia katika wodi ya watoto, wakatimua mbio na kutokea mlango wa nyuma.

“Wazingile wazingile,” sauti ilisikika.

“Watatokea huku, we pita kule,” mwingine aliamuru.

“Kwani kuna nini jamani?” Muuguzi mmoja aliuliza baada ya kuona watu asiowajua wakiingia wodini mwake.

“Kuna majambazi wawili wa kike tunawasaka, sisi ni polisi, mmewaona wameelekea wapi?” akauliza.

“Wamepita pale kwenye hako kamlango kadogo,” mgonjwa mmoja akaropoka, msinambe.

Gina na Jasmine, wakatulia tuli ndani ya chumba cha kubadilishia nguo wauguzi. Yule mtu aliyepewa maelekezo, akatembea kwa hadhari kubwa kuingia katika kile chumba, akasukuma mlango kwa mtutu wa SMG aliyoidhibiti mikononi mwake, ukimya ukamlaki, zaidi ya ukimya huo ni nguo tu zilizokuwa zikining’inia. Dr. Jasmine akatoka akiwa amevaa vazi lake la kidaktari, stethoscope yake shingoni, mikono mfukoni. Alipoukaribia mlango akakutana uso kwa uso na mtutu wa bunduki.

“We vipi huku na libunduki lako?” akamwuuliza.

“Tunatafuta majambazi wawili wa kike,” yule bwana akajieleza.

“Sasa majambazi ndio wakimbilie wodini, si watakamatwa tu, hakuna mtu huko,” Dr. Jasmine akajibu, huku akipishana na yule mtu, akakiendea kitanda kimojawapo chenye mgonjwa aliyewekewa drip, akamwangalia, “unaendeleaje?” akamwuliza.

“Naendelea vizuri,” akamjibu. Wakati anaongea na huyo mgonjwa alikuwa akimwangalia kwa chati yule mtu ambaye alitoka ndani ya chumba kile, na kuondoka zake.

***

“Wagonjwa na wafanyakazi hawatoi ushirikiano, twendeni zetu kabla wakuda hawajafika, lakini hakikisheni mianya yote ya kutokea nje ya hospitali hii inabanwa, wasitoke humu leo wala kesho,” yule mtu aliwaeleza wenzake huku akikwea Land Cruiser lenye rangi za polisi na namba za usajili za serikali. Wakaondoka zao.

Walipofika nje wakateremka na ile gari ikaondoka peke yake.

“Wewe, wewe na wewe mtasubiri hapa mlango mkuu, nyie wawili, kuna mlango wa pale pembeni mkaweke ulinzi wa siri, na nyie wawili kule nyuma, sawa?” akawapa majukumu.

“Sawa Kiongozi.”

“Mkiwaona wanajitokeza, signal  yetu ni ileile,” alipomaliza kuwaelekeaza akatokomea kizani. Utulivu ulirejea katika pembe za hospitali ile, maana wagonjwa wengine walipona baada ya kusikia milio ya risasi, watu walizagaa ikiwamo wagonjwa na wauguzi, walinzi nao walikuwa pale. Waliisitiri miili ya waliokufa kwa kuifunika na kuiacha hapo kungoja itifaki za kipolisi.

 

SHAMBA – DAR ES SALAAM

Simu ya Kamanda Amata ikaita, simu pekee ambayo ikiita lazima kuna jambo, akaichukua na kuifyatua kisha akaweka sikioni.

“…Kamanda, tupo msambweni, tumeshaangusha watatu na hapa tumezingirwa, lakini hatujui watu hawa ni polisi au vipi, kwani wamefika na gari ya polisi…” Gina aliongea kwa kunong’ona.

“Oh, poleni sana, mko salama?” Kamanda akauliza.

“…Tuko salama,”

“Kazi ya ofisi mmemaliza?” akauliza.

“…Ndiyo tumemaliza… hawa watu hawajaondoka, wanatusubiri nje kwa vyovyote… msaada please…” Gina akakta simu.

Kamanda Amata akampa taarifa hiyo Madam S.

“Shiit, kumbe adui tunae humuhumu! Ina maana ni polisi wanaotumwa kutekeleza haya, basi nimeelewa, hapa una mikono ya watu, sasa tunawasaidiaje na unajua wazi kuwa fimbo ya mbali…” Madam akasema.

“Tulia Madam, nishapata wazo,” Kamanda akajibu kisha akaiendea simu ya mezani, akazungusha tarakimu kadhaa, akasubiria.

“…Hello, Central Police Station hapa, tukusaidie nini?…” sauti ya WP iliijibu simu hiyo kutoka kituo kikuu cha Shinyanga.

“Kuna mauaji pale hospitali ya mkoa wa Shinyanga, naomba amkashughulikie,” kisha Kamanda akakata simu, akairudisha mahala pake na kuinua ile ya mfukoni, “Fanyeni kila mnaloweza mtoke haraka, nimewataarifu polisi,” akamwambia Gina.

***

Gina na Dr. Jasmine wakatoka na kutembea harakaharaka mpaka kwenye maegesho ya gari za hospitali, wakaikuta ambulance imeegeshwa pale, dereva alikuwa amesinzia ndani, wakamgongea wakaingia.

“Vipi?” akauliza kwa mgutuko.

“Polisi,” Gina akamjibu na kumuonesha kitambulisho cha polisi, “sasa sikia, tutoe hapa na gari yako kama unavyopeleka mgonjwa Muhimbili, kisha we tuache uwanja wa ndege urudi, mtu yeyote akikuuliza baadae mwambie ni polisi walikuchukua, haya haraka.”

Yule dereva hakuwa na hiana akaliwasha na kuwasha ‘kimwerumweru’ kule juu na kulitoa mahala pake, alifunguliwa lango kuu na kutoka kisha akaongeza kasi kuelekea Uwanja wa ndege.

***

Scoba akiwa na vijana wa Jeshi la Wananchi walizingira vichaka ambapo ndege ile ilitua, kilomita chache ndani ya mpaka wa Uganda. Ilikuwa ni kwenye barabara ndogo ambayo hata hawakuijua ilitokea wapi na kwenda wapi, hakukuwa na tatizo lolote, pori lilikuwa salama kabisa. baada ya kuhakikisha hilo, walivuta hatua huku wenzao wenye mitutu wakiwa wamelala kimya nyasini tayari kutoa ulinzi kama kuna lolote baya. Scoba aliufungua mlango wa ndege ulioonekana haukufungwa sawasawa, akatumia periscope kuangalia ndani, kulikuwa na watu waliokuwa wamelala vitini, shaghalabaghala, akaingia, pamoja na wale wapiganaji wa JW.

Ukimwya ulitawala, ni vivuta hewa tu vilikuwa vikining’inia huku na kue. Wakakagua kila mtu bila kumshika ili wasipoteze ushahidi wa alama za vidole. Kulikuwa na abiria kumi na moja, abiria wanne hawakuwepo kadiri ya hesabu waliyopewa na Katibu wa Wizara.

Scoba na wale maofisa wa jeshi walifanya ukaguzi ule vizuri mpaka kwenye chumba cha marubani na kuwakuta wote wakiwa kwenye usingizi mzito. Wakiwa ndani ya chumba cha rubani, Scoba alianza kujisikia kizunguzungu na kichwa chake kuwa kizito, akawapa ishara wale maofisa kutoka nje ya ndege hiyo haraka.

“Kuna dawa kali ya usingizi,” akawaeleza wenzake mara baada ya kunywa maji mengi na kunawa mengine.

 

SAA 4: 15 asubuhi.

MWANZA-Hospitali ya Sekou Toure

KATIKA WODI YA WATU MAALUMU (V.I.P) walikuwa wamelazwa watu kumi na nne, abiria kumi na moja na marubani watatu waliotolewa kwenye ndege ile na kufikishwa hapo kwa helkopta za jeshi la Tanzania.

Madam S na timu yake walikuwa wamejificha kwenye moja ya vyumba vinavyotumika kama ofisi kwenye hospitali hiyo. Aliwatazama kwa zamu mmoja baada ya mwingine, “hongereni kwa kazi,” akamtazama Gina, “safi sana mkamwana, umekomaa sasa, sikutegemea kama kutakuwa na hali hiyo pale Shinyanga, lakini umefanya vema, sio mbaya,” akamsifia.

“Wakati tunamsubiri Dr. Jasmine atupatia majibu ya hao watu huko, tujadili jambo, kwa nini Waziri afanye yote haya? Kwa manufaa ya nani,” Madam S akaanzisha mazungumzo.

“Hapana nikioanisha matukio, sidhani kama Mheshimiwa Waziri kafanya haya, hawa jamaa ni wataalam, swali dogo Madam, wamepataje gari la polisi kuwavamia hawa akina Jasmine, fikiria, gari iliyokuja kuleta askari pale Shinyanga na ile iliyokuja kwanza ni ileile na pale kituoni wanasema haikutoka, hawa ni Wataalam tunapambana na wajuzi, naamini sasa Waziri kafichwa mahala Fulani,” Kamanda akajibu.

“Chiba, alama za vidole kutoka kwenye ndege zinaleta majibu gani?” Madam akauliza.

“Hakuna majibu Madam, inaonekana watu hawa walijipanga kwani walivaa gloves,” Chiba alieleza.

Madam S akatikisa kichwa kana kwamba kaingiwa na mdudu sikioni, “hivi hiyo ndege mmeikagua vizuri kweli?” akauliza.

“Wanasema wameikagua kila kona,” akajibu Scoba.

“Ok, ngoja waamke hawa ndio watatupatia habari nzima na kuanzia hapo sasa tutajua mbivu na mbichi, Kamanda Amata kazi yangu ya jana ulifikia wapi?” Madam akaendelea kukusanya maelezo na kuyameza kichwani mwake.

“Kuhusu Robinson Dia-Gold LTD?

“Yeah!”

“Kuna kitu kimenisumbua kidogo, na lazima tukiangalie kwa makini na mapana kama kina uhusiano wowote na hili,” Kamnanda alianza.

“Enhe!” Madam akajiweka tayari na kila mtu akatega sikio.

“Nimejaribu kupitia mambo mengi juu ya kampuni na mmiliki wake, kati ya ambayo nimeyawekea alama ni hili lifuatalo; tajiri wa Robinsoni Dia-Gold LTD alikuwa na rafiki mkubwa wa kibiashara na muuza madini mkubwa huko Afrika Kusini aliyekuwa anamiliki kampuni ya The Great Khumalo Mines, na huyu Khumalo alikuwa na hisa nyingi katika kampuni ya Robinson, na katika kuendelea kusoma taarifa hizo ni kuwa huyu Khumalo aliuawa miaka miwili iliyopita, sikuona umaana wa mauaji hayo hata kama watu hao walikuwa marafiki, lakini sasa tarehe ya mauaji ilikuwa bado siku nne kampuni ya Robinson igawe faida za wenye hisa, na kama ingekuwa hivyo basi Khumalo angepata pesa nyingi sana kiasi kwamba kampuni hiyo ya Robinson ingetikisika kiuchumi, hapa nina wasiwasi, je si Robinson aliyetekeleza mauaji haya?” Kamanda akatulia.

Wote ndani ya chumba hicho wakabaki kimya hakuna aliyeongea, mara mlango ukasukumwa na Dr. Jasmine akaingia akiwa katika mavazi ya kawaida.

“Ndio Jasmine, lete habari sasa,” Madam alimdaka.

“Uh! Madam, baada ya kufanya uchunguzi wa kitabibu kupitia damu za wahanga, nimegundua kuwa watu wale wote walipewa  dawa aina ya Mandrax, kwa kiwango kikubwa sana kiasi kwamba hadi kuamka itachukua si chini ya masaa kumi na mbili yajayo,” akatulia.

“Itawezekanaje, walispray?” akauliza Madam.

“No!” Scoba akadakia, “sasa Napata picha, ile ndege tumekuta Oxygen Mask zote zimefunguka, ina maana waliunganisha na njia ya hewa kisha wakakasitisha mzunguko wa hewa ya kawaida, kiasi kwamba Rubani lazima afungue zile mask kuwasaidia abiria wake, hivyo ni rahisi wote kuivuta kwa mara moja,” akamaliza.

Madam S akatikisa kichwa kuashiria ameelewa.

“Madam, sasa unaamini kuwa tunaopambana nao wamajipanga kiasi gani, kwa sababu mpaka hawa watu wa kutupa sisi mwanga waamke, adui yetu atakuwa amefika Mars kama si Jupiter,” Kamanda akatoa rai.

“Usemalo ni kweli kabisa, Dr. Jasmin vipi hakuna vjia yoyote ya kuwafanya waamke mapema?” Madam S akauliza.

“Hapana, ni vizuri tuwangoje waamke wenyewe pia kwa usalama wa afya zao, kwa maana tukitumia dawa ya kuwaamsha haraka tunaweza kuwapoteza pia, haina haja ya haraka,” akajibu Jasmine.

“Ok, turudi kwenye hoja yetu, Kamanda Amata,” Madam akaendeleza mjadala.

“Nilikuwa nahitaji mawazo yenu kama mnaona kuna uzito katika mauji ya Khumalo na hisa za kampuni ya Robinson,” akaendelea Amata.

“Tena kumbuka kumbukumbu zinaonesaha kuwa Khumalo amekoswakoswa kuuawa mara kadhaa, si mara moja, kwa mujibu wa mtandao wake ambao mpaka sasa haujafungwa bado,” Chiba aliongezea.

Madam S aliendelea kuwasikiliza vijana wake walivyokuwa wakitiririsha maelezo.

“Nimewaelewa vyema, sasa naona kuna muunganiko katika mauaji ya Khumalo na huyu mtu anayejiita Robinson sasa tunaunganisha vipi na tukio hili?” akauliza.

“Madam, simple tu, kwenye ndege kulikuwa na mtu ambaye alikuwa anaiwakilisha kampuni ya Cunglia Gold Mines, hivyo inawezekana Robinson kafanya uharamia huu ama kwa kushirikiana na Waziri au kwa hujuma yoyote maana anaonekana ni mtu wa mbinu sana, hivyo hatoshindwa kufanay kama wale Waisrael waliokuja Uganda na kuwaokoa ndugu zao waliotekwa na Idd Amin, wakiwa na sare za UPDF, ndege ya Uganda, muda waliofika ni uleule ambao Idd Amin alitakiwa kufika pale, nani alijua kama wale ni Waisrael?” Gina akaongeza neno.

Ukimya ukatawala.

  • §§§§

Watu fulani wawili walikuwa wameketi katika chumba kilichojengwa chini ya ardhi katika moja ya nyumba za kifahari huko Mwanza, Pasiansi, muda wote walikuwa kimya hakuna aliongea na mwingine, katikati yao kulikuwa na chombo kidogo kama redio, kilichounganishwa na kompyuta ndogo kabisa, chombo hicho kilikuwa kikitoa sauti ya watu waliokuwa wakiongea kwenye kikao Fulani nje ya hapo. Watu hao walikuwa ama wakitabasamu au wakiongea kwa simu zao maalum kutoa taarifa kwa watu wao juu ya mpango unaopangwa na wale walio kikaoni. Mara hii mmoja akamtazama mwenzake na kumsemesha.

“Vipi hapo? Tumefanikiwa, bado?” akamwuliza yule mwingine

Fifty Fifty kaka” akajibu yule mwingine.

“Yaani huyu fala wao anayejifanya anajua sana maswala ya kompyuta, ningemuona ana akili kama angeichoma moto hiyo chip lakini kuendelea kuihifadhi akijua kwamba haifanyi kazi kwa kuitoa kwenye ile saa, imekula kwake, tena sasa ndio tunapata data za kutosha za jinsi wanavyojipanga,” Mwingine akajibu.

“Lakini mi nawaogopa hawa jamaa, mpaka wamegundua juu ya Khumalo, Robinson ina maana wapo hatua chache sana kutufikia, huyo mtu wa kompyuta sio mjinga, lazima kuna kitu anafanya, hivyo hapa tuwe na tahadhari kubwa ikiwezekana tuondoke zetu kwani kuendelea kuwa hapa kunaweza kutuletea tabu,” yule wa pili akaongeza na mwenzake akatikisa kichwa kuafiki.

“Ok mpe ripoti Boss!” akamwambia mwenzake ambaye alichukua simu yenye anenna ndefu na kuanza kuongea na mtu wa upande wa pili.

“Ok, anasema tuhamishe makazi, maana yake tuondoke sasa, mpaka mambo yakitulia, tuje kufanya awamu ya pili, lakini kwa hili labda yule mtu wetu atashtuka,” akaongea yule aliyekuwa na simu, kisha wakasubiri kidogo kabla ya kuzima hako kajimtambo kao.

***

Wakati mazungumzo yakiendelea kati ya Madam S na watu wake, mara kompyuta ndogo ya Chiba ikachora aina flani ya mistari kuwa kuna mawimbi yanakatwa, akaigeukia na kuacha mjadala ule kisha akaanza kubofyabofya  hapa na pale ili kujua ni vipi, alikuwa anatabasamu wakati akafanya hilo.

“Kamanda!” akaita, Kamanda Amata naye akaungana naye. Chiba akanakili namba kadhaa zilizoonekana katika kompyuta yake na kisha akaingiza kwenye mtandao mwingine, ramani ya ulimwengu ikajionesha dhahiri, akaendelea kucheza na namba zile kujaribu kuoanisha na vipimo halisi vya ardhi. Wakati huo wote walikuwa wamemzunguka Chiba kuangalia nini anafanya.

Chiba akageuka na kukuta kazungukwa, “Pasiansi kitalu namba 164 au 165 au 166 au 167 moja wapo,” akasema.

“Kuna nini?” Madam akauliza.

“Hapo ndipo mawasiliano yetu yanapotua,” akaeleza wakati akaisimama na kuchukua bastola yake akaiweka sawa na kuipachika kiunoni, Kamanda Amata akafanya hivyo, Gina nae akaunga.

Wakatoka wote na kuteremka ngazi kisha wakachukua gari ndogo yenye vyoo vyeusi wakaingia, Scoba akakamata usukani, wakapotea mtaani.

“Kama wasingezima huo mtambo wao, nisingeweza kuwagundua walipo,” Chiba alieleza.

“Ina maana watakuwa wanajipanga kuondoka hao, kwa nini wazime?” kamanda akauliza.

“Unajua, inaonekana walikuwa wakiendelea kunasa mazungumzo yetu, sasa kama wamesikia hatua ambayo tumefikia, hata ningekuwa mimi ningefunga virago na kuondoka haraka,” Chiba akaongeza kusema.

“Madam, hawa watu wasikimbie, zuia ndege zote kuruka pale Mwanza Airport,” kamanda akatoa rai.

“Dah! Umenena,” Madam S, akainua simu yake na kupiga kwa Meneja wa Mamlaka ya Viwanaja vya ndege kuomba ndege hata moja isiruke.

Muda si mrefu walifika mtaa wa Pasiansi, wakatafuta namba hizo na kuona nyumba nne zenye namba hizo zilizofuatana. Wakateremka kwenye gari yao, Madam S akaelekea dukani na kununua kinywaji lakini hapo alipo alihakikishwa ana uwezo wa kuziona nyumba zote hizo. Kisha Chiba, Kamanda na Gina wakatawanyika ilhali Scoba alikuwa akiendesha taratibu gari yake kati ya nyumba hizo.

Nyumba ya kwanza, ilikuwa nyumba ya kawaida kulikuwa na wapangaji tu, mwenye nyumba hakuwapo hapo.

Nyumba ya pili kulikuwa na familia moja inayoishi, ilikuwa nyumba ya kawaida tu. Nyumba ya tatu ilikuwa ni nyumba kubwa ya kisasa yenye kila kinachohitajika katika nyumba, bustani kubwa yenye bembea na maua ya kuvutia ilikuwa, na mfanyakazi tu aliyeonekana kumwagilia maji bustani hiyo ya kuvutia.

Gina akalijongelea geti na kubonyeza kengele, yule mfanyakazi akasogea.

“Nikusaidie nini dada?” akauliza kwa lafudhi ya Kisukuma.

“Namuulizia mwenye nyumba, yupo?” akauliza.

“Mwenye nyumba? Mi tangu nianze kazi hapa sijawahi kumuona mwenyenyumba, ni wageni tu wanaokuja na kuondoka,” akajibu.

“Fungua mlango,” Gina akaamuru.

“Sasa uwende wapi? Hakuna mtu humo ndani,” akasema huku akifungua geti na Gina akapita ndani.

Kamanda Amata akaiweka bastola yake vizuri, akaipachika miwani yake usoni akitazama pale mlangoni ambako Gina aliingia na kuielekea nyumba hiyo. Scoba akainua bunduki kubwa aina ya AK 47 iliyofungwa lensi yenye nguvu na kupachika dirishani, akaitazamisha kule kunako lile jumba, huku akichungulia taratibu kutazama kama kuna mtu yeyote ambaye ataleta tabu ili amfumue bila huruma.

“Usiende huko, hakuna mtu dada,” yule mfanyakazi akamwambia Gina. Wakati huohuo Kamanda Amata akaingia pale getini akasimama akitazama. Gina akaukaribia mlango mkubwa wa jumba hilo, Kamanda Amata akamtazama yule mfanyakazi ambaye aliuacha ule mpira wa maji na kuliendea bomba ambalo ameliunganisha na ule mpira wa maji, akaacha kumtazama Gina na kumfuata yule mfanyakazi taratibu.

Yule mfanyakazi akalififikia bomba na kufunga maji, wakati huo huo Kamanda Amata akasikia kama mtu akipiga kelele na mara kimya ghafla, akageuka nyuma hakumuona Gina.

“Gina! Gina! Ginaaaa!!!” akaita kwa nguvu, na muda huo huo Madam S na Chiba walijitoma katika uwa huo.

“Vipi?” Chiba akauliza akiwa na bastola mkononi.

“Gina amepotea ghafla,” Kamanda akajibu. Wakati akigeuka kutazama kule bombani alimshuhudia yule mfanyakazi akianguka vibaya kwenye wigo wa jumba hilo. Akamkimbilia, alikuwa anavuja damu, mguu wake umevunjwa kwa risasi mbaya kabisa.

“Ulikuwa unakimbia ee? Haya nieleze, umefanya nini?” Kamanda akauliza huku akiwa kamkanyaga kwenye jeraha lake, “husemi? We sugu siyo? Ujue sicheki na mtu sasa?” Kamanda Amata aliushika mguu wa yule mfanyakazi na kuuzungusha vibaya.

“Aaaaaaa niache, nasema…” akapiga kelele

“Sema, yule mwanamke yuko wapi?”

“Kuzimu, kaingia kuzimu!” akajibu.

“Kuzimu ndio wapi?

“Ku-zi-mu, ku-zi-mu, kwani we hukujui Kuzimu?” akamwuliza Amata. Kamanda akaunyonga kwa nguvu ule mguu.

“Aaaaaaaaaaaiiiiiiiigggggghhhhhhh!!!!!” mifupa ya mguu ilitawanyika vibaya.

“Na wenye nyumba wako wapi?” Kamanda akauliza.

“Hii nyumba ya wageni, wameondoka,” akajibu.

“Wameenda wapi?”

“Sijui, walikuwa hapa wiki mbili kaini leo wameondoka,” akazidi kutoa maelezo.

“Ok, wametoka saa ngapi na wamesema wabakwenda wapi?” Kamanda akazidi kuhoji

“Mi sijui kaka, niache basi,”

“Nioneshe, Kuzimu ni wapi?” akambana. Yule kijana akiwa na maumivu makali akamwonesha mkono kwenye bomba alilokuwa akitumia kuunganisha mpira wa maji. Kamanda Amata akamwacha na kuliendea lile bomba.

“Hey, go to hell!!!!” yule mfanyakazi akampigia kelele Amata. Kamanda alipogeuka nyuma alijikuta akitazamana na domo la Revolver, iliyokuwa imeshikwa barabara mkononi mwa yule kijana, ubaridi ukamteremka Kamanda kuanzia utosini mpaka unyanyoni. Paji lake la uso lilitengeneza makwinyanzi ya hasira, “niue kama una shabaha!” akasema. Yule kijana akatoa usalama wa ile bastola tayari kumlipua Kamanda, sura yake haikuonesha masihara hata kidogo.

 

 

ONTARIO-CANADA

JOPO LA WATU WATATU LILIKUWA limekutana tena kwa siri, ndani ya chumba chao cha mikutano kilicho chini ya ardhi lakini chenye kila kitu ambacho mwanadamu atakihitaji, walitazamana na kujikuta wote wapo.

“Karibuni tena,” alisema yule aliyeonekana kama kiongozi wa kikao kila mara, “haya semeni kwa kifupi, kikao chetu ni dakika tisa tu na tano za mwisho ni kufanya maamuzi.”

Mmoja wao ambaye alikuwa mweusi, yaani Mwafrika lakini sijui ni wa nchi gani alianza,

“Tumeweza kupata mzigo, lakini ile nchi ni hatari sana, sasa hivi msako mkali unafanyika na baadhi ya vibaraka tuliowaweka wamekwishapoteza maisha, nina wasiwasi na sisi kujulikana,” alimaliza kuongea, na hakutakiwa kuongea tena.

“Taarifa nilizozipata kutoka katika mtambo wetu ulioko huko Afrika Mashariki ni kuwa idara ya kijasusi ya Tanzania imeingia kazini kufanya uchunguzi wa sakata hili, kama wangefanya polisi wa kawaida hakika nisingekuwa na wasiwasi, lakini idara yao ya ujasusi ni hatari sana ni bora utafutwe na CIA watachelewa kukupata lakini TSA ni hatari sana,” mtu wa pili akasema na kisha kunyamaza kimya kwani muda wake ulikwisha.

Yule kiongozi wao, akashusha pumzi ndefu na kuwatazama watu wake, “hatutakiwi kuwa na mashaka, tunajua ni nini tunachofanya, huu ni mkataba na mkataba lazima ufanyike kadiri ya makubaliano yaliyomo ndani, sasa tupo kwenye kurasa zizlizofungwa kwa pini za dhahabu, kama hatoshtuka, tukimaliza hizo tutafika kurasa ya mwisho ambayo ni kummaliza yeye mwenyewe.” Akatulia kidogo na kuwatazama upya kisha akasema, “lakini sasa hapa kuna kazi mpya inaingia na ni lazima tuishughulikie kabla ya kutekeleza mpango wa pili wa  kurasa zenye pini ya dhahabu, nendeni tukutane hapa baada ya masaa kumi na nne tujue tunafanya nini,” akamaliza.

Wote wakatawanyuka na kutawanyika, katika kikao hicho hakuna aliyetakiwa kuhoji chochote isipokuwa kuitikia na kuongeza wazo tu

 

 

5

Mwanza

GINA ALIJIKUTA AKIDONDOKA KATIKA CHIMO au chumba kidogo chenye ukubwa wa mita moja nanusu ya mraba. Alianguka juu ya vitu vigumu, alijisikia maumivu sana, akajaribu kunyanyuka akipapasa huku na huko, giza lilitawala. Miguuni mwake alikuwa akihisi kama mikono ya watu ikimshika miguu mara kwa mara, wakati mwingine akahisi anakanyaga kitu kama nazi lakini hakuweza kuona chochote kutokana na giza nene ndani ya shimo lile. Akaingiza mkono mfukoni mwake kutafuta simu, akaitoa, akawasha tochi na kumulika ndani ya shimo hilo. Lo! Gina alishtuka sana akabaki katumbua macho! Mifupa ya watu ilijazana ndani ya chumba hicho kidogo, vitu alivyoviona kama nazi vilikuwa ni mafuvu ya binadamu. Akatetemeka kwa hofu, alihisi kama amefika kuzimu.

“Shiit!” akang’aka, huku akitetemeka sana, akainua simu yake na kubonya namba za Kamanda Amata, akaweka sikioni, hakuna kitu. Simu hiyo haikuita kabisa alipoichunguza akakuta ikimuonesha hakuna mtandao eneo hilo. Akachanganyikiwa, akatazama kwa kumulika kuta za shimo au chumba hicho, zilikuwa kuta laini sana zisizo na hata mkwaruzo, zilikuwa zimewekwa marumaru, harufu ya uvundo ilikuwa imetawala ndani yake. Hakujua afanye nini. Nitafia humu? Akajiuliza akikata tama.

 

***

Madam S na Chiba walikuwa ndani ya jumba hilo, kila mmoja bastola mkononi wakikagua chumba kimoja baada ya kingine. Kila chumba walichopita kilikuwa tupu, ni vitanda na vitu vingine tu.

“Chiba, nilinde,” Madam akamwambia Chiba kisha akaibana bastola yake kwenye kiuno cha suruali aliyovaa, akaanza kufungua kabati moja moja, kila moja lilikuwa tupu, zaidi ya mataulo na mashuka hakukuwa na jipya. Akatoka na kuingia chumba kingine, nako vivyo hivyo, akapita vyumba kama vinne hivi. Akiwa katika ujia mdogo wa kuelekea maliwato, akauona mlango mwingine pembeni, Chiba akiwa nyuma yake na bastola mkononi iliyokamatwa kwa mikono miwili tayari kutii amri yoyote itakayoamuriwa alikua nyuma ya Madam S akitazama kila kona kwa makini.

Katika masikio yao wote walikuwa wamepachika vifaa maalumu vilivyowafanya kuweza kuwasiliana muda wote, hivyo walikuwa wakisikia mahojiano ya Amata na yule kijana huko nje. Mlango ulio mbele ya Madam S ulikuwa umefungwa, aliutikisa tena na tena lakini ulifungwa kabisa, akaichomoa bastola yake na kukifumua kitasa, ukaachia, ndani kulikuwa ni kama stoo, vikolokolo vya ufundi na vitu mbalimbali vililundikana, akaishusha bastola yake na kuiweka tena kiunoni, akavuta hatua moja na kufika mlangoni, akasita kuingia, akatanguliza mkono aone kama kuna hatari yoyote ambayo ingemshambulia. Ghafla vitu kama misumari vilifyatuka kwenye pande mbili za yale mashelf na kutawanyika kila kona.

“Aaaaaaiiigghhh Shiiit!” Madam alilalamika maumivu pale msumari mmoja ulipotoboa kiganja cha mkono wake.

“Madam!!” Chiba akaita. Madam S akamuoneshea ishara ya mkono kuwa abaki pale pale na vilevile. Madam S akachomoa kale kamsumari mkononi mwake, kisha akatoa kitambaa chake cha shingoni na kujifunga kiganjani akidhibiti damu kutotoka kwa wingi. Alipohakikisha yuko sawa, akafanya tena mtindo uleule, akatanguliza mkono ndani ya chuma kile, hakukutokea chochote. Chumba hicho kilitegwa silaha maalumu ambapo mtu yeyote asiye rafiki na nyumba hiyo akiingia angeshambuliwa na bomu la misumari lakini kama ni mwenyeji anajua nini cha kufanya kwanza. Madam S akaingia na kutazama yale mashelfu yalivyojipanga. Hakugusa kitu, alikuwa akitazama tu, baadae akaanza kugusa na kutikisa hapa na pale, mahala fulani chini ya moja ya mashelfu hayo kulikuwa na kipande cha marumaru ambacho kilitofautiana ua moja na vingine. Si rahisi kwa mtu wa kawaida kugundua tofauri hiyo, akakikanyaga na mara shelf moja lililombele yake likasogea pembeni taratibu na kuacha mlango mmoja uliofungwa. Akashika kitasa na kukinyonga, ule mlango badala ya kufunguka ukafyatuka kwa juu na kuwa kama unaoanguka kwenda ndani taratibu, mbele yake kulibaki na uwazi ambao ni sawa na chumba kidogo, akasita kuingia.

***

Kamanda Amata alitulia palepale akipanga cha kufanya, hakuweza kugeuka kwani alijua wazi kuwa kwa kugeuka kwake basi kijana huyo angefyatua bastola yake.

“Ua!” akatamka. Yule kijana hakuelewa, wakati akishangaa, alijikuta akitupwa nyuma na kujibamiza kwenye nguzo ya umeme, akaanguka chini, marehemu, risasi ya Scoba ilifanya vitu vyake. Kamanda Amata akaliendea lile bomba na kutazama koki yake, ndipo alipogundua kuwa katikati ya koki kuna swichi ndogo ya rangi ya bronze, akajaribu kubonyeza na kuishika bila kuachia.

Mbele ya mlango wa kuingia nyuma kubwa pakafunguka, na shimo la urefu wa futi nane likawa wazi, ndani yake, mifupa, mafuvu na mabaki ya binadamu yalijazana, Gina alikuwa ndani yake.

“Kamandaaaa!!!” akaita. Kamanda akasikia sauti ya Gina, akamwita Scoba na kumwambia atazame humo ndani. Scoba akatoka garini na bunduki yake mkononi mpaka pale akachungulia ndani akamuona Gina. Scoba akatazama huku na kule, akaenda pembeni na kuchukua bomba la chuma lililolazwa pembeni, akaja nalo na kuweka katikati ya ile milango ya lile tundu, akaizuia isijifunge.

“Achia Kamanda,” akamwambia Amata ambaye bado alikuwa kaishikilia ile swichi, ile milango ikarudi lakini ilizuiwa na lile bomba. Scoba akakimbia garini na kutoa kamba ngumu ya kuvutia gari, akarudi na kwa pamoja na Amata wakatumbukiza huku kipande wakishika wao.

“Gina, Shika kamba hiyo,” Scoba akamwambia Gina kisha wakaanza kumvuta juu mpaka walipomtoa, lo!

“Hawa watu ni wakatili sana, ina maana ni watu wangapi wamefia kwenye shimo hili?” akauliza Kamanda.

“Na serikali haijui lolote, mnasikia tu mtu kapotea lakini hamumwoni tena,” Scoba akajisemea kwa sauti ya chini, hii lazima ifanyiwe kazi.

“Gina unajisikiaje?” Kamanda akamwuliza.

“Mwili unauma maana niliangukia juu mifupa, lakini niko poa,” akajibu. Akaitazama simu yake sasa ilimuonesha kuwa mtandao unapatikana.

“Vipi? Mbona washangaa?” Kamanda akamwuliza Gina.

“Nashangaa kule chini simu yangu ilikata mtandao lakini hapa inasoma,” Gina akaeleza.

“Lazima wafanye hivyo kwani bila hivyo hapa pangejulikana kitambo sana,” Kamanda akajibu, “Ok, Gina na Scoba wekeni ulinzi nje hakikisha watu wanakaa mbali na eneo hili, mi naenda ndani kuwasaidia Madam na Chiba,” akatoa maelekzo.

Timu nzima ya TSA ilikuwa katika eneo la jengo hilo, hii ilikuwa ni mara ya kwanza watu hawa hatari wa serikali ya Tanzania kuwapo katika kazi moja, hii ilimaanisha kazi ilikuwa nzito na haikutaka lelemama.

Ndani ya jumba lile Madam S alikuwa ameteremka chini kabisa ya jengo na wakati huohuo Amata aliungana nao.

“Usalama!” Kamanda akatamka.

“Usalama!” Chiba akajibu, bila hivyo ilikuwa ni rahisi kwa Chiba kufyatua risasi yake.

“Nje kwema vipi humu?”

“Utata mwingi Kamanda,” Chiba akajibu.

“Ok, shuka kwa Madam mi naweka ulinzi wenu,”  akamwambia Chiba, na wakati huo Chiba akashusha bastola yake na kuiweka kiunoni, akateremka ngazi kwenye ule mlango na kuungana na Madam kule chini. Huko chini Madam S alifika katika chumba kimoja kilichojengwa chini ya ardhi, kilikuwa ni chumba chenye mitambo mingi ya kielektroniki, Chiba naye akafika.

“Hapa ndipo walipokuwa wakinasa mawasiliano yetu,” akamwambia Madam.

Kisha wakatzama huku na kule kwenye vyumba vingine, chumba kimoja wakakuta kimefungwa.

“Chiba, vunja mlango!” Madam akamwamuru. Chiba aliruka teke moja kali kwa miguu miwili akauvunja mlango na kubaki wazi. Hawakuamini wanachokiona.

“Mheshimiwa!!!” Madam alang’aka na kuingia haraka ndani ya kile chumba, kisha Chiba akafuata.

Alikuwa Waziri wa Nishati na Madini, amefungwa katika kiti, usingizi mzito ulikuwa umempitia, Madam S akatazama huku na kule akamgusa hapa na pale.

“Haraka hospitali,” akamwambia Chiba, wakamwita Kamanda akateremka haraka, kwa kushirikiana walimtoa mahala pale na kumbeba mpaka juu.

“Scoba, ita polisi, waambie wafike hapa haraka sana,” Madam akatoa amri. Mwili wa Waziri ukapandishwa mpaka kwenye sebule kubwa, Madam S akapiga simu kwa Dr. Jasmin na kumwamuru afike haraka.

Dakika tano baadae, tayari vijana wa FFU wenye silaha za kutosha walifika na kutawanyika kuazunguka nyumba nzima, alkadhalika RPC wa Mwanza alifika kujionea hali halisi, wakati huo tayari Madam S na vijana wake washaingia garini, Mheshimiwa akapakiwa kwenye gari la wagonjwa na Dr. Jasmin alikuwa akimpa huduma ya kwanza, wakaondoka mahala pale.

***

Hali ya hewa ilikuwa imetulia kabisa katika Uwanja wa ndege wa Mwanza, abiria walioahirishiwa safari kwa muda walikuwa wamechoka kusubiri wakimlalamikia Meneja wa Uwanja kuwa kwa nini hawapi sababu ya kucheleweshewa safari zao. Wenye viherehere walikuwa washafika ofisini kwa Meneja huyo na kuanza kuchonga midomo yao.

“Kwa nini mnatufanyia hivyo jamani, nusu saa sasa imepita,” mmoja alilalama.

“Kama mmeshindwa kazi semeni bwana sio mnakuwa wababaishaji tu,” mwingine akadakia huku akirusha mikono yake juu huku na huko.

“Yaani nchi hii bwana, kila kitu wanachukulia kawaida tu,” sauti upande wa pili wa abirai ikasikika.

Meneja wa Uwanja kwa kutumia kipaza sauti cha matangazo akawatangazia watu ili kuwashusha presha.

“Mtusamehe ndugu abiria, kusimamaishwa kwa safari hatujaamua sisi wenyewe, hii ni amri ya serikali haina swali wala jibu ni matekelezo tu.”

Muda huo huo gari moja nyeusi ikasimama maegeshoni mwa uwanja huo. Madam S akifuatana na Kamanda Amata wakateremka na kutembea harakaharaka kuelekea katika ofisi ya Meneja huyo, wakamkuta ofisini huku askari wa polisi wakiwa mlangoni.

“Mnaenda wapi?” wale polisi wakawauliza.

“Tuna shida na Meneja,” Madam akajibu.

“Hamuwezi kumuona kwa sasa, ana kazi nyingi,” yule polisi akajibu.

“We! Usinipotezee muda, hujui unaongea na nani sawa?” Madam akaongea kwa hasira wakati huohuo Kamanda Amata alikwishafungua mlango na kuingia ndani, walimkuta Meneja kajiinamia.

“Oh, karibuni sana,” yule Meneja akawakaribisha mara baada ya kujitambulisha kwake, “Sasa tangu mliposema kuwa tuzuie ndege yoyote isiondoke tumefanya hivyo na mpaka sasa ndege zote nne zilizokuwa ziruke ndani ya saa mbili hizi bado zipo na abiria wake kama unavyowaona almanusura wanitoe macho ndiyo maana nimeweka polisi hapo mlangoni,” akaeleza.

“Ok, sasa ni hivi, kuna watu tunaowatafuta, lakini hatujui hata sura zao wala majina yao, kwa hiyo tutafanya gwaride la utambuzi sasa kwa abiria wote,” Madam akaeleza.

Dakika tano baadae, abiria wote 130 waliokuwa uwanjani hapo walipangwa na kutakiwa kuingia katika ofisi ya Meneja mmoja baada ya mwingine kisha kuelekea kwenye ndege zao. Zoezi lilichukua saa nzima, mahojiano makali ya kujua wapi unatoka, unakwenda na unafanya nini yalichukua nafasi lakini hayakuzaa matunda.

“Hapa hakuna mhalifu, wote wanaonekana raia wema tu,” Kamanda akasema, “Je; kuna ndege nyingine yoyote iliyoondoka kabla ya hizi?” akauliza.

“Ndiyo ipo ndege ya kukodi ya shirika la Darair , imeruka saa moja kabla hamjapiga simu,” meneja akajibu.

“Ilikuwa na abiria wangapi?”

“Imeondoka na abiria watatu tu, wawili wanaume na mmoja mwanamke,wote ni raia wa kigeni,” Meneja akaeleza.

“Ok, kama inawezekana nahitaji kujua taarifa zao kutoka kwa wakala wa kampuni hiyo zaidi ya hapo naomba uruhusu watu waondoke maana wamenuna wasije kupasuka,” Kamanda akaongea na kuchomekea utani kidogo ili kumfanya Meneja huyo asiogope sana.

***

Mikononi mwa Kamanda Amata na Madam S kulikuwa na picha sita za watu watatu, kila mmoja alitolewa nakala mbili za picha yake.

“Stephen Peterson, raia wa Norway, mfanyabiashara za madini, umri miaka 32, anaishi Texas Marekani, yupo nchini kwa wiki moja,” Kamanda Amata akamaliza kusoma, akaiweka pembeni taarifa hiyo, akachukua nyingine.

“Richard Clouch, mwandishi wa habari wa gazeti la Mirror la Uingereza, anaandika habari za Biashara na Uchumi naye alikuwa nchini kwa wiki moja anishi Manchester ana miaka 30,” akaiweka pembeni na kuchukua ya yule mwanamke, akaitazama mara mbili mbili.

“Jesca Jenny ana miaka 29, raia wa Honolulu, Mtalii, alikuwa nchini kwa wiki moja,” hii kidogo ilimvutia Kamanda Amata hasa ukizingatia jinsi watu hawa wenye taaluma tofauti kuwa pamoja. Alivutiwa zaidi na mwanamke huyu, akaitazama ile picha ya yule kwa umakini wa hali ya juu.

“Umesema wanaondoka na ndege gani?” akamwuliza mhudumu wa ofisi hiyo.

“Kwa taarifa za tiketi zao, wanaondoka na KLM leo saa sita usiku, wameelekea Dar es salaam sasa,” akajibu.

Kamanda Amata akamtazama Madam S, akamwona jinsi sura yake sasa ilivyoanza kuupoteza usichana na kuingiwa na uzee wa ghafla, “Mama, ni sawa?” akamwuliza.

“Si sawa hata kidogo,” akamgeukia yule mhudumu, “Ndege yenu iliyowasafirisha hawa watu imeshatua Dar es salaam?” akatupa swali.

“Ndiyo imetua nusu saa ilopita,” akajibu.

“Ok, asante sana, usihofu, tatizo ni kuwa hawa watu walikuwa nchini na kufanya kazi tofauti na vibali vyao ndio maana tunawafuatilia,” Kamanda akamweleza yule binti kisha wakaagana.

 

HOSPITALI YA SEKOU TOURE

  1. JASMINE, ALITULIA KITINI mbele yake akiwa na jopo zima la TSA, akainua bilauri yake yenye Tusker baridi akapiga mafunda matatu ya nguvu kisha akashusha pumzi ya kuridhika.

“Mheshimiwa vipi?” Kamanda akauliza.

“Ataamka muda si mrefu, kwani walimchoma sindano mbaya ya usingizi, lakini dawa waliyoitumia inambadala wake hivyo tumemchoma sindano nyingine ambayo itamzimua na kumwamsha mara moja,” akajibu Dr. Jasmine.

“Good,” akajibu Madam na kujiegemeza kwenye kiti hicho cha chuma, mara akakumbuka kitu, akajiweka sawa, “Jasmine, maana tumekuwa na mengi sana, hebu nambie kule Shinyanga mlipata nini?”

“Aaah, nilifanya uchunguzi wa miili kama ulivyoagiza, lakini kuna utata kidogo kwani maiti ya Mc Lean inaonekana na jeraha jembaba la bunduki ya kisasa inayotumiwa na majasusi wengi duniani ambayo haitoi sauti na ni ndogo pia sio rahisi mtu kuitambua kuwa ni bunduki, huwa inavaliwa kama saa ya mkono, na mtumiaji akikunja ngumi kisha kuirudisha chini, bunduki hiyo hujifyatua kwani trigger yake iko chini na ufyatua kwa kukandamizwa,” akawaeleza.

Madam akahifadhi hayo yote kichwani mwake. Akamtazama Kamanda Amata, “Niambie!”

“Sasa naanza kuingiwa na wasiwasi kama ni kweli Mheshimiwa waziri kafanya uhalifu huu, lakini pia labda wamemzunguka kama alishirikiana nao, ngoja aamke,” Kamanda akaeleza. Mara mlango ukagongwa, Dr. Jasmine akafungua, alikuwa muuguzi mmoja aliyekuja kumwita Daktari huyo, wakatoka haraka haraka na muuguzi yule.

Dakika kumi baadae Jasmine alirudi nakuleta habari njema, Mheshimiwa kaamka. Madam S na vijana wake waliinuka na wote wakaelekea kumwona Mheshimiwa huyo.

Chumba kipana cha V.I.P kilichokuwa na kila kitu ndani, kitanda kizuri, vinywaji vya kutosha na kila kitu, Kamanda alikitazama chumba hicho mwanzo mpaka mwisho. Ingekuwa Watanzania wote wanatibiwa hivyo wasingeogopa kifo, Kamnda akawaza.

Mheshimiwa Waziri alikuwa ameketi kwa msaada wa kitanda hicho, akiwatazama waliokuwa mbele yake, mara moja akamtambua Madam S.

Wakati huo wote Madam S alikuwa anajaribu kutazama hali ya Waziri huyo, kama ni ya woga, kutetemeka au kuna tofauti yoyote ile ambayo itamfanya amgundue kuwa ni mualifu.

Dr. Jasmine aliwaomba wasiohusika wapishe kwanza ili wafanye kazi yao. Sasa chumba kilibaki na watu saba tu.

“Pole sana Mkuu,” Madam alimpa pole.

“Asante sana, watu wabaya sana jamani,” akasema kwa sauti ya tabu kidogo.

“Unajua kuwa una kesi ya kujibu?” Madam akamuuliza.

“Kesi! kesi gani?” Mheshimiwa Waziri akajibu kwa kuuliza akionekana kushangaa kwa hilo. Madam S aliuliza makusudi tu ili kuona atalipokea vipi swala hilo.

“Unatakiwa Dar es salaam sasa hivi! Ukajibu tuhuma zako mbele ya Rais na kisha utapandishwa kizimbani,” Madam akamwambia bila kucheka.

 

 

 

DAR ES SALAAM

MADAM S NA KIKOSI CHAKE WALIKUWA wamekutana Shamba kama kawaida yao wanapokuwa na hoja nzito za kutafutia ufumbuzi, safari hii walikuwa na Mheshimiwa Waziri waliyemleta hapo kwa siri, taarifa za kupatikana kwake zilibanwa, hakuna chombo cha habari wala taasisi yoyote iliyoruhusiwa kutoa habari hiyo. Mheshimiwa Waziri alikuwa akipata kahawa huku akiendelea na matibabu chini ya Daktari Jasmine. Baada ya kuwa kapata nafuu na anaweza kuongea vizuri, akawekwa kwenye chumba maalum cha mazungumzo kilichokuwa na meza moja na viti vitatu tu, lakini upande wa pili Chiba alikuwa kwenye mitambo akisikiliza kila kitu ambacho waziri huyo alitakiwa kuzungumzia tuhuma hizo. Walikuwa wakisubiriwa watu watatu muhimu katika jumba hilo ‘Shamba’.

Dakika tano baadae, gari maalumu ya idara ya TSA iliyokuwa ikiendeshwa na Scoba ilikuwa ikiingia kupitia mlango wa nyuma wa jengo hilo kongwe maeneo ya Gezaulole, iliingia na kuegeshwa ndani kabisa mwa egesho la siri. Rais, Makamu wake na Waziri mkuu waliteremka, wakapokelewa na Madam S na Gina, wakakaribishwa ndani na kupitishwa moja kwa moja mpaka kwenye chumba maalum walichoandaliwa. Mpaka wanafika hapo waheshimiwa hao hawakujua wako wapi kwani gari waliotumia kufika nayo hapo haikuwa ikionesha chochote kutoka ndani hivyo abiria hakujua ni wapi anapelekwa.

“Sasa hapa ni wapi?” Waziri mkuu akamuuliza Gina.

“Mheshimiwa hapa nimahali pasipojulikana na mtu, hata mimi mwenyewe sipajui,” kisha wote wakacheka.

Kila mtu alipokuwa tayari katika mahala pake, Madam S na Kamanda Amata wakaanzisha mazungumzo na mheshimiwa waziri. Waziri hakujua kama kuna ugeni mzito ndani ya jengo hilo.

“Tulitua na ndege katika uwanja mdogo wa North Mara majira ya saa tatu asubuhi, nikiwa na wageni wangu wote na ujumbe niliofuatana nao, tukiwa pale tulifanya kila tulichotakiwa kufanya, tulikagua mgodi katika vitengo muhimu, tukaongea na meneja na wafanyakazi baadhi kuwasikiliza kero zao na pia kujua ufanisi wa kazi zao…”

Kamanda Amata akakatisha, “…Nikukatishe Mheshimiwa, hebu niambie juu ya wageni wako waliofuatana nawe, unawajua kiasi gani hasa hawa wa kutoka nje,” akahoji.

“Yeah, wale jamaa mwanzoni niliwaona ni watu wenye nia nzuri ya uwekezaji kwa sababu mmoja alikuwa ni muwakilishi wa kampuni ya Robinson Dia-Gold Mines ya Canada, na mwingine ni kutoka Cunglia Cold Mines ya Uingereza kila upande walikuja wawili, na watu hawa nilikutana nao miezi sita iliyopita karika mkutano maalumu wa uwekezaji huko Geneva ambako nilikwenda nikifuatana na katibu wangu.”

Mheshimiwa Waziri alielezea mengi sana juu ya safari hiyo.

“Ok, Sasa unajua una kesi gani ya kujibu?” Kamanda akamwuliza.

“Hapana na ndio maana nashangaa, sijui kesi yoyote ninayotuhumiwa kama ipo,” waziri akajibu, Madam S na kamanda Amata wakatazamana. Kisha wakawasha TV ndogo na kumuonesha habari iliyorekodiwa kutoka TVT ikielezea wizi wa almasi na vifo vya watu wawili huku yeye waziri akituhumiwa. Hali ya mshangao na mshtuko ilionekana ghafla usoni mwake, akaanza kupumua kwa nguvu.

“Tulia Mheshimiwa, usihofu, hii ni habari iliyotokea ndani ya masaa sabini na mbili yaliyopita, na wewe ni mhusika,kabla ya kupandishwa kizimbani tukakuleta hapa kwanza ili tujue ukweli,” Madam akaeleza.

“Haya tuambie uko vipi na tuhuma hizi, kwa nini umefanya wizi huu wa mali ya wavuja jasho wa Tanzania,” Kamanda akapiga swali la moja kwa moja.

“Hapana, hapana, sihusiki, nashangaa imekuwaje, unajua kilichotokea, mnajua mimi sikuwepo duniani kwa muda mpaka nimejikuta pale Mwanza hospitalini.”

“Haya, tuambie, nini unakumbuka cha mwisho katika safari yako?” Kamanda akauliza, “Naomba usiwadanganye Watanzania, kwa kuwa wewe umeiba na inafahamika hivyo,” Kamanda akamalizia.

“Hapana unajua nini, mnajua kilichotokea? Sasa naanza kuelewa, sasa naelewa, naelewa, tulipokuwa angani wakati tukitoka Mara kwenda Mwadui, tulikumbwa na hali mbaya ya hewa, (akatulia kidogo) kisha tukatangaziwa na rubani kutumia barakoa za oksijeni, basi, basi, hapana sikumbuki kingine, kweli, mi sijaiba, sihusiki…” Mheshimiwa alikuwa kama anaweweseka, hali hiyo ilijionesha wazi, Madam S akatikisa kichwa.

“Mheshimiwa,” akaita, “Mheshimiwa!” akaita tena, ukimya ukatawala, Dr. Jasmine akaingia haraka na mtungi wa kusaidia kupumua (Oxygen Concetrator), akamwekea puani kumsaidia kupumua, kisha kwa msaada na Kamanda Amata wakamtoa kitini na kusaidiana kumbeba mpaka kwenye kitanda, Dr. Jasmine akafanya kazi ya ziada ya kumuwekea drip ya glucose, kisha akachukua vifaa vya kupimia presha (sphygmomanometer na stethoscope ), akaviunganisha na kuchukua vipimo, dakika moja na sekunde kadhaa, akaitoa masikioni ile Stethoscope na kulegeza ile mashine ya presha pale mkononi mwa Mheshimiwa.

“Presha imeshuka, muacheni apumzike kwanza,” Dr. Jasmine aliwaeleza.

Mheshimiwa Rais na makamu wake pamoja na waziri mkuu, walibaki wakitazamana.

“Nini hiki?” Rais akamuuliza Waziri Mkuu.

“Hapa kuna utata, tena utata mkubwa sana hapa mimi ni kama naangalia muvi au nasoma vitabu vya kina Willy Gamba au Joram Kiango, sielewi elewi tu,” Waziri Mkuu akajibu. Mara mlango ukafunguliwa, Madam S akaingia katika chumba hicho.

“Ndio Madam!” Rais akadakia.

“Kama hivyo Mkuu, lakini usijali, ukweli wote utaupata na taarifa itakuja Ikulu ndani ya masaa sabini na mbili kwani tuna watu kumi na nne wa kufanya nao mahojiano,” Madam akawatoa hofu.

“Nakuamini sana pamoja na vijana wako, naona jinsi mlivyojipanga, lakini hebu nipe maoni yako maana hapa nakosa cha kuwajibu Watanzania, nakosa cha kuongea na waandishi wa habari juu ya kadhia hii, Ikulu haikaliki,” Rais akamwambia Madam S.

“Hatuwezi kusema kahusika katika wizi au la, ila tutakapohoji wengine tutaoanisha mambo kisha tutajua kipi ni kipi na hapo sasa ndiyo tutaingia kazini kukamata waliohusika, hata wawe  wanaishi Pluto au juani kote tutaenda, tupe muda Mheshimiwa Rais. Leo jioni tutakuwa na awamu ya pili ya mahojiano na watu wengine, tutajua mbichi na mbivu,” akamaliza.

***

Usiku huo tayari Kamanda Amata alikuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwl. Nyerere akaijaribu kuona kama anaweza kuwakamata watu wake, alikuwa amezinasa picha zao kichwani. Aliegesha gari akateremka na kufunga mlango nyuma yake. Akiwa ndani ya suti nadhifu iliyoficha moja ya bastola zake anayoipenda sana, Kamanda Amata akatembea taratibu kuelekea ofisi ndogo ya KLM. Pale alimkuta mwanadada mrembo akiwa ametulia ofisini mbele akitazama kompyuta kubwa aliyokuwa akiitumia kutatulia matatizo yake kikazi. Akakaribishwa naye akakaribia, akavuta kiti akakaa.

“Naitwa George Kamasi,” akajitambulisha uongo kisha akampa kitambulisho yule mwanadada, akakipokea na kukisoma, kilimwelezea Kamanda Amata kama George Kamasi, mwajiriwa wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika jeshi la Polisi kitengo cha uchunguzi wa makosa ya Jinai. Yule mwanadada akamrudishia, “Ehne bwana Kama… mh! Na hilo jina lako mpaka linatapisha,” akasema yule mwanadada.

“Uwe na adabu unapoongea na watu usiowajua,” Kamanda akapiga mkwara.

“Nikusaidie nini?” akauliza kwa utulivu baada ya kuona bastola iliyolazwa mezani kwa utulivu.

“Naomba unipe orodha ya wasafiri wako hasa wanaoelekea Uingereza, Canada na Honolulu,” Kamanda akaomba. Yule mwanadada akafanya harakaharaka kuitoa orodha hiyo kwenye mashine yake akaprinti na kumpa Kamanda Amata. Amata akaitazama haikumfurahisaha sana kwani Honolulu hakukuwa na abiria yoyote anayekwenda huko, Uingereza kulikuwa na abiria kumi na tano lakini wote walikuwa wanafunzi wa chuo kimojawapo cha huko ambao walikuja kwa utalii wa kimasomo na Canada kulikuwa na watu wawili, lakini wote wanawake. Akashusha pumzi. Ina maana wametucheza shere? Akajiuliza, akachukua zile karatasi na kuzikunja kisha akazitia katika mfuko wandani wa koti.

“Umeridhika?” yule mwanadada akauliza.

Kamanda Amata akamkazia jicho baya, “sijaridhika,” akamwambia.

“Sasa mimi nifanyeje ili uridhike?”

“Ulale na mimi leo,” Kamanda akamjibu bila kucheka.

“Ha ha ha ha huwa silali na wanaume ovyo ovyo, mi matawi ya juu nalala na Mapedeshee,” akajibu huku akinyanyuka.

“Hebu tulia hapo unaenda wapi? Unafikiri mi nimekuja kucheza hapa, akatoa karatasi nyingine na kumpatia, zilikuwa karatasi tatu, zenye picha za watu watatu tofauti.

“Hawa ni nani?” akauliza.

“Nataka uwatambue hao watu, kama wamekuja hapa kukata tiketi siku za nyuma, au unao katika ndege yako, hao ni majambazi wa Kimataifa na ukiwatetea leo unalala selo mwanamke jeuri,” Kamanda akazungumza kwa sauti kavu. Yule mwanadada akatazama zile picha, akachukua namba za tiketi zao na kuingiza kwenye mfumo wao wa kompyuta.

“Hamna watu kama hawa kwenye ndege yetu, kwanza tiketi zao ni feki, ona,” akamgeuzia kioo cha kompyuta, kisha akaongeza, “kama waliwaambia kuwa wanasafiri na ndege yetu leo, hatuna hawa abiria kaka.”

Kamanda Amata au Amata Ric akachukua zile karatasi zake na kurudisha kunakohusika. Akanyanyuka na kusimama wima.

“Ok, asante, na lile nililokwambia la kulala na mimi, tumeishia wapi?” Kamanda akachokoza.

“Heee! Hebu nitokee huko, we unafikiri mi wa kulalwa hovyo hovyo tu, nina watu wangu wenye pesa sio kama wewe unayetegemea kamshahara ka Wizara mwisho wa mweli, go fish,” akasema huku akimtazama Amata kwa jicho la dharau, mwisho akasonya.

“Ok, una maneno machafu wewe, ila ujue tu utaishia mikononi mwangu iwe kwa heri au kwa shari,” Kamanda akatoka na kuondoka.

***

“Yaani bila shaka yoyote tulitekwa, nakumbuka tukiwa tuko angani dakika thelathini baada ya kuruka kutoka Mara, hewa ndani ya ndege ilikuwa nzito sana, mzunguko wake ukawa hafifu, nilipotazama kwenye vipimo vyetu, vikaniashiria kuwa kuna shida katika mfumo wa oksijeni, hivyo sikuwa na budi ili kuokoa abiria wangu nikawaamuru kutumia hewa ya mtungi kwa kuvaa barakoa maalum kwa kazi hiyo, baada ya kuzivaa nikajikuta nashindwa kupumua sawasawa, kifua kinakuwa kizito, mwili unaishiwa nguvu, nikaitoa na kuitupa kando,” Rubani wa serikali aliyekuwa katika ndege ya msafara wa waziri alieleza kinagaubaga.

“Baada ya hapo uliona nini?” Madam akauliza.

“Baada ya hapo niliona kama kivuli cha mtu anayeingia ndani ya chumba cha rubani na kuwatoa wenzangu vitini, hapo sikuona tena kilichoendelea,” akajibu.

“Pole sana Kepteni. Kuna wizi mkubwa sana uliofanyika na ndege yako imetumiwa kubeba kasha tano za almasi zenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Trillion moja kwa hesabu ya haraka haraka,” Madam akamweleza. Yule Rubani akashtuka na kupigwa na hamaniko, “Lo! Itakuwa walewale wazungu, maana hata kabla hatujaondoka walikuwa wadadisi sana, mara waniulize aina ya ndege ninayoirusha, mfumo wake ukoje, mara hiki mara kile, ah, mi nikawa nawapotezea tu,” akawaambia.

Baada ya saa moja ndani ya chumba hicho cha mahojiano alikuwamo mwanadada mmoja mrembo tu, aliyesuka nywele zake kwa mtindo wa rasta za Kimasai zilizomkaa vizuri, Madam S alimkaribisha kitini na kuketi katika mtindo wa kutazama. Madam S alimtazama mwanadada huyo kwa dakika tano bila kumsemesha neno, kisha akafungua kinywa chake.

“Umeolewa?” akamwuliza.

“Hapana,” naye akajibu kwa sauti ya unyonge.

“Una bwana au mchumba?”

“Ndio, nina mchumba tutafunga ndoa mwezi ujao,” akaeleza.

“Nieleze Historia yako kwa kifupi,” Madam alimwomba na yule dada akafanya hivyo.

“Kwani samahani mama, hapa ni wapi nafanya nini? Ni haki yangu kujua kama Mtanzania,” yule mwanadada akauliza.

“Ok, we ni Mtanzania mzuri unayejua unachotakiwa kujua, hapa ni Hospitali ya vichaa, wewe umeletwa hapa baada ya kukamatwa ukitembea bila nguo mitaani,” Madam akamweleza.

“What? Mimi?” akashtuka na kusimama.

“Ndiyo wewe, ulikuwa unazunguka mtaani bila nguo kabisaaaaaa, ndio maana nikakuuliza una mchumba au Bwana,” Madam akamwelewesha.

Upande wa pili wa chumba, Chiba alipasua cheko aliloshindwa kuzuia, lakini bahati nzuri sauti haipiti chumba cha pili na wala haiwezi kuingilia ile rekodi anayoifanya ya mahojiano hayo.

Gina naye alikuwa hoi kwa kucheka, “mwe! Huyu bibi huyu anajijua mwenyewe, sasa ona alivyomvuruga dada wa watu halafu mwenyewe yuko sirias,” Gina alimwambia Chiba.

“Hebu nambie, cha mwisho unachokumbuka katika maisha yako, ulikuwa wapi?” Madam akaanza.

“Nilikuwa Musoma katika mgodi wa North Mara,” akajibu.

“Ulienda kufanya nini?”

“Nilifuatana na msafara wa waziri na wawekezaji wake katika kutembelea migodi ya serikali.”

“Enhe baada ya hapo,” Madam akahoji.

“Sijui kwa kweli na hisi tulipata ajali, maana tukiwa kwenye ndege hali ya hewa ilikuwa mbaya sana, sikumbuki kilichotokea zaidi isipokuwa nikajikuta hospitali,” akajibu. Kisha Madam S akamweleza kila kitu juu ya sakata la madini, yule mwanadada aliishiwa nguvu kabisa, macho yakamtoka pima.

“Usiposema ukweli, unafungwa, kwa maana wenzako wote wametoroka we ndio tumekukamata,” Madam akamtishia, “Uliwaonaje hao wawekezaji?” akaongeza swali.

“Aaa nimekutana na wawekezaji au wafanyabiashara wengi pale wizarani kwa kuwa mimi ofisi yangu ni mambo ya mawasiliano, ila hawa walikuwa walikuwa wahuni sana, halafu walikuwa hawatulii kwenye;  mara chooni, mara kwa mhudumu wa ndege,  mara sijui vitu gani, mmoja akawa ananitaka kimapenzi pindi tukirudi Dar,” akaeleza. Maneno haya yakamgusa Madam S, tofauti na wengine wote, huyu alijibu zaidi.

“Ulimkubalia?” akauliza.

“Hapana, ila alinipa kadi yake ya biashara kuwa tukirudi nimtafute ikiwezekana nikamtembelee Ulaya au yeye angekuja tena kwa ajili yangu,” akaeleza.

“Hongera mwenzetu umejipolea ‘Nyanyamkala’ la kizungu, sasa ungewasiliana naye vipi?” akauliza tena. Madam S alikuwa na maswali madogo madogo lakini yaliyoleta tija kwa kazi hiyo. Yule mwanadada akatoa kadi ya kibiashara akampa Madam S.

“Alinipa card yake hii hapa,” akamwonesha Madam S. akaichukua na kuigeuza geuza, akaitazamisha kwenye kioo kikubwa ambacho kama si mjanja huwezi kujua kama ni kioo, kisha akaigeuza upande wa pili na kuiweka mezani.

Kitendo cha kufanya hivyo, upande wa pili Chiba alielewa, hivyo aliipiga picha ile kadi kutoka upande wa pili na kuingia kumbukumbu zake kwenye kompyuta yake bila mwenye nayo kujua. Kutoka upande wa pili walipo Chiba na Gina, Chiba akaiingiza ile taswira ya kadi katika kompyuta maalum, iliyounganishwa na mtandao wa uhalifu duniani, akaagiza imletee majibu juu ya namba za simu, picha na maelezo mengine.

Madam S, akamruhusu yule mwanadada akapumzike, Dr. Jasmine akaingia na kumchukua kisha akampeleka katika chumba chake cha siri.

 

 

 

 

6

JOPO LILE LA WATU WATATU lilikutana tena mahala palepale, kama kawaida kila mmoja huwa ana njia yake ya kufika hapo, wakamkuta mkuu ameketi akiwasubiri, lakini alikuwa katika hali tofauti sana.

“Ndiyo Mkuu tumekutana kama ilivyo ada, tupe ripoti yako ulivyotuahidi kisha tujue tunafanya nini,” alipendekeza mjumbe mweusi.

“Tunahitaji kufanya kazi ya ziada ndugu zangu, kama tetesi zilivyokuwa kwanza lakini sasa nimeanza kuogopa, vijana wetu wamerudi, mzigo wa Almas umefika tulipoutaka ufike bila tabu, lakini njama imeteguliwa, wale jamaa wa TSA wameweza kugundua kuwa wizi ule haujafanywa na waziri wao, na hii inanitisha kwa sababu mpango wetu ulikuwa yule waziri afie mle ndani ili asionekane tena, kwa mtindo huo tungewajengea imani Watanzania kuwa ni waziri aliyefanya hivyo. Sasa wamempata, kambi yetu ya Mwanza imepekuliwa na kila kitu kiko wazi, hawa jamaa wanataka kupiga hatua ya pili, wanataka kuachana na ya nyumbani na kuwasaka wale makomandoo wetu tuliowatuma. Wakianza kuwachunguza na kufanikiwa kuwagundua, mambo yataharibika,” aliwaambia wajumbe walioonekana kupigwa na butwaa la mwaka.

“Yaani kanchi kale kanajifanya kana idara nzuri ya usalama? Tumewashinda CIA kwenye sakata la kuiba data pale Langley na mpaka leo wamekili kushindwa, tumewazidi kete KGB na tukapata siri za wanaotafutwa na majasusi hao, nini TSA? Ni kuwamaliza tu kabla hatujafanya kazi nyingine, kama ni kikwazo ni kuwapoteza tu, mbona kazi hiyo ni ndogo, kisha Tanzania itajikuta inaamka bila Jasusi hata mmoja,” akaongea kwa hasira yule Mwarabu.

“Sawa lakini tunafanyaje?” yule mkuu akawarudishia uamuzi.

“Tupeleke kikosi chetu cha siri, kikawapeleleze kikiwagundua na udhaifu wao basi ni kuutumia na kuwamaliza, wakati wao wanaomboleza, sisi tunamalizana na mtu wetu,” yule mweusi akaongea.

“Good Idea,” (wazo zuri) Mkuu akaitikia.

“Sasa naomba kila mmoja kwenye idara yake akahakikishe analifanya hilo, tukutane tena masaa sita yajayo tumalize kazi.

DAR ES SALAAM – SHAMBA

MADAM S ALISHUSHA FAILI DOGO yaani lenye kurasa chache mezani pake, katika ofisi ya siri huko ‘Shamba’, alijiridhisha na taarifa zote zilizowekwa na Chiba katika faili hilo juu ya mtu anyeitwa George Mc Field, Komandoo mtoro wa jeshi la Serbia, anayejihusisha na kazi za kukodi kufanya matukio yenye utata kama haya. Alikuja Tanzania mara ya pili akiwa bado ana kumbukumbu juu ya sakata la walilolipa utambulisho kama ‘Mwanamke Mwenye Juba Jeusi’ jinsi alivyoponea chupuchupu dhidi ya mkono wa Kamanda Amata, na mwenyewe alikiri kuwa huyo ni ‘Mwanaume wa chuma’. Kwa jinsi alivyoweza kujibadili kitaalamu akiwa huko kwao, aliamini wazi kuwa hatoweza kugundulika na mahasimu wake ambao walisikitika kuikosa roho yake akiwemo Madam S.

Madam S analikumbuka jina hili, anatabasamu anapogundua kuwa, mtu huyo kajibadilisha sura na muonekano wake lakini kashindwa kujibadilisha mbinu zake. Bomu dogo la misumari lililolipuka kwenye moja ya vyumba vya lile jumba kule Mwanza na kumuumiza Madam S mkononi lilimkumbusha lile ambalo lililipuka miaka kadhaa nyuma katika jumba la daktari mmoja huko Keko na kumuumiza kijana wake Amata, lilitegwa na Mc Field, hivyo hakuona ajabu kukutana tena na jina hilo.

“Ndege mjanja hunasa katika tundu bovu,” akajisemea huku akilisukuma lile faili pembeni na kulivuta lingine nalo akalichambua kutazama ndani yake kuna nini, mauaji tata ya Khumalo mwaka mmoja na nusu uliopita, lakini faili hilo halikukamilika kwani hakukuwa na taarifa za kutosha kutoka Afrika Kusini kama sakata hilo lilipatiwa ufumbuazi au la. Chiba alimaliza kurasa ya mwisho kwa kuweka kiulizo na kishangao, na chini akaweka sentensi moja yenye maneno ‘Khumalo na wizi wa almasi Tanzania,’ Madam S akagonga gonga kidole chake kwenye faili hilo, hii ilionesha mwanamama huyu anahitaji kujua jambo katika kisa hicho. Alikuwa peke yake ofisini, wakati wengine wote wametawanyika, isipokuwa Dr. Jasmine ambaye daima alikuwa jirani sana na Madam S hii ilitokana pia na umri kumtupa mkono. Akainua mkono wake, akacheza na saa yake kisha akaongea maneno fulani, akatulia na kusubiri.

***

Simu ya Kamanda Amata ikaita kwa sauti ya chini, akaichomoa mfukoni, akajua tu kuwa ni simu ya kirafiki ambayo haina madhara yoyote.

Akaitoa na kutazama, akatabasamu, Jenny.

Kamanda Amata alikwisha msahau mrembo huyu kutokana na kubanwa na majukumu, alipoona jina hilo likirukaruka kwenye kioo cha simu yake moyo wake ukachanua kwa furaha kama ua la saa sita, akavuta kumbukumbu za msichana huyo, katibu muhtasi wa ofisi ya mkurugenzi wa Mgodi wa Mwadui ambaye sasa ni Marehemu, Mc Lean.

Akabonyeza kitufe cha kijani na kuiweka jirani naye sio sikioni.

“Za saa hizi bro,” sauti ya Jenny ikasikika ikiongea kwa chini kidogo kana kwamba anaogopa kufumaniwa.

“Nzuri, unaendeleaje?” Kamanda akamjibu.

“Niko poa, sasa sikiliza…”

Kamanda kichwa chake kikafunguka mara moja, mrembo huyu anataka kumwambia nini, “Nakusikia, niambie,” akamjibu.

“Kuna kitu nimekiokota hapa lakini sijui ni kitu gani, labda wewe unaweza kukitambua, nimekihifadhi,” akamwambia Kamanda.

“Kikoje?”

“Sijui nikielezeeje, ni kama kikadi fulani laini kina rangi ya kijani, hiki kitu sijawahi kukiona ofisini, nimekikuta chooni,” akaeleza. Kamanda Amata hakuona umaana sana lakini hata hivyo kutokana na kazi yake huwa hatakiwi kumpuuza hata kipepeo au dondola, kila kitu kwake huwa kina maana na kinahitaji kufanyiwa kazi.

“Ok, usikitupe, kifiche, nitakupigia na kukuelekeza cha kufanya,” Kamanda akajibu na kukata simu. Alijaribu kuvuta taswira kuwa ni kitu gani lakini hakupata jibu la haraka haraka. Akampa Chiba hiyo taarifa, Chiba akamsisitizia Amata kutopuuza hata unyoya wa kuku.

“Kaka fanya juu chini tukipate inawezekana ikawa ni moja ya vitu vitakavyotusaidia,” alimwambia. Kamanda Amata akainua simu na kumpigia Jenny.

“Kesho, hakikisha unafika Mwanza na kuchukua ndege ya mchana kuja Dar, usikiache hicho kikadi maana ninakihitaji kuliko wewe,”nakamwambia na kukata simu. Wakati huohuo saa yake ikamfinya kuashiria kuna ujumbe unaingia. Akaruhusu na kuuvuta nje mkanda mdogo wenye ujumbe huo.

…Wahi kabla pilau halijachacha…

Akacheka kwa luga hizo za Madam S. Akafungua mlango wa gari na kuuyaacha maegesho ya Uwanja wa Ndege, polepole akaondoka zake.

***

Ndani ya afisi ya mwanamama huyo, Kamanda Amata akatua faili alilokuwa akilisoma, akaliweka mezani na kumtazama Madam S, akatikisa kichwa.

“Mbona kazi hii inataka kututoa jasho? George Mc Field yupo hapa, tena katika sakata hili? Sasa nimeelewa, nimeelewa nini kinaendelea, tuna kazi nzito sana,” akasema huku akinyanyuka na kulielekea jokofu lililokuwa likibaridisha vinywaji.

“Achana na hilo, nataka uende Afrika Kusini nakupa masaa sita tu ya kufanya kazi pale na kurudi, hivyo siku 2 tu uwe hapa kuanzia sasa ninavyoongea,” Madam S akamwambia Amata.

“Madam, hili halijaisha linakuja lingine tena?” akauliza.

“Hapana, ni hilihili, nataka ukafanye uchunguzi juu ya mauaji ya Khumalo, mazingira ya kifo, muuaji ikiwezekana uje na picha ya muuaji kama aliwahi kuonekana au ni shetani, maana hata shetani picha yake ipo, nimemaliza, potea! Hilo ni moja ya kesi hizihizi, na mimi utanikuta hapahapa siondoki mpaka urudi,” akamaliza.

“Sawa Madam, nimekuelewa,” akajibu.

Ilikuwa ni safari ya dharula lakini ni moja kupata majibu ya mambo fulani fulani ambayo yangeweza kutoa mwelekeo wa sakata zima linalosumbua vichwa vya wanausalama hawa. Baada ya saa moja Kamanda Amata alikuwa angani kuelekea Durban Afrika ya Kusini, akiwa ndegeni kwenye chumba cha V.I.P alikuwa akifikiri wapi pa kuanzia.

Saa sita maana yake sihitaji kulala, aliwaza bila jibu.

 

UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA

WA LUIS BOTHA-DURBAN S.A

‘Ukipita kwenye nyayo za mbwa utajua tu kaelekea wapi’  Kamanda Amata alikumbuka sentensi ya mwisho ya Madam S alipokuwa akiagana naye.

Nianzie wapi? Polisi, ofisini au nyumbani kwake? Alijiuliza na kukosa majibu. Akaitazama saa yake, ilikuwa ni saa tatu asubuhi, akateremka kutoka katika ndege hiyo, akakaribishwa na hali ya hewa ya upepo wa bahari. Kwa hatua za taratibu sana akajivuta kuelekea kwenye jengo la ukaguzi na moja kwa moja akaiendea kaunta na kukutana na mwanadada mmoja aliyekuwa hapo.

“Hauna mzigo wowote?” yule dada akauliza.

“Hapana, niko hivi unavyoniona,” Kamanda akajibu.

“Ok, karibu sana Durban Mr. James Ka..”

“..Kariuki, James Kariuki,” akamalizia Kamnada.

“Jisikie upo nyumbani,” yule mwanadada akamkaribisha.

“Asante.”

Saa nne na dakika tano ilimkuta mbele ya ghorofa la wastani, lililopambwa kwa maandishi mazuri yanayosomeka, KHUMALO TOWER, aliyatazama na kisha akavuta hatua na kuifikia kaunta ya mapokezi iliyokuwa na askari wanne wa kampuni binafsi ya ulinzi. Alipowaeleza kuwa anahitaji kufika katika ofisi za The Great Khumalo, akakaribishwa bila taabu. Akavuta hatua na kuchukua lifti akapanda mpaka ghorofa ya  saba.

Mbele yake kulikuwa na meza kubwa ya kisasa ambayo ilitanguliwa na mwanamke mmoja wa miaka thekathini hadi thelathini na tano hivi, alionekana kuwa ndiye aliyechukua cheo cha Mkurugenzi wa kampuni hiyo. Haikumchukua muda Kamanda kujua kuwa binti huyo ana unasaba wa karibu na marehemu kwani mbele kabisa ya meza hiyo kulikuwa na kibao chenye maandishi ya dhahabu Ms. Lereti Khumalo M.D.

“Karibu sana, japokuwa sina miadi na wewe ila nitakusikiliza kwa kuwa umetoka mbali kama ulivyonieleza,” yule mwanadada alimwambia Amata mara baada ya kujitambulisha.

“Asante kwa ukarimu wako mrembo, naitwa Mr. James Kariuki, ni Mkenya ninayeishi Tanzania, nimekuja bila miadi lakini nina jambo muhimu la kibiashara la kuzungumza,” akajieleza, lakini akaona kamshtuko fulani kutoka kwa yule mwanadada.

“Biashara gani? Kama almasi za wizi hatununui,” Lereti akamkatisha.

“Ha! Umejuaje?” Kamanda akajifanya kushangaa.

“Najua, nina habari zote za juu ya huo wizi kupitia vyombo vya habari, lakini ninyi Watanzania mmekuwa mabwege sana hata mnaibiwa kijinga na waziri wenu! Mnakamata na kunyonga tu,” akaeleza, mara hii alioneka kutulia vizuri kitini, “haya niambie biashara hiyo!”

“Nataka almasi,” Kamanda akaanzia hapo.

“Unataka almasi?” yule binti akarudia hiyo sentensi kwa kuuliza.

“Ndiyo, almasi hii imepotea mwaka mmoja na nusu, na mi nimetumwa kuitafuta, nimeambiwa wewe utanisaidia,” wakacheka pamoja na kugongesha mikono yao.

“Eeeh, Lereti, samahani, ninahitaji kujua mambo fulani kutoka kwako kwani nimekuja kikazi zaidi,” akaeleza mara hii kwa utulivu.

Lereti akatega sikio.

“Nahitaji ikiwezekana tuwe wawili tu,” akamwambia. Lereti akakunja uso na kuukunjua.

“Ni ngumu sana, ongea hapa, kama haiwezekani basi haiwezekani kwani ufalagha daima nakuwa nao na mpenzi wangu tu, sina falagha nyingine mimi.”

“Nipe nafasi.”

Baada ya mvutano, Lereti akakubali lakini kwa masharti magumu sana.

“Itabidi uvumilie kwa sababu bado nina machungu na kifo cha baba yangu, naogopa falagha na watu nisiowajua,” akaeleza huku akisimama. Mara vijana wanne wakaingia, wakamkagua Kamanda wakachukua bastola zake mbili na vitu vyote vya hatari, wakaweka pembeni, wakamfunga pingu mikono yake kwa nyuma na miguu pia ili asiweze kufanya lolote la hatari. Akaingizwa katika chumba cha wastani chenye kitanda kimoja kidogo, akaketishwa hapo na wale jamaa wakaondoka, dakika chache akaingia Lereti, na kuketi mbele yake.

“Haya unasemaje? Dakika kumi tafadhali.”

“Lereti, pole sana kwa kifo cha baba yako lakini hongera kwa kuweza kuendeleza biashara na kampuni yake, huu ni urithi tosha kwenu,” Kamanda akazungumza, “hivi gawio lenu la hisa kutoka kwa Robinson Dia-Gold LTD mlichukua?” akauliza.

Lereti alimkazia macho Kamanda, “wewe ni nani mbona unataka kujua mambo ya ndani sana?” akauliza, “hatukuchukua kabisa na wala sitaki kusikia.”

“Ok, je unafikiri kifo cha baba yako kinahusiana na hili?” Kamanda akarusha swali. Lereti akabaki midomo wazi, hakuwahi kufikiri wala kuwaza juu ya mambo hayo mawili kuwa na uhusiano.

“Kiukweli sijui kama vina husiana ijapokuwa ni wiki ileile baba alitakiwa kwenda Canada ila ndo hivyo,” akajibu.

“Mlifanikiwa kumpata au kumgundua muuaji?”

“Hapana, hata polisi na wana usalama wameshindwa kumpata mpaka leo mpaka kesho,” akajibu. Kamanda akatikisa kichwa juu-chini.

“Unataka tuongee nini Mr. Kariuki?”

“Juu ya kifo cha baba yako,” akamjibu kwa mkato. Lereti alishtuka sana.

“We kama nani?” akauliza.

“Mpelelezi pekee duniani aliyepewa kazi ya kuchunguza kifo cha baba yako,” akajibu.

Lereti akajikuta kwenye dimbwi la sintofahamu, amwamini au hasimwamini? Kitendawili.

“Mpelelezi, ina maana wewe ni mwenyeji wa South Africa?” akauliza.

“No, mimi nimetoka Tanzania, kumbuka Tanzania na Afrika Kusini tuna urafiki wa enzi na enzi, sasa serikali ya Tanzania haikuona haja ya kufumbia macho mauaji ya baba yako ambaye ni mfanya biashara maarufu hakuna asiyemjua, nami nimetumwa, usione kimya, tupo kazini na nina saa nne tu nirudi kwetu ili uchunguzi zaidi uendelee, tumkamate muuaji,” Kamanda akaeleza.

Lereti akatabasamu baada ya habari hiyo, akabonya kitufe fulani na wale vijana wakaingia.

“Mfungueni, mpeni vitu vyake,” akawaambia, wakafanya hivyo. Amata akawa huru tena.

“Sasa labda twende polisi wakakueleze kiundani walipofikia au kuishia,” Lereti akamwambia Amata.

“Haina haja, niambie wapi baba yako alipouawa, hapo ndipo ninapopataka hasa,” Kamanda akamwambia, baada ya hapo yakafuatia mazungumzo kidogo na baadae wakatoka wote mpaka nje ya jengo hilo, binti huyu alikuwa akilindwa na watu watatu wenye silaha na walioekana ni wapiganaji haswa.

“Mr. Kariuki, familia yangu ina maadui wengi ndio maana unaona mazingira yako hivi, samahani kwakukuona na kukufanya kama mhalifu,” akamwambia.

“Usijali,” akamtuliza. Wakaingia garini na kuondoka.

 

MONTE BLANC

Ndani ya jengo hilo refu kabisa, Kamanda Amata alisimama mbele ya mwanamke aliyeonekana mjanjamjanja hivi, aliyejipodoa mpaka akapodoka, mmiliki wa saluni kubwa ya urembo na huduma za kukandakanda mwili kwa wateja wake.

“Ndio, Mr. Khumalo alikuwa ni mteja wangu sana na nimemmiss kwelikweli,” yule mwanadada alimweleza Kamanda Amata.

“Nahitaji kujua mazingira aliyokufa na kama kuna yeyote anayejua ilikuwaje labda,” akaomba.

Yule mwanamke akamchukua mpaka kwenye vyumba vya kufanyia Masage, na kumuonesha chumba hicho.

“Humu! Kwa kweli ni jambo la utata sana, mfanya kazi wangu ambaye alikuwa akimfanyia masage kila ajapo hapa na kumliwaza kwa mengine, amefungwa kwa kosa hilo, inasemekana ndiye aliyeua,” yule mwanamke akaeleza.

“Nipe jina lake na ikiwezekana wapi kafungwa nikamuone,” Kamanda akaomba.

Bila shida, akamtajia jina akampa na jina la gereza. Kamanda akaagana naye, akaondoka na kurudi kwenye gari, akamkuta Lereti akimsubiri.

“Vipi?” akauliza kwa shauku.

“Unamjua Mesobhuja Annie?” akauliza Kamanda.

“Ndiyo, amefungwa kuwa yeye ni muuaji,” akajibu.

“Nataka kumuona,”

“Yupo gerezani huwezi kumuona kiurahisi namna hiyo,” Lereti alijibu.

 

GEREZA KUU KWAZULU NATAL

BAADA YA ITIFAKI MBALIMBALI na kujitambulisha kwa uwazi kwa wakuu hao wa gereza, Kamanda Amata alipewa dakika nne tu kumuona mwanamke huyo.

“Nihakikishie nitatoka humu, nimechoka si mimi niliyeua,” akajieleza Mesobhuja.

“Ndiyo, ukinieleza ukweli, utaachiwa na ndiyo maana nipo hapa,” Kamanda akamfariji.

“Alikuwa mwanamke, sijui aliingiaje ndani ya kile chumba cha kutolea huduma, nilikuwa nammasage mteja wangu akiwa kalala kifudifudi, mara ghafla niliondolewa na mwanamke huyo, Mzungu mwenye nywele ndefu, sikumjua, akanipa ishara ya kutulia kimya, nikaogopa sana, alifanya mauaji ya haraka kwa kumvunja uti wa mgongo, yule alikuwa ni muuaji by professional. Kisha aliwaita walinzi kuwa kuna shida. Nao akawaua kwa kuwagonganisha vichwa vyao kwa nguvu, kisha akaondoka. Basi! Nimejitetea sana kuwa si mimi muuaji lakini wapi, nimefungwa hapa kifungo cha maisha, nisaidie jamani, unihurumie dada, sikumuua baba yako.”

Maneno hayo toka kwa Mesobhuja yalimtoa machoa Lereti.

“Niambie, unakumbuka alivaaje mwanamke huyo?” Kamanda Amata akamwuliza.

“Ndiyo, alivaa suruali bluu angavu, brauzi nyeusi, na kikoti chenye rangi kama ya suruali yake, nywele alizifunga nyuma kwa kutumia mpira, alikuwa na miwani nyeusi, na alipovua mara moja kuniangalia, macho yake yanatisha kwa jinsi alivyojiweka make up,” akajibu.

“Unakumbuka muda? Hata kwa kuhisi,”

“Ilikuwa ni kati ya saa tatu narobo asubuhi na saa nne hivi,”

“Ok, asante, usijali tunalifanyia kazi,” Kamanda Amata akamwambia na kisha wakatoka.

Lerethi na Kamanda Amata wakatoka na kuwashukuru viongozi wa gereza hilo, akamwamuru dereva amrudishe katika jengo la Monte Blanc.

“Huko kuna nini?” Lereti aliuliza.

“Naenda kumalizia kazi, kisha naondoka zangu,” akajibu.

Walifika na kuingia tena, kama kawaida watu walikuwa wakimtazama sana mwanadada huyo kwa jinsi alivyo na umbo la kibantu, aliyependeza kwenye suti yake nadhifu kabisa, akizunguka na walinzi huku na huku.

“Mtoto wa Khumalo,” sauti zenye maneno au minong’ono kama hiyo zilisikika kwa waliosimama.

Kamanda Amata kwa utundu wake alifanikiwa kufika katika chumba kinachohifadhi kumbukumbu zote za usalama za jengo hilo, kulikuwa na kijana mmoja anayefanya kazi ndani yake. Alimsikiliza Kamanda Amata shida yake na baada ya kuoneshwa kitambulisho halisi cha Kamanda kinachomueleza kama Mpelelezi namba moja Tanzania na Afrika alikuwa haishi kutetemeka. Akavuta droo na kuchomoa disc moja akakiendea chombo maaluma na kuitumbukiza, kisha akawa anaangalia matukiao ya siku hiyo.

Akarudisha picha zile za CCTV mpaka picha ya mwaka mmoja na nusu uliopita, tarehe ile aliyouawa Khumalo, 16 Julai akairudisha mpaka saa 3:15 asubuhi na kutazma matokeo. Kama alivyotarajia, picha ya saa 3:47 ilimuonesha muuaji wa Khumalo, alivaa vilevile kama alivyoelekezwa na Mesobhuja, akarekodi kipande hicho na kisha kuondoka nacho, akamwachia randi 100 kijana huyo kisha akapotea.

***

Katika Uwanja wa Ndege wa Louis Botha, Kamanda Amata alikuwa akiagana na Lereti Khumalo. Binti huyu alishindwa kujizuia akamkumbatia kijana huyu shababi.

“Asante Kariuki, kwa saa hizi chache nimefurahi kuwa nawe, nakutakia kila lakheri ufanikiwe kumkamata huyo hayawani, na ukifanikiwa nitakupa zaidi nzuri sana ambayo sijawahi mpa yeyote duniani, unijulishe,” akamwambia Amata huku chozi likimtoka, “you are so Intelligency person,” akamalizia.

Lereti hakutaka kumwachia Kamanda, alibaki kumkumbatia huku chozi lake likitua kwenye koti la suti ya kijana huyo.

“Nahitaji kwenda,” akamwambia Lereti huku akiitazama saa yake kutokea mgongoni mwa mwanadada huyo, ilikuwa zimetimia saa tano. Kumbe nimeweza, akawaza. Lereti akamuachia kamanda, “ni muda mfupi lakini nahisi moyo wangu umekuamini sana kwa kila kitu,” Lereti akaeleza ya moyoni.

“Usihofu ni kawaida,” Kamanda akajibu huku akimpa kadi biashara kwa ajili ya mawasiliano, na Lereti akafanya vivyo hivyo.

Daima huwa ni vigumu sana kwa Kamanda Amata au mtu yeyote mwenye kazi kama yake kujitambulisha waziwazi ijapokuwa alichokifanya yeye ni kujitambulisha wazi lakini bado kwa kujificha, alijikuta anaukonga moyo wa mwanadada huyu mrembo mtoto wa Marehemu Gervas Khumalo, binti pekee katika familia lakini aliyeaminiwa sana na wazazi wake kuliko hata kaka zake watatu waliomtangulia. Alikuwa msomi anayejua maswala ya utawala mwenye Shahada ya Uzamivu katika nyanja hiyo, aliogopwa na wasomi kwa kuwa alikuwa ‘ngangari’ katika kutetea hoja au kitu, alikuwa na uwezo mkubwa wa kugeuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo. Wanaume walimdondoshea mate ya tamaa na uchu lakini hawakuwa na nafasi hata chembe ya kusema lolote, waliishia kula kwa macho. Kila mtu, hata walinzi wake walimshangaa pale uwanja wa ndege kumkumbatia mwanaume, tena aliyemuona kwa mara ya kwanza tu, asiyemjua kwa undani, ama kweli ‘Mapenzi yamerogwa’ aliandika mwandishi mmoja mashuhuri nchini Tanzania, Hussein Wamaywa.

 

 

07

IKULU – DAR ES SALAAM

MHESHIMIWA RAIS, HAKUAMINI KILE anachokiona mezani pake. Alikuwa katika ofisi yake ya siri kabisa, Kilimanjaro Square. Ofisi ambayo hata katibu wake hakuwahi kuingia na funguo zake daima alijua yeye anaziweka wapi. Akatikisa kichwa, akauma meno kwa hasira. Kabrasha moja lenye jalada jekundu lilikuwa mkononi mwake likibeba maandishi makubwa ya rangi ya dhahabu ‘The Order Of Being a President’, ndani yake mlikuwa na makubaliano au mkataba kati yake na wale waliokubali kumuweka madarakani kwa makubaliano maalumu. Kwa kuwa alishaambiwa kuwa nusu ya utawala wake akabidhi migodi yote mikubwa kwa maswahiba hao au tuwaite wahisani na wafadhili kwa lugha tuliyoizoea alijikuta hana la kufanya baada ya kugundua kuwa kipindi cha utawala kinamtupa mkono.

Kumbe miaka mitano si mingi, aliwaza huku akikuna kichwa chake ilhali hakikuwa kikiwasha.

Mshtuko mkubwa ulimfika pale alipokutana na sentensi finyu chini ya ukurasa wa mwisho kuwa, hatuwezi kufika kurasa ya mwisho bila kutekeleza kurasa inayoitangulia, moyo ulimpasuka, midomo ikamcheza, akashika pini ya dhahabu na kuifungua kurasa iliyobanwa barabara ambayo hakutakiwa kuifungua kabla. Kurasa yenye pini za dhahabu.

 

Utakuwa umetugeuka kwa kukiuka makubaliano yetu

Tutachukua madini na na mali nyingine kwa nguvu ili kurudisha gharama ulizotuingiza wakati wa kukupeleka Ikulu.

Tutachukua madini kwa jinsi tunayojua sisi, na hata ukijua kuwa ni sisi basi pia ujue kuwa umechelewa, usifanye lolote, bali utulie katika kiti chako, legeza ulinzi ili tufanikishe.

Kumbuka mkataba wetu, faida yetu lazima irudi mara tatu ya pesa tuliyowekeza.

Mwisho wa mkataba wetu ni huu, ukifungua kurasa hizi, ukazikaidi, tunaondoka na Roho yako

Kumbuka tupo kila mahali, mpaka kwenye kiti ulichokalia

Marafiki zako tunaokupenda sana.

 

Akashusha pumzi ndefu, mikono ilikuwa ikimtetemeka.

Nimekwisha, kwa nini nilijiingiza huku? Akawaza na kuwazua, hakuna jibu.

Tama mbaya, tena mbaya sana, Mh. Rais alijikuta katika hali ngumu, mwili ulilowa jasho wakati ofisi hiyo ilijazwa kwa baridi la mashine ya kupoza hewa.

Akajiuliza mengi, akagundua migogoro mingi na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi mbalimbali hasa nchi za dunia ya tatu ni inaweza kuwa ni ‘matekelezo ya mikataba’. Akaikumbuka Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mali, Afrika ya Kati, Somalia na nchi mbalimbali za Kiafrika zilizoingia kwenye migogoro mizito, akakumbuka marais waliouawa wakiwa nyadhifani, wakiwa bado wanakula maisha ya ufalme wao. Akajikuta akili yake ikitengana na ubongo.

Migogoro mingi katikla nchi zinazoendelea inasababishwa na mabwanyenye kutoka mataifa beberu ya nchi za dunia ya kwanza, ambazo zinapanga nani atatawala pale na nani kule ili wao wapenyeze fikra na tawala zao dhalimu. Bara la Afrika ni bara lililoathirika sana na Siasa za mtindo huu. Vita vilitawala kila kona, hakuna aliyejua amani, kila mtu alijijengea mazingira ya kujilinda yeye na familia yake, vikundi vya kigaidi viliiibuka kila wakati na kila mahali, jiuliuze vinapigania nini kwa maslahi ya nani, hata wapiganaji wenyewe hawajui na hawana jibu.

Kila kukicha, kule kumelipuliwa, 500 wametekwa, 200 wameuawa. Vyombo vya habari vya mataifa makubwa vinawekeza katika nchi masikini kutengeneza habari mbaya za Afrika, wanazisababisha wao na wanazitengeneza wao, wanaieleza historia mbaya ya bara letu. Sisi wenye bara letu hatukumbuki hata kutangaza historia nzuri na ya kupendeza ya Afrika na kubadili fikra za ulimwengu huu, kwa kuwa tunafanya kila kitu chini yao, basi hata habari za Afrika tunanakili kutoka katika vyombo vyao wenyewe. Hao ndio ‘King Makers’, nipe madini nikupe Bunduki, Jiue mwenyewe.

“No! Nooooooooooo!!!!” alipiga kelele bila kujijua akiwa katika ofisi ile, na hakuna aliyesikia kutoka nje, akaanza kuhema kwa nguvu, ofisi ile aliiona ndogo kama kiberiti, alihisi hatoshi.

Wataniua, akawaza.  Aibu, akajijibu.

Haiwezekani, nina Askari Polisi watalinda migodi, nina Jeshi la Wananchi watapambana na udhalimu wowote dhidi ya nchi yangu, nina Askari Magereza watawafunga wote watakaoleta shida dhidi ya utawala wangu awe mweusi au mweupe, nina watu wakakamavu wa Usalama wa Taifa watanilinda kila ninakokwenda hakuna risasi itakayokifikia kichwa change. Hawaniwezi, hawaniwezi kabisa. hapa nitamuweka yule, mgongoni kwangu atakaa yule kule, nitaongeza body guards kutoka wanne wa sasa watakuwa nane wa karibu, na kumi na sita watakaotawanyika, nitabadilisha gari la kutembelea, nitaagiza jipya, la kisasa lisilopenya risasi wala kulipuka kwa moto. Ah! Lakini wanaotengeneza gari si ni wao wenyewe, sasa nifanyeje, simwamini mtu, kama waziri katumiwa kuonekana kaiba almasi kumbe ni wao wenyewe waliojigeuza katika maumbo na sura, hawa ni hatari, nifanyeje, nisitoke ndani. Sasa nikialikwa kwenye shughuli za hadhara, itakuwaje, watanidungua.

Aaaaaa, ok sasa nakumbuka, walinidungua pale Bunju, lo! Hawakuniua, hawakushindwa kufanya hivyo, kwa nini nimechelewa kujua hili? Nani alitekeleza anayeweza kuupenya usalama wa nchi yangu uliotukuka ndani na nje, atakuwa mtaalam sana huyo, dereva wangu naye ni mwanajeshi, mpiganaji anayejuwa kuendesha gari katika ‘Defensive Driving’, ilikuwaje hakuona kama tunadunguliwa?

            Yote yalikuwa ni mawazo, akiwa anatazama saa aliyokuwa akiiona mishale yake ikikimbia kuliko kawaida, akiwa amelowa jasho kuliko, Mheshimiwa Rais alichanganyikiwa, yote yalikuja kwa mara moja. Aliona saa 24 za siku hazotoshi labda mchana uwe na saa 72, miezi kumi na mbili ya mwaka michache sana, labda ingekuwa ishirini hivi. Akajiegemeza kitini, akashusha pumzi, mwanga wa taa ulimpiga machoni, akayafinya.

Alihisi kuetetemeka mwili mzima, akafungua tai na kuitupa huko, akalegeza vifungo vya koti na shati lake apate hewa ingawaje mashine ya kupoza hewa ilikuwa ikiunguruma kwa nguvu zote.

Akafunga lile kabrasha, akalitia kwenye droo, akafunga kwa namba anazojua yeye.

***

Katika ofisi za wanausalama ndani ya jengo la Ikulu, mlio wa hatari ulisikika, Johnson Cheka, mwanausalama mwenye amri ya mwisho ya kusema Rais afanye hivi au asifanye alikuwa wa kwanza kutoka na kupiga hatua kumi na tano kufika pale kwenye mlango wa kuingia katika makazi ya Rais ambayo yapo ndani ya Ikulu, akafungua mlango na kuingia haraka, akaufikia mlango wa ofisi hiyo ndogo, akautikisa, umefungwa, akajaribu kuufungua umefungwa, akachomoa funguo zake za ajabu na kufanikiwa kuufungua, akamkuta rais amejilaza mezani akivujwa jasho jingi. Mara moja akamsogelea na kumwinua, kwa taabu kidogo akamfikisha kwenye kochi kubwa sebuleni, akainua redio yake na kumwita daktari huku yeye akiifuna afisi ile. Dakika moja tu daktari akafika, mara moja na kumchukua mpaka ghorofa ya chini ambako kuna hospitali ndogo yenye kila kitu iliyojengwa maalumu kwa familia ya Rais.

Johnson Cheka alisimama pembeni mwa kitanda akitazama pilikapilika za daktari na muuguzi wake. Dakika tano baade hali ikatulia. Cheka akamwita Mkuu wa itifaki akamweleza kubadili ratiba zote za Rais kwa siku tatu, hakutakiwa kuonana na mtu yeyote, alitakiwa kupumzika. Ilileta mshtuko kwa kila aliyejua, lakini bado ilikuwa ni siri kubwa sana.

Madam S alipata taarifa ya hali ya Rais, hakuweza kuchelewa, siku hiyohiyo alifika Ikulu kumjulia hali Mkuu wa Nchi kwa namna moja, bosi wake. Yeye haina tabu kufika anapotaka, alikaribishwa na kuongozwa mpaka aliko mkuu huyo. Mara baada ya kuwasili, Rais akatabasamu kumwona, akawataka wengine kutoka nje ili abaki kwa muda na mwanamama huyo.

“Nahitaji kufuma upya kikosi cha ulinzi,” ilikuwa ni kauli ambayo ilipenya masikioni mwa Madam S.

“Kwa nini,” Madam akauliza.

“Hali ya kiusalama ni mbaya, kwangu na kwa nchi,” akamweleza.

“Najua, sasa wataka kufanya nini?” Madam akauliza kwa kuwa alijua wazi kuwa kubadilisha au kuimarisha kikosi cha ulinzi cha Rais au kuwa na wasiwasi na walinzi wake tayari kuna jambo na jambo lenyewe kubwa si dogo.

“Nitakwambia, maana nikishaweka mambo sawa, wewe utahusika kujua,” akamwambia Madam S.

 

***

Kamanda amata aliwasilisha ripoti yake kwa Madam S na jopo zima la TSA juu ya mauaji na muuaji wa Mr. Gervas Khumalo.

“Sasa tuna nini lingine la kutafuta?,” Madam aliuliza, kisha akaongeza, “ huyu mwanamke, ndiye huyu tuliletewa picha kutoka Ufaransa, ndiye huyu tulicholewa picha na mchoraji wetu baada ya sakata la msafara wa rais, hizi hapa zinafanana kabisa, ni nani mwanamke huyu? Yuko wapi na anataka nini? Hilo ndilo la msingi sasa kuona, siwezi kusema akamatwe au aachwe, kwanza huyu ni nani?” Madam S akang’aka, alionekana wazi kuwa na hasira siku hiyo. Ukimya ukachukua nafasi yake, hakuna hata aliyekohoa. Kisha akaendelea kuleta utata mwingine.

“Sikilizeni, tena sikilieni kwa makini sana, rais anataka kufumua kikosi cha usalama na kukipanga upya, mimi nimemhoji sana kwa nini akanipa siri ifuatayo, siku msafara wake ulipodunguliwa, amegundua uzembe wa hali ya juu sana kiasi kwamba sasa anataka hata dereva wake achunguzwe…”

Kamanda akamkatisha, “sasa atafumua wapi ataacha wapi…?”

“Mi sijui, lakini yeye atakapokutana na mkurugenzi wa Usalama wa Taifa watajua,” akajibu.

“Inabidi kweli dereva achunguzwe, vipi kama hakuwa dereva tunayemjua? Chiba akauliza.

“Ndiyo utata, maana waziri walimtengeneza watashindwaje dereva, hakuna haja ya kupoteza muda, dereva inabidi afanyiwe uchunguzi haraka,” Madam akaongeza na kumpa kazi hiyo Scoba aitekeleze haraka iwezekanavyo.

 

ONTARIO CANADA

ROBINSON QUEBEC alikuwa kimya katika bustani yake kubwa iliyoizunguka nyumba yake kati jiji la Ontario nchini Canada, sura yake ilikuwa imekunjana kwa hasira. Akashusha sigara yake anayovuta na kukung’uta jivu lake katika kibweta kilichoandaliwa kwa kazi hiyo, kisha akamtazama aliyekuwa mbele yake.

“Tracy!” akaita.

“Yes, Boss!”

“Nilikuwa nikikuandaa kwa miaka yote kwa kazi ngumu na za hatari kama hizi, na zote umenifanyia vizuri kabisa zikapelekea hata ukapata kazi na mashirika makubwa kama KGB na wengine, sasa nataka nikupe kazi moja, hii naweza kuiita ngumu lakini wewe utaipima,” Robinson alimwambia Tracy Tasha aliyekuwa ameketi pembeni yake akisikiliza kwa utulivu sana kila kitu.

“Nakusikiliza,” alisema.

“Nakutuma tena Afrika Mashariki,” Bwana Robinson akatulia akimwangalia Tracy usoni.

“Kazi ileile au?” Tracy akauliza.

“Ndiyo, sasa ukaimalizie,” akavuta tena pafu moja, “mara hii nataka ukaondoe Roho ya rais wa Tanzania, kwani amekiuka makubalino yetu, nasi hatuna budi kutekeleza mkataba wetu,” akarudisha sigara kinywani, “sikia, iwe kwa sumu, kwa ajali au njia yoyote ile wewe ndiye ujuaye la kufanya, hakikisha ndani ya siku chache tu uwe umemaliza kazi na hapo watakaposhtuka juu ya kifo hicho ndipo tutapita nyuma kukusanya tunachotaka,” akamaliza.

“Ok, na vipi juu ya usalama wake? Yaani vikwazo vya kiusalama,” Tracy akauliza.

“Hivi kuna nchi ya Kiafrika ambayo ina usalama wa kukushinda wewe? Tanzania! Ah wapi, wala usiogope, hawana lolote ni kelele za ubahatishaji tu mbona mpaka leo hawajagundua kuwa dereva aliyemwendesha Rais siku ya tukio lililopita alikuwa Breyman?” Robinson akamwuliza Tracy.

“Ok, kesho nitaondoka,” akajibu.

“Sawa, uwende Kesho na ukafanye kazi kikamilifu, George Mc Field yuko pale kukusaidia kwa lolote, usihofu tumejipanga,” Robinson akamweleza.

“Sawa, hilo limepita,” Tarcy akanyanyuka na kubaki wima. Ni mwanamke mzuri kuwa mpenzi au mke wa mtu lakini dunia imembadili kimaisha amekuwa mnyama mbaya kuliko mnyama mwenyewe.

“Sikia Tracy, ulinzi wa Rais umebadilishwa saa chache zilizopita, nimepata hiyo taarifa kutoka vyanzo vyangu. Ameongeza watu wanaomzunguka na kuimarisha maeneo nyeti, hivyo nahitaji utumie weledi wako wa juu kabisa kuifanya kazi hiyo. Ukikamilisha, utajiri wako utaongezeka mara nne,” Robinson akamaliza huku akimshika makalio mwanadada huyo katili, alisahau kabisa kama anaweza kumgeuka na kumtoa roho.

 

 

UWANJA WA NDEGE WA

J.K NYERERE-DAR ES SALAAM

NDEGE KUBWA YA LUFTHANSA ilitua katika ardhi ya Dar es salaam, Rubani wa ndege hiyo na wasaidizi wake hawakujua kabisa kuwa wameiletea Tanzania maafa, maafa makubwa.

Tracy Tasha alikuwa wa mwisho kushuka katika ndege hiyo kubwa ya kisasa, hakuwa mgeni na nchi hii, kwa kuwa alishafika mara moja na hii ilikuwa ni mara ya pili. Alikuwa na kijibegi kidogo na mkoba mkononi mwake, akapita eneo la ukaguzi wa hati za usafiri bila tabu akitambulika kwa jina la Naomi Schubety, raia wa Venezuela, mwanafunzi wa chuo kimoja cha afya huko Marekani, John Hopkins.

“Karibu sana!” George Mc Field alimlaki mwanamke huyu, hawakuwahi kukutana, ilikuwa ni mara ya kwanza, Tracy akabaki kimya akimwangalia mtu huyu ambaye sasa alionekana katika mavazi  nadhifu, mwenye mwenye ndevu nyingi.

Tracy akatoa noti ya Paundi 100 akamwonesha, na Mc Field akatoa noti ya Shilingi 10000 akamwonesha, hiyo ilikuwa ni ishara ya utambulisho wao ambayo kila mmoja aliambiwa kwa wakati wake. Wakaingia garini na kuondoka kuelekea mjini.

“Umekuja kufanya kazi, siyo?” Mc Field akamwuliza Tracy.

“Ndiyo, ni hilo tu,” akajibu.

“Unapenda kufikia hoteli gani?”

“Aaa yoyote lakini nafikiri ya hali ya kati ingenifaa zaidi,” Tracy akaeleza.

“Ok,” Mc Field akaiacha barabara ya Nyerere na kuichukua ile ya Mandela kuelekea Ubungo.

“Land Mark Hotel, hapa patakufaa siyo?” akamwuliza.

“Yap, pako poa,” akajibu hukua akishuka katika gari. Akaagana na Mc Field kwa miadi ya kuonana usiku wa siku hiyo kwa mipango ya mwisho.

 

 

 

 

 

08

CANADA

          ROBINSON QUEBEC alikutana na washirika wake kama kawaida, hii ilikuwa mara tu baada ya kuondoka Tracy kuelekea Tanzania.

“Tumemaliza kazi! Tusubiri matokeo,” Robinson akawaeleza swahiba zake wawili.

“Safi sana, kama Tracy amekwenda, hilo ni amuzi sahihi, mwanamke yule huwa hashindiwi, na wala haogopi kitu, kuua ni starehe yake,” akajibu yule mjumbe mweusi.

“Ndiyo, na wameshakutana na Mc Field, kila kitu kiko sawa, tusihesabu hasara basi tuhesabu faida katika hili,” Robinson akaeleza.

“Sir. Robinson Quebec, uishi milele!” wakamtukuza. Baada ya hapo wakatawanyika wakisubiri kazi ya Tracy ikamilike ili nao wasonge mbele.

***

REJEA – SHAMBA

“Sasa ipo hivi, almasi za Mwadui hazikuibwa na waziri kama ilivyojulikana mwanzo,” Madam S alikuwa akifanya hitimisho la uchunguzi wa taasisi hiyo, akaendelea “sasa ni nani aliyeiba almasi hizo? Mpaka sasa tuna mtu huyu George Mc Field na nina uhakika hajaondoka nchini, na yeye atakuwa ndiye aliyejigeuza kuwa kama waziri, Amata anamjua huyu jamaa, huyu ni Jasusi mwenye uwezo wa kujigeuza hata akawa mjusi,” akatulia na kuwatazama vijana wake, “sasa tunaingia kazini, asakwe George Mc Field apatikane akiwa anapumua au hapumui, na swahiba zake, wakati huo ufanyike uchunguzi juu ya chanzo cha wizi wa almasi hizi, sote tunaingia kazini, na tutajipanga kama ifuatavyo…”

Kila mtu alibaki kimya, kila mmoja moyoni mwake aliona wazi kuwa haya ni maji mazito mpaka Madam S anahusisha watu wake wote kikazi kwa wakati mmoja, haikuwa kawaida kwa mwanamama huyo, yeye daima alimpa mtu mmoja kazi moja labda itokee inahitaji msaada wa karibu ndipo mngekuwa wawili, hata hivyo bado aligawa kazi pasi na wao kujua kama nani ana kazi ipi. Lakini  mara hii wote watano na yeye mwenyewe wa sita, kila mmoja aliona kazi ni kubwa na nzito. Baada ya kushusha bilauri yake iliyojaa sharubati ya embe akafungua kabrasha lake na kuliacha wazi mezani.

“Hali ya Mheshimiwa Rais ni mbaya, amepatwa na presha ya kushuka, sasa dawa yake tunayo sisi kuhakikisha utatuzi wa hili umepatikana, nimeongea naye kasema mabadiliko aliyoyazungumza kayakamilisha katika sekta ya ulinzi wa nchi hivyo msishangae. Sasa nataka tufanye kazi hii kwa kasi ya ajabu kidogo. Kamanda Amata utakuwa mstari wa mbele kabisa ukisaidiwa karibu na Gina katika mapambano, kila anayenukia harufu ya almasi za wizi, awe mkubwa awe mdogo, toa taarifa tumkamate mara moja, na atakayekataa kutii sheria bila shuruti basi we unajua jinsi ya kumtuliza. Scoba kama kawaida, utakuwa makini katika kuokoa na kukamata anayetakiwa kufanyiwa hivyo. Chiba utahakikisha unawaunganisha wote bila kuwapoteza katika mtandao, kunasa mawasiliano ya kila unayemhisi na kuto mwongozo kwao, nikiwa na maana kuwa ofisi yako sasa itaamia hapa au ndani ya gari yako maalumu kwa kazi hiyo wakati mimi na Jasmine tutakuwa hapa kwa msaada wa haraka…” akiwa hajammializa kusema hayo, mara sauti ya simu ya Chiba ikawashtua, akaitoa mfukoni na kuitazama, akawapa ishara ya kutulia.

“Terminal Two,” akawaambia na wote wakatega sikio kwa kuwa aliweka sauti kubwa.

“…Hello…” akaita

“Hello, Terminal Two hapa…”

“Nakusoma, endelea,”

“Kuna mzigo hapa umeingia, nina wasiwasi nao kwa picha ulizonipatia…”

“Ok tuma taarifa zote hapa haraka…” akamwamuru mtu huyo ambaye daima humtumia kunasa watu anaowahitaji. Mtu huyu ana kifuniko ‘undercover’ cha Idara ya Uhamiaji lakini kitengo cha usalama wa Taifa kinachofanya maswala ya utambuzi.

“Copy!”

Chiba akakata simu na kutulia.

“Kumekucha…. Kwa umakini wa huyu kijana lazima aliyeingia ana jambo,” Chiba akasema.

Wakati wakiendelea na mzungumzo, kompyuta ya Chiba ilikuwa imekwishapokea taarifa kutoka uwanja wa ndege, akazifungua na kuprint nakala kadhaa na picha zilizotumwa pamoja nazo.

Picha kumi na mbili za mnato zilizomuonesha mwanamke katika ‘engo’ mbalimbali, mbele nyuma, kutoka juu, usoni kwa karibu kifuani, mgongoni na mazingira mengine, kisha kulikuwa na picha ya mjongeo ambayo Chiba aliicheza kwenye kompyuta kubwa ya ofisini kwa Madam S na wote wakaishuhudia. Mwanamke huyo akipita katika ukaguzi, akitoka mlango wa ‘wanaowasili’ akisalimiana na mwenyeji wake, kisha wakiondoka lakini picha hiyo haikuweza kuonesha mtu huyo kaondoka na gari gani.

Kamanda Amata akazitazama zile picha kisha akampatia Chiba. Chiba akaziweka kwenye kifaa chake. Pamoja na zile ambazo Kamanda alizileta kutoka Afrika Kusini, na zile zilizotoka Ufaransa na zilizochorwa katika tukio la Bunju, kisha kwa kutumia kompyuta, softiwea maalumu akazioanisha ‘crossmatching’ kama ni mtu mmoja au ni watu tofauti. Ndani ya dakika kumi walipata jibu alikuwa ni mtu mmoja hata kama alijibadili namna gani. Softiwea hii iliyotengenezwa na Chiba akishirikiana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam ilikuwa ikifanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu sana, ikikufananisha pua, macho au maziwa kama we ni mwanamke au ndevu kama we ni mwanaume kwa kuwa waliiaminisha kuwa hata mtu ajibadili vipi kuna sehemu hatoweza kujibadili, hivyo ilitafuta sehemu ambayo ilikuwa na unasaba kisha ikaoanisha kutoka hapo.

Baada ya kupata picha kamili ya mwanmke huyo, akaiingiza katika mtandao wa usalama unaowatambua watu hatari duniani, kwanza alianza na ule wa CIA ambao ulimpa jibu lenye utata, akaingiza kwenye mtandao wa MOSSAD kama unamtambua mtu huyo nao ukaleta majibu kama yale yale baada ya kupitisha kwenye kioo picha zaidi ya 250.

“Shiit!” Kamanda Akang’aka.

Mtandao mwingine wa kijasusi wa KGB nao ukaleta majibu yanayofanana.

Tracy Tasha, raia wa Marekani, mzaliwa wa Jimbo la Arizona, mwenye miaka thelathini na moja, maelezo yaliendelea kumweleza kama muuaji hatari asiyekamatika, anayetafutwa kila kona ya dunia na kila kitengo kiwe cha kipolisi, kijasusi au mashirika binafsi. Ulimweleza kuwa hakamatiki, mitandao mingine ikampa jina la The Devil, wengi walieleza wazi kuwa wamekamata nyayo zake tu lakini mwenyewe hawakumkamata. Mtandao mwingine uliwafanya Madam S na jopo lake kucheka maana ulijitamba kuwa kamera zake za CCTV ndizo zenye uwezo wa kumkamata kila apitapo eneo fulani.

Taarifa zile zilimfanya Madam kushusha pumzi ndefu, akavua miwani yake na kujifikicha jicho la kushoto.

“Tutoe taarifa kwa wadau wanaomtafuta? Maana sisi huyu sio wa kwetu,” Madam S akauliza.

“Hapana, usitoe taarifa kabisa, kwani itakuwa vurugu kubwa hapa, na sisi lazima tumchunguze kwanza kaja kufanya nini, kisha tumuoneshe kuwa sasa kafika mwisho wa maisha yake…” kabla Kamanda hajamaliza kusema hayo Gina akadakia.

“Ningemshauri aandike urithi kama ana watoto,” wote wakacheka.

***

“Tumepata shida kidogo, windo letu halijaonekana nje sasa ni siku ya tatu, uchunguzi wetu wa mwisho ulimuonesha akiwa kwenye kasri lake lakini hajaonekana kutoka tena,” Mc Field alimweleza Tracy wakiwa wameketi katika moja ya viti vya sebule kubwa na pana katika hoteli ya Land Mark pale River Side Ubungo.

“Kama alitoka usiku je?” Tracy akauliza.

“Hapana watu wetu wako makini sana kumwangalia, kwa sababu unatakiwa umwangamize akiwa anatoka kwenye geti la Ikulu na si pengine popote,” Mc Field alizidi kueleza.

“No! Hiyo point mbaya sana Comrade! Kwenye lango ni pabaya kwa kuwa pana macho mengi,” Tracy akaonesha mashaka, “no! Siafiki kufanya kazi katika eneo hilo maana kwa vyovyote mtakuwa mmeniweka kwenye domo la mamba au we unaonaje?”

“Mitazamo ni tofauti, mi naona penye macho mengi ndipo penye uzembe wa kuangalia kwani macho hayo hutegeana,” Mc Field akamweleza.

“Ok, lakini mimi kama mimi ningependelea eneo lingine, ambalo siwezi kufanya makosa kudungua kwani nina shabaha ya ajabu haijawahi kushuhudiwa duniani, hujawahi kusikia kifo cha yule muuza dawa za kulevya kule Venezuela, Benitez Segudo, jinsi nilivyopenyeza risasi wakati mlango wa ndege ukifungwa na kumpata barabara, mlango unafunga na yeye huko ndani anakata roho,” akameza mate, “sasa hapa sio pa kuumiza kichwa kumpata mtu huyo, kwanza nipe muonekano wa eneo lenyewe.”

“Aisee ni wewe ulimdungua Benitez! Saluti kwako mwanamke. Ok, mwanamke unajiamini sana, lakini ingekuwa mimi ningepatumia hapo, katika geti kuu la kasri hilo la Mheshimiwa kuna barabara inayoteremka, kuelekea baharini kukutana na ile ya Ocean, pembeni au mkabala mwa lango hilo ukivuka barabara kuna jengo la wizara kisha chini yake kuna chuo, lakini hilo si eneo salama kwani linaangaliwa kwa kila njia iwe macho mabichi au macho magumu yote yako hapo, sasa nyuma ya chuo huku kuna jengo moja refu sana ambalo nilipanda mpaka juu, ni eneo zuri kutekeleza kazi hiyo, kwani ukitumia bunduki kubwa ya kisasa ni sekunde moja tu,” Mc Field alimweleza.

“Kutoka huko ghorofani mpaka kufika chini nitaondokaje? Wakizingira chini si nimekwisha,” Tracy aliwasiwasika sana kwa hilo.

“Yaani we bado kinda sana tofauti na sifa zako! Kwani umesahau Yesu aliwatokaje wale jamaa waliotaka kumtupa shimoni kule Nazareti? Alipita katikati yao na wasimwone kisha akaenda zake, na wewe utapita hapohapo wanapilizingira hilo jengo na hawatakuona.” Mc Field alieleza kwa uhakika zaidi.

“Ok, kwa kuwa kazi yako ni kuniokoa naamini litawezekana,” Tracy akajibu.

“Sasa sikiliza, kuna jambo moja nataka nikutahadharishe, mimi nilishakuja hapa miaka kumi ilopita kufanya kazi nyingine, nilipata wakati mgumu sana na ile kazi ilishindikana ijapokuwa mimi nilitoroka,” akaanza kueleza.

Tracy akajiweka sawa kitini akizitupia nywele zake ndefu mgongoni, akasikiliza kwa makini. Mc Field akatoa picha moja na kumtupia Tracy, akaidaka kwa ustadi na kuitazama, kijana mmoja nadhifu katika suti safi nyeusi iliyotanguliwa na shati la buluu, tai safi iliyomkaa vyema shingoni mwake akiwa ameketi kwenye meza moja na kinywaji kikiwa mbele yake.

“Sijajua kama yuko hai au amekufa maana sijaona makeke yake katika hili ila najua kuwa alisimamishwa kazi kipindi fulani,” Mac Field alieleza.

“Ni nani huyu?” Tracy akarusha swali. Mc Field akatulia kidogo kasha akasema.

“Bora ukutane na Israel mtoa roho, huyo mtu ni hatari sana, ni agent katika idara ya kijasusi ya hapa Tanzania, hawezekaniki, ni mkorofi, mpiganaji mwenye weledi uliopita maelezo, mjanja wa maneno na macho ana IQ kubwa ya kucheza na akili yako kisha ni muuaji asiye na huruma anaweza akitoa roho yako na kuifungia kwenye chupa, anaitwa Amata, Kamanda Amata,” akamaliza na kunyanyua kinywaji chake.

Tracy akashusha pumzi ndefu akiigeuza geuza ile picha, “siwezi kumwogopa huyu! Nikimuona nitapambana naye kwa mikono…”

“Usijaribu ujinga huo!” Mc Field alionya, “huyo sio binadamu wa kawaida, nahisi ni chuma kilichovalishwa ngozi ya mtu,” kisha wote wakacheka sana.

***

Katika kikao cha dharula cha ndani cha idara ya usalama wa taifa, kiliwakutanisha watu wa wakuu wa idara husika pamoja na rais. Lengo kubwa ilikuwa ni kujadili juu ya kuimarisha ulinzi Rais baada ya mabadiliko yalyofanyika.

“Nahitaji walinzi kumi na sita, wanne wawe mbele kabisa, wawili katikati na wane wengine wawe jirani nami kama kawaida kisha wanaobaki wawe nyuma, na hao wote wawe full na wawe wapiganaji hodari, ninyi wenyewe mnajua. Hali ya usalama wa Taifa na mimi mwenyewe ni mbaya sana, nataka mhakikishe kila kwenye mgodi mmeweka askari kanzu wane ili kupeleleza nini kinaendelea maana nahisi wizi huu unaweza ukatokea tena muda wowote. Wale tuliyowaondoa hawakuwa makini sasa najua hawa wapya watakua makini zaidi,” akawaambia.

Watu wakajiuliza mioyoni juu ya kauli hii aliyoitoa sasa, “Msishangae, siko tayari kuona almasi, dhahabu au Tanzanite inaondoka katika njia rahisi kama hii wakati vikosi vya ulinzi na usalama vipo, ni aibu, mnakumbuka tukio la Bunju?” wakajibu kwa kutikisa kichwa, “sasa kila dereva au anayekaa karibu nami mumchunguze kama ni yeye au sanamu, leo nitawaeleza kuwa aliyekuwa ananiendesha siku ile hakuwa dereva wangu, aliyeiba almasi mwadui hakuwa waziri, polisi aliyofuatana nao hawakuwa polisi wetu lakini sura, lugha, muonekano wao ulikuwa ni uleule, sasa mnaweza mkaamka kesho na rais mwingine hapa, sasa tusiaminine tena,” Rais alieleza kwa undani kila kitu kadiri alivyopewa taarifa kutoka TSA na onyo la mwisho juu ya mwanamke huyo hatari aliyeingia nchini. Waliona baadae kuwa Mwanamke huyo na kama kuna wengine wasakwe kimyakimya bila kelele ili kutowagutusha, hali ya tahadhari ikatolewa kwa watu wa idara ya Usalama wa Taifa kuwa makini na kila wanayekuwa na wasiwasi naye, ulinzi mpya ukaanza kazi mara moja, safu zikapangwa upya, mkuu wa kitengo kile akaondolewa akawekwa mwingine, akatolewa huyu kule akapelekwa kule, huyu na yule wakapelekwa mikoani, yule wa mkoa ule akaletwa huku ilimradi tu kuiweka safu mpya.

***

Kamanda Amata alikuwa na Chiba wakijadili hili na lile, “enhe nambie Jenny anasemaje?” akauliza.

“Oh, nilisahau, alileta kitu muhimu sana, alileta kadi inayotumiwa kubadili sauti ya mtu, na tumeichunguza ndipo tukapitisha moja kwa moja kwamba waziri hakuusika na ule wizi kwani alibanwa akalazimisha kusema maneno fulani wakati ile kadi ikirekodi na kisha aliyejifanya waziri ndiye akaitumia sauti hiyo,” Chiba akaeleza.

“Lazima tujivunie kuwa na wewe Chiba, ni mtu wa juu sana kwenye hii midude unajua wewe ndiyo huwa unanifanyia mi mambo kuwa mepesi,” wakacheka pamoja.

“Acha Bwana, sasa unataka kumwona Jenny?” Chiba akaanza.

“Mmmm hajaondoka?”

“Hapana, nilimwambia asiondoke mpaka utakaporudi, nimempangia chumba pale Rombo Green View, Sinza, naye amefurahi sana kusikia aonane nawe,” Chiba akaeleza.

“Aaa, wakati mbaya sana huu, unaweza kuwa kitandani na wenzako wanaiangamiza nchi,” Kamnda akajibu.

“Aaaa kaka! Kamanda leo wa kusema hivi! Hivi hivi! Siamini itakuwa umeokoka labda,” Chiba akatania.

JINIA – saa 3:25 asubuhi.

KAMANDA Amata alikuwa katika ofisi ya uhamiaji ndani ya Uwanja wa Ndege wa Dar es salaam sambasamba na Gina.

“Unasema ulimwona,” akauliza.

“Ndiyo nilimwona, akapokelewa na kasisi wa kanisa,” akajibu kijana wa uhamiaji aliyetuma taarifa za Tracy kwa Chiba.

Kasisi wa kanisa, akawaza Kamanda, “haya makanisa nayo yana mambo! Utakuta wanahifadhi majasusi humu humu si’ tumekaa tu,” akaeleza Kamanda, “hukuwaona hata wamepanda taksi gani au gari gani?” akauliza.

“Waliondoka na gari binafsi, Peugeot 404, TX 768 M,” akajibu yule kijana.

“Ok. Asante sana, nitafanyia kazi, tujue kaja hapa kwa nini,”

Kamanda na Gina walitoka eneo la Uwanja wa Ndege na kuliendea gari lao, wakaingia na kuketi, nyuma ya usukani alikuwa Gina. Kamanda akawasha simu na kupiga mamlaka ya mapato Tanzania na kuuliza namba za gari hilo TX 768 M ni mali ya nani. Baada ya dakika kumi hivi akapewa jibu kuwa ni mali ya kampuni moja ya kijerumani inayofanya kazi za kijamii huko vijijini, lakini ofisi yao ipo Dar es salaam, wakatajiwa anwani na mahali ilipo.

“Gina, twende Mtaa wa Mkwepu, plot namba 45C, “ Kamanda akamwamuru na Gina akaondoa gari kama alivyoelekezwa.

Walipofika walipandisha ngazi moja kwa moja mpaka ghorofa ya tatu ya jengo hilo, wakakuta kuna duka kubwa la kuuza vifaa vya maofisini, walipouliza wakaambiwa hao Wajerumani waliamisha ofisi kuelekea mtaa wa Ali Khan Upanga. Bila kusita Gina na Kamanda wakaongoza njia kuelekea huko, haikuwa tabu kuipata ofisi hiyo kwani walipopita tu shule ya Zanaki wakaiona kwa mbele wakaegesha gari, wakateremka kuingia katika nyumba hiyo yenye uzio mkubwa wa miba. Mlangoni palikuwa na mlinzi wa kampuni binafsi.

“Hawa jamaa waliondoka kwa likizo, ila watarudi, kwa sasa hawapo,” alieleza yule mlinzi.

“Ok, ni muda gani ambao hawapo hapa,” akauliza Gina.

“Ni kama wiki moja sasa,” akajibiwa.

“Sawa asante basi tutakuja wakati mwingine,” Gina akashukuru, wakaondoka na Amata kurudi garini.

Kamanda Amata alipoketi tena na Gina garini, akamtazama mwanadada huyo mrembo wa sura na ngozi nyeusi inayong’azwa kwa lishe bora na virutubisho makini, “sasa naongea na wewe kama mshirika wa kiofisi na sio wa kikazi, unafikiri kwa nini hawa watu wameenda likizo ndani ya wiki moja ambayo hiyo hiyo imetukia tukio hili?” akamwuliza.

“Hata mimi hapo moyo wangu unapiga chogo chemba, nashindwa kupata jibu, nahisi kuna jambo kati yake, any way, tunafanya nini sasa?” Gina akajibu na kuuliza.

“Hapa hatuna budi kulisaka gari lenye namba hizo, kwa kuwa mpaka sasa ni ufunguo pekee wa kazi yetu, hebu twende leo tukamtembelee rafiki yetu wa muda mrefu, nafikiri huyu anaweza kutusaidia kwa namna moja au nyingine,” Kamanda akamwambia Gina.

“Nani huyo?”

“We endesha gari mpaka kituo cha polisi kati,” Kamanda akaamuru.

“Aaaaa ok, nimeshamjua, na kweli ni wa siku nyingi sana,” Gina akaitikia.

Dakika nyingine ishirini na tano ziliwafikisha katika kituo cha polisi kati, walipoegesha gari wakashuka moja kwa moja na kuifuata kaunta kabla hawajapandisha ngazi ghorofa ya kwanza ambako walimkuta yule wanayemhitaji, Inspekta Simbeye.

“Karibu kijana, naona leo umefuatana na mrembo wako!” akakebehi.

“Ee Bwana si unajua tena lazima alinde,”

“Kabisa; hongera bibiye nasikia umeteuliwa katika idara nyeti ambayo wenzako wanaililikutwa kucha hadi wanagongana kwa waganga, lakini wewe aaaaa kiulaini umeikwaa,” Inspekta Simbeye kama kawaida yake akawa akimwaga utani, akawakaribisha na kuketi nao, “ndiyo Bwana Amata , najua tu kuwa ukija hapa basi huko yamekushinda,” akamwambia.

“Hapana, nikija hapa basi nataka usaidizi wa mapana na marefu, kuna hii namba hapa ya gari, naihitaji hii gari ama nijue sasa hivi iko wapi au imepita mtaa gani,” akamwambia Simbeye, akampa kijikaratasi kilichoandikwa hiyo namba. Inspekata Simbeye akakitazama kwa udadisi sana kile kijikaratasi, akafinya macho akafinyua, kisha akawatazama Gina na Amata, “ ok kwa hiyo mnataka vijana waingie kazini?” akauliza.

“Ndiyo maana tukaja kwako kwa maana wao vijana wako wanajua kunusa vitu kama hivi kwa haraka kutokana na mtandao walio nao,” Kamanda akeleza.

“Ok, nipe dakika kadhaa,” akainua simu ya mezani na kuzungurusha namba fulani kisha akamwita kijana mmoja. Dakika mbili yule kijana alikuwa kasimama kwa ukakamavu kabisa mbele ya Inspekata wake akiwa katika sare yake nadhifu nyeupe katika mkono wake wa kushoto akining’iniza ‘V’ tatu yaani alikuwa Sajini.

“Nataka upeleke taarifa kila point huko barabarani wakiiona hii gari leo wanipe taarifa haraka iwezekanavyo,” akatoa amri.

“Sawa Afande!” akajibu yule kijana na kutoa saluti ya utii kisha akaondoka zake.

***

Siku hiyo askari wa usalama barabarani waliongezeka mpaka kila mtu alishangaa, gari nyingi zilisimamishwa hii ikakuguliwa pale na ile kule ili mradi tu wajaribu kuipata ile wanayoitaka. Haikuwa kazi rahisi bali ilikuwa ngumu, madereva walikasirika sana maana walisimamishwa hata zaidi ya mara tano lakini hawakujua ni nini ambacho wenzao wanakitafuta. Siku ilienda kasi hakuna jibulolote lililoleta maatumaini. Kamanda Amata akiwa katika mgahawa wa Steers alianza kukata tamaa, maana alitegemea taarifa hiyo ingeweza kumpa njia ya kupenyea katika kulikabili swala hilo.

Akiwa anaweka weka vitu vyake vizuri tayari kuondoka katika mgahawa huo mara simu yake ikapata uhai mpya, namba iliyosomeka kiooni ilikuwa ni ile ya Simbeye. Kumekucha, akawaza, kisha akaibonyeza kile kidubwasha cha kusikilizia na kuiweka sikioni.

“Windo lako limeonekana, limetoka barabara ya Mandela na kuingia barabara ya Morogoro…” Sauti ya Simbeye ilieleza.

“Ok, nimekupata, naomba taarifa kila point anapopita mpaka atakaponikaribia, nipo mjini kati na sasa naelekea barabar ya Morogoro kutokea Mtaa wa Samora,” Kamanda akaeleza.

“Wrong, pita barabara ya Ohio ukatokee ile ya Bibi Titi kisha kunja kurudi Maktaba nafikiri atatumia njia hiyo,” Simbeye alieleza kana kwamba anajua mtu huyo anakwenda wapi. Kamanda Amata akatia gia na kuondoka pale Steers, moja kwa moja akaiacha Ohio na kuikamata ile ya Bibi Titi kuelekea Maktaba akiwa makini kabisa kutazama gari zinazokuja mbele yake, akafyatua nobu ya simu ya upepo yenye uwezo wa kunasa mawimbi ya simu zote za mtindo huo zinazopita ndani ya mita mia tano za mraba, akaweka vizuri signali za redio ya polisi akazipata na kusikiliza wanavyoelekezana juu ya gari hiyo.

“…Imepita hapa mataa ya Magomeni ova….”

“….Imeelekea Kinondoni, point ya Kinondoni tafadhali, ova!…”

Kamanda Amata alipiga U – turn pale maktaba na kurudi haraka akakunja kushoto kwenye makutano ya barabara ya Bibi Titi, Ohio na ile ya Ally Hassan Mwinyi, akaifuata hiyo kwa kasi akiwa na malengo mawili, ama kukutana nalo kwenye makutano ya Barabara ya Ally Hassan Mwinyi na Ile inayotoka Kinondoni.

“… imepita mataa ya Mwananyamala. Imenyoosha kuelekea Morocco, Ova…”

“….Endelea kunipa ripoti Ova!…”

Kamanda Amata akakaza mguu na kuongeza kasi kuwahi katika makutano ya Morroco maana kutoka hapo hakujua hasa ni wapi anaweza kuwaona tena.

“…imeelekea barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ova…”

Kamanda Amata aliposikia taarifa ya mwisho alikuwa tayari amefika karibu na Mbuyuni njia ya kwenda Kanisa la Sant Peter, akakunja kulia na kuifanya kama inataka kuingia barabara ya pili kuelekea mjini, akasimaman katikati akisubiri, wakati huo taa ziliwaka nyekundu, gari zikasimama. Kamanda Amata akatazama kwa haraka haraka, akaiona ile gari ikiwa imesimama ikisubiri foleni, akatazama kwa umakini ndani yake, alimuona mtu mmoja tu, mwanaume aliyekuwa ameketi nyuma ya usukani. Gari zilizpoanza kutembea, akavizia nyuma ya hiyo gari zikapita gari mbili kisha yeye akaingia hapo na kuifuatilia taratibu. Ile gari ilikwenda na kuingia katika maegesho ya Motel ya Agip katikati ya mji, mtu aliyekuwa humo akashuka, mwanaume mwenye tambo la haja, kwa harakaharaka Kamanda alimuona mpiganaji huyo akivuta hatua fupifupi na mguu wake akiwa akichechemea kwa mbali, akamkumbuka, George Mc Field, akatikisa kichwa, kisha akacheka, baada ya kugundua kuwa mtu huyo miaka kumi ilopita hakuwa akichechemea lakini kwa kipigo alichokipata kwa Kamanda Amata mara ya mwisho katika sakata la Mwanamke Mwenye Juba Jeusi kumbe lilimuacha na mguu mbovu. Akamtazama mpaka alipoingia ndani, akateremka garini na yeye kuiendea kaunta ya moteli hiyo.

Moustache alioubandika juu ya mdomo wake ulimbadili kiasi, na kofia kubwa aliyovaa ilimfanya aonekane mmoja wa ‘watumia pesa’. Amata akasimama jirani kabisa na Mc Field ambaye alikuwa amejibadili kiasi ila kwa Amata alimtambua kwa alama zake alizokuwa akizikumbuka. Kabla hajaongea na mhudumu wa kaunta jicho lake kali lilikuwa likitazama katika kaitabu ambacho Mc Field alikuwa akiweka saini, akaona namba ya chumba 206. Akajifanya anaulizia mtu fulani ambaye hayupo kabisa katika hoteli hiyo. Kisha akatoka mara baada ya kujibiwa kuwa mtu huyo hayupo. Akarudi garini na kuiondoa gari yake kisha akenda kuiegesha upande wa pili. Alijua wazi upande gani ambako kile chumba kilitazama, akaiacha gari yake na kurudi upande wa pili.

Chumba alichokitegemea, kikafunguliwa pazia, Amata hakuwa na haja ya kujua nini kinaendelea ndani ya chumba hicho, akatulia akisubiri. Ilichukua dakika arobaini na tano, pazia likafungwa tena. Kamanda akawa makini kuona  nini kinatokea, mara gari ile ikawashwa na kuondoka maegeshoni.

Kama kawaida, akasubiri dakika kumi na tano akaingia ndani ya hoteli ile na kukwea ngazi mpaka chumba namba 206 akautazama mlango kwa makini kama kuna alama yoyote iliyoachwa ambayo mtu huyo itamfanya agundue kuwa alitembelewa. Hakuona, akachukua funguo yake inayoweza kufungua vitaza 999, akaipachika na kucheza nayo sekunde nne tu mlango ukatii, akausukuma taratibu lakini alikumbuka lililompata Madam S, akatanguliza mkono wake huku akikubali kitakachotokea, alitegemea kutobolewa na misumari mibaya inayotegwa na Jasusi huyo mara nyingi, hakukuwa na kitu.

Akaingia kwa hatua mbili ndani, hakuwasha taa ijapokuwa giza lilikwishakijaza chumba hicho, akaichukuwa miwani yake na kuivaa, chumba chote kwake kikaangazwa na mwanga usioonekana na mtu mwingine, akatazama kwa macho, akakagua chumba hicho kwa macho, hakutaka kugusa chochote kile, kisha akachukua kijitufe kidogo mfano wa  big G, akakiendea kitanda akakitazama na kupachika kile kidubwasha uvunguni kwenye chaga, kisha akatoka taratibu na kukiacha chumba hicho, akarudi kwenye gari yake, akafungua saraka ya gari na kutoa kidubwasha kingine kama redio ndogo sana ukubwa wa kiberiti, akakiwasha ili kurekodi kila sauti itakayotokea ndani ya chumba hicho kisha yeye akaondoka zake kwa usafiri, mwingine huku ile gari akiiacha pale pae.

“Las Vegas Cassino!” akamwambia dereva aliyekuwa kimwendesha. Dakika chache baadae alikuwa katika Cassino hiyo kubwa iliyopo kwenye njia panda ya kuelekea Agha Khan kutokea Barabara ya Ally Hassan Mwinyi.

“Yes Kamanda,” Madam S akaiita kutoka nyuma yake wakati Amata akiwasha sigara kana kwamba yeye ni mvutaji.

“Agip Motel namba 206,”

“Maelekezo mengine,” akahoji Madam.

“Baada ya saa kadhaa, watoto wanacheza,” akajibu.

“Ok,” Madam akamalizia kwa kuitikia, akampita Kamanda na kuondoka zake, akaiendea gari yake, kukamata kitasa.

“Subiri!,” Kamanda akamshtua Madam S, kisha akampa ishara ya kurudi kwake, Madam akataii. Wakati Madam S alipokuwa anataka kufungua mlango wa gari, Kamanda Amata alimuona mmoja wa walinzi wa Cassino hiyo akichomoa kitu kama remote mfukoni mwake. Hiyo ilimpa ishara Kamanda kuwa kuna hatari inakaribia kutokea, Madam alaiporudi kwa Kamnda yule mtu akarudisha ile remote mfukoni mwake, na kupotea eneo lile mara moja.

“Hakuna usalama,” akamwambia Madam S

“Umeona nini?” Madam akauliza

“Gari yako lazima ina mlipuko, ngoja kidogo,” akajibu na kuifuata gari ya Madam S, akawasha saa yake na kuisogeza jirani, ikapiga kelele na kuwaka taa nyekundu, akamtazama Madam S.

“Wamejuaje kama niko hapa mpaka waniwekee bomu?” Madam S akauliza.

“Muwinda huwindwa mama! Acha hiyo gari tumia usafiri mwingine, tuonane kesho asubuhi,” Kamanda akamuaga mwanamama huyo na kutoka eneo lile. Kwa mwendo wa miguu akarudi kuifuata barabara ya Ally Hassan Mwinyi, akiwa taratibu njiani, nyuma yake kulikuwa na watu wawili wakija nao wakiwa wametokea katika casino ileile. Aliporudisha uso mbele akaona mtu mmoja akija upande huo, hakuonesha kugwaya, alitembea kwa mwendo uleule. Alipofika katikati, wa nyuma na wa mbele wakiwa umbali sawa, akasimama na kugeukia katika maua yaliyo mbele yake, akafungua zipu ya suruali na kujifanya anakojoa, akisubiri aone watu hao watachukua hatua gani. Alijua kama watasita basi ni wabaya kwake lakini kama si wabaya watapita na Hamsini zao.

Wale wawili wakasita kidogo, wakawa kama wanajiuliza jambo, yule mmoja akajifanya anafunga kamba za viatu, kwa vitendo hivyo Kamnda Amata akajua wazi kuwa anawindwa na amekwishwekwa katikati, akageuza na kurudi alikotoka kule kwenye wale wawili, akaona wakiwa na woga Fulani, akaongeza mwendo kuwaendea, akachanganya miguu kama anatroti.

“Simama!” wakamwamuru.

“Mna amri gani ya kunisimamisha mimi? Ninyi ni nani?” akauliza huku akiwapita.

Wale jamaa walimpa hatua mbili tu za kupita, wakageuka na mmoja wao akatoa kitu kama mpira akauzungusha katika viganja vyake, mwisho huu huku na huu kule tayari kwa kumkaba. Kwa haraka  akaupachika shingoni mwa Amata, hilo alilitegemea tangu mwanzo, na aliigundua hiyo mbinu. Akanyosa juu mikono kwa kuikunja mikono yake na ule mpira ukaivaa mikono, akaisukuma mbele na yule jamaa akajigonga kisogoni mwa Amata. Akajivua ule mpira na kugeuka haraka, konde moja alilolitupa, lilipiga shavuni mwa Yule mjing akaenda chini, yule wa pili akarusha ngumi akadakwa mkono, akauzungusha na kuuweka begani akauvunja, yowe la uchungu likamtoka yule jamaa. Wakati huo yule mmoja aliyekuwa akitokea mbele akawa amefika, mkononi alikuwa amekamata kitu kama bastola.  Amata akamwacha yule jamaa na kuchumpa kuingia kwenye maua, lo! Hakuangalia vizuri, kwenye yale maua kulikuwa na seng’enge yenye ncha kali sana, zikamchoma, kabla hajajinusuru yule jamaa akafyatua ile bastola yake, kitu kama msumari kikamchoma shingoni. Amata akajisikia ganzi, miguu akahisi ikipata ubaridi, taratibu akaanza kupoteza nuru. Kila alipojaribu kujitutumua hakuweza, akatulia na kukumbwa na giza nene.

“Mmemkamata?” sauti hiyo aliisikia kwa mbali sana.

“Aaa nimempata lakini Shebby kavunjwa mkono msaidieni,” akaendelea kuwasikia kwa taabu na mwisho masikio yake hayakuwa na nguvu tena za kusikia chochote.

 

SIKU ILIYOFUATA saa 3:30 asubuhi

MADAM S ALIINGIA OFISINI kwa kuchelewa kidogo, akamkuta Chiba akiwa anamsubiri.

“Vipi Chiba?” akuliza.

“Nimekuwa nakusubiri sana maana kila simu nikikupigia sikupati, nikaanza kuwa na wasiwasi,” Chiba akajibu.

“Ah, mbona simu zangu zilikuwa on zote? Kwa nini ulikuwa hunipati?” Madam S akatoa simu zake na kuziangalia zote zilikuwa sawa.

“Shida za mitandao hizi,” akamwambia kisha akaingia ofisini.

“Nipe jipya,” Madam S akamwambia huku akivuta kiti chake na kukaa.

“Hakuna jipya, ila sina taarifa yoyote ya Kamanda tangu jana nilipokuwa nawasikia mara ya mwisho pale Cassino ya Las Vegas,” akamweleza Madam.

“Aaaa Kamanda tuliachana kama saa nne hivi, na tangu hapo hata mimi sikumtafuta,” Madam S akajibu, akafikiri jambo kisha akaendelea kusema, “jana aliacha gari pale Motel Agip mtaa wa pili hivi, kuna information alikuwa anainasa, nafikiri atakuwa ameiendea, hebu mtafute kwa simu yake ya kwenye gari”.

Chiba akajaribu lakini simu iliishia kuita tu.

“Hayupo garini!”

“Jaribu nyumbani”.

Chiba akajaribu simu za nyumbani, zote hazikupatikana kabisa, “hakuna connection kabisa,” akamwambia Madam S.

“Mpigie Gina,” akatoa maelekezo. Chiba akampigia Gina akampata, akamwulizia juu ya Kamanda Amata, Gina hakuwa na jibu sawasawa, akamwambia atapita nyumbani kwake Kinondoni akamwone.

***

Kamanda Amata alikuwa kwenye kiti cha chuma, hakuwa na fahamu, mikono yake ilifungwa nyuma ya kiti hicho ilhali miguu yake ilikuwa imefungwa pamoja kwa kuzungushwa nyuma ya miguu ya mbele ya kiti hicho. Alikuwa amelala usingizi, shingo yake imeeinamia chini, udenda ukimtoka. Ndani ya chumba hicho cha wastani kulikuwa na vijana watatu wenye Sub Machine Gun kila mmoja iliyoshiba vizuri. Hawakuwa wakiongea, kila mmoja alisimama kona yake akiweka ulinzi madhubuti. Waliambiwa watoe taarifa pindi tu atakapoamka. Ilikuwa zimekwishapita saa kumi na mbili tangu adungwe dawa ile mbaya kabisa mwilini mwake ambayo huenda na kuudhoofisha milango yote ya fahamu.

Amata alianza kuhisi baridi kwa mbali sana, fahamu zilianza kumrudia, kidole chake cha kalulu kilianza kuchezacheza.

“Anaamka huyu! Oya waite jamaa!” mlinzi mmoja alitoa amri kwa walio nje. Ijapokuwa alikuwa kamanda peke yake katika chumba hicho kama mateka lakini walinzi wa ndani walikuwa watatu waliobeba SMG zilzizoshiba risasi, nje ya mlango kulikuwa na walinzi wengine wapatao watano nao walikuwa na silaha kama zizohizo. Kwa ujumla walimwogopa, labda kutokana na habari walizopewa juu ya uhatari wa mtu huyo.

***

Peugeot 404 iliegeshwa nje ya nyumba fulani katika eneo la Upanga, mtaa wa Ali Khan. George Mc Field ambaye tangu ameingia nchini alikuwa ameuvaa Uafrika-butu, alionekana Mwafrika lakini aliyepauka kidogo, hiyo ilitokana na kujibadilisha kwa ngozi yake kwa madawa maalumu na kuupoteza uhalisia wa uraia wake. Alikuwa Jasusi aliyetafutwa kila kona, alitekeleza mengi sana ya kuua, kuiba, kuteka, kutesa na mambo yanayofanana na hayo. Alijishauri mara kadhaa siku alipoapewa kazi ya kuja kufanya wizi wa almasi katika mgodi wa Mwadui, lakini kutokana na donge aliloahidiwa alikubali.

Akachagua watu watatu makini kati ya vijana wake, akawafundisha Kiswahili, mapigano, jinsi ya kutembea kama Watanzania, akaandaa mkakati makini wa kuiba almasi kwa kujifanya yeye ni Waziri wa Nishati na Madini. Kazi hii kwa Mc Field haikuwa ngumu sana, kwa kuwa yeye alikwishapitia kozi mbalimbali za Kijasusi na Ukomandoo aliiona kazi ndogo ila aliipenda kwa kuwa ilihusisha pia kuwapoteza watu uhalisia wa wanachokiona.

 

 

9

WIKI MOJA NYUMA

FORKER FRIENDSHIP, ndege ya serikali, iliondoka katika uwanja wa ndege mdogo wa mgodi wa North Mara kuelekea Mwadui. Wageni waliotumwa na makampuni kutoka nje kuja kwa ajili ya kutazama fursa za uwekezaji, walitulia vitini, walikuwa watatu, wazungu. Ndege ilipokaa sawa hewani na kuruhusiwa kufungua mikanda, mmoja wao alinyanyuka na kuelekea maliwato.

***

“Vipi, kuko sawa huko?” Mc Field aliuliza akiwa katika eneo la mizigo, amekaa akisubiri wakati, yeye aliingia ndegeni bila mtu yeyote kujua, alijifanya mmoja wa wafanyakazi wa ndege hiyo pale North Mara, akajificha katika behewa ya mizigo, akijibadiliasha hapa na pale mpaka akafanana kabisa na Mheshimiwa Waziri. Utaalamu wa hali ya juu unaotumiwa na Majasusi au wapelelezi mbalimbali huko nchi zilizoendelea. Mission ilishapangwa, kila kitu kilitengenezwa, ilibaki kuvaa tu.

“Yeah, tuko level nzuri kutoka usawa wa bahari,” akajibu yule mtu.

“Ok, zima pale, kisha pachika hako kamtungi katika hiyo pipe,” akamwelekeza, yule kijana akafanya hivyo, “subiri kidogo, dakika tano hivi, nitakujulisha,” akamwambia, kisha ukimya ukawakabili kati yao.

***

Ndani ya chumba cha rubani, mashine za kuonesha vipimo vya hewa, presha, kani mvuto, mwendo kasi na kadhalika, vilionesha hitilafu hasa katika upande wa presha na hewa safi. Rubani alijitahidi kurekebisha hapa na pale lakini ilikuwa ngumu, akainua kidubwasha cha kuongelea na kuwatangazia abiria kutumia hewa ya ziada inayotoka katika mitungi maalumu ndani ya ndege hiyo. Juu ya kila kiti, kwenye saraka kubwa za mizigo ya ndani zikachomoka barakoa za kuvaa puani kuweza kuvuta hewa safi.

Wakati huohuo kule chini kwenye mizigo, Mc Field na mwenzake wakaondoa mtungi wa oxygen kwenye ‘Chemical Oxygen Generator System’ na kupachika mtungi wao wenye dawa kali ya kulevya katika njia za kupitisha hewa safi. Haikuchukua dakika moja wote walikumbwa na usingizi mzito isipokuwa wale Wazungu tu ambao hawakugusa kabisa barakoa zile.

“Tayari, waambie wenzako mulete waziri huku chini. Yule kijana akafanya hivyo. Waziri akaletwa chini kwenye mizigo akiwa anapumua kwa tabu, Mc Field akachomoa kijikadi kidogo kilichounganishwa vizuri kwenye kompyuta ndogo.

“Soma hapa,” Mc Field akamwambia waziri. Mheshimiwa akabaki kakodoa macho tu, hakujua la kufanya, “soma hapa!” akamlazimisha na kumchapa kofi la usoni.

“Tu-na-hitaji -makasha ma-ta-no ya almasi sa-sa ni  amri  ku-to-ka I-ku-lu  ba-ru-a  hii – ha-pa”.

Kisha mmoja wa wale vijana akamdunga sindano na waziri akalala usingizi wa maana. Wanaume wakafanya walichotumwa.

***

Rejea sasa: Tracy Tasha…

TRACY TASHA ALIVIRIGA nywele zake na kuzifunga kwa nyuma, akaiweka miwani yake usoni, akachukua kitu kama kalamu  iliyokuwa na rangi inayofanana na ngozi yake  akakiendea kioo kikubwa na kuanza kujitengeneza uso wake vizuri kwa namna anayoijua yeye, alipohakikisha kajiweka tofauti, akafungua mkoba wake na kutoa stika moja ambayo aliibandika kwenye shavu lake. Stika ile ilitengenezwa taswira ya mtu aliyeshonwa jeraha kwa nyuzi saba. Akatoka nje ya hoteli na kuingia katika tax iliyokuwa ikimsubiri, “mtaa wa Ally Khan mkabala na Zanaki Sekondari,” almwambia dereva kisha yeye akaketi kiti cha nyuma bila kuongea zaidi hata pale alipoulizwa maswali kadhaa na dereva huyo hakujibu zaidi ya kutikisa kichwa tu.

Dakika arobaini na tano ziliwatosha kupambana na foleni na kuingia katika eneo husika. Tracy alilipa na kuachana na dereva huyo, alipopotea, akavuka barabara na kuingia kwenye geti dogo katika nyumba aliyihitaji. Ilikuwa nyumba kubwa ambayo nyuma yake kulikuwa na banda kubwa lililojengwa kwa matofali ya kupangwa, ndani yake kulikuwa na kitu kama handaki ambacho watu wengi hawakujua hilo.

“Karibu sana, this way please,” George Mc Field alimkaribisha Tracy na kisha wote wakashuka handakini.

***

Kamanda Amata alikuwa ameendelea kuketi palepale alipofungwa, akili yake ilisharudiwa na fahamu kamili, lakini bado alijifanya hajaamka sawasawa, aliweza kusikia kila kitu kilichoendelea, alijuwa wazi kuwa ni nani anayesubiriwa na alisubiri kuona kama hao wanaokuja ndio wale anaowahitaji, alihitaji kuwajua. Kwa mara kadhaa alijaribu kujitikisa na kuona kama kamba zile zimemfunga sawasawa, mikononi alishindwa hata kujitikisa lakini miguuni nako ilikuwa hivyo hivyo, akatulia na kufumbua jicho moja kwa mbali, akawahesabu wote waliokuwa ndani, ni watatu tu na bunduki zao.

Nikileta makeke tu natobolewa kwa risasi zenye hasira, akawaza. Mara akasikia lango likifunguliwa upande wa juu na watu waliokuwa wakiongea kwa lugha ya Kiingereza wakaingia ndani ya eneo hilo.

Sekunde chache tu watu wawili walikuwa mbele yake, yule mgeni wa kiume akatikisa kichwa chake na kijana mmoja akaweka pembeni bunduki yake, akakunja mikono ya shati lake. Kamanda Amata akajua sasa kumekucha. Yule bwana alimsogelea, akamatazama Amata. Akamwinua uso wake, Kamanda akafumbua macho yote mawili akamwangalia, yule jamaa akasita kidogo maana alishaambiwa uhatari wa kiumbe huyo. Akaita wenzake wamuweke sawa. Amata akafunguliwa kamba na kuondolewa kitini, kamba za miguuni zikarudishhiwa kisha zile za mikononi zikafungwa kwa nyuma lakini wale vijana wakamkamata huku na huku upande wa nyuma na yule mwingine akaanza kumshindilia makonde ya tumboni, makonde ya nguvu. Amata alivumilia lakini nguvu za mikono za yule Bwana zilikuwa zikimwingia kisawasawa, damu zikaanza kumtoka kinywani.

“Ha! Ha! Ha! Haaaaaa! Mwacheni! Kamanda Amata, leo au niseme sasa, umefika mwisho wako, na lazima ufe sambamba na yule tunayemtaka au tuliyetumwa kumtoa roho yake,” Mc Field akamwambia Kamanda huku akimgeuza uso wake uliowiva kuwa mwekundu. Alihema kwa taabu sana, “Mc Fi-e-ld, uta-lipa, utalipa, na-kwa-mbia utalipa,” akamwambia kwa sauti ya taabu. George Mc Field akastuka kidogo baada ya kusikia jina lake likitajwa, akajiuliza pamoja na kujibadili inawezekanaje kuwa kajulikana kirahisi namna hii, akajikaza.

“Nani anayekudanganya hayo? Sikia mpumbavu wewe, kabla hujafa nitataka kukupa siri moja nzito ambayo utakufa na hautaweza kuifikisha popote pale, na siri hiyo ni kuwa kesho tunaondoa roho ya mtu mkubwa sana hapa katika Taifa lenu,” Mc Field alizidi kutamba wakati Tracy akiwa kasimama kando mikono yake kaifungamanisha kifuani mwake, akitafuna pipi mpira isiyokwisha.

Konde moja zito la Mc Field lilitua katika shavu la Kamanda Amata, akahisi taya lake limevunjika, kabla hajatulia akapata lingine la upande wa pili.

“Sikia we Bwege, nimekuja tena nikiwa na hasira mbili, na kazi moja! Nadhani umenielewa, leo hutoona jua la nje, kibibi chako kinahaha huko duniani kukutafuta na hakitakuona tena,” Mc Field alimweleza Amata.

“Utalipa, ha-ta mimi ukiniua, yu-po nyu-ma atakayekuua kwa kwa niaba yangu, atakutenganisha kichwa na kiwiliwili chako,” Kamanda akaeleza.

“Ha! Ha! Ha! Ha! Haaaaaa!!!!” Mc Field akacheka sana, “nani unayemtegemea, huyu hapa au mwingine?” Mara mlango mwingine ukafunguliwa, Gina akasukumiwa ndani na kuanguka sakafuni. Kamanda Amata alitamani aruke kumdaka Gina ambaye alijibwaga vibaya sakafuni.

“Tunapotaka kufanya kazi, huwa tumejipanga, wewe na huyu malaya wako wote leo mnaenda kuzimu,” Mc Field alijigamba. Kamanda Amata alikuwa amefura kwa hasira kali, akimtazama Gina aliyekuwa chini hajiwezi, ilionekana amepata kipigo kisicho cha kawaida.

Tracy Tasha alivuta hatua na kumsogelea Gina, alivuta mguu wake na kumtandika Gina teke kali la usoni. Gina akatupwa upande wa pili, akabaki chali damu zikimvuja puani na kinywani. Mguu wa Tracy ulienda juu na kubaki hewani kwa sekunde kadhaa kabla hajaushusha chini kwa maringo, kisha akatembea kama Miss kumwendea Amata.

“Huyu ndiye ulienipa vitisho juu yake? Eti Kamanda, kamanda? Makamanda wametulizwa kwa mkono huu,” akaupunga mkono wake hewani, akamtazama Mc Field, “hakuna mwanaume wa chuma wala nini, hapa ni utepetevu tu,” akamalizia kisha akarudi alipokuwa. Mc Field alitabasamu huku akitikisa kichwa chake juu chini, akimwangalia mwanamke huyu anayetembea kwa madaha, mrembo wa sura na mzuri wa shepu, lakini mwenye roho iliyojaa kutu.

“Kamanda Amata una la kusema? Sasa ni saa saba inaenda saa nane, muda wetu unayoyoma, huyu mwanamke ndiye atakayekuua wewe usiku wa leo kwa kukukata kichwa chako,” Mac Field alimwambia Kamanda.

“Hata kama, La- la-ki-ni, kwa-nza nitaku-ua we-we,” akimaanisha Mc Field, “pili we-we mwana-m-ke uta-ji-ua –mwenye- we,” aliongea kwa tabu. Mc Field na Tracy wakaondoka ndani ya chumba kile wakiacha maagizo kuwa watu hao washughulikiwe ipasavyo.

***

Ilikuwa ni vigumu sana kwa Madam S kuamini kuwa Kamanda na Gina wametekwa, haikuingia akilini. Wamempataje kirahisi hivyo? Alijiuliza bila ya kupata jibu. kila mara alikuwa akimwita Chiba ofisini na kumwambia hili au lile, alionekana wazi amechanganyikiwa. Chiba alijaribu kumtafuta Kamanda kwa simu zake lakini ilikuwa ni ngumu sana kwake kupata jibu kuwa wapi yupo kwani simu zake zilikuwa zikisoma eneo la mwisho la Upanga, Las Vegas Cassino.

“ Wameniweza!” alijiambia moyoni, “Scoba!” akaita.

Scoba akageuka kumtazama Chiba.

“Harakati lazima ziendelee kaka, hatujui Gina na Kamanda wako wapi mpaka sasa, na wala wako katika hali gani, hivyo tufanye juu chini kupata jibu,” Chiba, TSA 2, ilikuwa ni nafasi yake sasa kutoa majukumu.

“Iendee gari ya Kamanda pale Motel Agip kuna information inayoweza kutusaidia,” akaamuru na Scoba akawasha gari yake na kuondoka. Kama alivyoeelekezwa. Gari ya Amata ilikuwa palepale, Scoba kwa tahadhari ya hali ya juu sana akiendea ile gari, hakuhitaji kuiendesha, moja kwa moja aliifungua droo iliyokuwa imefungwa kwa lock maalum, akachukua anchotaka, alipogeuka tu kuondoka kuiacha ile gari, nyuma yake mlipuko mkubwa ukatokea, ile gari ikanyanyuliwa juu  na kuvingirishwa mara kadhaa kabla haijatua juu ya gari nyingine ambazo nazo zilidaka moto, kizaazaa.

Scoba, alitupwa na ule msukumo uliotokana na mlipuko, akatua katika mlango wa vioo wa duka moja la madawa, akaanguka nao mpaka ndani. Mtaa mzima ulikuwa ni hekaheka kila mtu akitaka kunusuru gari yake na kusahau uhai, wapo waliofanikiwa lakini pia wapo ambao gari zao ziliteketea kabisa.

Tukio hilo lilivuta wengi sana mahala hapo, hii ilimsaidia Scoba kuondoka taratibu na kuielekea taksi iliyokuwa jirani. Ulikuwa ni mlipuko ambao mtu yeyote hakuutegemea hasa kwa jiji kama la Dar es salaam ambalo utulivu na amani zimekuwa ni desturi kwa wakazi wake.

***

“Pole Scoba, lakini haujaumia sana,” Dkt. Jasmine alimpa pole Scoba huku akimpa huduma ya kwanza katika chumba cha siri kilicho ndani ya ofisi ya Madam S. Damu kiasi zilikuwa zikimvuja katika upande mmoja wa kichwa chake baada ya kujikata vibaya kwa kioo pale alipoangukia, akaufungua mkono wake na kumpa Madam S kile kidubwasha.

“Mpe Chiba,” akamwambia.

Ilikuwa ni kinasa sauti kidogo kilichofichwa katika gari ya Kamanda Amata, Chiba alikichukua na kukiunganisha na mitambo yake, kisha akafuatilia mazungumzo yaliyokuwa humo kwa makini. Ndipo alipogundua kuwa Kamanda Amata ametekwa kadiri ya mazungumzo ya mtu aliyekuwa akiongea na simu katika chumba cha Motel hiyo. Aliendelea kufuatilia mazunguzmao hayo lakini hakujua kabisa ni wapi watakuwa wamemficha Amata. Chiba na wengine vichwa vilianza kuwazunguka.

“Tutapajuaje? Kumbuka Mc Field anamjua vizuri sana Amata, hawezi kumpa nafasi zaidi ya kumuua tu. Ndiyo, Amata anaweza kujiokoa lakini ni kazi ngumu sana kwa mtu kama Mc Field ambaye anauju uwezo wa kamanda, mtu kama yule hawezi kurudia kosa,” Madam S alimwambia Chiba huku akijifuta machozi.

“Ok, Madam, najua cha kufanya ila sasa tuandae Kikosi cha Ukombozi,” Chiba alitoa ushauri.

“Sawa, ni wewe mwenyewe na Scoba mtafanya kazi hiyo, hakikisheni inazaa matunda,” akampa maagizo, kisha akamsogelea Chiba, “ukikutana na Mc Field usijipime kupambana naye, tumia silaha, mmalize,” akamnong’oneza kisha akarudi kitini.

Chiba akairekodi ile sauti kwenye kompyuta yake na kuwasiliana na rafiki yake wa karibu sana katika moja mitandao maarufu ya simu, akampa kazi ya kutafuta watu hao walikuwa wakiongea wapi na wapi.

Dakika tano baadae alipewa taarifa kuwa mmoja alikuwa eneo la Mjini Kati maana mnara uliosoma ulikuwa ni ule wa jirani na jengo la Kitega Uchumi la Bima na mtu wa pili alionekana kuwa mitaa ya Zanaki Sekondari kwani mnara uliomsoma ni ule wa jirani na chuo cha ufundi cha Dar – Tech, upande wa nyuma. Chiba alijiridhisha na maelezo hayo na akamuomba mtu huyo amwambie namba hizo kwa sasa zinasoma wapi ili waweze kuwafuatilia watu hao. Jibu alilopata ni kuwa moja ya namba hizo ilikuwa imezimwa lakini nyingine bado ilionekana ipo mitaa hiyo ya Upanga, Mtaa wa Aly Khan.

“Scoba, upo poa? Tunaweza kuingia kazini?” Chiba alimwuliza. Scoba akaitikia kwa kichwa kushiria kuwa yuko fiti na anaweza mapambano, wakatoka katika chumba hicho na kufungua kijistoo kidogo, wakachagua silaha zinazofaa kwa kazi hiyo.

“Vipi mbona mnapakaua?” Madam akauliza.

“Tunaenda kupambana na jeshi, so lazima tujiweke kamili,” Chiba akajibu. Scoba akachagua Short Gun double barell, akaijaza risasi, bastola mbili aina ya PK 380 akazitia kibindon. Chiba akatazama huku na kule akainua silaha inayoitwa Heckler and Koch UMP , akaitia begani na nyingine ndogo ndogo kama visu, kamba za plastic, wakatoka wakavitia kwenye buti la gari na wao wakabaki na bastola mbilimbili zilizosheheni risasi. Wakaondoka na kuelekea Upanga.

 

 

 

10

AMATA ALIKUWA MDHOOFU sana baada ya kipigo alichokipata kutoka kwa wale jamaa mara baada ya Mc Field na Tasha kuondoka katika eneo lile, walikuwa wakimpiga huku wakimcheka sana na kila mmoja alijiona mshindi katika hilo, damu zilikuwa zikimvuja, wakati huo Gina hakuwa na nguvu hata ya kusimama.

“Sasa kinachofuata ni kufanya mapenzi na huyu malaya wako huku wewe ukiangalia,” mmoja wale jamaa akamwambia Amata.

Yule jamaa akamwendea Gina na kuanza kumfungua suruali aliyokuwa amevaa, huku wenzake wakishangilia na kupiga picha za video. Kitendo kile kilimuuzi sana Amata, kikampa hasira, hasira ambayo ilirudisha nguvu za ziada mwilini mwake. Mmoja wa wale vijana akamsogele Amata.

“Usijifanye huoni, angalia huku tunachomfanya malaya wako kisha picha zote tunapeleka kwa wakubwa zako,” akamwambia Kamanda huku akimshika kidevu kumgeuzia sura kule alikokuwa Gina. Ni dakika au nukta hiyo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu sana na Amata, aligeuka ghafla na kudaka kidole cha yule jamaa kwa meno, akamuuma na kukikata kisha akakitema chini.

“Aiiiiiigggggghhhhhh!!!!! Ananing’ata mjinga huyuuu!” yule bwana akalia kwa uchungu sana, wenzake wakagutuka na kusogea kumsaidia. Kamanda Amata aliruka akiwa na kamba miguuni na mikononi, akajikunja kisha miguu yake akaipitisha katikati ya mikono yake na kutua nyuma huku mikono sasa ikiwa mbele. Akaanguka kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kusimama sawasawa, akabiringita na kuifikia nguzo iliyosimikwa kushikia jengo hilo, akajiinua na kuketi, harakaharaka akashika ile kamba ya miguuni na kuifungua haikumpa tabu aliivuta tu ikalegea.

Kabla hajamaliza, alipata teke la mgongoni, mtu mwingine akaja kwa mbele na kurusha teke ambalo lingetua usoni au kifuani lakini Amata akalizuia kwa mikono yake iliyofungwa, akaunasa ule mguu na kuubana vizuri.

Kamba ya miguuni ikawa imekwishauacha mguu wake, akazungusha mguu na kumtia ngwala yule aliyemdaka mguu, jamaa akajibwaga chini akifikia kisogo, akatoa ukelele wa kifo. Mara hii alijikuta amezungukwa, akajiinua haraka na kuruka samasoti, risasi zikachimba chini na nyingine kwenye nguzo. Wakati yeye akitua chini alitua na wawili, mmoja alimshindilia vipepsi viwili vya pamoja na mwingine, akamshushia mateke makali, wote wakaenda chini, akabiringita na kujificha nyuma ya kasha kubwa la bati gumu, likamkinga dhidi ya adui zake.

“Oya, akitoroka huyo, tumekwisha!” Sauti ya mmoja ikasikika.

“Hatoki mtu hapa! Mzungukeni,” mwingine akatoa amri.

“We Chulubi, hakikisha huyo mwanamke umemfungia ndani, tushughulike na huyu mbwa koko,” sauti hii na maneno hayo yalimtia hasira Amata. Akiwa tayari ameiondoa kamba mikononi mwake kwa meno, alilisukuma lile kasha na kisha akajitumbukiza na kuseleleka nalo, risasi zikapiga juu yake lakini hazikuweza kuliathiri kwa lolote. Liliposimama akaruka nje na alipotua akambamiza mmoja mwenye bunduki, akaenda chini na bunduki ikitoka mikononi, akaruka samasoti akatua na kuiokota ile AK 47, akaitekenya na wawili walikuwa chini wakitupwa hewani na kugalagala wakigombania roho zao.

“Uwiiiiii! Mi nilisema, nilisema mimi!” mmoja akapiga kelele huku akikimbia kupanda ngazi za kutokea juu, lakini mara naye akarudishwa ndani kwa risasi, akajibwaga chali katika sakafu isiyokwisha.

Kamanda Amata akashangaa, alipotazama juu akaona vivuli vya watu vikiteremka katika ile ngazi, akajibana nyuma ya nguzo akiwa anatweta.

“Kamanda Amata!” ile sauti ikaita, mara moja aliitambua sauti ya Chiba.

“Chiba!” Naye akajibu huku akishusha bunduki yake na kutoka nyuma ya nguzo, hakumaliza hata hatua mbili, alihisi kitu cha moto kikipita katika mkono wake, ilikuwa ni risasi iliyopigwa kutoka nyuma na mtu mmoja aliyebwagwa hapo kwa kipigo. Kamanda aligeuka akiwa na maumivu lakini kabla hajafanya lolote risasi ilipenya katikati ya paji la uso la yule kijana huyo na kufumua sehemu ya nyuma ya kichwa chake.

Kamanda alipogeuka mbele alikuta bastola ya Scoba ikiwa bado imekamatwa barabara mkononi mwake.

“Asante Scoba, Gina hali yake ni mbaya, tumsaidie,” akawaambia na mara wakaweka silaha zao vyema lakini Scoba alibaki kasimama na bunduki mkononi kuhakikisha ulinzi.

“Tufanye haraka kabla polisi hawajafika,” Chiba alieleza. Pamoja na jeraha mkononi mwa Kamanda Amata lakini alijitahidi kusaidia na Chiba akambeba Gina mabegani mwake.

Scoba alikuwa wa mwisho kutoka katika ile nyumba pale Upanga, wakaliendea gari na kuingia kisha Scoba akabonyeza kitufe fulani na mlipuko mkubwa ukatokea kwenye ile nyumba, akaiondoa gari eneo hilo na kuacha kelele za wafanya biashara zikiita ‘Majambazi, Majambazi’

***

“Haujaumia sana Kamanda, risasi haijagonga mfupa, imejeruhi nyama tu,” Jasmine alimtia moyo Kamanda huku akiendelea kumshona jeraha lake.

“Ndani ya saa 24 lazima watu hawa wawe mikononi mwetu ama marehemu au wazima,” kamanda alikuwa akiongea huku akionekana kuwa na hasira sana juu ya adui zake.

Gina alikuwa amelazwa juu ya kitanda, chupa ya maji ikiwa juu ya linga, alikuwa na bendeji kiasi usoni na nyingine mkononi, alikuwa macho na alikuwa anaelewa kila kitu.

“Kamanda upumzike, tutafanya kazi ya kuwanasa sisi tuliobaki,” Chiba alimwambia Amata.

“Hapana, nasema hapana, nichome ganzi tafadhali, nataka kuingia katika mapambano, mpaka nijue mwisho wao au mwisho wangu,” Kamanda aliongea kwa hasira.

  • §§§§

Madam S alisimama mbele ya Amata aliyekuwa sasa ameketi, akijaribu kuvuta akili na kuyapitia matukio.

“Kamanda,” akaita kwa upole, “unajisikiaje sasa?”

“Najisikia hasira Madam,” akajibu huku akigeuka, alionekana wazi mwili wake umejeruhiwa.

“Upumzike,” Madama akamsihi.

“No! hiyo haipo kwenye kamusi yangu, kumbuka adui ataona kambi yake imefumuliwa je atakaa hapa? Nikipumzika mpaka nipate nguvu tayari atakua London,” Kamanda akaeleza. Madam S akajifuta uso wake kwa viganja vya mikono, “Gina, anaendeleaje?” akauliza.

“Kaondolewa kapelekwa Shamba kwa matibabu zaidi, Gina amepigwa sana, ameumia sana,” Kamanda akajibu huku akiinuka, akasimama sambamba na Madam S, “sikia Madam, naongea kwa sauti ya chini, kuna mkakati mzito unaoendelea, hawa jamaa wametumwa kuondoa roho ya Mkuu wan chi, that is it!” akamtazama Madam.

“Ndiyo, lakini hatujajua kwa nini mpaka sasa wanataka kutekeleza hilo,” Madam akaongeze huku akimpita Kamanda na kukivuta kiti chake, akaketi na kuegemea meza, “Keti Kamanda!” akamwambia.

“Hii ni kitu nzito Kamanda, ni ya siri na ni nzito, sana lazima ishughulikiwe kikamilifu. Kwanza tushughulike na hawa waliokuja, tukiwatia mkononi wao sasa watatuambia nani aliyewatuma, hao sasa tutawafanyia kazi baadae kwa siri,” Madam akamwambia Kamanda.

“Ndio, lazima tukate mpaka shina sio matawi tu,” Kamanda akaongeza, “Mheshimiwa Rais anaendeleaje na afya yake?”

“Alipata mshtuko, sasa yuko sawa, na kesho ataongea na waandishi wa habari asubuhi saa nne palepale Ikulu, kuhusu hali halisi ya yaliyotokea, moja la kudunguliwa msafara wake na pili la kuibwa kwa almasi,” Madam akajibu.

“Hapana, sio wakati sahihi wa kufanya hivyo, Mheshimiwa hasijitokeze hadharani, akijitokeza anaweza kuwa amejianika wazi mbele ya muuaji,” kamanda akamwambia Madam.

“Amata, nimemwambia hayo, lakini inaonekana kuna kitu anaficha, sasa hii ni hatari kwa usalama wa nchi, sisi tunamlinda wakati mwingine inabidi atusikilize, ila safari hii amelazimisha kuongea na waandishi,” Madam akaeleza huku akipigapiga meza.

“Nimekuelewa, wacha iwe!”

Akanyanyuka kitini na kujitazama huku na huku, “naondoka Madam,” akarudisha mlango na kushuka ngazi taratibu, akaingia kwenye gari moja wapo ya ofisi na kutoka eneo hilo.

Simu ya kwenye gari ikaanza kuita, akainyakua na kuiweka sikioni.

“…Uwe mwangalifu we mtoto bado nakuhitaji,” Madam akamwambia. Kamanda Amata akaongeza kasi ya gari akaiacha barabara ya Ohio na kukamata ile ya Ally Hassna Mwinyi, akapita daraja la Surrender na kupinda kushoto mpaka nyumbani kwake Kinondoni. Akaegesha gari karibu na baa ya jirani. Akateremka na kuiendea nyumba yake. Alipoufikia mlango tu, akasita kidogo, kwa akili ya harakaharaka akajua nyumba yake imeingiliwa, akaichomoa bastola yake kutoka kwenye soksi, akaiweka tayari, akafungua mlango taratibu akaingia ndani kwa kunyata, kila alipotazama palipekuliwa, lakini hakukuwa na dalili yoyote ya mtu, akafungua chumba chake na kukuta hali ni hiyohiyo, kila kitu shaghalabaghala, akajua kwa vyovyote kulikuwa na purukushani. Akaenda mahali anapoficha zana zake za kazi na kabrasha za muhimu. Ni picha kubwa ya ukutani, akaibofya upande mmoja, ikaachia na kuteremka, akabonyeza tarakimu fulani na mahala hapo pakafunguka, akatazama kila kitu kipo sawa. Akapaacha na kwenda kwenye chumba chake cha siri ambako huficha kompyuta  yake inayoweza kuona kila kitu kinachotukia umo ndani ikisaidiwa na vijikamera vidogo vidogo zilivyofungwa katika kona tofauti. Akafungua mlango na kujifungia ndani.

Ni chumba kidogo ambacho mlango wake kwa upande wa nje ni kabati lililoja viatu na makorokoro yasiyo na maana. Akawasha kompyuta hiyo iliyo mezani. Akarudisha nyuma matukio mpaka alipoona tukio lililotukia, akaanza kutazama.

Kwanza aliona mlango ukifunguliwa, Gina akaingia na kuita, kisha akaingia katika chumba cha Kamanda, akiendelea kuita. Hapo Kamanda akajua bila shaka Gina alikamatiwa hapo nyumbani kwake. Mara akaona kwenye ile picha mlango ukifunguliwa na watu watatu wakiingia, wakamvamia Gina kule chumbani. Gina akapigana nao kwa nguvu zote, akawaumiza vibaya mpaka ikabidi watumia kitu kizito kumpiga kichwani akazimia, wakambeba na kuondoka naye.

Kamanda Amata akashusha pumzi ndefu. Akainuka na kutoka ndani ya kile chumba, akaingia chumbani mwake na kuoga kisha akajilaza kwa dakika kadhaa akisubiri muda muafaka wa msako, lakini kichwani alijiuliza aanzie wapi, hakupata pengine zaidi ya Motel Agip.

Muda ulipotimu, akajianda kwa mavazi ya kazi, akachukua silaha zake muhimu na kuzitia kwenye kona mbalimbali za nguo yake, kisha bastola moja akaitupa kitandani na kuilalia kwa mgongo, yeye akiwa chali. Kichwa chake kilikuwa kikipanga na kupangua.

***

Mc Field aliikusanya mikono yake kifuani, kichwa kilikuwa kikimzunguka, hakujua nini anapaswa kufanya. Hata alichokuwa anakiangalia hapo dirishani hakukielewa, ndipo alipokumbuka kuwa hata hajarudi hotelini kwake. Akashusha mikono yake na kugeuka kumtazama Tracy aliyekuwa katingwa na kompyuta yake ndogo.

“Tracy,” akaita, Tracy akainua uso, “umeona kazi ilivyo nzito ee? Yule ndiyo Kamanda Amata, katorokaje pale, hawa ndio TSA, wanatisha,” akamwambia.

“Na sasa tunafanyaje, maana tumeambiwa tuwadhibiti hawa ndio tutimize lengo letu,” Tracy akajibu, “Lazima wameokolewa, uwezo wa huyo Kamanda sijui Amata ni mdogo sana, hawezi kunitisha mimi,” akajigamba.

“Ok sasa tunabadilisha program,” Mc Field akamwambia Tracy.

“Enhe, tunafanyaje, maana mimi haya mengine siyajui, mi nataka kumaliza kazi yangu tu niondoke,” Tracy akadakia na kuifunga kompyuta yake. Mc Field akachomoa kipande cha gazeti moja la kiingereza, akamtupia mezani. ‘Rais kulihutubia Taifa’, ilikuwa ni habari iliyopewa uzito wa juu mbele ya gazeti hilo, akaisoma habari hiyo na kukiweka mezani.

“Asante Mc Field, kesho naenda kumaliza kazi yangu, naomba niandalie usafiri wa kuondokea tafadhali, maana hiyo ndiyo kazi yako,” Tracy akasema huku akijifunga nywele zake vizuri.

“Hilo lisikuumize kichwa, nitanunua tiketi usiku huu huu, nafikiri kutoka hapa tuondoke na ndege ya kukodi mpaka Nairobi kisha pale wewe utachukua ndege na mimi nitarudi kwa kutumia usafiri wa barabara. Uzuri wa ndege ya kukodi unachagua muda wa wewe kuondoka, kwa hiyo, ukimaliza kazi, mara moja nitakutorosha, hilo niachie mimi,” Mc Field akamtoa hofu Tracy.

“Sawa, kama mambo yakienda sawa basi kesho saa tatu hivi tayari bendera zao zitakuwa nusu mlingoti, huwa sibahatishi kabisa,” Tracy alisimama na kuagana na Mc Field.

“Sasa mpango wote mimi nitaupabga usiku huu, wewe relax maliza kazi na mi nitakuwa pale tayari kukuondoa salama,” MC Field alipokwisha kusema hayo akatoka katika hotel ya Land Mark na kuchukua gari ileile anayoitumia ,TX, akaondoka zake.

Tracy alisogelea kabati la nguo katika chumba cha hoteli hiyo, akavuta kijibegi chake na kukitupia mezani, akakifungua katika mfuko wa pembeni kabisa kuangali kama zana zake zipo, naam zote zilikuwepo, zimetulia tuli kama alivyoziweka.

“You have got a job,” akazinong’oneza. Kisha akaufunga na kuurudisha mahala pake. Akaitazama saa yake mkononi ikamwambia ni saa nne za usiku.

***

Gina alijisikia vizuri kiasi chini ya matibabu ya hali ya juu kutoka kwa Dr. Jasmine, aliweza hata kusimama na kutembea kidogo japo alilalamika kuwa kichwa ni kizito sana. Kila mtu alifurahi.

“Walinipiga kichwani kama si rungu basi gongo kubwa sana, niliona sayari zote tisa kisha giza,” akamweleza Jasmine, “Kamanda Amata yuko wapi?” akahoji.

“Yupo, yeye ni mzima na sasa yupo kazini kama kawaida,” Jasmine akamjibu.

“Dr Jasmine, wale jamaa ni wauaji, naomba nikamsaidie Kamanda, atakuwa matatani sasa,” Gina alikuwa akiongea kama anayeweweseka.

“Hapana, we ni mgonjwa bado, pumzika kwanza,” Jasmine alimshika mkono na kumlaza kitandani kisha akamchoma sindano ya usingizi ili apate kumpumzisha mwili wake, Gina akalala fofofo.

Simu ya mezani ikaita kwa fujo, Dr. Jasmine akaiwahi na kuiweka sikioni.

“Hello!”

“Yeah, unaongea na Kamanda Amata, Chiba yuko wapi? (…) mwambie afanye juu chini anione usiku huu nina shida naye nyeti sana”.

“Umesomeka Kamanda,” Dr Jasmine akajibu na kukata simu.

***

CLUB BILICANAS – saa 6:23 usiku

KULIKUWA NA WATU WENGI kila kona ya jumba hili la starehe, jumba linalotikisa jiji zima la Dar es salaam kwa umaarufu wake. Wavulana wa kisasa na wadada wao walijazana, wanaocheza disco twende wanaovuta sigara au bangi sawa tu, wanaouza miili wakiwa nusu uchi kila kona walikuwa wakijivinjari kutega mawindo yao. Hapa ndio palikuwa mahala pa kila uovu, wapo waliokuwa wakipanga mbinu za kuvunja, kutia mimba, kutoa mimba na kila jambo lilizungumziwa humo.

Akiwa ndani ya suruali yake ya cadet nyeusi, fulana nyeusi na kizibao cheusi juu ambacho ndani yake kilisheheni zana za kijasusi za kuua na kutoa pumzi za watu, kwenye soksi zake akiwa kabana bastola mbili, moja huku na nyingine kule, akapanda juu ya kiti kimoja kirefu, kati ya viti vingi vilivyokuwa hapo mbele ya kaunta hiyo kubwa ya kisasa, akiangalia kushoto, na kulia kila mmoja alikuwa na kinywaji kizito mkononi mwake, ama akinywa yeye au akimnywesha binti aliyekuwa naye hapo, kisha wanapigana mabusu. Akawatazama kwa wote kwa tuo, akawaona jinsi walivyo safi, hakuna mwenye mawaa yoyote zaidi ya funguo za gari mfukoni au sarafu za mia mia na mia mbili mia mbili, akatabasamu, akaishusha miwani yake na kuiweka kwenye mfuko wa kile kizibao, kisha akatoa kofia pama yake iliyokunjwa huku na kule kama ya Marlboro, mandevu yake yalimfanya aonekane kama jambazi sugu. Kila mtu alimgwaya kwa mawazo kama si kukaa mbali naye.

Kama kawaida ya warembo, mmoja akajipitishapitisha ili apate chochote kwa mtu huyo, lakini kama angejua kuwa mtu mwenyewe kaja kwa kazi zake asingepoteza muda.

“Unataka nini?”kamwuliza yule binti.

Binti akamtazama usoni mtu huyo na kumrembulia macho.

“Sihitaji hiyo biashara, chukua unachokunywa upotee,” yule mtu akamwambia yule binti, kisha akageukia kaunta.

Nipe Tonic Water na Konyagi ndogo, usisahau vipande vya barafu,” akaagiza, na kinywaji kikaletwa.

Mara akahisi anaguswaguswa mgongoni, akaelewa maana yake nini, akainua glass na kujimiminia kinywani, kisha akateremka na kuacha vinywaji pale kaunta na noti ya elfu kumi, akamfuata huyo aliyemgusa. Wakatoka pamoja mpaka nje. Wakaingia kati kichochoro kimoja.

“Kamanda! Hata mimi sikukujua,” Chiba alizungumza.

“Kawaida tu, leo nina kazi kubwa kaka, nataka uwe nami,” Kamanda Amata akamwambia Chiba.

“Usijali nipo jirani yako,” akaingiza mkono katika kimkoba chake, akatoa bastola moja nyeusi safi kabisa, ukiitazama unaweza kusema ni ya plastiki. Kamanda akaitazama, akatikisa kichwa.

“Ya Kirussia,” akatamka.

“Ndiyo, lakini nimekaa chini nikaimodifai tena, sasa ni ya Kitanzania,” aliposema hayo Chiba waote wakacheka, “tazama hapa,” akashika katikati mahala kwenye tumbo panapojaa risasi kabla hazijafyatuliwa, akapazungusha kwa namna yake na kufyatua kitu kama pini akakiamishia mahala pengine lakini vyote hivyo alivifanya kwa mkono mmoja.

“Ukishaweka hapa, Kamanda, Umejiua!” akamwambia. Kamanda Amata akaitazama na kujaribu kufanya vile alivyoambiwa, “safi sana Chiba, tunajivunia kuwa na mtu kama wewe.” Akaipachika ile bastola katika kizibao chake.

***

Majira kama ya saa saba hivi, Amata alikuwa akiambaa ambaa na korido za maduka na maofisi, akaufuata mtaa wa Samora na kuipita picha ya Askari akaikuta barabara ya Pamba na kukunja kulia, kisha akaingia kwa ndani kidogo akapita kituo cha mafuta na kuibukia katika ukuta wa hoteli anayoitaka, Motel ya Agip.

Kama mwenyeji, aliingilia mlango wa nyuma ambao hutumika na watu wa usafi kuingilia ndani, akapenyapenya  mpaka alipoukuta mlango wa pili akautikisa umefungwa, akachukua funguo zake na kuchezesha kidogo tu, mlango ukakubali, alipoufungua ili apite, kulikuwa na watu wanatokea upande huo, akaurudishia na kujibana nyuma yake. Walipopita naye akafuata, viatu vyake havikufanya kelele hata kidogo, akazikwea ngazi mpaka mlango namba 206. Akasimama kwa sekunde kadhaa, akatzama huku na huko, hakuna mtu, zaidi ni miungurumo ya mashine za kupoza hewa zilizokuwa zikiunguruma ndani ya vyumba hivyo, ukiacha hiyo ni sauti za watu walio kwenyea raha zao, wakipiga kelela za malalamiko ya raha. Akachukua kamera ndogo yenye umbo ka waya na akaipenyeza kwenye tundu la ufunguo mpaka upande wa pili, akapiga picha na kuitoa, akachomeka katika simu yake na kutazama, ndani kote ni salama, hakuna mtu. Akairudisha, akatia funguo na kuufungua mlango na kuingia ndani. Alipohakikisha kila kitu kipo sawa, na usalama wa kutosha, akavuta kiti akaketi nyuma ya mlango akitazama kitandani, pembeni akajiwekea pombe kali akinywa.

Mwanga hafifu ulikuwa ukimulika ndani ya chumba hicho, akiwa kajibana nyuma ya mlango kwenye kiti kidogo, akachomoa bastola yake kwenye soksi, akaiweka chini sakafuni kisha kwenye kizibao chake akatoa kiwambo cha sauti akaichukua ile bastola na kuifunga barabara ili isilete kelele itakapokuwa kazini. Akaitazama saa yake, inakimbilia saa nane usiku.

Mara akasikia sauti ya viatu ikija upande huo kutoka kwenye korido upande wa nje, akaiinua bastola yake na kuiweka tayari, lakini akili yake ilitambua kuwa sauti ya viatu hivyo ni kama vya kike na pia mwendo akautambua kuwa ni wa kike, akasubiri aone maana alijua wazi kuwa Mc Field ana uwezo wa kujifanya hata Mwanamke ili tu atimize lengo lake.

“Ulinitoroka kipindi kile leo huchomoki,” akajisemea huku akijikuta hasira zikimtawala taratibu. Mara funguo ikapachikwa katika tundu lake, ikafungua mlango, Kamanda Amata akatulia kungoja kuona nani anayeingia.

Mwanamke, aliyeonekana kama Mwarabu, mweupe, mrefu kiasi, mikononi alikuwa na mkoba, vazi jeusi linalometemeta lilikuwa limefunika mwili wake juu kabisa ya mapaja na kuishia juu kidogo ya matiti. Kamanda Amata akameza mate, kisha akalegeza mkono ulioshika bastola yake. Yule Mwanamke akaiendea swichi, alipotaka tu kuwasha, akashangaa taa ile inawaka sekunde mbili kabla yeye hajawasha, akashtuka. Mara akasikia kitu kama glass ikiwekwa mezani, akageuka na kukutana uso kwa uso na domo la bastola ya Amata. Mwanamke yule akaanza kutetemeka.

“Usiniue nakusihi!” aliongea kwa sauti ya woga na kubembeleza.

“Huwa siui warembo kama wewe, jibu maswali yangu mawili tu,” Kamanda akamwambia huku akiweka sawa kofia yake aina ya pama kichwani, “wewe ni nani?”

“Aaaa! Aaaa! mimi naitwa Amba,” akajibu, lakini lafudhi yake ilionesha kabisa kuwa hakuwa Mtazania.

“Swali la nyongeza kabla ya la pili, unatokea wapi na unafanya nini hapa?” akamuuliza.

“Mimi natokea Afrika ya Kusini, nipo Tanzania kwa miaka miwili sasa, nafanya kazi Las Vegas Cassino, huyu ni mteja wangu tangu afike hapa miezi mine ilopita, huwa nakuja kumstarehesha kwa ujira mnono, nafikiri umenielewa, niache niende,” akajibu haraka haraka huku akirudishia viatu vyake miguuni tayari kuondoka.

Amata akamuoneshea ishara ya kuwa hawezi kuondoka.

“Swali la pili, mteja wako yuko wapi?” akamhoji tena.

“Anakuja, amesema kuna kazi anamalizia kufanya lakini anakuja akanambia mimi nitangulie huku anikute,” akajibu kwa ufasaha.

“Good girl, sasa huwezi kuondoka, panda kitandani umsubiri mteja wako, tena tulia kimya, lete mkoba wako hapa,” akamwamuru, yule Mwanamke akaupeleka mkoba, Kamanda akaukagua ndani, akakuta vipodozi, simu, pedi, helleni, pete ya dhahabu na mikufu, bangili za kisasa, kitita cha pesa za kigeni na funguo za gari.

“Ok,” akauweka ule mkoba chini huku mkononi akiwa kabaki na simu ya yule Mwanamke, “Msubiri mteja wako kama ulivyopanga kumsubiri,” akamwambia. Lakini yule Mwanamke akabaki haelewi anachoambiwa.

“Huelewi? Vua nguo zako panda kitandani jifunike umsubiri, mi sina shida na wewe nina shida na mteja wako ambaye hata mimi ni mteja wangu vilevile,” akamwambia. Yule mwanamke akavua kigauni chake, akabaki na sidiria nyeusi, na chupi mchinjo ya rangi hiyo hiyo. Akavua sidiria, lo, Amata akaona akili ikimwenda mbio maana titi zilizojaa vizuri zilikipendezesha kifua chake, wekundu wake uliweza kumfanya Mwanaume yeyote rijali apate shida katika suruali yake, akaondoa na ile chupi akabaki kama alivyo, Kamanda Amata alilisanifu umbo mwororo la Amba. Yule Mwanamke akapanda kitandani na kuvuta shuka mpaka kidevuni, Amata akazima taa.

***

Majira ya saa tisa usiku, Kamanda Amata alihisi mlango ukitikisika, mara ukafunguliwa kwa kasi kwa minajiri ya kumbamiza pale alipo. Mc Field aliingia haraka bastola mkononi na kuwahi kutazama nyuma ya mlango, hamna mtu, isipokuwa chupa ya pombe na bastola.

“Shiit!” akashangaa na kutamka kwa sauti ya chini. Wakati huo Amba nae alikuwa amekurupuka kwa kishindo kile.

“Tulia vivyohivyo, umeingia mikononi mwangu tena,” Sauti ya Kamanda ilisikika nyuma yake.

Kumbe Kamanda Amata baada ya kuhakikisha kuwa Amba amepitiwa na usingizi alitoka pale alipo na kujificha bafuni akiwa amejua wazi hila za adui wake kwani alishajua kwa vyovyote huko aliko anafuatilia mazungumzo yake na mwanamke huyo, na alijua kwa vyovyote atajua ni wapi alipokaa kutokana na vyombo vyake vya mawasiliano jinsi alivyoviunganisha. Mc Field alijikuta hana ujanja, amewahiwa, akataka kugeuka kumtazama mtu huyo.

“Tulia, weka bastola yako chini. No! No! usiiname irushe chini,” akamwambia, maana alijua kujitikisa kidogo mtu huyo anaweza kuleta madhara makubwa, “safi sana, umekuwa kijana mpole sana siku hizi na si mtukutu kama zamani,” maneno hayo ya dharau yalimtia hasira Mc Field. Alitamani amrukie Amata lakini alijikuta hana ujanja, alibakiwa na mbinu moja tu na alikuwa akitafuta jinsi ya kuitumia.

“Geuka, mikono yako ikiwa juu,” akamwamuru. Mc Field akageuka.

“Ha ha ha ha leo una sura ya Kihindi, hivi wewe kwa nini umekuwa mwoga namna hiyo siku hizi? Umeanza kuzeeka ee? Basi leo ndiyo mwisho wako, roho yako nitaitia kwenye mfuko wa ruruali yangu. Nani amekutuma kuja huku tena? Kufanya nini?” akamtupia maswali baada ya kumkejeli.

“Hilo hupaswi kujua mbwa mweusi kama wewe, waume zenu wanaowalisha ndiyo walionituma, nimetumwa kuua, kukuua wewe!” alipojibu tu, akashusha mkono haraka, Kamanda Amata alikuwa keshaona hiyo, aljirusha akabiringita upande wa pili wa chumba, risasi nyembaba ikapiga kwenye kabati la vioo likatawanyika. Amata akajinyanyua haraka, alipotulia tu, ngumi kali ya Mc Field ikatua shavuni, ya pili ikadakwa sawia.

Amba alikurupuka kutoka pale kitandani akajikunyata kwenye kona ya chumba. George Mc Field akatumia kichwa kumpiga Amata, Amata akamwachia ule mkono, akayumba na kuanguka chini, akajibamiza ukutani, akamwona Mc Field akimjia na kisu mkononi, akavuta stuli ndogo na kuirusha kwa mikono ikampiga Mc Field usoni, kisu kikamtoka mkononi. Kamanda akanyanyuka, akapiga round kick, miguu yake ikamchapa Mc Field sawia kichwani ikampeleka mpaka kitandani. Mc Field akajirusha upande wa pili wa kitanda kulikuwa na ua la plastic lililowekwa katika bilauri kubwa la kioo, akaliinua na kwa kutumia mkono wake wa kulia uliojaa vizuri akalirusha kwa Amata. Hakika kama angekuwa mtu wa kawaida bilauri lile lingemuumiza vibaya lakini Amata alilipiga kiustadi kwa mikono yake na likatawanyika vipande vipande, akamwona Mc Field hewani akija kama Mbogo aliyejeruhiwa, Amata akamuepa, jamaa akatua chini peke yake.

Mzungu huyo akatega mikono yake katika mtindo mahili wa kung fu kumkabili Amata, miguu yake aliipanga katika namna ya kupendeza na mikono yake ilizunguka taratibu ikionesha jisi pigo lijalo litakavyomaliza kazi. Usoni mwake tayari damu zilikuwa zikitiririka. Kamanda Amata naye akaweka mtindo mwingine wa Kung fu naye akasimama kwa namna yake kumkabili Mc Field, hakuna aliyetabasamu wala kucheka, kila mtu alikuwa na ‘pepo la mauti’.

Amba, alinyanyuka pale kwenye kona na kuiwahi bastola ya Mc Field iliyokuwa chini, Kamanda Amata akaona hilo, alipogeuka kidogo tu, maana alijua hatari inayokuja, alijikuta akipata mapigo matatu ya Kung fu ambayo hakuweza kuyakinga hata kidogo, maumivu makali yakalifikia bega lake akahisi kama limevunjika. Mc Field akaanza kumpelekea mashambulizi ya haraka haraka ambayo yalimpoteza kabisa Amata, akaanguka chini kama gunia la karanga, akajigeuza na kulala kifudifudi.

“Mwisho wako umefika, unafikiri kila mtu ni wa kuchezea, sasa leo Tanzania itakuomboleza wewe na Rais wako,” Mc Field alimwambia Amata kwa hasira huku akiuma meno, alikuwa akimsogelea taratibu pale alipo.

“Inuka, nikumalize, mbwa mweusi we! Akamkamata ukosi wa kizibao alichovaa na kumburuza, nitakuuwa kwa kukuchinja, nitatenganisha kichwa na kiwiliwili chako,” alimwambia huku akimburuza kumpeleka bafuni. Amata alikuwa hoi, mkono wake ulikuwa umevimba, damu zikimtoka upya kwenye jeraha lake, lakini hakuona haja ya kuuawa kikondoo. Aliukamata mguu wa Mc Fiel kwa mkono uliobaki, Mc Field akashtuka na kuinama kumtazama, kwa kutumia mkono uleule uliovimba alimdaka shati na kumvuta mpaka chini kisha akamshindilia konde zito la kwenye koromeo, Mc Field akalegea na kukohoa sana.

***

“Vipi?” Madam S aliuliza.

Chiba akamtazama kabla ya kumjibu, “saa kumi inakaribia,” akajibu. Scoba bado alikuwa kwenye usukani akiendesha taratibu.

“Gari ya Mc Field hii hapa maegeshoni,” Chiba akamwambia Madam.

“Kamanda yuko kwenye mtanange,” akamwambia Madam S huku akiweka bastola yake vyema, “nisubirini hapa,” akawaambia Scoba na Madam S.

Utulivu ulitawala katika mitaa ya katikati ya jiji, na hata katika Motel. Hata wahudumu wa mapokezi walionekana wanasinzia kwenye makochi wakiangalia TV, hakuna aliyejua wala kuhisi nini kinatukia muda huo ghorofa ya pili, ya jengo hilo. Maana mapambano ya watu wazima yalikuwa ni mapambano ya kimya kimya.

Madam S alikuwa na mawazo mengi sana usiku huo, maana alijiuliza maswali yasiyo na majibu, umri nao ulimfanya ashindwe kupata majibu ya haraka haraka. Alikuwa ametulia tuli katika gari kiti cha nyuma.

“Bora hata sikuwahi kuolewa!” akasema. Scoba akamtazama na kucheka, “kwa nini?” akamwuliza.

“Namna hii si ngeshaachika maana hata huyo mume angenipa talaka, saa tisa hii mwanamke niko nje sihudumii ndoa,” akaongea huku akicheka.

“Hivi Madam huna hata mtoto wa dawa?” Scoba akauliza.

“Ninao!” akajibu.

“Wangapi?”

“Watano,”

“Watano!” Chiba akashangaa.

“Ndiyo, watano, wa kike wawili na wa kiume watatu ila ni watukutu balaa, ndio wananifanya mi nisilale mpaka sasa,” akawajibu. Wote wakacheka kizungu bila kutoa sauti.

Chiba akiwa katika kujiandaa kuelekea katika ile motel, mara walisikia sauti ya kioo kinachovunjika na sekunde chache kitu kama jiwe au furushi kilitua juu ya gari moja iliyokuwa imeegesha upande mmoja wa motel hiyo.

“Nini ?” Madam akauliza. Akaivuta bastola yake na kuelekea kule alikoenda Chiba, Scoba alibaki nje ya gari akitazama lakini akiwa tayari kwa lolote.

***

Amata akatazama dirisha lililopasuka ambalo Mc Field alipita hapo baada ya kuchezea kichapo kikali.

Baada ya kumshindilia lile konde pale chini, Mc Field alijifanya bado ana uwezo mkubwa wa mapambano, ndipo alipojikurupua na kumbwaga Amata kando, lakini kabla hajajiweka sawa, alichezea karate kali zenye mapigo ya kifo kutoka kwa Amata kiasi kwamba aliona hawezi kujitetea hasa alipopigwa pigo kali na kuvunjwa mbavu tatu, aliamua kujiokoa kwa kujirusha dirishani lakini hali yake tayari ilikuwa mbaya.

Akarudisha macho kwa yule mrembo, Amba, “vaa nguo zako!” akamwambia huku akijitazama ule mkono uliovimba. Amba akavaa harakaharaka. Saa ya Kamanda Amata ikaanza kumfinya mkononi, akaingiza mkono kwenye moja ya mifuko ya kizibao chake na kutoa kifaa maalum cha mawasiliano.

“Yes!” akatamka.

“Tupo, tumefika!” ilikuwa sauti ya Madam S.

“Ok, kama unaweza panda 206 haraka uone cha kuona. Chiba hifadhi huo mwili kama hauna uhai,” akamaliza.

“We mwanamke, usipende kuwa na wapenzi usiowajua, angekuua huyu, ni jambazi,” Amata akamwambia Amba.

Mlango ukagongwa na Madam S akaingia.

“Pole Kamanda, naona mkono wako umepata shida,” Madam alisema.

“Ndio, nahisi kama mifupa imepishana,” akajibu.

“Scoba akuwahishe kwa Jasmine ukapate matibabu, hili la hapa niachie mimi na Chiba,” Madam akamwambia Amata.

“Sawa!” akajibu na kumtazama yule Amba, “twende huku,” akamwamuru huku moyoni akimmeza mate.

Madam S ndipo akagundua kuwa kuna mtu wa tatu mle ndani, akamtazama binti huyo kwa tuo, “nani huyu?” akauliza.

“Ah, wafanyabiashara hai,” Amata akajibu huku akimswaga nje Amba. Wakafika mahali pa mapokezi wakakutana na mhudumu wa hapo. Kamanda Amata akamatzama bila kuongea kitu.

“Unalala sana, unaweza kuvamiwa na kuuawa hivihivi!” akamwambia, “haya, sasa hakuna kupokea wageni kwenye hotel hii mpaka mpate kibali kingine cha serikali, tunaiweka chini ya uangalizi kwa masaa machache na kufanya ukaguzi wa chumba kwa chumba naomba uhakikishe wageni wote wasitoke kuanzia sasa,” Kamanda akatoa amri huku akimwonesha kitambulisho uinspekta wa polisi.

“Sawa, lakini ni swala la kumwambia meneja, maana wengine wana ndege alfajiri hii,” yule mhudumu akamwambia Amata.

“Mpigie simu meneja mwambie afike hapa haraka,” alipomalisa kusema hayo akaongoza nje, akamchukua Amba na kumtia kwenye gari.

***

“Ulifikiri safari hii utatoroka tena? Utafia hapa hapa,” alimwambia Mac Field aliyekuwa hoi na pingu mkononi ilhali mnyororo miguuni mwake.

“Mtie kwenye buti,” Kamanda akamwambia Scoba, Mc Field akatiwa kwenye buti ya gari, kisha yeye na Amata wakaingia ndani.

“Shamba,” akamwambia Scoba.

“Na huyu mwanamke?” akauliza.

“Hapana, huyu tunamtupa shimoni hapo mbele,” Amata akajibu na gari ikaondolewa, mtaa wa kwanza, wa pili.

“Simama hapa,” akamwambia Scoba kisha akamtazama Amba, “teremka, ondoka na usimsimulie mtu chochote ulichokiona,” akamwambia kisha akaketi vizuri. Amba akateremka na kukimbilia mitaani.

***

Gari ya Scoba ikaegeshwa vizuri mahala pake, Kamanda Amata akateremka na kufungua buti, wakamshusha Mc Field kisha wakamkokota na kumwingiza kwenye chumba kimoja kisicho na madirisha wala ndani hakikuwa na chochote isipokuwa sakafu na choo tu.

“Kaa humu, nakuja unijibu maswali yangu kabla sijakuua,” Kamanda akafunga mlango kwa namba maalumu.

Dr. Jasmin akampokea Kamanda na kumpa tiba zote zinazowezekana, akamfunga bendeji maalum mkononi na kumwekea kamba ya kuvalia shingoni.

Dakika arobaini na tano baadae, Madam S na Chiba waliwasili, wakiwa na begi moja na suitcase kubwa, wakaliweka mahali. Kisha likafunguliwa kila mtu akiwa anaona.

“Mnaona kazi hii?” Madam aliwaeleza vijana wake. Ndani ya begi hilo waligundua vitu vingi sana vinavyotumika kujibadili sura, dawa za kunenepesha kwa muda mfupi na kukondesha kwa muda mfupi, vitambulisho zaidi ya hamsini vya idara mbalimbali kilichowagusa zaidi ni kile cha dereva wa Rais, hati za safari za nchi mbalimbali, maburungutu ya Kitanzania na za kigeni, silaha za kila aina, bastola, viwambo vyake na silaha nyngi za kijasusi.

“Hii ni hatari sana,” Gina aliongea kwa sauti ya chini. Wote walibaki midomo wazi, begi hilo lilikuwa limetengenezwa kwa malighafi ambayo ukilipitisha kwenye mashine za ukaguzi zinazotumia x-rays itakuonesha tu ndani kuna nguo na vitabu hata kama ndani hamna kitu, na hii ilimfanya mtu huyu kuweza kupenya kwenye vizuizi vya viwanja vingi vya ndege.

“Kamleteni hapa!” Madam akatoa amri. Chiba na Scoba wakaenda kwenye kile chumba kumleta Mc Field, wakamkamata huku na huku na kwenda naye. Wakamtupa sakafuni na kuchomoa bastola zao, risasi ya kwanza ya Chiba ikapiga kanyagio la mguu wa Mc Field, yowe la maumivu likamtoka.

“Sasa tutuambie lengo zaidi la kuja hapa ni lipi, na nani kakutuma?” Kamanda Amata alimwuliza Mc Field aliyekuwa akigugumia kwa maumivu ya mguu wake pamoja na mbavu zake, hakujibu kitu.

Amata akamwendea pale chini, “hutaki kujibu sio? Niambie aliyekutuma na madhumuni yakuja hapa”. Badala ya kumjibu akamtemea mate usoni. Amata akashikwa na hasira, akampiga teke la kilo nyingi na jamaa akarudi chini chali, akatulia tuli huku povu likamtoka mdomoni.

Chiba akamuwahi na kumbana mashavu yake kwa vidole, maana alijuwa kuwa tayari mtu huyo anajiua kwa kidoge cha sumu. Hakuna aliyemwona wakati gani kameza kidonge hicho.

“Shiiit!” Chiba akapiga ukelele alipomwona mjinga huyo keshalegea na macho kumtoka, akawatzama wenzake waliokuwa kimya, “limejiua!” akasema.

“Awasalimie babu zake,” Madam S akasema.

 

 

 

11

ONTARIO – CANADA

WAKATI HUKU KWETU ILIKUWA ni alfajiri ya saa kumi kule kwao ilikuwa saa mbili usiku. Sir Robinson Quebec alikuwa akiweka sawa miwani yake akiwatazama wale washirika wake wa karibu sana katika sakata lao hilo. Kila mmoja likuwa na shauku ya kusikiliza nini kimejiri huko Afrika Mashariki.

“Usiku wa manane, ambapo kule ni asubuhi ya saa nne, ukurasa wa mwisho wa mkataba wetu na yule mheshimiwa utafungwa,” akawaambia.

Yule mjumbe mweusi naye akatoa taarifa yake, “Na pia alfajiri hii kutafanyika tukio lingine katika mgodi wa Tanzanite kule Mererani kwa kupata kasha zingine tano za madini hayo, kila kitu kipo sawa unasubiriwa muda tu”.

“Kwa ujumla tumepata ushindi kwa kutekeleza makubaliano ya mkataba wetu, upande mmoja umeshindwa na sisi tunatekeleza kile tulichokubaliana, hakuna wa kutulaumu, kama tulivyofanya Congo, Liberia, hivyo hivyo tu,” akaeleza yule mjumbe wa tatu.

Watu hawa watatu walikuwa ni matajiri sana huko ughaibuni, walifadhili nchi nyingi sana na kutengeneza Marais wengi sana hasa Afrika na Asia wakikuwezesha upate utawala na wao uwape sehemu ya mali asili ili wafaidi, kurudisha gaharama zao na kupata faida juu. Kwa jina lingine ni ‘King Makers’.

Walipanga kukutana siku hii ili kupiga mstari mwekundu kati yao na yule waliyemweka madarakani katika nchi ya Tanzania, kwa kuwa alikuwa amekiuka makubaliano. Waliketi hapo wakisubiri taarifa mbili, moja ni wizi mwingine wa madini huko Arusha Mererani, pili ni kifo cha mtu wao, mteja wao, Rais wa nchi. Kila mara walikuwa wakiangalia saa, masikio yao yakiwa makini kusubiri mngurumo wa simu iliyotegwa mezani hapo.

 

IKULU saa 4:00 asubuhi

NJE ya jengo la Ikulu, Makao Makuu ya Rais kulikuwa na watu wengi wakiwa kwenye viti na wengine wakiwa wamesimama hapa na pale. Walijulikana kuwa ni waandishi wa habari kwa kamera walizokuwa wamebeba mabegani mwao, wengine wakionekana kuandika hiki na kile. Bado katika lango kuu kulikuwa na wengine wanaongia, wakikaguliwa kila kona na vijana wa jeshi la polisi na askari kanzu waliowekwa hapo kuhakikisha ulinzi unakuwepo.

Watu wa televisheni nao walitega kamera zao hapa na pale ili kuhakikisha wanapata picha nzuri kadiri iwekanavyo, wakirekebisha vinasa sauti vyao na huku magari yao makubwa yenye mitambo ndani yake yakiwa tayari kupeleka maangazo hayo moja kwa moja kwa wananchi.

Huko majumbani nako kila mmoja alifanya kazi harakaharaka ili awahi kutazama au kusikiliza nini Rais wa nchi anataka kuliambia taifa. Na hali hii ilitokana na utata wa mambo makubwa mawili, kudunguliwa msafara wa Rais kule Bunju na wizi wa almasi uliofanyika Mwadui ukimhusisha Waziri wa Nisahati na Madini. Ilikuwa siku ya aina yake. Kila mtu aliisubiri saa nne na nusu ifike. Kwenye migahawa, mabaa, maofisini wote walikuwa tayari kusikiliza hotuba ile, na kila mmoja akisubiri jibu la maswali yake.

 

***

Kila mtu alikuwa tayari kajipanga kwa tukio hilo, hawakuwa na amani kabisa ijapokuwa Mc Field alikuwa tayari marehemu lakini bado hawakufanikiwa kumpata mshirika wake.

“Nina wasiwasi anaweza akafanya maajabu hapa,” Kamanda Amata akawaeleza wengine.

“Ndio, daima inabidi tuwe katika tahadhari,” Chiba akaongezea. Punde tu Madam S akawasili ofisini.

“Poleni najua mmenisubiri sana lakini foleni za jiji letu mnazijua na sote ni wahanga, haya bila kuchelewa, si mnajua Mkuu atahutubia asubuhi hii? Basi tujiweke tayari. Chiba kazi yako unaijua, hakikisha unakamata mawimbi yoyote ya sauti chochote katika maeneo hayo, hakikisha unakata mawimbi yote ya simu kilomita nne za mraba. Scoba utakuwa tayari kuratibu usafiri kama itahitajika, Gina unajisikiaje sasa?” Madam akakatisha maelekezo.

“Niko sawa Madam,” Gina akajibu.

“Ok, Gina na Kamanda nawarudisha katika kazi yenu, mtakuwa kwenye viwanja vya Ikulu kuangalia kila kinachoendelea, mimi nipo hapa wala sitoki, mawasiliano yasikatike mpaka itakapoamriwa. Chiba kumbuka usikate frequency tunayoitumia, sawa?” Madam akamaliza.

Wote wanne ukimuacha Jasmine ambaye alibaki ofisini na Madam, walichukuwa vifaa vyao vya mawasiliano na kupachika masikioni, wakajaribu vyote na Chiba akawapata sawia kabisa, wakabeba bastola na vifaa vingine muhimu katika kazi zao kadiri walivyoweza.

***

Taksi yenye rangi ya kijani, ilisimama karibu kabisa na lango la Ikulu, eneo ambalo liliandaliwa kwa waandishi wote kushuka hapo. Mwanamke mwenye shepu tamu kwa kuiona kwa macho aliteremka akiwa na video kamera kubwa mkononi mwake, akalifikia lango akasimamishwa kwa ukaguzi. Ndani ya chumba kidogo alikaguliwa na kuonekana yuko sawa hakuwa na silaha wala kitu chochote cha hatari. Kitambulisho chake kilionesha kuwa ni mwanahabari kutoka kituo kikubwa cha luninga duniani NBC. Akapita na kuungana na waandishi wengine.

Katikati ya kamera nyingi akaweka ile ya kwake na kuhakikisha amekwishaiweka sawa kwa kazi.

***

Saa nne na nusu kama ilivyopangwa, Rais wa Jamhuri alijitokeza na kukaribishwa kwa makofi baada ya kutoonekana kwa takribani siku tano.

Mbele ya jopo la waandishi na wanausalama, Rais alianza kutoa hotuba yake iliyojawa na maneno mazuri na matamu.

Tracy Tasha aliingiwa na wasiwasi, kila alipojaribu kumtafuta Mc Field hakumpata simuni, mpango waliopanga ilikuwa wakutane hapo, lakini alishangaa kutomuona swahiba wake, akajua kwa vyovyote atakuwa tayari katika kona aliyomwambia atamkuta. Kupitia kamera yake alikuwa akiitembeza kuangalia wote waliokuwa mbele, licha ya Rais na walinzi wake walioonekana kuwa makini katika kutazama huku na kule, alimwona mtu ambaye alimfanya moyo wake ulipuke.

Kamanda Amata alisimama pembeni kabisa mwa jukwaa kuu, akiwa na ile plasta yake kubwa mkononi na mkono huo kuuning’iniza shingoni, Tracy akatabasamu, akajua hapa hana mkono mmoja hawezi chochote. Akatazama na wengine wote akaona walivyojipanga na jinsi walivyojiweka bastola zao ndani ya makoti yao. Tracy alitazama tena kwa makini sana hali nzima ya usalama, akaangalia wapi na wakati gani ataweza kuifanya kazi yake, akakumbuka maelekezo ya Mc Field wapi pa kutokea pindi akikamilisha hilo.

***

Kamanda Amata, alitulia kama sanamu, macho yake yaliyofichwa kwa miwani nyeusi yalikuwa yakimtalii kila aliyekuwa mbele, ilikuwa ikipiga picha, ikivuta na kurudisha na kuhifadhi katika kadi sakima ndogo iliyokuwa imepachikwa katika kona moja ya miwani hiyo.

“Point one, ova!” Chiba akaita

“Point one, Clean, ova!” sauti ya Kamanda Amata ikajibu na wote wakaisikia vizuri.

“Point two, ova!”

“Point two, Clean, ova!” Gina akajibu kutoka juu dirishani ambapo aliweza kuwaona watu wote kwa chini.

Chiba alikuwa akiangalia kila tukio kupitia luninga zake ndogo ndani ya gari aliyoiegesha nje ya ukuta wa Ikulu, picha zote alizipata kupitia miwani ya Gina na Amata. Alikuwa akikamata mawimbi mbalimbali ya mawasiliano yaliyokuwa yakikatisha eneo hilo, alizima mawasiliano yote ya simu kilomita nne za mraba, aliweza kuchuja kila frequency inayokatiza usawa wake. Tracy aliiangalia saa yake mara kwa mara. Kitendo hicho kilimfanya Kamanda Amata kumuona na kumtambua, aliishika miwani yake na kumvuta karibu, picha yake haikuwa ngeni hata kidogo.

“Ground zero! Ground Zero! Ova!” akaita. Chiba akaipokea na kutazama kwenye kijiluninga chake, akaona sura ya Tracy Tasha akiwa nyuma ya kamera kubwa ya video.

“Roja, point one kazini, Ova!” Chiba akaita lakini ilikuwa ni kupeleka ujumbe.

“Copy, point one kazini, ova” Kamanda akajibu.

“Point two, stand by! Ova” Chiba akatoa ujumbe tena.

“Copy, point two standby, ova!” Gina akajibu, akashusha mkono chini na kuinua bunduki aina ya SR 25 iliyotengenezwa huko USA. Bunduki ya maana, maalumu kwa kudungua, ilibuniwa na Eugene Stoner yenye urefu wa inch 44.0. Gina aliipachika dirishani na kuweka jicho lake katika lensi iliyofungwa juu yake na kumwangalia vizuri yule mwanamke.

***

Tracy Tasha aligeuza kamera yake na kumtazama tena Kamanda Amata, hakumuona. Alihisi akili yake inaganda ghafla, alitazama kwa chati huku na kule lakini hakumuona Amata mahala aliposimama, akahisi kuchanganyikiwa. Hakuhitaji kupoteza muda, hakuona sababu ya hilo, aliigeuza kamera yake kwa Mheshimiwa Rais, akamweka vizuri katika kioo chake cha kuvuta, akakijaza kifua cha Mkuu huyo, kisha kidole chake chembamba kikabonyeza kitufe chekundu cha kuiruhusu kamera hiyo ianze kunasa picha. Kizaazaa.

Ni nukta ileile, Rais alitupwa hewani, walinzi wake walichanganyikiwa, wale wa nyuma walijitahidi kumdaka lakini wote sita wakarudi chini bila kipingamizi, wale wa mbele wakageuka mara moja, na kumwendea Mkuu, haraka sana tayari eneo lile likawa katika hali ya taharuki. Waandishi wa habari walihaha kupata picha ya hiki na kile, askari wa FFU waliingia na kuzingira eneo lile kujua nini kimetokea.

Tracy Tasha, alijishika kiuno katikati ya watu waliokuwa wakihaha huku na kule. Alikuwa akiangalia nini cha kufanya. Macho yake yalitazama juu ya jengo la ikulu na kujikuta akitazama na domo la SR 25, akajua pamenuka, akabinya kijitufe kingine kwenye ile kamera yake na yote ikalipuka na kutoa moshi mzito uliowafanya watu kuchanganyikiwa na kukohoa huku wengine wakitokwa na machozi yaliyochanganyika na kamasi jembamba.

Gina alitoa jicho lake katika lensi ya lile bunduki kwani alishachelewa kupiga, Tracy alipotea katikati ya ule moshi.

“Shiiit! Mwanaharamu wa kike,” Gina aling’aka alipojikuta kazidiwa kete na Tracy. Aliendelea kutazama kwa lenzi mtu mmoja baada ya mwingine huku kinywani mwake akiendelea kutukana matusi anayoyajua yeye mwenyewe.

Kamanda Amata alipata wakati mgumu, alikuwa akimfuatilia Tracy kwa utaratibu maalumu kabla hajafanya kile anachotaka kufanya, mara kizaazaa kilipoanza alijikuta akibabaika, hakujua amuendee Tracy au arudi kumsaidia mheshimiwa, ilikuwa ngumu. Lakini alipokuwa akitafakari hilo, ni nukta hiyohiyo aliposikia kishindo cha pili kilichozua mtafaruku, moshi mzito uliomfanya hata yeye achanganyikiwe ulizagaa.

“Point one, point one!” Chiba aliita.

“Hali tete, mheshimiwa kaangushwa!” kamanda Amata alijibu haraka.

“Man down!” Chiba alipigwa na butwaa.

“Ametoroka! Ametoweka!” Gina alipeleka ujumbe.

Kamanda Amata bastola mkononi, alihaha kutafuta huku na kule akiwa tayari ameweka miwani yake usoni ili kumtambua mtu huyo hakumuona.

***

Madam S alikurupuka katika kiti chake, “Jasmin, nifuate haraka chukua silaha!” akatoa amri nia Dr. Jasmine akafanya hivyo, hawakuwa na haja ya kutumia gari.

“Vipi Madam, kuna nini?” akauliza.

“Mkuu wa nchi amedunguliwa,” akajibu huku akimalizia kuchomeka bastola katika kiuno cha suruali yake ya suti. Wakatoka nje na kuvuka barabara, kizaa kilionekana, gari za polisi zilikuwa zikipiga ving’ora kwa fujo zikitanda katika njia zote, kila mtu aliye karibu na ukuta wa Ikulu aliondolewa na aliyetiliwa mashaka alitupiwa kwenye gari za polisi. Mitaa ilichafuka, kuanzia Hazina Ndogo mpaka Magogoni kuzunguka mpaka hospitali ya Ocean Road, kwa ujumla kila upande ulimwagwa askari wakipekuwa mpaka kwenye vichaka.

Madam S aliingia getini na kukuta kizaazaa bado kikiendelea, waandishi wote walikamatwa na kuwekwa mahala pamoja. Ilibidi kwa haraka lifanyike gwaride la utambuzi.

Kamanda Amata aliifuata gari ya polisi iliyokuja na mbwa, akamwomba askari mmoja ashuke na mbwa wake. Wakafuatana mpaka pale kwenye mabaki ya kamera ya Tracy, yule mbwa alinusa hapa na pale huku akitoa kilio chake cha ajabu, kisha akaanza kufuata uelekeo fulani, Kamanda na yule polisi walifuatana kumfuata mbwa huyo. Mbwa aliwaongoza mpaka kwenye ukuta, umbali wa mita kama 200 hivi kutoka eneo la tukio, kisha yule mbwa akasimama mahala na kuendelea kunusa hapa na pale bila kwenda popote.

***

Tracy alipoona tayari domo la SR 25 linamwelekea yeye alijuwa wazi kuwa sasa mambo yameharibika. Kamera yake ambayo ilikuwa na bunduki ndani yake yenye kubeba risasi tatu tu, pia ilifungwa mabomu mawili ya machozi, akayafyatua mara moja,  ikatawanyika vipande vipande. Tracy alijiangusha chini na kubiringita kisha akaibukia nyuma ya waandishi wa habari. Wakati watu wakiendelea kukohoa, na kutokwa machozi, Tracy alivuta hatua ndefu na kuufikia ukuta kisha bila hata kuugusa alijirusha sama soti akatua nje ya ukuta huo. Lakini alijikuta na wakati mgumu sana pale alipojua kuwa Mc Field alitakiwa kuwa hapo, hakuwepo. Akachanganyikiwa, hivyo ikabidi ajiokoe mwenyewe kwa nguvu zake, alivuka barabara ya Magogoni kwa haraka na kuingia katika Chuo cha Utumishi wa Umma, akiwa jirani na ofisi za chuo, alikutana na mwalimu mmoja wa kike, akamwita na kumwambia kuwa ana shida naye ofisini, wakaingia.

Tracy alitoka nje ya ofisi hiyo akiwa na mavazi ya yule mwalimu. Wakati wanafunzi na wafanyakazi wakikimbilia mbele ya jengo hilo kujua kulikoni, Tracy alipita katikati yao na kutokomea. Ving’ora vya polisi vilimchanganya kiasi Fulani, alishindwa upande gani aelekee, akapita jengo la kwanza na la pili, akaibukia nyuma, hakuona njia nyingine ya kutoroka, akaivuta hijab aliyoipata kutoka kwa yule Mwalimu, akajiweka vizuri kichwani mwake.

***

Kamanda Amata akiwa na mbwa wa Polisi, walizunguka nje ya ukuta na mbwa yule akaipata tena harufu ya Tracy na kuvuka barabara mpaka kwenye ofisi za Chuo cha Utumishi, walipoingia ofisini, walimkuta yule Mwalimu akiwa hana uhai, nguo zote za Tracy zikiwa pembeni, na yule Mwalimu alikuwa kama alivyo.

“Shiit! Katuweza, Mtuhumiwa ameruka kihunzi!” aliongea kwenye kinasa sauti chake.

“Lazima akamatwe!” Gina akajibu.

“Point one! Upande wa Mashariki tafadhali, kuna mtu anayejaribu kujipenyeza katika kundi la wachuuzi wa samaki akielekea upande tofauti na wengine wote,” Chiba alitoa hadhari hiyo, akiwa anakamata picha kutoka katika satellite.

“Point One kazini,” Kamanda akajibu.

“Point two, ongeza nguvu tafadhali,” Chiba akaomba.

“Point two kazini,” Gina akajibu.

“Ground zero…. Ground zero…” sauti ya Madam ilifika kwa wote, aliyekusudiwa akajibu.

“Nakusoma,” akajibu Chiba.

“Nipe dira yako!” akamwambia.

“Mashariki, soko la samaki, usawa wa bahari,”

“Copy!” Madam S akajibu.

***

Tracy, alijitahidi kupenya kwenye kundi la watu kwa minajiri ya kufika baharini, aliamini akifika tu baharini, kamanda na kikosi chake hawatamwona tena kwani mbinu za kutoroka kwa njia hiyo alikuwa akizijua vyema. Kila alipogeuka nyuma alimwona Kamanda Amata akimfuata kwa umakini wa hali ya juu huku mkononi mwake amekamata bastola ndogo sana.

“Hey! Stop!!” Kamanda alitoa amri lakini Tracy hakusimama. Kamanda Amata akpiga risasi hewani na watu wote wakatawanyika, wengine wakianguka chini na kukanyagana vibaya. Tracy akapata kipingamizi kipya, lakini bado hakuonesha udhaifu, alichomoa bastola yake, akageuka nyuma na kumfyatulia Amata, ambaye tayari aliliona hilo, Kamanda Amata akajitupa na kubingirita chini ile risasi ikamkosa na kujeruhi mwingine nyuma yake. Akanyanyuka haraka na kumtazama Tracy, hakumuona.

Akiwa na bastola yake mkononi, akatazama huku na huku.

“Point one, Chumba cha kuhifadhia Samaki,” Chiba akatoa maelekezo kwani alikuwa akiendelea kumfuatilia Tracy kwa mtandao.

“Point one kazini,” Kamanda akajibu huku akiingia katika chumba kikubwa kilichopangwa majokofu mengi makubwa makubwa.

Ukimya ulitawala, harufu ya samaki ilikijaza chumba hicho, kelele za pepezo za pangaboi zilisikika. Bastola mkononi, Amata alikuwa makini kupekuwa uchochoro mmoja baada ya mwingine.

***

Katika chumba cha siri kabisa, Rais aliteremshwa kwa lifti maalum na kuingizwa ndani ya chumba hicho chenye kila aina ya mtambo tiba kwa huduma ya kwanza. Akiwa na chupa ya maji iliyokuwa ikiendelea kuingia mwilini mwake, alikuwa kimya kayafumba macho yake. Wanausalama wa Ikulu walihaha huku na kule kujaribu kuokoa maisha yake kwa maana walijua wazi kuwa Taifa liko kwenye taharuki kwani hakuna cha kuficha, hotuba ile ilikuwa ikienda moja kwa moja hewani na watu waliitazama kwa televisheni. Walimlaza juu ya kitanda na wote wakasogea pembeni kutazama kinachoendelea maana mshangao na bumbuwazi ulikuwa dhahiri shahiri nyusoni mwao.

Ni siku moja ilikuwa imepita tangu Rais ajiimarishie ulinzi wake binafsi kwa kuifumua idara ya Usalama wa Taifa na jambo hilo linatokea, kila mtu alichanganyikiwa.

Ukimya ulichukua nafasi ya kila kitu katika chumba hicho, watu wachache wasiozidi watatu ukiachana na Daktari walikuwa wamebaki, wengine walitoka nje kuhakikisha mtuhumiwa anatiwa mkononi.

Polisi nao walizingira jengo lote la Ikulu na viunga vyake, barabara za kuingia na kutoka ziloikuwa zimefungwa haikuruhusiwa gari kuingia eneo hilo wala zilizo katika eneo hilo kutoka. Kila kona mbwa wa Polisi walifanya kazi ya kukagua kwa kunusa kila gari na kila mtu. Mbwa hao wenye mafunzo maalum waliweza kutambua harufu ya kitu chochote hatari hususan milipuko.

Madam S, aliingia katika chumba alichokuwa amelazwa Rais, akifuatana na Dr. Jasmine nyuma yake. Mlango mzito ukajirudisha nyuma yao, mlango uliotengenezwa kwa madini ya kutokuingiza risasi. Walimkuta Mheshimiwa amelala kimya kabisa kitandani, daktari akiwa kasimama pembeni.

“Vipi mbona hakuna tiba yoyote inayoendelea?” akauliza.

“Amenipa ishara nimuache,” yule daktari akajibu.

Kisha akamgeukia mtu wa kwanza  ambaye ni afisa usalama wa Taifa mwenye mamlaka yote ya juu kwa Rais. Yeye alikuwa amesimama pembeni mwa kitanda, “kinachoendelea?”

“Usafiri unaandaliwa na muda si mrefu tutaondoka kuelekea London kwa matibabu, “ akajibu. Madam S akasimama na kumtazama Mheshimiwa ambaye alikuwa kajilaza kwa utulivu na suti yake ileile ikiwa mwilini, damu nzito iliyoganda juu ya kifua chake ilitengeneza jeraha zito na la kutisha ambalo lilijificha nyuma ya au ndani ya suti hiyo.

***

Kamanda Amata alijikuta akipewa dhoruba kali ya mapigo ya karate yaliyodhamiria kuua, yakitokea nyuma yake, akayumba na kujiweka sawa, kisha akageuka nyuma na kukutana na mapigo mengine yaliyopigwa kiufundi, haraka haraka na yaliyomchanganya kupita kawaida.

Huyu mwanamke si wa kawaida, akawaza Amata wakati tayari yupo chini akijifuta damu iliyokuwa ikimtoka katika pachipachi za kinywa chake. Tracy akasimama sakafuni kwa mtindo wa kuvutia, akiwa tayari kwa mapigano na kijana huyo mtanashati. Wakati wanawake wenzake walikuwa wakitafuta nafasi ya kufanya nae mapenzi ili tu wajisifie, yeye alikuwa anatafuta nafasi ya kupigana naye. Kamanda Amata alijizoazoa pale chini, alihisi mkono wake kutonesheka tena. Tracy alijirusha kwa namna ya ajabu kwa minajiri ya kutua na shingo ya Amata lakini hapo ndipo alipopajutia. Amata alijitupa pembeni na Tracy akatua peke yake, alipomtazama Amata tayari alikuwa mbele yake; pigo moja la maana likapiga katikati ya sura yake nzuri, Tracy alishuhudia nyota nyingi mbele yake, kabla hajatulia pigo zito la pili likatua mbavuni, Tracy akajikuta analegea, hana la kujitetea. Pigo la tatu lililokuwa linalenga kutoboa tumbo la Tracy na kufumua takataka zote za tumboni, lilikingwa kiustadi sana. Tracy akaunyonga mkoni wa Amata ule ambao umefungwa bendeji ambao mwenyewe aliutumia bila kujali. Akaunyonga kwa nguvu, maumivu makali yakapenya kwenye mishipa ya Amata, akabana meno kwa maumivu hayo, alijifyatua na kupiga kichwa kimoja maridadi, Tracy alihisi kama jiwe limepiga kwenye mwamba wa pua, akamwacha Kamanda na kurudi nyuma, akasimama akihisi kama kitu kinatoka ndani ya pua yake, damu.

Tracy akawa kama mbogo aliyejeruhiwa, sasa alimkamia adui wake, akajiwekea yamini moyoni mwake, ama zangu ama zake. Aliruka na kutua juu ya moja ya jokofu kubwa akinuwia kushusha kipigo kwa Kamanda kutokea juu, lo, alicheza pata potea, kwani hilo adui yake alilitegemea baada ya kusoma macho ya mwanamke huyo kabla, aliunyanua mguu wake na kupiga ngwala moja safi iliyopita millimita chache juu ya jokofu hilo huku mguu mwingine bado ukiwa umesimama juu ya sakafu. Miguu ya Tracy ilitua na kukutana na mguu wa Kamanda Amata. Tracy alijikuta akirudishwa hewani sasa kwa mtindo wa kuangushwa vibaya lakini kwa ustadi wake na ufundi wa mapigano alijigeuza hewani mara ya pili na kupoteza lengo la Amata, akatua chini na kukutana na guu lenye nguvu lililotua kifuani mwake, akatupwa nyuma na kupiga mgongo kwenye jokofu. Alipokaza macho yake ambayo yalikuwa yakipoteza nuru, alimwona Amata bado akiwa kaweka mguu juu, hajaushusha chini.

Tracy alihema kwa nguvu, damu zikiendelea kumvuja puani.

“Umekamatika Tracy Tasha, muuaji mwenye taaluma, na wewe utauawa kitaalamu vile vile na amini usiamini utajiua mwenyewe,” Amata alimwambia kwa Kiingereza safi huku akishusha mguu wake chini.

“Si-we-zi ku-fa ki-ko-ndoo,” alijibu kwa lugha hiyo hiyo, lakini kwa shida sana, sauti yake ilikuwa ikimezwa na maumivu makali.

“Sasa utanyongwa Tanzania, Mzungu muuaji wewe, uliona haitoshi kumuua Khumalo, Touzony na sasa ukaamua kuja Afrika Mashariki? Basi aliyekutuma amekuuza, alijua wazi kuwa hapa ndiyo kaburi lako kama mwenzako Mc Field ambaye tangu jana tayari yuko motoni bila shaka na wewe anakusubiri kule ili mkamuue shetani kama mnaweza kuua,” Kamanda alimwambia Tracy.

Tracy alikunja sura baada ya kusikia kuwa Mc Field alikuwa tayari marehemu, mara picha ya karatasi ya mwili wa Mc Field ikadondoka mbele yake, akaiokota na kuitazama.

“Tunakufahamu sana, na tulikuwa tunakusubiri, Serikali ya Tanzania haiwezi kuangushwa na nguvu yenu vibaraka na sasa utanambia ni nani aliyekupa kazi ili naye nikamshughulikie hata akiwa na ulinzi wa namna gani,” Kamanda alimweleza.

“Maneno mengi hayavunji mfupa,” Tracy alijibu huku akiikunja ile picha na kuitia kinywani. Alifyatuka kutoka pale alipo na kushusha kipigo kizito kwa Kamanda Amata. Kasi aliyokuwa anaitumia Tracy kupeleka mapigo kwa mikono na miguu ilimshangaza Amata. Tangu alipoanza kupambana na watu wenye ujuzi mbalimbali huyu alikuwa tofauti. Amata alikuwa makini, alikinga mapigo yote kumi na nane na hakuna hata moja lililopata, pigo la mwisho Tracy alijinyoosha na kupiga msamba akiwa anakwepa teka kali la Amata ambalo lingetua ubavuni mwake basi bila shaka lingevunja mbavu za kutosha. Akajikuta akimkosa, akajirusha upande wa pili na Tracy aliyedha, aliyenuia kushusha pigo kwenye korodani alimkosa na kujikuta kabaki peke yake. Akanyanyuka harka na kukutana na konde zito la usoni, akapepesuka kidogo kabla hajatulia, konde la pili, la tatu, la nne, la tano, la sita, la saba, Tracy chali, sura ya urembo yote ilikuwa nyekundu.

Akajinyanyua tena haraka na kusaimama wima, akamfuata Amata kwa kasi. Mwenzake akamkwepa na kumtwisha konde la kilo nyingi lililotua tumboni, Tracy akaganda akiwa kajishika tumbo, damu ikimtoka kinywani na macho yakimtoka pima. Kamanda Amata alikuwa katulia palepale, akisubiri Tracy ajibwage chini maana alijua kwa kilo za ngumi hiyo hawezi kupona tena na akipona hatokufa tena.

***

Watu walikuwa wamejazana katika mlango mkubwa wa jengo hilo wakiangalia mapigano yale yaliyokuwa yakiendelea, walishangaa mwanamke huyo alivyokuwa akifanya minyumbuliko ya ajabu katika mpambano huo.

“Huyu atakuwa Cynthia Rothrock huyu!” mmoja akamwambia mwenzake, wengine wakacheka.

Mara ving’ora vya polisi vikasikika kuja eneo hilo, watu wakaanza kusogea nyuma.

“Eeeee wanoko haooo!!!” akasikika kijana mmoja mchuuzi wa samaki.

Gina akiwa na bastola mkononi, alikuwa akikimbia nyuma yake akifuatiwa na Chiba kisha polisi na maafisa wengine wa usalama wote walikuwa wakielekea huko.

Katika soko hilo la samaki kulikuwa ni mshike mshike, kila mmoja alitaka aone kinachotukia lakini gari ya FFU ilifika na kuwataka watu wote kusogea mbali na eneo.

***

Tracy Tasha bado alijiinamia mkono wake mmoja ukishika tumbo lake na mwingine ukiwa umeushika ule mkono wa Amata uliopiga ngumi, alitulia kwa sekunde chache, damu zikimtoka kinywani na puani.

“Nani boss wako? Nani kakutuma?” Kamanda akauliza.

Tracy hakuweza kuongea chochote, akajiachia kutoka katika mwili wa Kamanda na kuanguka chini, akiwa hana nguvu ya kufanya lolote. Amata akamtazama mrembo yule aliyelala kwa ubavu sakafuni, akamsukuma kwa mguu na kumuweka chali. Tracy akajiinua kwa tabu, akajivuta na kuegemea moja ya jokofu lililo hapo, akipumua kwa shida. Kamanda akachuchumaa akimwangalia usoni.

“Bado kidogo utakufa, kama ulivyoua wengine wote, lakini kabla hujafa, nani boss wako, nani unayemfanyia kazi hii?” akamwuliza.

“Rho-bin-son Que-be-bec!” akajibu kwa tabu kisha akamtemea Kamanda mate yaliyochanganyika na damu usoni.

“Huna maana kama mkia wa mbuzi, mwanamke hayawani kabisa! Kwa kuwa sina desturi ya kuua warembo kama wewe,” akachomoa bastola yake aliyokabidhiwa na Chiba jana yake, “shika hii, ina risasi mbili tu ndani, jiue mwenyewe!” akamshikisha kwenye kiganja chake. Kamanda Amata akasimama pembeni.

“Jiue mwenyewe, mi nasubiri hapa,” akamwambia. Tracy Tasha hakuwa na nguvu yoyote ya kufanya lolote. Kamanda Amata akageukia mlangoni na kuvuta hatua kuondoka eneo hilo wakati alipowaona Gina, Chiba na baadhi ya polisi wakiingia katika jengo lile.

“Pole sana Kamanda!” Gina alitoa pole huku akiipachika bastola yake kiunoni mwake, na kumwendea Amata.

“Pole Kamanda na hongera sana!” Chiba nae alitoa pongezi, lakini mara ghafla wote wakasimama na kutazama kwa mshangao kule alikokuwako mwanamke adui.

Tracy Tasha, alisimama wima, mkononi mwake akiwa na bastola inayomtazama Kamanda Amata kisogoni.

“Hautapata nafasi ya kujutia kosa ulilofanya, nimehakiki kuna risasi mbili, moja itakuua wewe na nyingine itanimaliza mimi,” Tracy aliongea kwa sauti ya kichovu. Kamanda Amata akasimama kimya, mara akasikia mlio wa kilinda usalama cha bastola hiyo kikiondolewa.

“Hah! Hah! Hah! Hah! Hah! mwili wangu hauwezi kuguswa ukiwa hai na ninyi watu weusi, hamna hadhi, na we huwtopata nafasi ya kujisifu kuwa umeniua na kuandika historia hiyo duniani katika duru za usalama, adios amigos,” Tracy aliendelea kusema huku shabaha yake ikiwa sawia.

Akapachika kidole kwenye kifyatulio na kufyatua bastola ile, bastola ikaruhusu risasi moja kutoka kuelekea kwa Kamanda Amata.

Trace alishangaa kuona bastola ile inapiga kinyume, risasi ilitokea upande wa nyuma na kupiga kifuani kwake, Tracy akatoa yowe la uchungu na kujibwaga chini, kifua chake kilikuwa kikivuja damu.

Kamanda Amata hakugeuka nyuma, “asante Chiba kwa teknolojia yako, nimekukubali,” akampigia salute na kisha akaondoka eneo hilo.

***

MADAM S alijikuta akiruka kwa furaha alipopata taarifa ya kifo cha Tracy Tasha, hakuweza kuvumilia. Akampa taarifa hiyo Dr. Jasmine ambaye naye alikuwa mwenye furaha sana kwa hilo.

“Unaweza kupona sasa Mheshimiwa Rais, adui zako tumewamaliza,” madam akamwambia  Rais aliyekuwa amelala kimya kitandani. Mara akainuka na kuketi.

“Asante sana Selina, uliloliota ndilo haswa lililotokea,” akaongea, kisha akavua shati lake kila mtu akashangaa isipokuwa Madam S. kifuani mwake alivua kitu cha plastiki chanye madonge ya damu ndani ya mapakiti, risasi moja kubwa ilikuwa imenasa katika dude hilo. Haikumdhuru, alikingwa, akalitoa na kulitupa pembeni.

“Naomba muwaambie waandishi wa habari, wasitoe habari yoyote zaidi ya kuwa Rais amedunguliwa basi, na hali yake ni mbaya, waandike hivyo hivyo,” maneno hayo alimwambia msemaji wa Ikulu naye akatoka na kwenda chumba maalumu ambako alionana na waandishi waliokuwepo.

“…kwa kifupi, kama mlivyoona, Rais ameshambuliwa, ameumia vibaya na hali yake ni mbaya, hivyo Ikulu itamsafirisha mchana huu kwenda London kwa matibabu, taarifa yoyote mpya mtapewa kutoka hapa tu, asanteni.” Msemaji wa Ikulu alimaliza mazungumzo yake, akanyanyuka. Waandishi wa habari waliokuwepo walianza kumgombania kumtupia maswali lakini aliondolewa mara moja na watu wa Usalama wa Taifa, mlango ukafungwa, na dakika hiyo hiyo gari maalumu ya wagonjwa ikawasili Ikulu, kama ilivyopangwa, akafungwa vizuri katika kitanda.

“Mchome sindano!” Madam S akamwambia daktari wa Rais. Naye akafanya hivyo na usingizi mzito ukamchukua.

Ni watu wasiozidi watano waliojua kuwa Rais ni mzima kabisa lakini wengine wote waliaminishwa hivyo kuwa Mheshimiwa ana hali mbaya.

Msafara wa gari za Ikulu ukaondoka kuelekea Uwanja wa Ndege.

***

“Kamanda Amata,” sauti iliita kutoka nyuma yake. Akageuka na kumwona Madam S akiwa na faili moja mkononi. Amata alikuwa amesimama katika sehemu ya mbele ya nyumba kubwa huko Gezaulole, mkono wake ukiwa na bandeji nyingine kubwa. Akageuka na kumtazama Madam S.

“Yes Mom,” akaitikia na kuitoa miwani yake usoni.

“Mheshimiwa Rais anakupongeza kwa kazi ulioifanya, anakubali sana uwepo wako hapa nchini na hususan katika idara nyeti kama hii, nimetoka kuzungumza naye sasa hivi, tumekubaliana jambo moja,” akamkabidhi lile faili ambalo juu yake lilikuwa limeandikwa Rhobinson Quebec na chini yake maandishi mazito ‘Wanted’, akatazama na kumwangalia Madam S.

“Roho yake tu wala hatumwitaji akiwa hai,” kisha akageuka na kuondoka.

 

 

12

SIKU TATU BAADAE

“Ooooh babe, you are so sweet hubby!” Lereti binti wa Khumalo alikuwa akilalamika kitandani, juu yake Kamanda Amata alikuwa akimfanyia manjonjo ya maana.

“Mmmh! Oooh yeah utainjoy sana mama!” akambembeleza.

“Again, please…” malalamiko yakaendelea, miguno ya mahaba ikachukua nafasi kila mtu alikuwa kazama katika dunia nyingine kabisa.  Amata alilihusudu umbo la Lereti kwa jinsi lilivyo katika katikati na kutengeneza nane, mapaja yaliyojaa vyema na kuzungukwa kwa nyama nzito na ngozi laini yalizidi kuupeleka mbio moyo wake.

“Hii ndio zawadi yangu kama nilivyokuahidi, na kwa nini hukunambia kama wewe ni mpelelezi  mashuhuri Afrika na Ulimwenguni?” Lereti akamwambia.

“Aaaaa hayo hapa si mahala pake mtoto mzuri,” akamjibu.

“Sasa roho yangu kwatuuuu!!! Umemuua yule hayawani aliyeniulia baba yangu kipenzi, sasa niue na mimi niue kimapenzi,” Lereti alibembeleza kimahaba, kwa sauti ya kitoto huku akichezea kifua cha dume hilo. Akamtazama usoni na kumyonya ulimi.

“Kamanda Amata, kuua kwako kama chai ya asubuhi” akamwambia.

“Na mapenzi kwa watoto wazuri kama pumzi ya kila siku,” kamanda akamalizia.

“Niue na mimi ….” Akazidi kulalama huku akijinyonganyonga.

“Jiue mwenyewe!” Amata akamjibu.

<<< MWISHO >>>

© Richard R. MWAMBE

JAMVI LA SIMULIZI

Jamvilasimulizi@gmail.com… 0766 974865

 

NB
Riwaya hii haijafanyiwa uhariri, hivyo makosa ya kisarufi na masimulizi, ni tatizo la mwandishi mwenyewe.

 

 

 

 

 

 

 

Share

Leave a Reply

Translate »
error: OPS! Content is protected !! Imezuiwa